Hivi majuzi, Dk. Ali Mohammed Shein alihudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais wa visiwa vya Comoro zilizofanyika mjini Moroni. Habari zinasema alikwenda huko kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, ambaye ndiye aliyealikwa rasmi. Picha zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zilimuonesha Dk. Shein akiwa amekaa katika safu ya nyuma na ya mwisho kabisa akiwa yuko pamoja na wageni wengine walioelezwa kuwa ni mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao.

Inaonesha watu walitegemea kwa Kiongozi wa daraja yake akiwa ni Rais wa Zanzibar basi itifaki ingekuwa kwa yeye kukaa na marais ‘wenzake‘. Tukio hilo likaibua mjadala katika mitandao ya kijamii. Wapo waliotafsiri kitendo kile kuwa ni udhalilishwaji wa mamlaka na haiba ya Zanzibar kimataifa kwa “kumdogosha” kulikopitiliza ‘Rais‘ wa Zanzibar.

Na Awadh Ali Said
Na Awadh Ali Said

Wapo walioshangazwa na uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumtuma ‘rais mwenzake‘ kumuwakilisha katika medani za kimataifa. Wapo walioona kuwa hadhari stahiki haikuchukuliwa katika uamuzi ule ambao matokeo yake umemtosa ‘rais‘ wao katika idhilali huko ughaibuni. Hawa hoja yao ni kuwa kwa muundo wa Muungano wetu hivi ulivyo kwa wakati huu, si busara kwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumtuma rais wa Zanzibar kumuwakilisha popote nje ya nchi. Kwa vipi? Tujadili tartibu.

Muungano huu ulipoasisiwa mwaka 1964 kupitia Mkataba wa Muungano ilielezwa katika kifungu cha 3(b) cha Mkataba huo kuwa Rais wa Zanzibar, kwa wadhifa wake huo, anakuwa mmoja kati ya Makamu wawili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania moja kwa moja. Itifaki na madaraka yake kwa ndani na nje ya nchi ililkuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kufuatia ujio wa mfumo wa vyama vingi vya siasa mnamo mwaka 1992, nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uongozi ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikaleta taharuki.

Taharuki hii ilichangiwa na uimara wa Upinzani ulivyo katika siasa za Zanzibar. Hofu ikawa endapo Upinzani ungeshinda urais wa Zanzibar na kwa hali ya kikatiba ilivyo kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano ni wazi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa mtu kutoka upinzani. Na hilo likaonekana halivumiliki. Halivumiliki kwa sababu kikatiba nakamu wa rais ndiye msaidizi mkuu wa rais na litokeapo lolote la Kikatiba litalopelekea rais kutomudu majukumu yake au kama hayupo, Makamu anashika khatamu za utawala wa nchi.

Mbali na hilo, ilionekana hakutakuwa na siri tena kwa chama kinachoshika madaraka na serikali yake kwa vile mpinzani ameingia sebuleni kwa kupitia mlango wa nyuma. Kulikwepa hilo, mnamo mwaka 1994 yakafanywa Mabadiliko ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ambayo yalimuondoa Rais wa Zanzibar katika nafasi yake ya Umakamu badala yake ukaanzishwa mfumo wa mgombea mwenza; kwa maana kuwa endapo mgombea wa urais akitoka upande mmoja wa Muungano, basi mgombea mwenza ni sharti atoke upande wa pili wa Muungano. Na kwamba Rais wa Zanzibar asiwe tena makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ila badala yake nafasi ya umakamu wa Rais ikafidiwa kwa nafasi ya kuwa mjumbe tu katika Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa lugha nyepesi ni kuwa nafasi ya umakamu wa Rais ilifidiwa kwa nafasi ya uwaziri. Jambo hili lilileta mvutano na sokomoko kubwa katika uhai wa Muungano. Kwa kweli Wazanzibari wa mirengo yote ya kisiasa hawakuufurahia kabisa uamuzi huo na waliupinga waziwazi. Kwa mfano, mnamo mwaka 1995 Wazanzibari 50 wakiongozwa na Bw. Mtumwa Said Haji (sasa ni marehemu) walifungua shauri la kikatiba Mahkama Kuu ya Tanzania wakimshitaki Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupinga Mabadiliko ya 11 ya Katiba ambayo yalimfanya Rais wa Zanzibar kuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri badala ya nafasi ya Umakamu wa Rais kama ilivyo katika Mkataba wa Muungano. Walipinga uvunjwaji wa Mkataba wa Muungano; uvunjwaji ambao kimsingi ulilenga kuiondolea Zanzibar nafasi yake kama Mshirika kamili ndani ya Muungano. Kwa sababu zilizo dhahir, malalamiko yao yalitupiliwa mbali Mahkamani.

Rais wa Zanzibar wa wakati huo, Dk. Salmin Amour Juma, alikacha kula kiapo cha Uwaziri kwa madai kuwa Rais wa Nchi hawezi kula kiapo mbele ya Rais mwenzake. Kwa hivyo, Ilibidi marekebisho yafanywe ili Rais wa Zanzibar asile kiapo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali ale kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wengine wakahoji ni vipi unakataa kula kiapo kwa Rais mwenzako ila unaridhia kula kiapo kwa mtu ambae ni mteule wa Rais mwenzako!!!. Hali ya sasa ya Kikatiba ilivyo ni kuwa katika Ngazi ya Uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar nafasi yake ni Mjumbe tu wa kawaida katika Baraza la Mawaziri asiye na la ziada yoyote kiitifaki na kimadaraka juu ya Mawaziri wengineo. Alilozidi yeye ni kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hana mamlaka ya kumfuta Uwaziri kwa vile yeye ameingia humo kwa wadhifa wake (ex-officio) na sio kwa kuteuliwa.

Tuiangalie nafasi ya Rais wa Zanzibar ilivyo sasa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Ibara ya 54 (1) inasema:

“Kutakuwa na Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake watakuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, RAIS WA ZANZIBAR na Mawaziri wote”.

Mbali na Rais wa Zanzibar kufanywa Mjumbe tu wa Baraza la Mawaziri, lakini pia Ibara zinazofuata zimemuweka katika nafasi sawa na Waziri yoyote wa kawaida katika Baraza hilo. Ibara ya 54 (2) inayozungumzia uendeshaji wa Baraza la Mawaziri haikumpa Rais wa Zanzibar nafasi yoyote ya kiuongozi katika Baraza hilo zaidi ya ujumbe wake wa kawaida; inasomeka:

“Rais atahudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri na ndiye atakayeongoza mikutano hiyo. Na endapo Rais hayupo basi mikutano itaongozwa na Makamu wa Rais na kama wote wawili Rais na Makamu wa Rais hawapo Waziri Mkuu ndiye ataongoza Mikutano hiyo”

Hivyo katika kikao cha Baraza la Mawaziri ambacho Rais wa Zanzibar amehudhuria na ikatokea Rais na Makamu hawapo, Rais wa Zanzibar anakuwa chini ya Waziri Mkuu. Hata pale Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anapokuwa hayupo au ameshindwa kutekeleza majukumu yake ya urais, basi Rais wa Zanzibar hana nafasi yoyote na anabaki kama Mjumbe wa kawaida wa Baraza la Mawaziri. Kifungu cha 37(3) kinasomeka:

“Endapo Rais atakuwa hayupo katika Jamhuri ya Muungano au atashindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu nyingine yoyote, kazi na shughuli za Rais zitatekelezwa na wafuatao kwa kufuata mpangilio ufuato, yaani: a) Makamu wa Rais au kama nafasi yake iwazi au kama naye hayupo au ni mgonjwa, basi; b) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano.”

Kwa muktadha wa Katiba, tukirudi katika hoja ya msingi ya jinsi Rais wa Zanzibar alivyochukuliwa kiitifaki huko Comoro ni wazi kuwa ‘Rais wa Zanzibar‘ alichukuliwa kama Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alietumwa kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo kwa wadhifa huo wa Ujumbe wa Baraza la Mawaziri ni wazi kuwa hakuna udhalilishaji wowote ila hio ndio stahiki ya mhudhuriaji wa Wadhifa wake.

Pengine iliyochanganya baadhi yetu ni pale tulipoona ADC (Aide de Camp) wa Rais, maarufu kama Body Guard wa Rais, alivyokuwa hajatulia katika nafasi maalum. Ila inawezekana kuwa hili lilitokana na mkanganyiko kuwa Rais wa Zanzibar pale hakuwepo kama Rais bali Mjumbe wa Baraza la Mawaziri ambaye taratibu za kilimwengu ni kuwa hategemewi kuambatana na ADC.

Ukweli ni kuwa hata hili suala la Rais wa Zanzibar kuambatana na ADC wa kijeshi au kupigiwa mizinga ya heshima ya kijeshi limekuwa linaelezwa kuleta ukakasi katika anga za itifaki ya kijeshi kwa vile hayo ni mambo maalum ambayo hufanyiwa Kiongozi Mkuu wa Nchi ambaye ndie Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania.

Wenye hoja hiyo wanashikilia kuwa Rais wa Zanzibar hana sifa hiyo; yaani si Rais mwenye “Sovereign powers” bali ni Rais mwenye mamlaka ya ndani tu. Pamoja na kuzikubali hisia za waliokirihika na tukio lile, lakini hiyo ndio hali halisi ya Muungano wetu kwa mujibu wa muundo tulionao.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.