Ni Qur’an ndiyo inayouliza swali hilo katika sura yake ya 95, aya ya 7. Namna ilivyokuwa na miujiza, katika aya ya 4 ya sura hiyo hiyo, Qur’an inaelezea namna Mwenyezi Mungu anavyojisifu kwa kumuumba mwanaadamu kwa umbile lililo bora kabisa, lakini kisha, hapo hapo, inafuatia aya ya 5 inayoonesha nguvu nyengine za Muumba kuwa ni kuumbuwa – mwanaadamu kushushwa kuwa chini kuliko walio chini. Walio chini ni akina nani? Ni wowote wachafu, dhaifu, wakosefu, na ila nyengine mbaya ambazo ungeweza kuzifikiria. Hata mende wa chooni anakuwa bora siku ya Muumba kumuumbuwa mwanaadamu inapofika.

Sisi tusio na maarifa ya tafsiri na taawili huwa tunaona kwenye Qur’an muna vinyume-mbele vingi, lakini ukweli ni kuwa kila mtu anaposogea kwenye kuisoma Qur’an yenyewe, ndipo anapozidi kuuona utukufu wa Mungu, sio tu kwenye hili la kuumba na kuumbuwa, bali pia hata kwenye lugha anayoitumia katika kuuelezea uwezo wake usio mipaka. Hata alipouliza swali hilo, si kwamba Mungu hakuwa na jawabu yake. Hapana. Aliuliza ili kutupa mazingatio sisi tunaoyasoma maneno yake.

Mungu ametuumba sisi na tulivyovitengeza sisi kwa mikono yetu, na kimojawapo ni hiki kijidude kinachoitwa simu ya mkononi, ambacho mwanaadamu amekigundua na kila kukicha anakiboresha zaidi. Tangu kilikuwa ni kijidude cha kusema na kusikiana tu kwa sauti tu, mpaka kikawa cha kuandikiana maandishi na saa hizi kimekuwa ni zaidi ya chombo cha habari. Nakiona kinaanza kubeba taswira ya kiumbe chenye mapenzi na hisia kiasi ya kwamba wengi wetu hatuwezi kutengana nacho.

Wakati jaala ya maisha inaweza kukunyima utajiri wa fedha au hangaiko la malimwengu likakunyima ukuruba na watu, lakini hiki kijidude hakikutendei ubaya huo. Badala yake kinakupa utajiri wa kutosha na usuhuba usio na masharti, kwa kukumiminia taarifa kila baada ya dakika, kama si sekunde.

shein shein2Ndani ya kipindi cha masaa 24, simu yako ya mkononi inakuwa imeshakupatia taarifa zaidi ya 1,001 na inakuwachia mwenyewe uhuru wa kuamua ipi uichukuwe, ipi uiwache, ipi uiamini, ipi uikanushe, ipi uisambaze, ipi uifute, ipi uichekee, ipi uinunie. Unaweza ukauliza hili la mawasiliano ya simu lina uhusiano gani na nguvu za Mungu kwenye kuumba na kuumbua? Upo.

Ndani ya masaa haya 24, simu yangu ya mkononi kupitia mitandao mbalimbali niliyoiunga nayo imeshanipatia taarifa kadhaa kutoka nyumbani kwetu, umbali wa maili 4,329 kutoka hapa nilipo. Kama ningekuwa nimetumia ndege aina ya Cessna 172 inayoruka kwa kasi ya kilomita 200 kwa saa, basi ningelitumia masaa 34 na dakika 49 kufika nyumbani kwenda kuyaona na kuyajuwa (au kuyashuhudia) ambayo simu yangu imeniletea hapa hapa kiganjani. Hata kwa ndege aina ya Airbus A320 inayosafiri kwa kilomita 800 kwa saa, basi bado ningelitumia masaa 8 na dakika 42 – robo nzima ya siku.

Mimi ndani ya mawasiliano haya ya simu, nauona uwezo wa Mungu usio mipaka na nashuhudia pia akiwaumba na kuwaumbua viumbe vyake kupitia taarifa ambazo zinatumwa na kutumiliwa humu. Kwa mfano, ndani ya masaa haya 24, simu yangu imeshanipa taarifa kadhaa, zikiwemo picha, sauti na vidio, na tatu kati yake zimebakia kichwani mwangu kwa muda mrefu, maana zinaonesha uwezo huo wa Mungu kwa viumbe vyake – uwezo wa kuumba na kuumbua:

i. Picha za Dk. Ali Mohamed Shein akiwa kwenye jukwaa la wageni waalikwa, mstari wa nyuma kabisa karibu na ukuta, mjini Moroni, visiwa vya Komoro, akishiriki kuapishwa kwa rais mpya wa serikali ya shirikisho la visiwa hivyo, Azali Asoumani Bounakheir.

ii. Picha za vidio za aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi, akiwa anaburuzwa kutoka nyumba ya wageni, akituhumiwa kufumaniwa na mkewe akiwa na mtoto wake wa kambu.

iii. Nakala ya barua ya Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar, Salum Msangi, kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kumuarifu kuwa yale mahojiano aliyotaka kumfanyia Ijumaa ya leo tarehe 27 Mei 2016 hayapo tena “kwa sababu zilizo nje ya uwezo” wa jeshi la Polisi.

Kwa sababu ya muda, leo hii nitazungumzia hilo la kwanza tu – la kuumbuliwa kwa Dk. Shein.

Dk. Shein aliambiwa kuwa ametumwa na Rais John Magufuli kwenda kumuwakilisha kwenye sherehe za kuapishwa kwa Rais Bounakheir. Mpaka hapo hapana tatizo. Lakini tatizo linaanza pale mtu anapoanza uchambuzi.

Kwanza, Dk. Shein amerejea kwenye hatamu za kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya Chama chake cha Mapinduzi (CCM) kushirikiana na vyombo vya ulinzi kuuharibu uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba na kisha kujiweka madarakani kwa waliouita uchaguzi wa Machi 20. Wengi wanaamini kuwa CUF ilishinda uchaguzi wa Oktoba 25, lakini vyombo vya dola vikaizuia kutangazwa na hivyo kuzuiwa kuunda serikali.

Mwenzake wa Comoro, Azali Asoumani, ameingia madarakani akitokea upinzani na ambao ulikumbwa na mashaka hayo hayo ya kutaka kuzuiliwa na chama tawala na vyombo vya dola, lakini ukafanikiwa kupenya hata kwenye uchaguzi wa marudio wa baadhi ya vituo tu katika kisiwa cha Anjouan. Hii ni kusema, Dk. Shein aliyepo madarakani kwa nguvu za vyombo vya dola ameumbuliwa kwa kupelekwa ashuhudie kuapishwa kwa anayeingia madarakani kwa nguvu za kura za wananchi. Kwani Mungu si hakimu wa mahakimu?

Pili, visiwa vya Komoro na visiwa vya Zanzibar vina uhusiano wa karne kadhaa baina yao, wakati huo hata hakujawahi kufikiriwa kwamba kutakuwa na nchi itakayoitwa Tanganyika na baadaye Tanzania. Inapotokezea rais wa Tanzania anamtaka mtu anayejihesabu kuwa ni rais wa Zanzibar akamuwakilishe kwenye sherehe za kuapishwa kwa rais wa Komoro, hakika huku ni kuumbuliwa kukubwa si kwa Dk. Shein peke yake, bali kwa Zanzibar nzima.

msangiNafasi ya Zanzibar kwa Komoro ni nafasi ya kaka na ndugu yake wa tumbo moja. Nafsini mwangu itaniumiza sana siku ambayo rafiki wa kaka yangu tuliyezaliwa tumbo moja ataniomba nimuwakilishe kwenye harusi ya kaka yangu huyo, tena sababu yenyewe ni kuwa mimi ni mjumbe tu wa huyo rafiki wa kaka yangu na sio kuwa nina nafasi au heshima sawa naye.

Tatu, kama nilivyosema, picha zilizosambaa kwenye simu zetu za mikononi zinamuonesha Dk. Shein akiwa amewekwa mstari wa nyuma kabisa, karibu sana na ukuta, akiwa safu moja na mabalozi wa mataifa mengine wanaowakilisha nchi zao kwenye sherehe hiyo, na sio kwenye safu ya mbele wanapokaa viongozi wakuu wa serikali na dola.

Inaonekana kuwa hata kama Rais Magufuli alimtuma Dk. Shein akamuwakilishe kwenye sherehe hizo, basi hakumtaka aende kama rais wa Zanzibar, bali kama mjumbe wa baraza la mawaziri la Tanzania, cheo ambacho hakina uzito wowote kwenye majukwaa kama haya.

Niliwahi kumuonya Dk. Shein baada ya kuamua kujivunjia heshima yake kwa kujiweka madarakani bila ya ridhaa ya wananchi wa Zanzibar kwamba daima kioo kitamuambia: “Wewe ni Ali tu!” Nadhani ndiyo alivyoisikia sauti ikimuambia kule nyuma alikoketi kwenye jukwaa la Moroni.

One thought on “Dk. Shein, Dadi na Msangi, kwani Mungu si Mbora wa kuhukumu?”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.