Katika pitapita yangu mtandaoni jioni ya tarehe 22 Mei 2016 nimekuta taarifa ya idhari kwenye ukurasa wa Facebook wa ITV. Ni taarifa ya Balozi Seif Ali Idd akiwatahadharisha wafanyakazi wa serikali kutothubutu kubagua wananchi kwenye maeneo yao ya kazi kama utii wa agizo la aliyoiita kauli ya Maalim Seif Sharif Hamad ya kuwataka watu kuwagomea wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa ziara yake alioifanya kisiwani Pemba kwenye siku za karibuni na ambayo, hapana shaka, ilikuwa ya mafanikio makubwa na pigo jingine la kisiasa kwa CCM na serikali zake.

Pengine ni weweseko au hali ambayo mara nyingi husababishwa na mtawala kukosa imani na ithibati ya mtawaliwa. Kwamba kawaida ya mtawala asiyekubalika kwa watawaliwa, hana awazacho kichwani mwake zaidi ya mipango mibaya dhidi ya yule anaye mtawala kwa nguvu. Kwamba mtawala huyu anaweza kuwa ndio gwiji wakuasisi nakusimika misingi fulani mibaya kwa manufaa yake na serikali yake lakini asione ubaya wa hilo ingawa nafsini mwakeanajuwa kwamba hili nifanyalo sio zuri. Hii ni kwavile nafsi imepewa uwezo wakujua baya na zuri.
Na Ahmad Abu Farsi
Na Ahmad Abu Farsi

Jioni ya siku ya Alkhamis wiki jana, nilibahatika kuketi mahala jirani ya barabara kuu itokayo Micheweni kuelekea mijini yaani Chake au Wete. Eneo hili lina makutano ya barabara kuu hivyo pirikapirika za magari huwa nyingi muda wote.

 

Hata hivyo tofauti na siku nyingine, jioni hii ilitawaliwa na utulivu barabarani huku shughuli za watu kimaisha zikiendelea kama kawaida. Katika eneo la makutano ya barabara alisimama trafiki ambaye ni kijana mrefu na nguo zake nyeupe. Uwepo wa askari eneo lile ulinifanya nijiulize kimoyomoyo, “kulikoni” askari huyu kuwa mahali hapa muda huu”? Nilijiuliza kwa vile ni nadra sana kumkuta askari wa usalama barabarani akiwa barabarani hadi saa 12 jioni katika kisiwa hichi cha Pemba. Kwani kwa miezi kadhaa ya uwepo wangu kwenye kisiwa hiki, hii ni mara yangu ya kwanza. Hata hivyo baada ya sekunde chache za kujidadisi mwenyewe, nagundua kwamba pamoja na uwepo wa trafiki yule pale njia panda, pia walikuwepo askari kanzu wengi mno kwenye eneo hili.

Mazingira ya eneo hili yakanifanya nitake kujua zaidi na ikanilazimu kuwauliza maalwatani kadhaa wa eneo lile ambao kama kawaida yao walijazana kwenye vibaraza vyao huku kofia zao zikiwa kwenye mapaji ya nyuso zao karibia kudondoka chini lakini hazidondoki. Hapa nikajiuliza tena, “wana nini leo mamwinyi wa Kipemba?” Nikasogea karibu yao na kujiunga nao na bila kukawia nikauliza suali juu ya eneo kujaa askari kanzu, ambapo bila watu kumunyamunya maneno wakanijibu, “weye mwandishi mzima hujuwi kama leo Balozi yuko Micheweni, uko wapi weye yakhee!”
Alikuwa Balozi Seif Ali Idd ambaye alifanya ziara yake kisiwani Pemba ambako alifanikiwa kutembelea maeneo kadhaa kwa wilaya zote za kisiwa cha Pemba. Ambapo miongoni mwa maeneo aliyofika ni katika kijiji cha Kiuyu Maziwa Ng’ombe, eneo ambalo siku za karibuni lilikumbwa na ghasia ambazo zilipelekea polisi wa kutuliza ghasia kufika eneo hilo na kuanza kupiga hovyo mabomu ya machozi kijiji kizima.
Balozi Seif alifika na kwenda kumpa pole sheha huyo kwa tukio hilo pamoja na familia yake ambayo sio siri kwamba ni familia ambayo inaishi kwenye mazingira magumu sana yatokanayo na kuzungukwa na idadi kubwa ya wananchi wenye mrengo tofauti wa kisiasa tena mioyoni waliojaa machungu ya dhulma za kila aina zifanywazo na serikali kupitia masheha kama mawakala wao.
Hivyo kutokana na matendo ya kibaguzi ambayo husimamiwa na masheha katika ngazi za chini, hii kama familia ya sheha ilikuwa na haki zote kuishi kwenye hali ya uoga kwani haikuwa jambo jepesi na rahisi kutuliza ghababu za raia wale nakuweza kujiamini mia kwa mia kwamba familia iko salama.
Nilibahatika kufika eneo hili siku ya tukio la polisi kuripua mabomu na miongoni mwa matukio ambayo sitoyasahau maishani mwangu, ni tukio la polisi mmoja kuniwekea mtutu wa bunduki kwenye paji langu la uso na kisha kunitukana matusi ya nguoni utadhani nilifika mahali pale nami kugombana nao. Niliandamwa na kukogeshwa matusi huku nikitishiwa kuripuliwa kwa mtutu wa bunduki yakufyatulia bomu la machozi kama alivyo ripuliwa mwandishi mwenzangu Daudi Mwangosi kule mkoani Iringa miaka kadhaa iliopita.
Baada ya kashikashi hili la polisi, niliamriwa kuondoka mara moja eneo lile huku nikiwacha nyuma mabomu yakiendelea kuungurumishwa kwenye vijumba vya raia wanyonge tena wanukao umaskini wakutisha. Hatimaye nilifanikiwa kurudi tena eneo hili nikiwa na kamanda wa mkoa Mzee Hassan Nasir. Hata hivyo pia sikuachiwa, kwani kulingana na niliyoyakuta baada yakurejea na kamanda huyu, safari hii polisi walidhibiti vitendea kazi vyangu vikiwemo kamera na tablet yangu ambayo ndio kama roho yangu.
Nimesema hivi kwa vile kifaa hiki huniwezesha kuihabarisha dunia tukio lolote kwa muda wa sekunde chache. Kwamba naweza iseti ikawa yapiga picha nakurusha mitandaoni hapohapo tofauti na kamera ambayo lazma uiunganishe na kompyuta ndipo utume picha.
Tukio lililo pelekea kupokwa vifaa na polisi ni lile la vijana wa Kizanzibari wa Kiuyu kulazimishwa wazamishe vichwa vyao nakugaragazwa kwenye dimbwi la maji machafu ambayo yalituama mahali hapo kwa masiku kadhaa nakujaa viluilui vya maradhi.
Pamoja na vifaa vyangu vya kazi kudhibitiwa, nyenzo kuu ambazo ni akili na macho nilibakia navyo hivyo nikaona nakuchambua kila nilicho bahatika kukiona . Nilimuona bibi mtu mzima ambaye ni mgonjwa kwa miaka kadhaa akiwa hoi kwa kuburuzwa na polisi, lakini pia nilishuhudia mikebe miwili ya mabomu ya machozi ambayo imeripuliwa kwenye chumba cha binti mwenye kichanga cha masaa manne. Kwamba binti huyu alijifungua saa 1moja asubuhi na saa nne mjiuka anza kutandikwa mabomu ya machozi! Nilishuhudia kuta na bati za misikiti pia zikiwa zimetobolewa matundu makubwa kwakudondokewa na mikebe ya mabomu. Nilishuhudia nyumba zikiwa zimevunjwa milango na vifaa kama pikipiki na baiskeli kuharibiwa kwakukatwa mipira kwa kisu au kitu chenyencha kali!
Baada ya matukio haya nilioshuhudia, ndio siku chache akawasili Balozi Seif kwenda kutowa pole kwa sheha ambaye matufali kadhaa na kitalu cha miti viliharibiwa vibaya. Hata hivyo hapa napata mashaka kidogo. Kwamba ukiacha sheha, wapo wananchi wengine ambao wamekumbwa na madhara ya tukio hili hivyo nilimtarajia Balozi Seif angefanya ziara yakuwapa pole na wengine ambao walikubwa na athari hizo. Lakini kinyume na hivyo, Balozi Seif kaishia kwa sheha pekee kana kwamba hawa waathirika wengine si sehemu ya raia au walipa kodi wa nchi hii, jee huu tuupe jina gani kinyume na ubaguzi? Tena ubaguzi ambao Balozi Seif anaukemea kwa mkwala mkali wa kumfukuza yeyote kazi akimbagua mtu!
Inawezekana Balozi Seif kasahau hivyo tuna wajibu kumkumbusha. Balozi Seif ubaguzi mumeuasisi nakuuabudu nyinyi na chama chenu bila kificho. Ni masheha hawa tulioshuhudia wakiwanyima haki wenye haki kwenye chaguzi mbalimbali. Ni masheha hawa tulioshuhudia wakiwanyima watu haki yakupata vitambulisho vya Uzanzibari. Ni masheha hawa tulioshuhudia wakiwanyima watu haki yakupata vyeti vyao vya kuzaliwa. Ni masheha hawa ambao tuliwashuhudia wakisimamia dhulma dhidi ya Wazanzibari kwenye uchaguzi mweusi wa March 20. Ni hawa Balozi Seif na ndio sababu ya wewe kutoka ulipo toka ukaja kuwafariji kwa uchache wao na huku ukiwadharau wengine wengi eti kwa sababu ya kuwa mrengo tofauti na wewe, jee, ziko wapi busara ambazo kiogozi anapaswa kuwa nazo?
Hakika ujio wako balozi Seif umedhihirisha kwamba wewe na wenzako si viongozi wa Wazanzibari kwa umoja wao bali kundi dogo lenye kulazimisha uongozi kwa njia za mtutu na mabomu kama yalivyo orodheshwa kwenye kitabu cha matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu na hili nililo lishuhudia juzi Kiuyu. Hakika siamini kama nchi huendeshwa hivi na ikasonga mbele. Bali nikionacho mbele yangu ni watu kuogopa dubwana waliloliunda na kuliamini na sasa limewageuka, hawana raha tena!
Tanbihi: Mwandishi wa Makala hii, Ahmad Abu Faris, ni mwandishi wa habari anayeishi kisiwani Pemba na anapatikana kwa nambari ya simu 00255 774-581264.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.