Haupo uwezekano wakupanda fitna kisha uvune wema au chuki na baadae uvune upendo. Utachokipanda ndicho utachokivuna. Hii husemwa kwamba ukipanda ubaya, utavuna ubaya.

Suala la mshikamano limezungumzwa nakusisitizwa sana ndani ya vitabu vitakatifu. Kusisitizwa nakuzungumzwa kwa suala hili hakukuwa kwa bahati mbaya bali ndio msingi wa ustawi, mapenzi na huruma baina ya viumbe. Ni chimbuko la mafanikio yawezayo ipeleka mbele jamii yoyote iwe ya binadamu au viumbe wengine.

Inapofika mahala kuibuka kundi nakuona suala la mshikamano si jambo la msingi na hivyo lastahili kupuuzwa, hio huwa ishara yakusambaratika kwa kundi hilo. Husambaratika kwakumeguka vipande vipande ingawa huweza chukua muda kusambaratika kwake hadi likawa halipo au halisikiki tena.

Na Ahmad Abu Farsi
Na Ahmad Abu Farsi

Mfano wa karibu na wenye kuendana na maelezo yangu ni Chama Cha Mapinduzi-CCM. Chama hiki kimetenda dhambi ambayo asilani haitokibakisha ndani ya ardhi ya Unguja na Pemba. Ni dhambi ambayo hutafuna chini kwa chini mithili ya moto wa pumba. Ni dhambi ambayo haichagui na badala yake humtafuna yeyote awaye pasi nakujali cheo au hadhi ya mtu. Ni dhambi ambayo ikifikia kiwango fulani, watu hugeuka mazimwi wakalana wao kwa wao.

Hivi nani angetarajia kwamba siku moja Mansour Yussuf Himid au Mzee wetu Hassan Nasor Moyo angefukuzwa uana chama wa CCM kwakosa lakusimamia mshikamano wa Wazanzibari? Nani miongoni mwetu angetarajia kuona masheikh wakiswekwa magerezani ugenini kwa kosa lakutetea mshikamano wa Wazanzibari? Nani miongoni mwetu angetarajia kuona mtu mwenye umri kama wa Jecha Salim Jecha angekubali kuigawa nakuifisidi nchi kwakuitengenezea msingi mbaya wa mgawanyiko mbaya wa kisiasa eti kwa sababu yakuwaridhisha wenye uchu na uroho wa madaraka?

Kitendo cha mzee huyu kufuta uchaguzi wa October 25, kilikuwa sawa nakuisambaratisha Zanzibar nakuirudisha nyuma na sio kuipeleka mbele. Ni kitendo ambacho kitaendelea kumtafuna yeye na kizazi chake kwa miaka kadhaa ijayo. Ni kitendo ambacho kitamfanya ahukumike vibaya kwenye historia ya Zanzibar. Ni kitendo kitachomfanya aendelee kupokea laana na dua mbaya za wanyonge walio dhulumiwa kupitia mikono yake.

Inapofikia mahali linapotamkwa jina la mtu na kisha kuitikiwa kwa neno LAANATU LLAH, hapo hamna salama na ipo siku utaishi kwenye ardhi hii kwa udhalili mkubwa. Mifano ya hili ipo na wala kwa Zanzibar haipo mbali. Wapo walioshabikia dhulma na leo hupita mabarabarani wakivua nguo na ilhali wengine waliojiona majabari nakujivika majina ya ukakamavu dhidi ya wanyonge, leo hutatasa kuta ndipo waweze fika vyumbani mwao! Allah kawafumba macho na sasa jeuri na kibri chote kwisha.

Ni masiku kadhaa sasa tumekuwa tukishuhudia matukio yakutia aibu nakudhalilisha hapa kisiwani Pemba. Nimekuwa na bahati kuyashuhudia matukio haya kwa macho yangu. Nimeshuhudia tukio lakusukumwa nakuangushwa chini mama mtu mzima tena mgonjwa. Tukio hili lilifanywa na askari wakutuliza ghasia huko Kiuyu maziwa ng’ombe. Nimeshuhudia tukio jingine la binti mwenye kichanga cha masaa manne akirushiwa mabomu mawili ya machozi ndani ya chumba alicho jifungua. Nimeshuhudia tukio la vijana kadhaa wakigaragazwa kwenye dimbwi la maji machafu na polisi mithili ya polisi wa enzi za kaburu dhidi ya weusi wa Afrika ya Kusini. Nimeshuhudia magari na maduka yakufungiwa kwakutotoa huduma kwa wana CCM.

Hata hivyo wengi hawakumbuki chanzo cha yote haya. Na sasa wajualo nikulazimisha mshikamano kwa mtutu na mabomu ya machozi. Wamesahau kwamba punde tu walikuwa wakishangilia dhulma ya Jecha kwa hawa wanaowalazimisha kutoa ushirikiano. Hawakumbuki na hawakuwa na muda kumwambia Jecha kwamba utupelekako siko na badala yake wao na wafuasi wao walifurahia matendo ya Jecha yakusaliti maamuzi halali waliofanya Wazanzibari. Walijitia pambani wakiamini jeshi lipo litawalinda dhidi ya hasira za raia waliokataa kutawaliwa na wao.

Dunia imebadilika sambamba na mbinu za mapambano. Kwasasa raia dhaifu hawapambani na serikali zao kwa njia zakuingia barabarani. Bali hutumia njia mbadala ambazo hazitopelekea kuumizwa na watawala maimla na mamluki wao . Kwasasa si rahisi kumminia mnyonge risasi eti kisa kaandamana kupinga udhalimu wa mtawala. Pia sio rahisi kumkamata mnyonge eti kisa kakataa kumuuzia mwana chama wa chama fulani, hapana, mbinu zimebadilika na sasa wana CCM wanauziwa kama kawaida ila watu hawanunui toka kwao, wanasomeshwa namba!

Raia wameamua kutokuwa na mafungamano na CCM kwavile CCM wenyewe hawahitaji mafungamano mazuri na raia. Wenyewe husema” kama CCM wanajua umuhimu wa mshikamano baina yetu, wasingethubutu kudharau juhudi za Dr Karume na Maalim Seif. Lakini kwavile kutengana kwetu wao wanakufurahia, acha tutengane ili wafurahi zaidi”.

Tumefika mahala kwamba kwenye gari yenye watu kumi na tisa ambao ni CUF, akiingia mwana CCM mmoja,watu wote hushuka na wakamwachia pekee garini, jee, nani atachoma mafuta kwa abiria mmoja. Si kwamba huzuwiwa asipande, lahasha, huachiwa gari afaidi!

Mgomo huu hauishii kwenye magari pekee bali hata kwenye vijiwe vya kahawa na maduka. Kwamba muuzaji huambiwa achague hiari yake kuwauzia wana CCM au wana CUF. Jee, ikiwa mtaa mzima una wana CUF mia mbili na CCM wawili, utakubali ukose wateja mia mbili kwa CCM wawili?

Siyaandiki haya kwakuyasikia bali nayashuhudia. Barza moja ya kahawa ambayo hutumiwa sana na Bwana Dadi Faki Dadi ambaye ni mkuu wa mkoa wa zamani wa Kaskazini, imehamishwa baada ya mhe Dadi na wenzake kuitumia sehemu hii kwakwenda kunywa kahawa. Baraza imehamishwa baada ya muuzaji kukosa wateja ambao wengi ni wana CUF. Shemeji yangu ambaye ni mke wa mdogo wangu, amefuatwa nakuambiwa achague kuwauzia wana CCM au wana CUF. Sasa mtihani unakuja kwamba CUF wapo mia kadhaa na CCM hawazidi sita mtaa mzima. Si kwamba raia wanakwambia usiwauzie wana CCM, la hasha bali hukwambia uchague kati ya kuwauzia wao wana CUF wapenda mshikamano au CCM wapenda madaraka hata kwa risasi na mabomu!

Kama CCM hawakuona umuhimu wakusimamia haki na uadilifu, pia haitowezekana kuleta amani na mshikamano kwa njia ya bunduki na mabomu ya machozi!

Tanbihi: Mwandishi wa makala hii, Ahmad Abu Farsi, ni mwandishi wa habari anayeishi kisiwani Pemba. Anapatikana kwa simu kupitia nambari: +255774581264

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.