Serikali ya Tanganyika inayojidai kwamba ndiyo ya Muungano imesimamia kuvunjwa kwa Katiba ya Zanzibar kwa kuiweka kwa nguvu Serikali haramu huko Zanzibar. Nasema hivi kwa sababu kulikuwa hakuna msingi wowote wa kikatiba wala kisheria wa kufuta uchaguzi wa Zanzibar ambao ulifanyika kwa amani na washindi kutangazwa na kupewa shahada za ushindi. Madhila yote hayo yalirudisha nyuma sana maendeleo ya Zanzibar; na Serikali ya hii inayojinasibu kuwa ni ya Muungano ikaridhia hayo yote ilimradi tu CCM Zanzibar ibaki madarakani bila ridhaa ya wananchi.

 

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO, MHESHIMIWA ALLY SALEH (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU BAJETI YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17 Chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016

1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, awali kabisa napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu Azza wa Jala kutuleta hapa sote katika Bunge hili tukufu na kutupa uhai na afya ili tujadili yale yenye maslahi na nchi aliyotubarikia. Pia namshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kuniteua kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira.
Mheshimiwa Spika, napenda piakuchukua nafasi hii kuwapongeza viongozi wote wakuu wa vyama vinavyounda UKAWA kwa kazi kubwa waliyofanya ya kujenga umoja na mshikamano baina ya vyama hivyo jambo ambalo limetupatia ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita. Ijapokuwa watawala ambao kimsingi walikuwa ni mawakala wa CCM walitupora ushindi kwa hila lakini cha moto walikiona.
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mnyimi wa fadhila kama sitawashukuru wapiga kura wangu ambao walisimama kidete na kunipatia kura tele hadi nikapata ushindi wa kishindo. Aidha, naishukuru sana familia yangu kwa support kubwa waliyonipa na kwa uvumilivu wao kutokana na kutumia muda wangu mwingi kwenye masuala ya siasa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano imeendeleza muundo wa asili wa kuwa na wizara mahsusi inayoshughulikia mambo ya Muungano na mara nyingi Waziri wa Wizara hii amekuwa ni Mzanzibari ili kutimiza ule msemo kwamba; mchawi mpe mtoto alee; na hivi karibuni imekuwa ikipakatishwa kitoto cha Mazingira.
Mheshimiwa Spika, hii ni Wizara inayotarajiwa kuwa muhimu katika kusimamia na kuendeleza Muungano, wenye ridhaa na haki kwa pande zote mbili, lakini wizara hii haina muundo, dhamira na ghera ya kutimiza hilo na ndio maana Muungano umekuwa ukipita katika mtihani mkubwa na kufifia kwa haiba yake kiasi ambacho tumediriki kufuta maadhimisho yake mwaka huu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashiriki katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira ikiwa na moyo mzito kwa sababu tunajua hatuwezi kuepuka kujadili hali ya kisiasa Zanzibar; jambo ambalo Serikali hii ya Tanganyika iliyojivika koti la Muungano haipendi kutokana na ukoloni na unyonyaji inaoufanya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza, Zanzibar imetekwa na Jeshi la Tanganyika. Tangu kipindi cha uchaguzi Mkuu wa kwanza wa Rais na Wawakilishi hadi uchaguzi wa marudio na mpaka sasa majeshi ya JWTZ yapo Zanzibar in full combat, kana kwamba nchi yetu ipo vitani.
Mheshimiwa Spika, kama Jeshi la Tanganyika linatumika kuulazimisha Muungano, ni dhahiri kwamba Muungano huo hauna ridhaa ya wananchi na kwa sababu hiyo hautadumu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa Serikali hii ya awamu ya tano kwamba; kama kweli ina nia ya kuuenzi na kuudumisha Muungano basi, izingatie maoni ya wanananchi waliyoyatoa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu muundo wa Muungano ili kuwa na Muungano unaoridhiwa na wananchi wa pande zote mbili za Muungano.

2.0 UKANDAMIZAJI WA DEMOKRASIA KATIKA CHAGUZI ZANZIBAR
2.1. Uchaguzi wa Zanzibar wa Oktoba, 2015
Mheshimiwa Spika nimetangulia kusema awali juu ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara lakini tukashuhudia uchaguzi uliotoa Rais wa Muungano na Wabunge wa Muungano ukitenganishwa na ule ambao vyama vya siasa vilikuwa vikiwania Urais wa Zanzibar, Uwakilishi na Udiwani.
Mheshimiwa Spika, sababu iliyotolewa ya utenganisho huo ilikuwa ni kwamba; chaguzi hizo mbili zilisimamiwa na Tume mbili mbali mbali na huru na zenye sheria zake na mamlaka zake. Hoja hii ikawa ndio nguzo kuu ya Serikali ya Muungano kukubali uharamia uliofanywa na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar kwa madai kuwa haikuwa na nguvu ya kuingilia hali iliyojitokeza Zanzibar ya kubakwa demokrasia.

Serikali ya Muungano ikakubali kujibereuza katika wajibu wake, sio wa kuingilia kama ilivyotaka ieleweke, ikajipotosha yenyewe. Serikali ya Muungano ikachagua kwa hasara kubwa kuilinda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya CCM kwa kujificha nyuma ya kichaka batili cha kisheria, huku ikijua dhahiri kwamba ilikuwa na wajibu mkubwa zaidi wa kikatiba kusimamia demokrasia.
Mheshimiwa Spika, hii bila ya shaka haikuwa mara ya kwanza mikono ya Serikali ya Muungano kuchafuka kutokana na chaguzi za Zanzibar bali imeanza toka katika Uchaguzi Mkuu wa mwanzo wa vyama vingi mwaka 1995 ambapo CUF ilishinda uchaguzi lakini Serikali ya Muungano ikachagua kuibeba CCM Zanzibar na ikawa ni sehemu ya dhulma kubwa kwa Wazanzibari waliotaka mabadiliko mwanzo tu wa kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Mwalimu Julius Nyerere wakati huo akapendekeza kuundwa serikali ya pamoja lakini akapuuzwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina haja ya kutaja yaliyotokea katika chaguzi za Zanzibar mwaka 2000 na 2005 lakini itoshe tu kusema kuwa matokeo ya chaguzi zote hizo tatu za mwanzo yalizua mizozo, migomo, mikwamo, mauaji, ukiukwaji wa haki za binaadamu, ukimbizi wa Wazanzibari, miafaka na hatimaye serikali ya umoja wa kitaifa.
Mheshimiwa Spika, ili kudhirisha kwamba Serikali haina nia njema na Muungano huu, imefanya hila zote za kuuharibu uchaguzi wa kidemokrasia uliofanyika Zainzibar, ambao dhahiri shahiri chama cha CUF kilishinda, na hatimaye kuvunja msingi wa Serikali ya Umoja wa kitaifa uliowekwa na Katiba ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanganyika inayojidai kwamba ndiyo ya Muungano imesimamia kuvunjwa kwa Katiba ya Zanzibar kwa kuiweka kwa nguvu Serikali haramu huko Zanzibar. Nasema hivi kwa sababu kulikuwa hakuna msingi wowote wa kikatiba wala kisheria wa kufuta uchaguzi wa Zanzibar ambao ulifanyika kwa amani na washindi kutangazwa na kupewa shahada za ushindi. Madhila yote hayo yalirudisha nyuma sana maendeleo ya Zanzibar; na Serikali ya hii inayojinasibu kuwa ni ya Muungano ikaridhia hayo yote ilimradi tu CCM Zanzibar ibaki madarakani bila ridhaa ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, wakati tukinyamazia yetu ya ndani Serikali ya Tanzania imekuwa msemaji hodari wa demokrasia za wengine. Tumekemea hodari kusemea ukandamizaji wa demokrasia katika nchi nyingine lakini kwetu tunaendelea kujivika “kilemba cha ukoka” kwamba; sisi ni kisiwa cha amani wakati kilichopo ni utawala wa kibabe unaothubutu hata kulifunga bunge mdomo kwa kuamuru vyombo vya habari visitoe habari za bunge live.
2.2. Uchaguzi wa Marudio Zanzibar
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni haja ya kuzungumzia Uchaguzi wa Marudio maana haukupasa kuwepo. Katika huo ulioitwa uchaguzi, Serikali ya Muungano ilipeleka majeshi na silaha Zanzibar ili kuhakikisha kuwa malengo yao ya kuendelea kuitawala Zanzibar kimabavu yapo palepale.
Mheshimiwa Spika, haihitaji sayansi ya kurusha roketi kujua kuwa matokeo ya Uchaguzi wa Machi 20 huko Zanzibar yalikuwa ni ya kupika, kuungaunga na kujalizajaliza, kugeuza kura za Maalim Seif na kupewa Dk. Shein na hata kumpa serwa asiyostahiki, ndio maana urais wake hauna uhalali kwa maana ya misingi ya kidemokrasia.

3. MATUMIZI MABAYA YA JESHI LA WANANCHI KATIKA SIASA ZA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika, wakati Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limepata heshima kubwa katika medani za kimataifa kwa nidhamu yake na uhodari wake wa kulinda amani katika nchi nyingine baada ya machafuko kutokana na demokrasia katika nchi hizo kwenda kombo; Serikali ya Jamhuri ya Muungano imekuwa ikilitumia Jeshi hili vibaya kwa kulipeleka Zanzibar kwenda kusaidia kufanya ghilba za uchaguzi na hivyo kujikuta kwamba linashiriki katika uvunjifu wa amani balada ya kulinda amani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, imebainika kwamba nyakati za uchaguzi Zanzibar vikosi vya Jeshi la Wananchi (JWTZ) vimeshuhudiwa vikihusika katika vitendo vya uonevu huko Zanzibar. Aidha, Chama cha Wananchi CUF kilishatoa taarifa kwa Serikali ya Muungano kwamba kipindi cha uchaguzi Zanzibar, Jeshi lilionekana likifanya uandikishaji wa wapiga kura katika makambi yao nje ya utaratibu wa uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga lakini malalamiko hayo yalipuuzwa na hakuna hatua yoyote “hata ya kukemea tu” iliyochukuliwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni kwa nini inalitumia vibaya Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika masuala ya kisiasa?

4. HASARA ILIYOPATIKANA KWA KULAZIMISHA CCM KUTAWALA KWA NGUVU ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Muungano imekubali kuingia gharama na kubeba lawama zote duniani ili kuibeba CCM na kulazimisha itawale Zanzibar kwa nguvu.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Muungano imeingia hasara ya kukatikwa misaada na Marekani kupitia Shirika lake la Milenium Challenge Corporation (MCC) kwa kiwango cha dola za Kimarekani milioni 473 (takribani shilingi Trilioni moja za kitanzania). Watanzania walio wengi hawajui ukweli kuhusu suala la MCC, Serikali ya Muungano iliamua kuchagua kupoteza fedha za MCC ili iweze kuendelea kuitawala Zanzibar kupitia chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu masharti ya misaada hii ni kukuza demokrasia katika nchi husika. Hivyo Serikali ilivyoamua kubaka demokrasia Zanzibar ilijua athari zake ni pamoja na kupoteza misaada ya namna hiyo. Kwa hiyo, Serikali ya Muungano isijidai kwamba ina uwezo wa kujitegemea na kwa hiyo haihitaji misaada huo ni uwongo kwani hata bajeti ya Serikali ni tegemezi kwa asilimia 37. 5. Nasema hivi kwa sababu sura ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 iliyowasilishwa na waziri wa fedha katika kikao cha Wabunge wote, Dar es Salaam inaonesha kwamba takribani shilingi trilioni 11.1 katika bajeti hiyo ni fedha zitakazotokana na misaada na mikopo ya nje na ndani yenye masharti nafuu na kibiashara. Ukichukua kiwango hicho ukagawanya kwa bajeti yote ya shilingi trilioni 29.5 ukazidisha kwa mia utakuta kwamba Bajeti ya Serikali ni tegemezi kwa asilimia hizo nilizotaja.

5. HAKI ZA BINAADAMU
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Muungano ndiyo yenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo haki za binadamu ambayo nchi yetu imeridhia.
Nasema hivi kwa kuwa Serikali ya Muungano ndio iliyotia saini katika mikataba hiyo na pia ndio inayopaswa kuwajibika nje ya nchi na kubanwa kutimiza masharti ya mikataba hiyo na katika kufanya hivyo kuhakikisha inasimamia kikamilifu Tanzania Bara na Zanzibar.
Hata kama jambo hili si la Muungano, lakini sheria iliyoanzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetanuliwa hadi Zanzibar , ijapokuwa suala la haki za binadamu na utawala bora haliangukii katika Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.
Mheshimiwa Spika, inasikitisha kuona Serikali ya Muungano imejitenga kabisa na wajibu wake wa kusimamia suala la haki za binaadamu huko Zanzibar. Wakati Ofisi ya Makamu wa Rais ilikuwa mstari wa mbele kufuatilia suala la Uchaguzi Mkuu wa 2015 na pia ule wa marudio wa Machi 20, 2016, imekuwa kimya wakati ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ukifanywa bila kisisi.
Mheshimiwa Spika, makundi haramu yaliyopewa jina la ‘Mazombie’ yamefanya vitendo vya nuni na firauni. Wameteka na kupiga raia, wameharibu mali na kuchoma bila kisisi na kutumia jahara gari za Serikali na baadhi ya matendo yao yakifanywa hadharani. Jeshi la Polisi chombo cha Muungano limekuwa likisema halijui kama kuna makundi hayo na wala vitendo vyao.
Mheshimiwa Spika, ndani ya Bunge hili Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein Mwinyi wamesema eti hawajui chochote kuhusu matendo hayo ya dhulma ya wale wanaoitwa Mazombie.
Wakati Panya Road ilipotikisa Dar es salaam ilichukua muda mchache tu kufyagiwa wote, hata manyoya yao hayakuonekana Lakini kwa kuwa mazombie wamekuwa wakiinufaisha CCM Zanzibar, Serikali ya Muungano imelinyamazia kimya.
Mheshimiwa Spika, wakati vikundi vyenye sura ya kigaidi almaarufu kama Mazombie wanawafanyia wananchi wa Zanzibar vitendo vya kihalifu na jeshi la polisi kushindwa kuwakamata, jeshi hilo limekuwa likiwakamata raia wema alimradi ni wanachama au wapenzi wa CUF na kuwabambika kesi za uongo. Katika kipindi cha uchaguzi Zanzibar, takriban watu 250 wamekamatwa na polisi wakiwemo viongozi wakuu wa CUF mfano Naibu Katibu Mkuu wa CUF Nassor Mazrui na wajumbe wa Kampeni Mansour Himid na Muhammed Riamy na kubambikiwa kesi kama vile kuchoma moto nyumba, na matukio ya ulipuaji wa mabomu alimradi kuijengea CUF taswira mbaya mbele ya jamii.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora ilifanya wajibu wake juu ya yaliojiri Zanzibar lakini Serikali ya Muungano imekalia ripoti ya taasisi hiyo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa wito kwa Serikali ya Muungano kuiweka wazi ripoti hiyo ili wale wote waliohusika kuhujumu haki za Binadamu katika matuko mbalimbali huko Zanzibar waweze kuchukuliwa hatua za kisheria au kama ambavyo tume hiyo itakuwa imependekeza.
Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inazitaka taasisi za kimataifa za kulinda haki za binadamu ikiwemo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuchukua hatua kwa kuanzisha jalada la uchunguzi dhidi ya uvunjwaji wa haki za Binadamu ambao umefanyika Zanzibar na unaoendelea kufanyika na hatimaye wale wote waliohusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria kwa uhalifu ambao wameutenda dhidi ya binadamu wenzao.

6.0 HOFU YA KUVUNJIKA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa yote yanayotokea Zanzibar ni kutokana na ‘mawazo-pingu’ kuwa kukiwa na mabadiliko ya uongozi Zanzibar basi Muungano wa Tanzania utavunjika. Haya ni mawazo potofu lakini yameshika mizizi ndani ya watu wenye sat-wa kwenye siasa na usalama nchini mwetu.
Mheshimiwa Spika, hofu hii imejengwa na kupaliliwa kila uchao na mbinu za kila aina kuandaliwa kila mwaka wa uchaguzi ili kuibakisha CCM madarakani na kuinyima CUF ushindi wake mwaka nenda mwaka rudi. CUF sio tu wamekuwa wakidima, lakini pia wakinyimwa haki yao kwa sababu ya hofu ya kupandikizwa.
Lakini kwa hakika ukweli uko kinyume chake kabisa. Ni CUF na kiongozi wake Maalim Seif ndio wanaolinda Muungano huu hadi kufika ulipofika. Ni umakini wa Maalim Seif na utulivu wa CUF ndipo Muungano upo hapa ulipo la sivyo nchi ingekuwa imeingia katika vurugu kitambo. Chama kimenyang’anywa ushindi mara tano, na bado kinatafuta suluhu na maridhiano, jamani wanyonge wanyongeni lakini haki zao wapeni.
Na kama kungia katika hatari ya kuvunjika Muungano basi moja ya sababu itakuwa kuendelea kuinyima CUF haki yake, maana itafika siku subira itakuwa na mwisho.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hofu hiyo hiyo isiyo na msingi Serikali ya Muungano imeshiriki katika kuiondosha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) huko Zanzibar mafanikio ambayo yaliiondoshea Zanzibar mivutano ya siasa na kuielekeza katika siasa za kistaarabu na maridhiano. Ni vema Watanzania wakajua kuwa Serikali ya Muungano imewanyima Wazanzibari kuendesha nchi yao kwa maridhiano.

7.0 KERO ZA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika kwa sababu ya kukosa dhamira ya kweli ya kisiasa, na muundo usiokidhi haja, Muungano umekuwa na matatizo mengi na mengine yakidumu kadri ya umri wa Muungano wenyewe. Muungano huu umekosa taratibu za kikatiba na kisheria za kutatua migongano, mivutano au uchukuaji wa madaraka (Usurp of Power) unaofanywa na Serikali ya Muungano dhidi ya Zanzibar na kadhalika Zanzibar inapojitutumua kudai haki na stahiki zake katika Muungano ambazo hazitimizwi.
Tuliitupa au tuliipiga teke fursa adhimu ya kutengeneza mfumo mzuri wa Muungano kupitia Mapendekezo ya Tume ya Warioba, lakini CCM wakaipindisha nia hiyo kupitia Bunge la Katiba. Katiba Pendekezwa itatubakisha pale pale kuwa Muungano usio na majibu kwa masuala mengi hata jepesi tu la muundo wa Baraza la Mawaziri wanaokuwa Wizara zao hazina mamlaka na Zanzibar, kutaja mojawapo.
Mheshimiwa Spika, Wengi tunaamini hizo zinazoitwa KERO za Muungano zinatumika kama mtaji wa kisiasa na kila zinapobakia au kuzuka nyingine na zisipatiwe suluhu ndipo mtaji huo unapokuwa mkubwa zaidi. Mtaji huu unatumika kuwazuga watu, yaani Watanzania kuwa kero ni sehemu ya Muungano na kuwa zote zimetatuliwa isipokuwa chache tu, yaani kuwaaminisha Watanzania kuwa Muungano ni wa usawa na wa haki ilhali hakuna nia kabisa ya kumaliza kero za Muungano.
Mheshimiwa Spika, aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Bunge la kumi, Mheshimiwa Tundu Lissu alizungumzia kwa kina juu ya suala la Mgawano wa Mapato ya Muungano na jinsi Zanzibar inavyopunjika na jinsi mfumo huo ulivyogeuza Zanzibar kuwa koloni. Hilo ni katika suala la fedha ambazo zinatokana na wafadhili yaani mgao wa asilimia 4.5.
Mheshimiwa Spika, pamoja na takwimu kuonyesha kuwa kiasi fulani cha fedha hupelekwa Zanzibar lakini bado kiwango hakijafikia asilimia ambayo imekubalika na pande hizo mbili ambapo kiwango hicho hakijawahi kuvuka asilimia 2.8. Tatizo hili limekuwa la nenda rudi miaka mingi bila suluhu ya kweli na ya kudumu.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Lissu fedha hizo hujumuisha pia makandokando mengine kadhaa ila hutajwa na kutiwa katika kapu moja ambalo huonekana limenona. Alisema kwa mwaka juzi Zanzibar iliyopaswa kupokea shs billion 71.23 ilipewa asilimia kumi tu ya fedha hizo. Inasikitisha kwamba; Ripoti ya Utekelezaji ya Ofisi ya Makamu wa Rais iliyopelekwa katika Kamati ya Katiba na Sheria haikugusia chochote juu ya eneo hili muhimu la masuala ya fedha za Muungano na mgawanyo wake.
Mheshimiwa Spika, Kitu kingine kinachohusu fedha ambacho kwa kukosekana nia ya kisiasa hakijapatiwa ufumbuzi pamoja na kuundwa kwa Tume ya Pamoja ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano ya 1984 ni suala la sehemu ya Zanzibar katika mtaji uliounda Benki Kuu ya Tanzania ikiwa ni fedha za Zanzibar kutokana na iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Leo miaka 50 tangu kuundwa kwa Benki Kuu hakuna suluhu ya suala hilo. Suala hilo maarufu kama Hisa za Zanzibar, lilitolewa agizo na Bunge kwa Serikali kuleta Bungeni taarifa yake, lakini limepuuzwa na Zanzibar haijapata fedha zake halali. Kisingizio ni kutopata taarifa jambo ambalo linatia khofu kuwa taarifa hizo hazitapatikana tena.
Mheshimiwa Spika, kimsingi kuna utata mkubwa juu ya mgawanyo na matumizi ya fedha za Muungano. Ripoti ya Tume ya Pamoja ya Fedha imesema wazi kuwa kiasi kikubwa cha fedha za Muungano hutumika kwa mambo yasio ya Muungano, lakini Serikali ya Muungano imekuwa ikikalia mapendekezo ya kutenganisha matumizi ya fedha za Muungano, ikijua inaidhulumu Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, kero za Muungano zinazidi kuongezeka kutokana na uzembe wa viongozi walipewa dhamana ya kuusimamia muungano. Maamuzi kuhusu masuala muhimu ya muunagano kama vile ajira za Wazanzibari katika Muungano au ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za kimataifa, au utozaji kodi mara mbili kwa wafanyabiashara wa Zanzibar yanachukua muda mrefu mno kiasi cha kuongeza kero juu ya zile zilizokuwepo toka mwanzo.
Ndio maana, kutokana na kero hizi zisizo na utatuzi Wazanzibari, katika maoni ya Tume ya Warioba wakataka tuwe na Serikali ya Mkataba jambo ambalo liliungwa mkono na Tume hiyo kwa kuja na pendekezo la muundo wa shirikisho katika Jamhuri ya Tanzania.
8. HITIMISHO
Suala zima la kujadili Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali kwa 2016/2017 limekuja katika wakati mbaya kabisa na inaiwia vigumu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuchangia kwa kikamilifu kwa faida ya taifa.
Kitendo cha Serikali kukaidi kukamilisha matakwa ya kisheria ya kutengeneza Instruments na Mawaziri kufanya kazi bila instrument hakikubaliki kwa sababu ndizo ambazo zingeonyesha mipaka na mamlaka ya kila Waziri katika Wizara aliyokabidhiwa kuifanyia kazi, inaonyesha ni jinsi gani Serikali isivyosikivu kutimiza matakwa ya kisheria.
Pili, vitendo vya Serikali kuhaulisha fedha zilizopitishwa na Bunge kwenye fungu moja kwenda fungu jengine la matumizi, bila ya taratibu kufuatwa ni tatizo jingine la utumiaji vibaya wa madaraka.
Tatu, ni kitendo cha kulikosesha Bunge afya kuzuia lisionyeshwe kwa umma kwa kutumia visingizio mbali mbali na kuhusisha Uongozi wa Bunge kufanya maamuzi ambayo hayazingatia kupitia Kamati zake ziliozoundwa mahsusi kufanya maamuzi makubwa ya Kibunge.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ina utaka umma wa Tanzania uelewe kwamba hayo ndio yanayofanywa na Serikali inayoogozwa na CCM na uamuzi wetu ni kupinga matendo hayo kwa niaba ya umma wa Tanzania ambao sauti yao iko kwetu.

………………………………..
Ally Saleh (Mb),
WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO
2 Mei 2016

One thought on ““Ikiwa gharama ya Muungano ni kuiua demokrasia Z’bar, basi hautapona””

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.