Tundu Lissu

“Kilele cha matumizi haya ya mabavu ya kijeshi ni Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ambako vibaraka wa Tanganyika katika Zanzibar walikataliwa kabisa na wananchi wa Zanzibar katika Uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani. Ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tu ndilo ambalo limehakikisha kwamba vibaraka hawa waliokataliwa na wananchi wao, wanaendelea kubakia madarakani.”

MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.) KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA 2016/2017

(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2016)

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,

Kabla ya kufanya kazi ambayo ninatakiwa kuifanya kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu na ambayo umeniitia, naomba – kwa ridhaa yako – niseme maneno machache juu ya jambo binafsi linalonihusu mimi na familia yangu. Tarehe 7 Aprili, 2016, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Singida katika Bunge la Kumi, Mheshimiwa Christina Lissu Mughwai, alifariki dunia katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam. Marehemu alikuwa dada yangu na mdogo wangu wa kuzaliwa.

Kufuatia kifo chake, na licha ya kuwa hakuwa Mbunge tena, uongozi wa Bunge lako tukufu ulichukua jukumu la kuhakikisha Marehemu Christina Mughwai anazikwa kwa heshima zote zinazostahili Mbunge. Waheshimiwa Wabunge – kwa namna mbali mbali – walishiriki katika kuhakikisha mpendwa wetu anapata mazishi ya heshima kubwa. Baadhi yenu hata mlifunga safari ya kumsindikiza Marehemu hadi nyumbani kwetu Kijiji cha Mahambe, Wilaya ya Ikungi ambapo mazishi yalifanyika tarehe 13 Aprili, 2016.

Na sio Bunge na Waheshimiwa Wabunge tu. Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano mwenyewe, Dkt. John Pombe Magufuli, ilishiriki moja kwa moja katika mazishi hayo. Licha ya shughuli zake nyingi, Rais mwenyewe alikuja kuupokea mwili wa Marehemu na kutoa heshima zake katika Ukumbi wa kihistoria wa Karimjee. Na baadae kwenye mazishi nyumbani kwetu Mahambe, Rais alimtuma Waziri wake, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, kuja kuiwakilisha Serikali katika mazishi hayo. Tulipata kila aina ya msaada tuliohitaji kutoka kwa Bunge, Serikali na Waheshimiwa Wabunge. Hatukuwa wapweke. Hamkutuacha peke yetu katika majonzi yetu. Mlilia na sisi, na mlitufuta machozi. Mlitufariji sana katika kipindi chote cha kilio chetu. Mliufanya msiba wetu kuwa msiba wenu.

Kwa sababu zote hizi, Mheshimiwa Spika, nimetumwa na waliomzaa na kumlea Marehemu Christina Mughwai; nimeagizwa na ndugu zake na marafiki zake na jirani zake, kutoa shukrani zao za dhati kabisa kwa uongozi wa Bunge lako tukufu, kwa Waheshimiwa Wabunge wote na kwa Rais na Mama John Pombe Magufuli na Serikali yake yote, kwa ajili ya wema na upendo na heshima mliyotupatia wakati wa mazishi ya mpendwa wetu Christina Lissu Mughwai. Mwenyezi Mungu awazidishie pale mlikopungukiwa na awabariki sana.

Baada ya kusema haya, Mheshimiwa Spika, sasa naomba nitimize wajibu wangu wa kibunge kama Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kuhusu hoja iliyoko mezani. Na naomba niweke wazi mapema kwamba nitakayoyasema hapa hayatawafurahisha wengi, ndani na nje ya Ukumbi huu wa Bunge lako tukufu. Hata hivyo, kama alivyosema Frederick Douglass, babu wa harakati za kudai haki za watu weusi wa Marekani ya wakati wa utumwa wa Waafrika zaidi ya miaka mia moja na hamsini iliyopita, “he is a lover of his country who rebukes its sins rather than justify them”, yaani, “ni mpenzi wa nchi yake yule anayekemea madhambi yake badala ya kuyahalalisha.”

UTAWALA BILA SHERIA!

Mheshimiwa Spika,

Tarehe 15 Aprili, 1980, Bunge hili lilitunga Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kiuwaziri, Sheria Na. 10 ya 1980. Sheria hiyo ilipata ridhaa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na kuanza kutumika Mei Mosi ya 1980. Pamoja na mambo mengine, Sheria hiyo ilimpatia mamlaka ya kuainisha idara, shughuli na mambo mengine ambayo kwayo kazi na majukumu yake amebaki nayo yeye mwenyewe au ameyakasimu kwa Mawaziri na tarehe ya kuanza kutekeleza majukumu hayo.

Tangu wakati huo, imekuwa ni sheria, na sehemu ya mila na desturi ya kikatiba ya nchi yetu, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kuainisha – kwa kupitia Tangazo lililochapishwa katika Gazeti la Serikali – Wizara, idara, shughuli na mambo mengine ambayo Rais amejibakizia mwenyewe, na yale ambayo amekasimu majukumu yake kwa Mawaziri. Utafiti wetu unaonyesha mambo yafuatayo katika miaka 36 na ya utekelezaji wa Sheria hii:

  1. Mwaka 1981, Rais Nyerere alitoa Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 1981 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 1981, ambalo lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 16 la tarehe 6 Februari, 1981;
  2. Mwaka 1986, Rais Ali Hassan Mwinyi alitoa Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 1986 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 1986), ambalo lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 29 la 1986;

  3. Mwaka 2000, Rais Benjamin William Mkapa alitoa Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2000 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2000), ambalo lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 468 la 2000;

  4. Mwaka 2006 Rais Jakaya Mrisho Kikwete alitoa Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2006 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2006), ambalo lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 2 la tarehe 13 Januari, 2006. Tangazo hilo lilifuta Matangazo mengine yote ya miaka ya nyuma;

  5. Mwaka 2010 Rais Kikwete alitoa Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2010). Tangazo hilo lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17 Disemba, 2010. Kama ilivyokuwa kwa Tangazo la mwaka 2006, Tangazo la 2010 lilifuta Matangazo mengine yote yaliyotolewa kabla ya tarehe 17 Disemba, 2010.

Mheshimiwa Spika,

Katikati ya Matangazo haya, Marais waliomtangulia wa nchi yetu Rais Magufuli, katika vipindi tofauti tofauti, wamekuwa wakitumia mamlaka yao chini ya kifungu cha 5(1) cha Sheria, kufanya marekebisho katika majukumu ya kiuwaziri ambayo yalikuwa chini ya Rais mwenyewe, au aliyakasimisha kwa Mawaziri. Hivyo, kwa mfano, mwaka 1982, Mwalimu Nyerere alitoa Tangazo la Serikali Na. 133 la 1982 kwa ajili hiyo. Mwaka 1984, Mwalimu Nyerere alifanya marekebisho mengine kupitia Tangazo la Serikali Na. 210 la 1984.

Aidha, mwaka 1987, Rais Mwinyi alifanya marekebisho kupitia Tangazo la Serikali Na. 206 la tarehe 17 Aprili, 1987. Mwaka uliofuata, Rais Mwinyi alifanya marekebisho mengine kupitia Tangazo la Serikali Na. 42 la tarehe 26 Februari, 1988. Vile vile, mwaka 2003, Rais Mkapa alitoa Tangazo la Serikali Na. 142 la tarehe 16 Mei, 2003. Mwaka huo huo, Rais Mkapa alifanya marekebisho mengine kupitia Tangazo la Serikali Na. 413 la tarehe 19 Disemba, 2003. Aidha, mwaka uliofuata Rais Mkapa alifanya marekebisho mara mbili kupitia Tangazo la Serikali Na. 79 la tarehe 12 Machi, 2004, na Tangazo la Serikali Na. 523 la tarehe 3 Disemba, 2004.

Mheshimiwa Spika,

Tumeelezea jambo hili kwa kirefu kiasi kwa sababu lina umuhimu mkubwa kikatiba na kisheria. Rais hatakiwi kugawa wizara, idara za serikali na majukumu ya kiuwaziri kiholela. Haya ni majukumu ya umma na, kwa sababu hiyo, ni lazima yafanywe kwa kufuata taratibu za kisheria zilizopo. Kwa upande wao, Mawaziri wanatakiwa kutekeleza majukumu waliyokasimiwa na Rais kwa mujibu wa Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kiuwaziri. Majukumu hayo lazima kwanza yatamkwe, yafafanuliwe na kuainishwa katika Tangazo lililochapishwa kwa ajili hiyo katika Gazeti la Serikali. Ndio maana, kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria hiyo, ushahidi pekee na wa mwisho juu ya suala kama Waziri ana mamlaka katika jambo fulani, ni Tangazo la Rais lililochapishwa chini ya kifungu hicho.

Mheshimiwa Spika,

Kwa sababu ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inapenda Bunge hili lizifahamu, licha ya mabadiliko makubwa katika, idadi, muundo na majukumu ya Wizara mbali mbali, hadi tunapoandika Maoni haya, Rais Magufuli hajatoa Tangazo lolote juu ya majukumu ya kiuwaziri ambayo yeye mwenyewe amejibakishia na/au yale ambayo ameyakasimu kwa Mawaziri aliowateua. Tofauti na alivyofanya Rais Kikwete na Serikali yake mwaka 2010, hakuna Mbunge hata mmoja ndani ya Ukumbi huu ambaye amepatiwa nakala ya Tangazo lolote lililochapishwa kwa mujibu wa Sheria.

Licha ya madai ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu katika hotuba yake Bungeni ya tarehe 22 Aprili ya mwezi uliopita, Bunge lako tukufu halijapatiwa nakala hata moja inayothibitisha kwamba Mawaziri walioteuliwa na Rais Magufuli, na ambao wamekuwa wakifanya mambo mbali mbali kwa kofia za kiuwaziri, wanatekeleza majukumu waliyokasimishwa kwa mujibu wa Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kiuwaziri.

Ukweli ni kwamba hata Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, amekiri kwamba Serikali inaendeshwa bila kuwa na alichokiita ‘instrument.’ Kwa maneno yake mwenyewe, wakati akifanya majumuisho ya hoja za Wabunge kwa Ofisi yake tarehe 27 Aprili, Waziri Mkuu amesema kwamba “instrument za Wizara zote zimeshakamilika na zimesainiwa (tarehe) 20/04; sasa tunasubiri kutangaza, wakati wowote Mheshimiwa Rais atakapoamua kutangaza zitakuwa zimetoka.” Maana ya kauli hii ni kwamba hakuna instrument yoyote iliyotangazwa kama inavyotakiwa na kifungu cha 5(1) cha Sheria.

Mheshimiwa Spika,

Maana na athari ya kisheria ya kutokuwepo kwa Tangazo la ukasimishaji wa majukumu ya kiuwaziri ni kubwa sana. Wengi wa Mawaziri wa Serikali hii waliteuliwa na Rais Magufuli tarehe 10 Disemba, 2015. ‘Viporo’ vilivyobakia kwenye Baraza la Mawaziri vilikamilishwa tarehe 23 Disemba, 2015. Tangu wakati huo hadi sasa, Mawaziri wamefanya mambo mengi. ‘Wametumbua majipu’ katika Wizara zao na taasisi zilizo chini yake kwa kufukuza, kuachisha, kusimamisha kazi au kuhamisha watendaji na watumishi mbali mbali wa Wizara au taasisi hizo. Wamefanya maamuzi juu ya matumizi ya fedha na rasilmali nyingine za umma.

Yote waliyoyafanya wameyafanya kinyume cha sheria. Hawakuwa na mamlaka ya kufanya waliyoyafanya kwa sababu Mawaziri hawa hawajakasimishwa mamlaka ya utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kiuwaziri. Watendaji na watumishi wote ambao wametumbuliwa majipu na mawaziri hawa wana haki na uwezo wa kwenda mahakamani na kuomba Mahakama zetu zitengue utumbuaji wa majipu waliofanyiwa na Mawaziri wasiokuwa na mamlaka hayo kinyume cha Sheria hii.

Ushauri wangu wa bure kwa watendaji na watumishi hao ni kwamba wakafungue mashauri Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga kutumbuliwa kwao majipu na watu wanaojiita Mawaziri lakini hawana hata job description! Kwenda kwao mahakamani sio kutawasaidia kupata haki zao, bali pia kutakomesha vitendo vya kuendesha nchi kienyeji enyeji na bila kufuata sheria, vinavyoelekea kushamiri chini ya utawala huu wa Rais John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Spika,

Kila mtu anafahamu kwamba Rais John Pombe Magufuli sio mwanasheria. Hata hivyo, pamoja na kutokuwa mwanasheria, Rais Magufuli naye anatakiwa kufuata sheria za nchi. Hayuko juu ya sheria. Kiapo chake kinamtaka ‘kuilinda, kuitetea na kuihifadhi’ Katiba ya nchi yetu na sheria zake. Aidha, Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika, kama inavyotamka ibara ya 9(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, “… kuhakikisha … kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa.”

Kwa sababu Rais Magufuli sio mwanasheria, ameteua Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye – kwa maneno ya ibara ya 59(3) ya Katiba – “ndiye mashauri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo ya sheria na … atawajibika kutoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo yote ya kisheria….” Aidha, kwa sababu hiyo hiyo, Rais Magufuli ameteua Waziri wa Katiba na Sheria ili, kama inavyotakiwa na ibara ya 54(3), awe mshauri wake mkuu katika utekelezaji wa madaraka yake katika masuala ya kikatiba na kisheria.

Kwa bahati nzuri, Rais Magufuli amemteua pia Dkt. Harrison George Mwakyembe – mmoja wa wasomi wa juu kabisa wa sheria katika nchi yetu – kuwa Waziri wake wa Katiba na Sheria. Vile vile, Rais Magufuli amemteua Dkt. Sifuni Ernest Mchome – msomi mwingine wa juu kabisa wa sheria – kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria; na Bwana Amon Anastazi Mpanju, mwanasheria mwingine tena, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo. Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inataka kupatiwa majibu sahihi ni kwa nini wanasheria wabobezi wote hawa wameshindwa kumshauri Rais Magufuli kutoa Tangazo la kukasimisha majukumu ya kiuwaziri kwa Mawaziri mbali mbali aliowateua karibu miezi sita iliyopita. Serikali inaendeshwa kama mali binafsi ya Rais Magufuli, bila kufuata wala kuheshimu sheria, sio tu kwa sababu Rais Magufuli ana viashiria vyote vya utawala wa kiimla, bali pia kwa sababu anaelekea kutokuwa na washauri katika masuala ya katiba na sheria za nchi.

Kwa kuangalia mifano ya Matangazo mbali mbali ambayo yametolewa na watangulizi wa Rais Magufuli tangu Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kiuwaziri ilipotungwa mwaka 1980, hata mwanafunzi wa sheria wa mwaka wa kwanza angeweza kumtengenezea Rais Magufuli draft ya Tangazo la aina hiyo. Iweje watu wenye shahada za uzamivu na uzamili katika sheria washindwe kufanya hivyo kwa karibu nusu mwaka tangu wateuliwe? Kama ni majipu ya kutumbuliwa na Rais Magufuli, basi wasomi hawa wa sheria ni majipu na wanastahili kutumbuliwa. Itatushangaza sana endapo Rais Magufuli atayafumbia macho majipu haya.

UCHAGUZI WA ZANZIBAR NA UKOLONI WA TANGANYIKA

Mheshimiwa Spika,

Sasa naomba nizungumzie masuala ya kikatiba yanayohusu Muungano wetu. Kwa wasiofahamu Katiba yetu na wanaoweza kuhoji kwa nini tunazungumzia masuala ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar katika hoja iliyoko mezani, Sura ya Nne yote ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano inahusu ‘Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (na Rais wa Zanzibar), Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.’ Aidha, ibara ya 104 ya Katiba yetu imewekwa mahsusi kwa ajili ya ‘Uchaguzi wa Kiongozi wa Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.’ Kwa sababu hizi, ni halali kabisa kuzungumzia yaliyotokea Zanzibar katika hoja iliyoko mezani.

Mheshimiwa Spika,

Katika Maoni yake juu ya Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu – baada ya uchambuzi wa kina wa masuala ya fedha za Muungano – ilisema yafuatayo kuhusu mahusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar tangu Muungano wetu uzaliwe tarehe 26 Aprili, 1964:

“Kwa vyovyote vile, takwimu hizi zinaonyesha kwamba, kwa sababu ya Muungano huu, uhusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni uhusiano wa kinyonyaji. Kwa sababu hiyo, huu ni uhusiano wa kikoloni. Ni uhusiano kati ya ‘himaya’ ya Tanganyika na ‘koloni’ lake la Zanzibar. Himaya za kikoloni huwa zinadhibiti masuala yote ya ulinzi na usalama, mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, uraia, kodi, fedha, sarafu na benki kuu ya makoloni yao. Na himaya za kikoloni huwa zinatumia nguvu na udhibiti wao wa masuala haya kuyanyonya makoloni yao kiuchumi, kuyadidimiza kijamii na kuyatawala kisiasa. Hivi ndivyo ambavyo imekuwa kwa mahuasiano kati ya Tanganyika na Zanzibar tangu kuzaliwa kwa Muungano huu tarehe 26 Aprili, 1964.”

Mheshimiwa Spika,

Tangu mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964, hadi leo hii, Tanganyika imeidhibiti Zanzibar kijeshi na kisiasa. Ukweli ni kwamba – kama ambavyo Harith Ghassany ameonyesha katika kitabu chake Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia – Serikali ya Tanganyika ilishiriki kwa kiasi kikubwa katika maandalizi ya Mapinduzi, ikiwemo kutoa silaha na mafunzo ya kijeshi katika mashamba ya mkonge ya Sakura Estates, Pangani, Tanga, kwa walioipindua Serikali ya Waziri Mkuu Mohamed Shamte na Sultan Jamshid bin Abdullah.

Aidha, siku tatu tu baada ya Mapinduzi hayo, Serikali ya Tanganyika – kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje na Ulinzi Oscar Salatiel Kambona – ilipeleka vikosi vya Tanganyika Rifles, Jeshi la Tanganyika, ili kuidhibiti Zanzibar kijeshi. Mambo yote haya yamejulikana kwa miaka mingi na wasomi na wanazuoni wa Muungano huu, na yamechapishwa katika vitabu na machapisho mengine rasmi ya kitaaluma ndani na nje ya Tanzania.

Kwa kutumia udhibiti wake wa kijeshi, Tanganyika imedhibiti pia siasa za Zanzibar. Watawala wa Tanganyika ndio wanaoamua nani awe mtawala wa Zanzibar na wamefanya hivyo tangu mwaka 1964. Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi asingekuwa Rais wa Zanzibar baada ya kuuawa kwa Sheikh Abeid Amani Karume mwaka 1972 bila ‘ushawishi’ wa Mwalimu Nyerere na Serikali ya Tanganyika. Na kama ambavyo wanazuoni wa Muungano huu, kama vile Profesa Issa G. Shivji wameonyesha, Jumbe asingeng’olewa madarakani mwaka 1984 bila shinikizo la Mwalimu Nyerere na watu wake hapa Dodoma. Aidha, Rais Mwinyi na Marais wengine wote wa Zanzibar waliomfuatia, ‘wametengenezewa’ Dodoma na sio Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,

Tarehe 20 Aprili, 1968, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo wakati akihojiwa na gazeti la The Observer la London, Uingereza: “If the mass of the people of Zanzibar should, without external manipulation, and for some reason of their own, decide that the Union was prejudicial to their existence, I could not bomb them into submission…. The Union would have ceased to exist when the consent of its constituent members was withdrawn.” Yaani, “endapo umma wa wananchi wa Zanzibar wataamua, bila kurubuniwa kutoka nje na kwa sababu zao wenyewe, kwamba Muungano unaathiri kuendelea kuwepo kwao, sitaweza kuwalazimisha kwa kuwapiga mabomu…. Muungano hautaendelea kuwepo pale ridhaa ya washirika wake itakapoondolewa.”

Alichokisema Baba wa Taifa kwamba hatakifanya, Serikali ya Tanganyika imekifanya kwa zaidi ya miaka ishirini sasa. Kabla ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa mwaka 1992, udhibiti wa Tanganyika kwa siasa za Zanzibar ulifanyika kwa kutumia dhana ya ‘chama kushika hatamu.’ Katika zama za vyama vingi, wananchi wa Zanzibar wamekuwa wapinzani wakubwa wa ukoloni wa Tanganyika kwa nchi yao. Kwa sababu hiyo, tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Serikali ya Tanganyika imetumia mabavu ya kijeshi ya wazi wazi ili kuwaweka madarakani vibaraka wake na kuendelea kuitawala Zanzibar.

Kilele cha matumizi haya ya mabavu ya kijeshi ni Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ambako vibaraka wa Tanganyika katika Zanzibar walikataliwa kabisa na wananchi wa Zanzibar katika Uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani. Ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tu ndilo ambalo limehakikisha kwamba vibaraka hawa waliokataliwa na wananchi wao, wanaendelea kubakia madarakani.

Kwa maoni yetu, Mheshimiwa Spika, katika mazingira haya, tatizo la msingi la Zanzibar sio Jecha Salim Jecha wala ZEC wala Ali Mohamed Shein. Hawa ni vibaraka tu wasiokuwa na nguvu wala uhalali wowote. Bila nguvu ya Tanganyika vibaraka hawa hawawezi kudumu madarakani kwa muda mrefu. Tatizo la msingi ni ukoloni wa Tanganyika kwa Zanzibar ambao umevikwa joho la Muungano. Bila kulivua joho hili na kushona lingine badala yake, Zanzibar haitakuwa huru na itaendelea kutawaliwa na Tanganyika kisiasa, kiuchumi na kijeshi.

KUNYAMAZISHA UPINZANI NI KUKARIBISHA UDIKTETA!

Mheshimiwa Spika,

Mwanaharakati mmoja wa haki za binadamu wa karne ya 19 aliwahi kuandika kwamba: “Once a government is committed to the principle of silencing the opposition, it has only one way to go, and that is down the path of increasingly repressive measures, until it becomes a source of terror to all its citizens and creates a country where everyone lives in fear”, yaani “pale serikali inapoamua kunyamazisha upinzani, inakuwa na njia moja tu ya kupita, nayo ni njia ya kuongezeka kwa vitendo vya kikandamizaji, mpaka serikali hiyo inakuwa chanzo cha hofu kwa wananchi wake wote na inatengeneza nchi ambapo kila mmoja anaishi kwa hofu.”

Maneno haya yametimia katika nchi yetu. Kwa sababu ya kubaka demokrasia kwa kutumia nguvu za kijeshi Zanzibar ili kukipokonya Chama cha Wananchi (CUF) ushindi wake halali, Serikali hii ya hapa kazi tu imeingia katika njia ya kuongezeka kwa vitendo vya kikandamizaji kila mahali katika nchi yetu. Katika Jiji la Tanga ambako CCM ilikataliwa na wananchi, Serikali hii ilitumia ghilba na mabavu ya kila aina kuhakikisha CCM inanyakua Umeya wa Jiji hilo. Leo viongozi wa vyama vya UKAWA na madiwani waliochaguliwa na wananchi wanakabiliwa na mashtaka ya kutengeneza kwa sababu tu ya kukataa kwao kutawaliwa na watu ambao hawakupata ridhaa ya wananchi.

Hivyo ndivyo ilivyotokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, ambako ilibidi Mbunge wa Jimbo la Kilombero na mjumbe halali wa Halmashauri hiyo atolewe kwa nguvu na mapolisi ili kuiwezesha CCM, iliyokataliwa na wananchi kwenye kura, kushinda nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya. Sasa Mbunge huyo naye anakabiliwa na mashtaka ya jinai mahakamani kwa kosa la kutetea demokrasia na utawala wa sheria na kukataa utawala wa mabavu na udikteta.

Katika Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri zake, licha ya nguvu kubwa na hila nyingi zilizotumiwa na Serikali hii, wananchi wa Dar es Salaam na viongozi wao wa UKAWA walifanikiwa kutetea maamuzi ya wapiga kura na kuzuia jaribio la kubaka demokrasia kwa kuweka Mameya wa chama kilichokataliwa na wananchi kwenye uchaguzi. Hata hivyo, badala ya kuchukua hatua za kijinai dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji, Mwanasheria wa Jiji na Katibu Tawala wa Mkoa waliodiriki hata kugushi hati ya amri ya Mahakama kwa lengo la kuzuia uchaguzi halali wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, leo wanaokabiliwa na mashtaka ya jinai ni Wabunge Halima James Mdee, Saed Ahmed Kubenea na Mwita Mwikwabe Waitara waliohakikisha kwamba uhuni huu wa kisiasa haufanikiwi katika Jiji la Dar es Salaam.

Na sio vyama vya siasa na wanasiasa tu ambao wameangukiwa na adha hii ya Serikali kuingia katika njia ya ukandamizaji. Kwa sababu Rais anatumbua majipu hadharani na, hasa, kwenye vyombo vya habari, sasa Mawaziri nao wanatumbua majipu ya Wizara zao hadharani. Haijalishi kwamba Waziri hawa sio mamlaka ya kinidhamu ya utumishi wa umma na, kama tulivyoonyesha, wala hawajakasimishwa majukumu yoyote kisheria, sasa Mawaziri wanafukuza au kusimamisha au kuhamisha watumishi wa umma walio chini yao.

Wakuu wa Mikoa nao sasa wanatumbua majipu mikoani; wanasimamisha Wakurugenzi wa Halmashauri za Serikali za Mitaa na watumishi wengine wa serikali za mitaa bila kujali kwamba hawana mamlaka yoyote kisheria ya kufanya hivyo. Na siku hizi haipiti wiki moja bila kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba Mkuu wa Mkoa au Wilaya fulani ameamuru ameamuru afisa huyu ama yule wa Halmashauri, au diwani huyu au yule, akamatwe kwa sababu hii au ile.

Wote hawa wanafanya hivyo ili wajionyeshe kwamba wanafanya kazi ya Bwana Mkubwa ili asije akawatumbua majipu wao wenyewe. Hofu ya kutumbuliwa majipu ama na Rais mwenyewe ama na Mawaziri ama na Wakuu wake wa Mikoa na Wilaya wake sasa imetanda kila mahali katika utumishi wa umma. Hofu hii inatokana na ukweli kwamba katika kutumbua majipu huku, hakuna tena kufuata utaratibu wa kinidhamu uliowekwa na sheria za nchi yetu. Sasa hatua hizo zinachukuliwa na wasio na mamlaka kisheria katika majukwaa ya kisiasa au kwenye mikutano ya waandishi habari. Na hakuna aliye salama, kuanzia Katibu Mkuu Kiongozi hadi nesi wa hospitalini na mfagizi wa ofisini. Nchi yetu imeingia katika mteremko wenye utelezi mwingi kuelekea kwenye dola la kidikteta.

Mheshimiwa Spika,

Kwa vile Serikali hii ya Rais Magufuli imekumbatia dhana ya kunyamazisha upinzani dhidi yake, uhuru wa vyombo vya habari umewekwa rehani. Kwa kuwa Bunge hili lilijitokeza, katika miaka kumi ya utawala wa Rais Kikwete, kama chombo chenye nguvu ya kuiwajibisha Serikali na watendaji wake, Serikali ya hapa kazi tu imeamua kulinyamazisha na kulifanya kama lilivyokuwa wakati wa miaka ya ‘chama kushika hatamu’, yaani chombo cha kupiga muhuri na kuhalalisha maamuzi ya watawala.

Wala sio siri tena kwamba Kamati za Kudumu za Bunge hili zimepangiwa nje ya Bunge na mamlaka ambazo sio za kikatiba wala kikanuni. Na wala sio siri tena kwamba sasa Bunge hili linaongozwa kwa maagizo ya Ikulu. Ndio maana kila kiongozi wa Bunge sasa anajipendekeza Ikulu kwa vitendo ambavyo mara nyingine vinafedhehesha, kama vile kumpelekea Rais Magufuli fedha zilizoidhinishwa na Bunge hili kwa ajili ya matumizi yake ili zikanunue madawati ya mashule. Kufuta matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ni sehemu tu ya mkakati wa kulinyamazisha Bunge ili lisiendelee kuwa chombo cha kuiwajibisha Serikali.

Mkakati wenyewe ni kunyamazisha upinzani dhidi ya utawala huu. Mkakati huu umelenga vile vile kunyamazisha vyombo binafsi vya habari ambavyo wakati mwingine vimekuwa ni sauti ya upinzani kwa watawala wa nchi hii. Ndio maana hata nusu mwaka haikupita na Serikali hii ikaanza kufuta – sio kufungia! – magazeti binafsi yanayotoa habari zisizowapendeza watawala, na kutishia hatua hiyo hiyo kwa magazeti mengine.

Mheshimiwa Spika,

Hata Mahakama ya Tanzania haijapona wimbi hili la ‘kuongezeka kwa vitendo vya kikandamizaji.’ Ibara ya 107A(1) ya Katiba ya nchi yetu inatamka wazi kwamba “mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama.” Aidha, ibara ya 107B ya Katiba hiyo imeweka wazi kwamba “katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi.”

Licha ya msimamo huu wa kikatiba, Serikali hii ya hapa kazi tu imeanza kuingilia uhuru wa mahakama kwa njia za ajabu, kama sio za kutisha. Kwa mfano, wakati wa sherehe za ufunguzi wa mwaka wa kimahakama mwanzoni mwa mwezi Februari ya mwaka huu, Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Bwana Charles Rwechungura alitoa mfano wa Mkuu wa Wilaya ya Babati, Crispin TP Meela (mwenyewe mwanasheria na mwanachama wa TLS!) aliyeamuru hakimu mmoja wa Mahakama ya Mwanzo akamatwe na kuwekwa mahabusu baada ya hakimu huyo kutoa hukumu ambayo haikumfurahisha Mkuu wa Wilaya.

Kitendo kama hicho kiliwahi kutokea katika miaka ya 1970 wakati Mkuu wa Mkoa wa Mara alipoamuru watuhumiwa waliopewa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Musoma wakamatwe na kurudishwa rumande. Hakimu Mkazi aliyewapa watuhumiwa hao dhamana alichukua hatua ya kumjulisha Jaji Mkuu, wakati huo Marehemu Francis Lucas Nyalali juu ya kitendo hicho cha Mkuu wa Mkoa. Siku hiyo hiyo taarifa hizo zilimfikia Rais Nyerere na wiki mbili baadae Mkuu wa Mkoa alihamishwa kutoka Mkoa wa Mara. Leo hakimu anakamatwa kwa amri ya Mkuu wa Wilaya lakini kwa sababu ya hofu iliyotanda ya kutumbuliwa majipu, Jaji Mkuu na Mahakama nzima imenyamaza kimya.

MAJIPU YA MAHAKAMA!

Mheshimiwa Spika,

Sasa naomba nizungumzie masuala ya Mahakama ya Tanzania ambayo, kwa sababu ya utamaduni uliojengeka kwa miaka mingi wa kulindana, hayazungumzwi. Tarehe 30 Novemba, 2014, Bunge hili lilipitisha kwa kauli moja Maazimio ya Bunge Kuhusu Hoja ya Taarifa Maalum ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Taarifa ya Ukaguzi Maalum Kuhusiana na Miamala Iliyofanyika Katika Akaunti ya ‘Escrow’ ya Tegeta Pamoja na Umiliki wa Kampuni ya IPTL, maarufu kama Maazimio ya Tegeta Escrow Account.

Azimio la 4 la Maazimio ya Tegeta Escrow Escrow lilisema yafuatayo: “KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba katika watu waliotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania; KWA KUWA, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 … imeweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia nidhamu ya Majaji; KWA KUWA, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi wa Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Majaji; NA KWA KUWA, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji unamruhusu Rais kumsimamisha kazi Jaji au Majaji husika wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi yake unaendelea; HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.”

Mheshimiwa Spika,

Baada ya Bunge lako tukufu kupitisha maazimio haya, tarehe 22 Disemba, 2014, Rais Jakaya Kikwete aliwahutubia ‘Wazee wa Dar es Salaam’ ambako alisema yafuatayo kuhusu Azimio la Majaji wa Tegeta Escrow: “Azimio hili nimelipokea, (na) tumelijadili. Hata hivyo, itabidi tufuate utaratibu wa kikatiba na kisheria wa kushughulikia masuala ya namna hiyo. Inatakiwa suala kama hili lianzie kwenye Mhimili wa Mahakama yenyewe na siyo kwa Rais au Bunge. Tume ya (Utumishi wa) Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kumtaka Rais aunde Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua Jaji yeyote pale inapodhihirika kuwa amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo. Nashauri suala hili tumuachie Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie atakavyoona inafaa.”

Mheshimiwa Spika,

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari mwaka jana, baada ya maelezo hayo ya Rais Kikwete, Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman aliunda jopo la Majaji watatu, chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mbarouk Salim Mbarouk wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Aidha, mwishoni mwa mwaka jana, Jaji Mkuu Othman aliwaambia waandishi habari kuwa taarifa ya uchunguzi ya Tume ya Jaji Mbarouk ilikuwa ‘imeiva.’ Cha kushangaza, Mheshimiwa Spika, tangu kuiva kwa taarifa hiyo, Jaji Mkuu Othman, na Serikali hii ya CCM, wamepata kigugumizi kikubwa cha ‘kuipakua’ ili Bunge lako tukufu na Watanzania kwa ujumla ‘waile’! Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inamtaka mtoa hoja alieleze Bunge lako tukufu iliko taarifa ya uchunguzi wa Majaji wa Tegeta Escrow na kwa nini haijaletwa mbele ya Bunge lako tukufu kwa taarifa au kwa mjadala.

SOMO KUTOKA KENYA

Mheshimiwa Spika,

Hatuna budi kujifunza namna ya kushughulikia masuala ya maadili ya Majaji wetu kutoka kwa jirani zetu. Naomba, katika hili, kutoa mfano wa hivi karibuni kutoka nchini Kenya. Mapema mwaka huu, Jaji Phillip Tunoi wa Mahakama ya Juu (Supreme Court) ya Kenya alituhumiwa katika kashfa inayofanana na kashfa ya Majaji wa Tegeta Escrow. Mara baada ya tuhuma dhidi ya Jaji Tunoi kutolewa hadharani, Jaji Mkuu wa Kenya, Dkt. Willy Mutunga, aliunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma hizo. Mnamo tarehe 5 Februari ya mwaka huu, ndani ya kipindi cha wiki mbili, Jaji Mkuu Mutunga alimkabidhi Rais Uhuru Kenyatta taarifa ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Jaji Tunoi. Kwetu Tanzania ni zaidi ya mwaka na nusu tangu Bunge lako tukufu lipitishe azimio la kuunda Tume ya kuwachunguza Majaji wa Tegeta Escrow na Jaji Mkuu wetu anaelekea kuwa amekalia taarifa ya uchunguzi huo, kama kweli ulifanyika.

Tarehe 12 Februari, 2016, Kamati ya Kudumu ya Fedha za Serikali (PAC) ya Bunge la Kenya ilitoa taarifa iliyomtuhumu Jaji Mkuu Mutunga kuwa hachukui hatua zozote dhidi ya vitendo vya rushwa vinavyofanywa na Majaji, Wasajili na Mahakimu wa Kenya. PAC ya Kenya ilimtaka Jaji Mkuu Mutunga kuwajibika ama kuwajibishwa, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwenye nafasi ya Jaji Mkuu wa Kenya kwa kushindwa kudhibiti maadili ya maafisa hao wa Mahakama ya Kenya.

Siku moja baadae, Jaji Mkuu Mutunga aliijibu PAC kwa kutoa takwimu zilizothibitisha jitihada za Mahakama ya Kenya katika kukabiliana na rushwa na ufisadi ndani ya Mahakama hiyo. Kwa maelezo ya Jaji Mkuu Mutunga, “… three judges have been referred to a tribunal … on allegations of corruption, a few others are under consideration in the Judicial Service Commission, a Chief Registrar and five Directors have been dismissed, 9 magistrates and 65 Judicial Staff are facing disciplinary proceedings, some have been dismissed or retired in the public interests….”

Kwetu Tanzania, kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe (MB), Akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara Kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 mwezi uliopita: “Tume (ya Utumishi wa Mahakama) ilishughulikia jumla ya mashauri 14 ya nidhamu kwa watumishi wa mahakama na kutolewa uamuzi. Katika hayo watumishi 10 walifukuzwa kazi baada ya kupatikana na hatia ya utovu wa nidhamu na mengine 4 yanafanyiwa uchunguzi zaidi.”

Na kwa kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, mara ya mwisho Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliwahi kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa utovu wa maadili ilikuwa ni mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1990, wakati Jaji Mwakibete alipoondolewa na Rais Ali Hassan Mwinyi kwa tuhuma za rushwa na baada ya kuundiwa Tume ya Uchunguzi ya Kijaji. Tangu wakati huo, inaelekea Majaji wa Tanzania wamekuwa malaika na watakatifu wasiokula kula rushwa wala kufanya makosa mengine ya utovu wa maadili, maana hakuna hata mmoja ambaye ameundiwa Tume ya Uchunguzi ya Kijaji au kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu.

Hii, Mheshimiwa Spika, haiwezi kuwa kweli. Kwa jinsi ambavyo tuhuma za rushwa na ufisadi katika ngazi zote za Mahakama ya Tanzania zimekuwa kubwa na kwa miaka mingi, ni wazi hatuna malaika wala watakatifu katika Mahakama ya Tanzania. Na kwa ushahidi wa Addendum Juu ya Uteuzi wa Majaji niliyoitoa kufuatia Maoni yangu mbele ya Bunge lako tukufu ya tarehe 13 Julai, 2012, matatizo ya utovu wa maadili katika Mahakama zetu za juu ni makubwa sana.

Kwa sababu hiyo, ni lazima sisi kama Bunge na kama taifa tutumbue majibu makubwa na mengi ya Mahakama ya Tanzania. Bunge lako tukufu lisinyamaze kwa hofu ya kuwaudhi Majaji na Mahakimu wetu. Kukosekana kwa haki katika Mahakama zetu kutapelekea machafuko katika nchi yetu. Kama kiongozi maarufu wa Mapinduzi ya Mexico ya 1910, Emiliano Zapata, alivyowahi kusema: “If there is no justice for the people, let there be no peace for the government”, yaani “kama hakuna haki kwa wananchi, basi kusiwe na amani kwa serikali.”Tundu Antiphas Mughwai Lissu

MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

MEI 5, 2016

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.