Kuna matukio kadhaa yametokea usiku wa jana (Mei 19) hapa kisiwani Pemba. Kubwa miongoni mwao ni tukio la magari ya polisi (Defender) kuingia mitaani na kuwafukuza raia kwenye maeneo mbalimbali kama vile kwenye matawi na maskani za Chama cha Wananchi (CUF) na pia kwenye mabaraza ya kahawa. Zoezi hili lilifanyika nyakati za usiku muda ambao wengi huwa kwenye maeneo haya kwa lengo lakusaka mkate wa kesho wa watoto zao.
Hili ni jambo lisilokubalika kutendewa raia wanyonge khasa kwenye mazingira tulivu ambayo hayavunji amani seuse kumyima usingizi yeyote miongoni mwetu.
ahmad
Na Ahmad Abu Farsi

Pengine yawezekana pakawepo na sababu za watu kuzuwiwa kutoka nje ya nyumba zao zaidi ya saa mbili kama alivyofanya mkuu wa mkoa mmoja hivi karibuni. Lakini si sasa muda ambao uchaguzi ushafanyika na aliyetakiwa na dola kuwa raisi tayari keshakuwa. Kile wakifanyacho sasa polisi wetu nikuendelea kutishwa na vuvuli vyao wenyewe. Nikutishwa kwavile hakuna sababu yakulazimisha watu kuondoka kwenye shughuli zakuwapatia rizki na watoto wao usiku wa saa mbili.

Hata hivyo, yawezekana pia kuwepo matukio ya watu kutokuwa na mahusiano mema kwenye jamii kiasi cha wengine kutokuwa huru kujumuika na wengine kwenye maeneo kama haya ambayo nao ni haki yao kuwepo. Lakini ifahamike kwamba suala la mshikamano ni suala limgusalo kila mwanajamii pasi nakujali chama au dini yake. Lakini pia hapawezi kuwepo na mshikamano iwapo tumeamua kushabikia dhulma kwa mwenye kustahili haki.
Hakuna uwezekano wakuileta pamoja jamii ilihali tuliamua kwa maksudi kusimamia dhulma dhidi ya kundi kubwa la jamii tunayoishi nayo, kuzungumza nayo sambamba nakushirikiana nayo kwenye kila jambo. Hatuwezi kupata suluhu ya tatizo kwa njia hizi zakutimua wauza kahawa vibarazani bali tunazidisha ukubwa wake.
Nadhani umefika muda wa ama wakubwa kuikubali kweli wakaaitendea haki au kila kundi kuwa na kijiwe chake, maduka, magari, masoko na vingine vingi. Nalisema hili nikiamini suala la jamii ya Pemba kuwa pamoja ni jambo gumu kwani wengi miongoni mwa wanajamii, wamepoteza matumaini ya mabadiliko kwa njia ya kura na wanacho amini sasa ni kile Waingereza wakiitacho passive resistance ambayo ni ngumu kuidhibiti hata ukiwa na nguvu ya vifaru.
Wajengeeni vijiwe vyao ili apendae kujumuika nao aende na asopenda atulie apendapo. Wanunulieni magari maalumu yawabebe nakuwapeleka watakako na wala sio kulazimisha madereva kuchoma mafuta ya shilingi 7,000 kwa kusafirisha abiria wa shilingi 1,500.
Hakuna sababu polisi kujiingiza nakukubali kutumiwa na wanasiasa wenye kuitazama haki kwa jicho kengeza. Kwamba kumdhulumu raia sio dhulma bali dhulma ni raia kudai haki yake kwa njia yakutoshirikiana na yule mwenye kushabikia dhulma dhidi yake. Polisi wawe walinzi wa amani na sio vikaragosi vya masheha wasiojuwa wafanyalo.
Ni imani yangu kwamba ndani ya jeshi hili wapo watu wenye ufahamu uliotukuka na mapenzi mema kwa nchi hii. Hivyo niwasihi kwakuwaeleza kwamba, wafanyiwayo raia hapa Pemba sio haki na kama walikuwa hawajuwi basi wajuwe. Wajuwe kwamba vijana wao wanaoenda kwenye doria nyakati za usiku, husumbua mno raia wanyonge wakaao vibarazani kudunduliza mia mia za kahawa ili kustiri familia zao. Huu si uungwana, huu si ustaarabu, tujisahihishe ili kuiepusha jamii na madhila.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.