Picha inayosawiri makala hii niliipiga tarehe 24 Julai 2010, nje ya msikiti wa Ijtimai, Fuoni, magharibi ya kisiwa cha Unguja. Angalia huyo mtoto mkono wa kushoto ambaye anawania kumpa mkono Maalim Seif Sharif Hamad. Nakisia kuwa wakati huo alikuwa na miaka 12 au 13, umri ambao anao mtoto wangu wa kwanza hivi sasa. Kwa hivyo, sasa ana miaka 18 au 19 na yumkini alikuwa mpigakura kwenye uchaguzi wa Oktoba 25. Naamini alimpigia kura Maalim Seif.

Wakati napiga picha ya mvulana huyu akiwania kumpa mkono Maalim Seif siku hiyo, kumbukumbu ya siku ya kwanza kumuona kiongozi huyu uso kwa macho ilinirejea kichwani mwangu. Nakumbuka, nikiwa na umri wa miaka 7 au 8, Maalim Seif alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar na alikuja kutembelea Kambi ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Msaani, wakati huo bonde la Msaani lilikuwa kwenye mpango wa MTAKULA aliouanzisha yeye kwa ajili ya kuitosheleza Zanzibar kwa chakula.

Baada ya ziara yake, akaamua kukutana na wananchi wanaoishi pembezoni mwa bonde hilo na kambi yenyewe ya JKU, awasikilize malalamiko au maoni yao. Mmoja wao alikuwa baba yangu (Allah amrehemu), ambaye wakati huo alikuwa anakaribia au amepindukia kidogo miaka 60. Malalamiko yake yalikuwa ni juu ya sehemu ya shamba letu la Mti Mkuu ambalo lilichukuliwa na uongozi wa JKU bila ya ridhaa yake na tena likiwa halihusiki kabisa na bonde la Msaani unakolimwa mpunga wa mradi wa MTAKULA.

Wananchi wakiwania kumpa mkono Maalim Seif Sharif Hamad, siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Julai 2010, Fuoni Zanzibar.
Wananchi wakiwania kumpa mkono Maalim Seif Sharif Hamad, siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Julai 2010, Fuoni Zanzibar.

 

Nadhani chini ya mpango huu wa MTAKULA serikali ilikuwa imewaruhusu JKU kuchukuwa ardhi yoyote ambayo wanaona inafaa baada ya makubaliano na wenye ardhi hiyo. Lakini yetu sisi ilikuwa upande wa juu na sio bondeni, hivyo haikufaa kulimwa mpunga wa umwagiliaji. Mkutano ulifanyika kwenye banda la JKU na baba akasimama kuelezea malalamiko yake.

Wakati huo, bado kiwango cha woga wa wananchi kwa serikali kilikuwa kikubwa na ilitaka ujasiri kwa mzee wa kijijini kusimama mbele ya umma kulisema Jeshi hilo kwa ubaya. Maalim Seif akamuuliza baba yangu: “Je, umeshapeleka malalamiko yako haya kwa ngazi husika?” Baba akamuambia alishapeleka, na ameshafika hadi kwa mkuu wa mkoa wa Kaskazini Pemba wa wakati huo, Maalim Masoud Omar Said (Allah amrehemu), ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo, akiwa meza kuu.

Huyu Maalim Masoud alikuwa pia mtu wa Pandani, yeye akitokea Kwa Mwewe kwa Mabatawi, sisi wa Mchangani. Alikuwa katika wasomi wa kwanza wa Pandani, nadhani alifika Makerere. Baadaye, kama ilivyokuwa kwa mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, Maalim Juma Ngwali (Allah amrehemu), alikuja akawa muasisi wa CUF.

Maalim Seif alipomgeukia Maalim Masoud kumuuliza, Maalim Masoud akamruka baba yangu. “Hapana, Bwa’ Khelef hujawahi kuja na suala hili!” Baba yangu akainuka kama katiwa moto, tena kwa hasira: “Bwan’ Masoud, wataka nije hapo tusutane?” Akawa anatia mkono mfukoni kutoa barua za Mkuu wa JKU, Mkuu wa Wilaya, Chameni Mzee Juma Mansour na yake yeye mkuu wa mkoa. Baba alikuwa na tabia, ambayo amenirithisha mimi, ya kuweka kumbukumbu ya maandishi ya takribani kila kitu. Mwenyewe alijifundisha kusoma, kuandika na kuhesabu kwa hati za Kizungu akiwa mtu mzima, lakini alikuwa anajuwa kuyafanya yote kwa uhodari mkubwa.

Maalim Seif akajuwa kuwa hapa aibu itazuka. “Basi mzee. Suala lako litashughulikiwa mara moja.” Siku hiyo, nilitoka njia nzima nimemshika mkono baba yangu nikijirusha huku na kule kwa furaha. Nadhani moyoni nilikuwa najionea fakhari kuwa baba yangu amesimama mbele ya serikali yote na akasema kwa ushujaa. Hadithi zote zilikuwa kuhusu yeye siku hiyo.

Maalim Masoud alikuja kumtembelea baba dukani kwetu siku chache baadaye. Nakumbuka alikuwa anaendesha gari ya Land Rover rangi ya chai ya maziwa. Mazungumzo yao sikuyasikia, lakini baada ya kiasi cha mwezi hivi, tukarejeshewa shamba letu. Shamba lenyewe si kubwa, lakini lilitosha kutupa wasaa wa kulima muhogo na viazi na kupanda minazi, ambayo masikini baba yangu hakuwahi kuishi akaja akaona ikizaa.

Picha nzima ya mkasa wenyewe imesalia hadi leo kichwani mwangu kama mkanda wa vidio. Nakumbuka mvua, matope, utelezi wa mlima wa Kombo Hawana, sare za kijani za JKU, mpunga uliowanda kwenye chanjaa la Msaani, sura yake Maalim Seif, kanzu aliyovaa baba na kofia yake ya kudengua, sura za watoto wenzangu waliokuwepo na yote.

Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona Maalim Seif uso kwa macho. Huyu ndiye Maalim Seif alivyojiwasilisha kwangu nikiwa mtoto wa miaka 7, na hiyo ndiyo kumbukumbu aliyoniwacha nayo hadi leo nikiwa nakaribia miaka 40. Mtu wa haki wa zama zote. Jana, leo na kesho.

Siku nyengine nitakuja kusimulia namna ambavyo mwaka mmoja baadaye nilikuja kumuambia kuwa “nataka kuwa kama Maalim”, naye akaniambia “kuwa”, lakini bahati mbaya sikuwa.

One thought on “Maalim Seif, mtu aliyekuwa na daima atakayekuwa”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.