Dk. Ali Mohamed Shein

Nimeipitia bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kugundua kuwa haitekelezeki na kiini macho cha kiwango cha shahada ya uzamifu (PhD). Kwa haraka haraka nimebaini masuala yafuatayo:

Kwanza, bajeti ya jumla iliyotangazwa ni shilingi bilioni 841.5 kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 445.6 zitatumika kwa matumizi ya kawaida (chai, mishahara n.k.) na shilingi bilioni 395.9 zitatumika kwa kazi za maendeleo.

Pili, vyanzo vya mapato vya bajeti hiyo ni Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) kukusanya shilingi bilioni 188.8, wakati Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) itakusanya shilingi bilioni 237.4. Kwa hiyo, jumla Wazanzibari mtakusanya shilingi bilioni 426.2 ambayo ni chini ya nusu ya bajeti nzima mliyopitishiwa.

Na Julius Mtatiro
Na Julius Mtatiro

Tatu, mambo kadhaa ambayo yangeliongeza “vimakusanyo” huku na kule yamefutwa, nadhani, kwa lengo la kulinda uhalali wa watawala. Ambapo mshahara wa kima cha chini umepandishwa kutoka shilingi 150, 000 hadi 300,000, kodi ya mishahara ya wafanyakazi wa kipato cha chini imepunguzwa kutoka asilimia 13 hadi 9 (kama alivyofanya Rais John Magufuli huku Bara) na ongezeko la kodi “kwa lengo la kupunguza mzigo kwa wananchi” limezuiwa.

Nne, Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Dk.Khalid Salum Mohamed, anasema bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo kupungua kwa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo; na ndiyo maana bajeti hiyo itajikita zaidi katika kuweka kipaumbele cha makusanyo ya kodi ya ndani.

Sasa maoni yangu ni haya yafuatayo:

Kwanza, bajeti ya matumizi ya kawaida ni kubwa zaidi kuliko ile ya maendeleo.

Pili, bajeti haioneshi ni namna gani itaziba pengo la shilingi bilioni takribani 400 ambazo hazitakusanywa na ZRB wala TRA.

Tatu, bajeti haioneshi ni nchi gani wahisani zitaisaidia bajeti ya Zanzibar ya mwaka huu na waziri anakiri wazi kuwa wahisani wamechanja mbuga.

Nne, bajeti inaweka mkazo kwenye makusanyo ya ndani baada ya wafadhili kukataa kuisaidia Zanzibar, bila kukumbuka kuwa makusanyo ya ndani – na hasa biashara za bandari – zimeshayumba na zinatarajiwa kuyumba zaidi mwaka huu. Sijui hao ZRB na TRA watafikiaje malengo ya ukusanyaji ili walau watekeleze hata nusu ya bajeti iliyopitishwa.

Tano, katika utekelezaji wa bajeti zilizopita, TRA na ZRB walikusanya viwango vya chini kuliko vinavyotarajiwa na ndivyo itakuwa pia mwaka huu.

Sita, chini ya utawala wa CCM, Zanzibar imeshindwa kujijengea uchumi wake, Wazanzibari mumeendelea kutegemea misaada ya wahisani, fedha kutoka Tanzania Bara na kadhalika. Mumeachwa kabisa kiuchumi na visiwa mkakati (strategic islands) vilivyotapakaa kote duniani na bajeti hii inaendelea kudhihirisha kuwa bado munahitaji utawala kutoka Tanganyika, nami nadhani watawala wako tayari kuendeleza hila zao juu yenu.

Nimalizie kama nilivyoanza: bajeti hii ni changa la macho la kiwango cha PhD. Jipangeni upya na kujifunga mikanda hasa, maana mutapita kwenye wakati mgumu sana miaka hii michache, siyo kisiasa tu, bali pia na kiuchumi.

Niwatanabahishe jambo moja: Mzee Joseph Sinde Warioba (Waziri Mkuu Mstaafu, Mwana CCM, Mtanganyika), Mzee Salim Ahmed Salim (Kiongozi Mwandamizi wa CCM, Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa ya Afrika, Mzanzibari) na raia wengine waandamizi wa taifa hili (Wazanzibari + Watanganyika = Watanzania) walikuleteeni Katiba Mpya ambayo ingetoa fursa kubwa kwa Zanzibar kujiamulia masuala yake ya kisiasa na kiuchumi.

Walioongoza kumnafiki na kumtukana Jaji Warioba na kina Dk. Salim ni wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba  kutoka Zanzibar, wana-CCM kindakindaki. Mukaikataa Zanzibar itakayowafanya mjiamulie masuala yenu wenyewe.

Sasa endeleeni kusubiri shilingi bilioni 100 za TRA kwa sababu mnasubiri mletewe, nasi tutaendelea kuwakusanyia na kuwaletea mapato yenu huko huko. Tusubirieni.

Kidumu Chama Cha Mapinduzi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.