Zanzibar Digitilized Generation
Nimepata taarifa za yanayoendelea sasa kisiwani Pemba na yamenikumbusha mbali. Hapa nitasimulia kidogo. Kuelekea uchaguzi mkuu wa kwanza visiwani Zanzibar tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi (mwaka 1995), mimi nilikuwa natimiza miaka 18 na bado nilikuwa naishi kijijini kwetu nilikozaliwa na kukulia. Panaitwa Mchangani, wakati huo ilikuwa ni sehemu jimbo la Pandani (siku hizi ni sehemu ya jimbo la Wete kupitia ule mpango wa kupunguza viti vya uwakilishi kisiwani Pemba), mkoa wa Kaskazini Pemba.

Huo ndio uchaguzi wangu wa kwanza na wa pekee kupiga kura. Tangu wakati huo, sijawahi tena kuruhusiwa kupiga kura ndani ya ardhi ya Zanzibar, lakini hadi leo naona fakhari kwamba nilikuwa sehemu kubwa ya wakaazi wa kisiwa cha Pemba ambao waliendeleza mila na utamaduni wa kisiasa wa kisiwa hicho, yaani kumkataa mtawala kwa njia za amani – kwa sanduku la kura. Kufuatia kukataliwa huko – na kwa wingi ambao yumkini hakikuwa kimeukisia – chama tawala, CCM, kikaamua kuwaadhibu wakaazi wa kisiwa hicho (au bora kusema kikaamua kuwaongezea adhabu, maana hilo la kuadhibiwa halikuwa limeanza mwaka huo tu).
 
Kwa kutumia askari polisi na vijana wa maskani zake, ambao sisi tuliwapachika jina la “Melody”, CCM ilirejesha enzi za watu kupigwa mikwaju wakiwa wamekaa kwenye vikao vyao vya kahawa, kuvamiwa usiku wakitoka msikitini, kupakiwa vinyesi maskuli na visima vyao, na kukamatwa ovyo ovyo wakisweka ndani. Nilikuwa nikisikia hadithi za Pemba kushuhudia zama hizo baina ya mwaka 1964 na hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980 ikiwa mikononi mwa akina Ali Sultan Issa, Marehemu Hassan Diria na Abdallah Rashind Mamba, kwa kuwataja wachache. 
 
Kwa hivyo, labda haikuwa ajabu pale mkasa wa Skuli ya Shengejuu ulipotokea. Skuli hiyo ipo kijiji cha Pembeni, ambacho kinatenganishwa na kijiji changu bonde la Msaani. Kwa hakika, sio kutenganishwa hasa, maana watu wa vijiji hivi na viambo vyake ni wale wale. Kwa mfano, ubabani kwangu mimi ni Shengejuu, kando kidogo ya Pembeni, wakati huo wazee wetu walikuwa wanasogeasogea na hivyo wengine wakaondoka Shengejuu kuhamia Weyani, kisha Mvimbe, kisha Mikongweni, kisha Mti Mkuu na Mchangani ambapo nilizaliwa na kulelewa mimi. Pembeni penyewe ni umamani kwa kwa babu yangu mzalia baba na wakati mkasa huu ninaosimulia unatokea, nyumba ya shangazi wa baba yangu, Bibi yangu Bint Tamimu Bin Khamis na za watoto wake, zilikuwa pua na mdomo na Skuli yenyewe ya Shengejuu. Mbali na ami zangu Rashid na Amour bin Ali bin Mana’a, na mama wadogo zangu kupitia mama yangu mlezi, ambao walikuja kuwa waathirika wakubwa wa mkasa mzima.

Ulikuwa ni mwaka 1995 mwishoni au 1996 mwanzoni. Wakaazi wa hapo walikuwa wamechoshwa na upuuzi wa kila siku skuli wanayosoma watoto wao kuchomwa moto na au visima vyao kutiwa vinyesi na “watu wasiojuilikana” kisha wakakamatwa wao na watoto wao, kuwekwa ndani, kuteswa na kulazimika kuchangishana fedha nyingi kuwatoa polisi.

 
Nimesahau ulikuwa ni mwezi gani, lakini nakumbuka hali ya hewa ilikuwa ni jua kali mchana na mbaamwezi kali usiku. Wakaamua kuweka doria yao wenyewe kuwanasa. Na wakafanikiwa. Waliwatia mkononi maafisa wa usalama, gari yao, na hata magaloni ya petroli na ndoo za kinyesi. Wakawatia adabu vizuri. Mmoja wao, tukimuita Omar Mamvi, kwa kuwa alikuwa na nywele nyeupe tupu na aliyekuwa afisa usalama wa taifa mkoa wa Kaskazini Pemba, alikimbia kwa miguu kutoka Pembeni, akavuuka chanjaa la Msaani, akapita kwetu Mchangani, akashukia Tunda, akapandisha Tungamaaa hadi Wete kwa miguu, nadhani bila kupumzika pahala.
 
Hadithi hii ilikuja kugeuzwa kinyume mbele na vyombo vya usalama na vya habari vya serikali, na ikasemwa kuwa wakaazi wa kijiji cha Shengejuu waliivamia gari ya maafisa wa usalama ikiwa kwenye doria ya kawaida, wakawapiga maafisa hao na kuiba silaha. Kwa zaidi ya mwezi mzima, wakaazi wa eneo hilo na vyambo vya jirani wakageuzwa ngoma ya Kimanga na vyombo vyote vijiitavyo vya usalama. Walivamiwa mchana, jioni na usiku. Walipigwa kadiri ambavyo wapigaji waliona inafaa. Polisi walidai wanaitafuta silaha waliyosema iliibiwa.
 
Nawakumbuka baadhi yao, kama ami yangu Hamad Mahadhi, ambao walikuwa watu wazima sana, na ambao vipigo vya wakati huo ndivyo vilivyowalaza vitandani hadi mauti kuwachukuwa. Matokeo yake, nyumba zikahamwa, wanawake na watoto wakawa wanalala maporini. Vijana wa maskani na wizi wakatumia fursa hiyo kuiba kila mkono wao walichoweza kukifikia. Pembeni ikawa mahame. Maisha yao yaliharibiwa kwa kipindi kirefu.
 
Lakini kitu kimoja kilipatikana kwa mkasa huu: ilikuwa ndio mwisho wa kusikia tukio lolote la kuchomwa moto skuli au kutiwa kinyesi kisima baada ya hapo popote pale kisiwani Pemba. Watu wa Pembeni walipata machungu, lakini waliisaidia Pemba nzima, angalau kwenye hili moja na angalau kwa kipindi hicho.
 
Hata hivyo, baadaye masaibu kama haya yalijirejea tena kisiwani Pemba baada ya uchaguzi wa 2000 na hata wa 2005. Safari hii kikihusika kijiji cha Jitenge, Ziwani, na Piki. Bila ya kutaja maafa ya Januari 2001 baada ya maandamano ya kudai Katiba Mpya, marudio ya uchaguzi na tume mpya. Kipindi hicho nilikuwa nimeshahama Pemba na kuhamia kisiwani Unguja, ambako niliyashuhudia sehemu ya mateso kama hayo kwenye maeneo ya Kinuni, Bububu, Kianga na Tomondo kwa nyakati na viwango tafauti.
 
Hivi sasa, miaka 20 baada ya mkasa huo niliousimulia, nami nikiwa niko umbali wa maili maelfu kadhaa kutoka nchi niliyozaliwa na kukulia, kumbukumbu hizi zinanijia mbichi mbele ya macho yangu – kama ndio kwanza haya yanatokea. Nimekumbushwa kwa kuwa kunaonekana kunajengwa mazingira ya kurejelewa ya kama yale – vipigo, kukamatwa watu ovyo ovyo, na bila ya kusahau hali ngumu ya maisha inayowakabili watu. Dhamira na moyo wa wakaazi wa kisiwa cha Pemba dhidi ya CCM hazijageuzwa. 
 
Lakini kuna jambo limebadilika hapo katikati. Uwezo wa watu wa sasa, vijana wanaounganishwa na mawasiliano ya kisasa, wana tafauti sana na tulivyokuwa sisi wakati huo. Nilikuwa na miaka 18 wakati kura ya Oktoba 1995 inapigwa, sikuwa nimewahi hata kuiona simu ya mkononi, sikwambii kuitumia. Lakini hivi sasa hakuna kijana mwenye umri kama huo kijijini kwangu Mchangani ambaye hamiliki simu ya mkononi, na wengi wameunganishwa kwenye mitandao kadhaa ya kijamii.

Hawa ni watu wengine. Hawa si akina miye; na CCM na serikali zake isiwachezee mchezo ambao ikituchezea siye.

2 thoughts on “Ni hatari kuwachezea vijana wa zama hizi”

  1. Naam alhabib, swadakta. Punde Kitwanga katumbuliwa na dunia nzima ishajua. Dunia twazurura nayo mifukoni kama si viganjani! Nakumbuka enzi za ubarobaro wangu nilikuwa na mpenzi wangu wa Kisweden akiitwa Anne Ravelin, kujua habari baina yetu ikituchukua miezi miwili kwa njia ya posta. Lakini leo sekunde chache kwa njia ya watsap, Facebook au twitter.

  2. Ahsante sana kwa Makala yako hii. inatupa muangaza wa kujuwa yaliotokea wakati huo na haya yanayotokea hii leo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.