Watanzania wanaadhimisha miaka 52 ya Muungano wao wa Tanganyika na Zanzibar. Hongera. Siku 104 nyuma kutoka sasa Watanzania pia waliadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba nimeshuhudia kwa macho yangu matukio hayo mawili makubwa ya kihistoria na maendeleo yake hadi leo. Kwangu mimi matukeo hayo mawili yamefungamana. Bila ya kutokea Mapinduzi ya Zanzibar (12.01.1964) sifikiri kwamba tungekuwa na Muungano huu wa Tanzania tunaouadhimisha. Japokuwa Hayati Mwalimu Nyerere (Muasisi wa Muungano pamoja na Hayati Mzee Karume) aliwahi kunukuliwa akisema kwamba hata kama Chama cha Afro-Shirazi, ASP, cha Zanzibar kingeingia madarakani kwa njia za kikatiba na si kwa njia ya mapinduzi, Muungano bado ungefanyika. Mimi sina hakika.

Kwa sisi wanafunzi wachache wa Kizanzibari (ungeweza kuihesabu idadi yetu kwa vidole vya mikono miwili) tuliokuwa tukisoma wakati huo katika Shule ya Sekondari ya Aga Khan (sasa Tambaza ) mjini Dar es Salaam, habari ya Mapinduzi ya serikali yaliotokea Zanzibar Januari 12, 1964 yalitufikia kwa mshangao mkubwa. Akili zetu za ujana wakati huo zilivurugika kutokana na habari hiyo, japokuwa kila wakati tulitakiwa na wazee wetu tujielekeze zaidi katika masomo na si katika siasa za mivutano zilizotawala nyumbani wakati huo. Ilipopita miaka ndipo wengi wetu tulipotambua kwamba Mapinduzi hayo yalifungamana pia na siasa kubwa zaidi kuliko vimo vyetu vichanga vya utoto. Mwishowe tuligundua kwamba kumbe wadau katika Mapinduzi hayo walikuwa si Wazanzibari peke yao.

Na Othman Miraji
Na Othman Miraji

Na pale Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulipoundwa, Aprili 26, 1964 baadae ndipo kila mmoja wetu alipogundua kwa ghafla kwamba mnamo siku moja tu amegeuka kutoka kuwa raia wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Pia kwamba Zanzibar haitokuwa tena na kiti chake katika Umoja wa Mataifa, lakini kutoka wakati huo itawakilishwa na kiti kimoja cha taifa jipya lenye jina la Tanzania. Tuligundua baadae pia kwamba wadau wa Muungano walikuwa ni wengi, yakiwemo madola mkuu yaliokuwa yakisuguana katika Vita Baridi baina ya kambi ya kibepari ya Magharibi na ya kikoministi ya Mashariki. Madola hayo yalisaka kila njia ili kuwa na ushawishi katika uchoraji wa ramani ya njia itakayopitia Tanzania katika siku za mbele.Yalikuweko maslahi kadhaa yaliopingana ndani ya Muungano huo. Kujiuliza masuali mengi wakati huo kulikuwa hakuna faida. Kwa vyovyote Muungano ulishaundwa, hamna litakaloweza kuubadilisha ukweli huo. Baadhi yetu tulijiuliza mbona mambo yalikwenda fasta fasta, kasi ilikuwa kubwa mno? Tulijijibu wenyewe kwamba kulikuwa hakuna wakati wa kudurusu nini kilichoamuliwa jana, hakuna wakati wa kuulizana na kushauriana. Kwanini? Sijui.

Licha ya kwamba kila mmoja wetu baada ya kumaliza shule alielekea njia yake- baadhi walienda vyuo vikuu na wengine kutafuta ajira- nilishangaa kwamba katika shule za madaraja yote na pia katika vyuo vya juu katika pande zote mbili za Muungano hakujatolewa elimu juu ya Muungano. Si tu wanafunzi katika masomo yao ya historia na elimu ya uraia, lakini pia Watanzania, kwa ujumla, hawakupewa maarifa na kuelemishwa kwa undani juu ya Muungano wao, faida zake na sabababu zilizopelekea uundwe. Nilishangaa pia kuona vipi Muungano huo ulivyofanywa kuwa zaidi mali ya viogozi badala ya kuwa mali halali ya wananchi wote wa pande mbili. Lakini nilijitosheleza kwamba Muungano wa watu wa pande mbili hizo ulikuweko kwa miaka na dahari, na hautavunjika, ila tu huu wa sasa umesadifu kuandikwa karatasini na wanasiasa.

Katika miaka ya sitini tulikuwa tunaishi wakati wa Vuguvugu la Mwamko wa Afrika, tukivutiwa na tunu za Afrika ilioyoungana. Viongozi wetu waliotuongoza kuelekea ukombozi, akina Nkurumah wa Ghana, Jamal Abdel Nasser wa Misri, Julius Nyerere wa Tanganyika na Jomo Kenyatta wa Kenya walituambia kwamba Afrika ili iweze kusikika vilivyo na kuwa na nguvu katika jukwaa la kimataifa lazima nchi za Afrika ziungane. Nkurumah alienda mbali kutaka Afrika ilio na serikali, bunge, jeshi na rais mmoja. Mwalimu Nyerere alimtahadharisha mkuu huyo wa Ghana na kumwambia aste aste, polepole. Kwanza tuanze na Muungano wa nchi zilioko katika mkoa mmoja mmoja. Baadhi ya vijana wa wakati huo walivutiwa na Muungano wa Tanzania, kama kianzio cha ndoto ya kuwa na Muungano wa Afrika nzima. Hawajajali kwamba matayarisho yake hayajawa ya kutosha na kwamba wananchi wa pande hizo mbili hawakushauriwa kabla. Hata baadhi ya mawaziri wa huko Zanzibar walikuwa hawana taarifa hadi siku za mwisho kabla ya kutiwa saini Mkataba wa Muungano. Kwa vijana hao, lakini, lengo ndilo lilikuwa muhimu zaidi kuliko njia za kupita kulifikia lengo lenyewe.

Hadi miaka ya karibuni (baada ya kuanza mfumo wa vyama vingi vya siasa) ilikuwa mwiko kuzungumzia juu ya suala la Muungano na manung’uniko ( yaliyoitwa “Kero”) juu ya Muungano huo yalifichwa chini ya mkeka. Mara nyingi kero hizo zilisikika zaidi kutoka upande wa Zanzibar kuliko wa Tanganyika. Ni kawaida yule anayehisi anapoteza zaidi ndiye anayelalamika zaidi. Huenda kwa mujibu wa tarakimu za kifedha ikaonekana upande mmoja unabeba mzigo mkubwa zaidi kuliko vile inavostahiki au inapunjwa zaidi kuliko inavostahiki. Lakini kwa vile kunakosekana uwazi na kwamba Muungano umekuwa ukiendeshwa kwa kuoneana muhali na kienyeji kuliko kuwa wa kisayansi na wa kitarakimu, ni rahisi kwa kila upande kudai kwamba unaonewa na si kwamba unaonea.

Muungano wa Tanzania haujajengeka kwa nguvu za tarakimu na za kifedha, lakini, kama walivyosema waasisi wake, kutokana na udugu wa kihistoria wa watu wake. Ni Muungano wa Damu ambao si rahisi kuvunjika kwa sababu za kifedha. Muhimu zaidi ikumbukwe kwamba ni Zanzibar iliyowachia mamlaka yake ya juu kabisa ya kiutawala na utambulisho wake wa kimatifa, mambo ambayo kabisa mtu hawezi kuyatathmini kwa vipimo vya fedha na tarakimu.

Japokuwa hapo awali Mkataba wa Muungano ulitaka taasisi mbili za kutunga sheria- Bunge kwa upande wa Tanganyika na Baraza la Mapinduzi kwa upande wa Zanzibar- mwishowe ziidhinishe ibara ziliomo ndani ya Mkataba huo, kuna watu wanaodai kwamba kwa upande wa Zanzibar jambo hilo halijafanyika. Hivyo kuna wanasheria wa masuala ya katiba wanaouwekea alama ya kuuliza uhalali wa Mkataba huo. Lakini hayo, baada ya kupita miaka 52 ya Muungano na kama Wajerumani wanavyosema, hiyo ni theluji ilionyesha jana. Imeshayayuka. Au kwa msemo wa Kiswahili: Yaliopita si ndwele, tugange yajayo. Mkataba wa Muungano ulitaja mambo 11 tu yawe masuala ya Muungano, lakini sasa yameengezwa na kufikia 23. Hiyo ni kusema mamlaka ya Zanzibar ndani ya Muungano yamezidi kufifia.

Tume ya Marehemu Jaji Francis Nyalali iliyochunguza mwaka 1991 juu ya utayarifu wa Watanzania kama wanautaka mfufo wa vyama vingi vya siasa ilitaka utaratibu wa sasa wa kuwa na serikali mbili- ya Muungano na ya Zanzibar- ubadilishwe na uwe wa Shirikisho. Tume hiyo ilikubali kwamba kuna matataizo ndani ya Muungano na ikasema ingekuwa busara kero kuhusu Muungano huo zisikilizwe na zitafutiwa ufumbuzi. Lakini walitokea watu waliosema kwamba mfumo wa Shirikisho utafungua njia kwa Muungano wenyewe kuvunjika. Kuna watu walioamini na bado wanaamini kwamba Mapinduzi ya Zanzibar yasingedumu hadi leo bila ya kuweko Muungano.

Udhaifu ninaouona mimi ni kwamba Watanzania wa pande zote mbili za Muungano hawajaelezewa kinagaubaga sababu za kuunganishwa hapo April 1964. Inasemekana Hayati Mzee Karume wa Zanzibar alilikubali wazo la Muungano kutoka kwa Hayati Mwalimu Nyerere wa Tanganyika kama njia kwa serikali mpya ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na ulinzi dhidi ya jaribio lolote la wapinga mapinduzi wa ndani na nje ya Zanzibar kutaka kuipindua serikali yake.

Ndani ya Baraza la Mapinduzi la Zanzibar kulikuweko pia watu waliokuwa wanafuata siasa za mrengo wa kikoministi na wa shoto ambao Mzee Karume inadaiwa alihisi wangeweza kutishia uongozi wake.

Lakini watafiti wengine wanahoji kwamba kulikuweko mbinyo mkubwa kutoka nchi za Magharibi, hasa kutoka Marekani, ili Mapinduzi ya Zanzibar yadhibitiwe kwa vile yalionekana kuwa ni ya hatari na huenda yangeeneza ushawishi wa Wakominsiti na wa nchi za Kambi ya Mashariki katika eneo zima la Mashariki ya Afrika. Wamarekani hawajataka kucheza bahati nasibu na halafu washindwe na kuiona Zanzibar inageuka kuwa „ Cuba ya Afrika Mashariki“. Wao waliiona Jamhuri ya kimapinduzi ya Watu wa Zanzibar kuwa ati ni kibaraka wa madola ya Mashariki, hivyo kwa wao Wamarekani Muungano wa Tanganyika ( iliokuwa wakati huo inasaidiwa sana na nchi za Magharibi) na Zanzibar ni njia bora ya kuzuwia kusambaa hatari ya ukoministi.

Haijapita miaka, Mapinduzi ya Zanzibar yaligeuka na yalianza „kuwatafuna watoto wake“ yenyewe, licha ya wapinzani wake wa asili. Hofu ilienea Visiwani na kuna watu waliopotea bila ya kujulikana hatima zao hadi leo. Wazanzibari wengi walikimbilia Tanzania Bara kunusuru maisha yao au wakihofia kwamba wangewekwa vizuizini. Baadhi ya wale waliofukuzwa makazini Zanzibar waliweza kujipatia ajira Bara na wengine kwenda ng’ambo. Serikali ya Muungano mjini Dar es Salaam ilijua fika nini kilichokuwa kinatendeka Zanzibar, lakini wachambuzi wanasema wakuu wa Bara hawajataka kujiingiza katika mambo ya ndani ya Visiwani. Walihofia wasije kuwakasirisha wakuu wa huko Zanzibar. Yote huenda ni kuulinda Muungano usipate mtikisiko na labda kuvunjika. Na hasa inavyosemekana kwamba katika miezi ya mwisho kabla ya kuuawa Hayati Mzee Karume uhusiano baina yake na Hayati Mwalimu Nyerere ulikuwa si wa uchangamfu mkubwa kama ulivyokuwa hapo mwanzo.

Malengo makubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo Chama cha Afro Shirazi yalijivunia nayo – kuondosha ubaguzi wa makabila na wa rangi, kuhakikisha kuna huduma za kijamii kwa watu wote, kutokomeza umaskini, kutoa bure huduma muhimu za kijami za elimu, afya pamoja na maji – yalianza kusahauliwa polepole. Badala yake viongozi walijikusanyia mali na kuwa kama masultani wepya, huku uhuru wa raia wa kutoa maoni ukibanwa.

Wahakiki wanasema kwamba Mzee Hayati Karume aliposaini Mkataba wa Muungano alifikiri Tanganyika na Zanzibar zinaingia katika Mfumo wa Shirikisho la nchi mbili zitakazokuwa na mamlaka mengi, tena sawa, kila moja katika mambo yake ya ndani, na mambo machache yawe ya Muungano. Kabla ya nchi zote za Afrika Mashariki kuwa huru, wazo la kuundwa Shirikisho la Afrika Mashariki baada ya uhuru lilikuweko na kupigiwa upatu sana. Inafikiriwa na baadhi ya watu kwamba kiongozi huyo wa Zanzibar wakati huo hajafikiria kwamba Muungano huo utakuwa kama huu wa sasa ambao unaweka mamlaka mengi sana kwa serikali ya Muungano. Utaratibu wa serikali ya Tanganyika kuwa ni ileile ya Muungano ulikusudiwa uwe kwa muda mfupi sana, labda mwaka mmoja, hadi pale katiba mpya ya kudumu ya Muungano itakapotungwa. Lakini hadi leo mfumo huu ungaliko, bado unaendelea, ikiwa ni miaka 52 tangu kuanzishwa Muungano. Hoja iliotolewa kwa miaka mingi kutoka upande wa Zanzibar ni kwamba hakuna msingi wowote wa kusema kwamba Tanganyika imepoteza utambulisho wake ndani ya Muungano huu. Kwa hakika Tanganyika imevaa joho la Muungano na imejipanua kimamlaka. Ni mamlaka ya Zanzibar, kama inavotajwa katika Mkataba wa Muungano, ndio ya kulindwa na kuendelezwa ili kwamba, kama alivosema Hayati Mwalimu Nyerere mara kadhaa, kusiweko dhana kwamba Tanganyika ilio kubwa na yenye rasilimali nyingi zaidi “imeimeza” Zanzibar ilio ndogo kieneo na kwa idadi ya wakaazi.

Ukweli ni kwamba kila miaka ilivyoenda utambulisho wa Zanzibar ndani ya Muungano, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni, unapungua. Hilo ni jambao ambalo Wazanzibari wengi linawasumbua hata kufikia hadi wengi wao sasa wanataka mfumo wa serikali tatu kama Tume ya Katiba Mpya ya Jaji Warioba ilivyopendekeza miaka miwili ilopita. Katika uchunguzi wake, tume hiyo imegundu kwamba zaidi ya asilimia 60 ya Wazanzibar wanataka Muungano wa Mkataba baina ya Tanganyika na Zanzibar.

Wazanzibari wanalikumbuka baraza la mawaziri la mwanzo la serikali ya Muungano hapo mwaka 1964, chini ya Hayati Mwalimu Nyerere kama rais. Lilikuwa na mawaziri 20 ( akiwemo mwanasheria mkuu wa kutoka upande wa Bara asiyekuwa na kura). Kati yao 13 walikuwa wanatokea Bara (Nyerere, Kawawa, Kambona, Munanka, Maswanya, Mgonja, Shaba, Eliofoo, Jamal, Bryceson, Tewa, Sijaona na Lusinde) na 7 walitokea Zanzibar (Karume, Jumbe, Hanga, Idriss Abdulwakili, Babu, Hasnu Makame na Hassan N. Moyo). Linganisha na baraza la Mawaziri la sasa chini ya Rais Magufuli ambalo lina mawaziri 23 (pamoja na mwanasheria mkuu wa serikali kutoka Bara asiyekuwa na kura) . Lina Wazanzibari wanne tu (Makamo wa rais Bi Samia Suluhu, Dk. Shein – kutokana na mamlaka aliyokuwa nayo kama rais wa Zanzibar – Dk. Hussein Mwinyi na Profesa Makame Mbarawa.

Tangu kuweko Muungano hakuna Mzanzibari aliyewahi kushika nafasi za juu katika taasisi za Muungano kama Benki Kuu, jeshi au polisi. Kuna idadi ndogo sana ya Wazanzibari wanaofanya kazi katika balozi za Tanzania nchi za nje na pia sehemu ya Zanzibar katika michango inayopata Tanzania kama misaada, mikopo au ruzuku kutoka nchi na taasisi za nje ni haba mno. Ilipokataliwa Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu Duniani, OIC, kwa kuambiwa kwamba masuala ya mambo ya kigeni na ushirikiano wa kimataifa yako chini ya serikali ya Muungano, Wazanzibari wengi walihuzunishwa. Mfumo wa serikali ya Muungano wa utozaji na ukusanyaji kodi umelaumiwa mara kadhaa na wafanya biashara wa Zanzibar kwamba unawaonea, hautilii maanani kwamba uchumi wa Zanzibar ni wa kivisiwa, tafauti na ule wa Bara.

Hadi mwaka 1992 ulipoingia mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, maoni yeyote yaliyohoji au kuonesha kutoridhika na mfumo wa Muungano uliokuweko yalinyamazishwa. Lakini watu waliendelea kuelezea maoni yao na kutaka kuchangia katika kutunga mustakbali mwema wa Muungano wao. Marais wa Zanzibar waliopita, Mzee Jumbe, Dr. Salmin Amour na pia Dr. Amani Karume hawajawa na wakati rahisi pale walipokuwa wanasimama kidete kabisa kutetea maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano. Mara kadhaa maalalamiko aliyokuwa akiyatoa aliyekuwa makamo rais wa kwanza wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff, juu ya kupunjwa Zanzibar katika faida za Muungano yamekuwa yakibezwa kutokana tu na maslahi ya kichama badala ya kushughulikiwa.

Zanzibar inahitaji iuangalie uhusiano wake namna ulivyo na Tanzania Bara kwani unatoa sura kwamba Tanganyika ndio mlinzi wa serikali ya Zanzibar kwa vyovyote vile, bila ya kujali nini kinatokea ndani kwenyewe Visiwani. Maadam chama tawala cha CCM kinabakia madarakani katika pande zote mbili za Muungano. Maono ya CCM tangu kuundwa kwake kuelekea Zanzibar yamekuwa kuwekea uzito zaidi suala la usalama katika visiwa hivyo kuliko lile la maendeleo.

Zanzibar imeshindwa kutamba na kuingia kwa njia huru katika mikataba ya kiuchumi na kifedha bila ya ridhaa ya serikali ya Muungano. Haiwezi kufurukuta na kuwa na siasa zake huru juu ya mambo ya fedha na sarafu zinaoambatana na mikakati yake ya maendeleo, kwa vile masuala hayo ni ya Muungano. Siasa zozote mbovu za Benki Kuu ya Tanzania zinaumiza moja kwa moja uchumi wa Zanzibar. Kugharimia urari wa malipo huko Bara kunaiumiza pia Zanzibar- ughali wa maisha kupanda na kuweko mriupuko wa bei za bidhaa.

Ukitizama uzoefu wa Miungano katika sehemu nyingine za dunia ni kwamba pale Muungano unapokuwa baina ya nchi kubwa na nchi ndogo kunakuweko kila wakati hofu ya nchi ndogo „kumezwa“ na nchi kubwa. Miungano kama hiyo iliojengeka kwa hofu kutoka upande mmoja haijadumu, imevunjika. Mifano mizuri ni ile iliokuweko baina ya Misri na Syria na kuundwa Muungano wa Jamhuri ya Kiarabu baina ya mwaka 1958-1961. Wasyria walihiyari kujitoa kutoka Muungano huo kwa vile waliona hatamu na nyadhifa nyingi za juu katika serikali ya Muungano zilikamatwa na Wamisri.

Shirikisho la Senegambia ambalo lilikuwa baina ya Senegal na Gambia, nchi mbili huko Afrika Magharibi, lilikufa mwaka wa 1989 baada ya kudumu miaka saba tu. Gambia ilikataa kuwa na mfumo wa serikali ya Muungano ikihofia kumezwa na Senegal ilio kubwa kieneo na kwa idadi ya wakaazi. Pia tusiusahau Muungano wa Kisoviet (Urusi) baina Russia na Jamhuri nyingine za Kisoviet na ambao ulisambaratika mwaka 1999 baada ya kuweko kwa karibu miaka 80. Waeritrea wilikataa kubakia ndani ya Ethiopia na walikamata bunduki kupigana dhidi ya majeshi ya Ethiopia ili kuikomboa nchi yao baada ya kukaliwa kwa zaidi ya miaka 20. Watu wa nchi ndogo ya Timor Mashariki huko Kusini Mashariki ya Asia baada ya Mreno kuondoka nchini mwao mwaka 1975 hawajakubali ukoloni huo nafasi yake ichukuliwe na ukoloni wa nchi kubwa jirani ya Indonesia. Walipigana hadi walipopata uhuru mwaka 2002. Wasahara Magharibi huko Afrika Kusini wanapigana, hawataki kulikubali takwa la Morocco kwamba nchi yao iwe sehemu ya miliki ya Ufalme wa Morocco.

Baadhi ya wakati huzushwa suala kama Tanganyika au Zanzibar zitamudu kuishi kila moja peke yake bila ya Muungano. Suala hilo hasa linaelekezwa zaidi kwa Zanzibar kama inaweza kuishi bila ya Tanganyika. Tanganyika inaweza sana, ukiangalia uchumi wake mkubwa. Lakini haitopenda kuwa na jirani ambaye hatabiriki, hajulikani atakuwa vipi baada ya kuvunjika Muungano. Hiyo ndio maana Rais aliyepita wa Muungano, Jakaya Kikwete, alimwambia wazi hivi karibuni katibu mkuu wa Chama cha Upinzani cha CUF, Maalim Seif Shariff, kwamba CCM inahofia kwamba pindi Maalim Seif Shariff atakuwa rais wa Zanzibar basi atauvunja Muugano. Hilo Maalim Seif Shariff amelikataa moja kwa moja, na kusisitiza kwamba yeye ni muumini wa Muungano, lakini Muungano anaoutaka ni ule wa haki. Anasema Muungano wa sasa unaibana Zanzibar na anakumbusha msemo wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Mzee Karume, kwamba Muungano ni kama koti. Usishange mtu anapotaka kulivua pale linapombana sana na kushindwa kupumua. Maalim Seif Shariff anashikilia kwamba yeye ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa urais wa Zanzibar wa Oktoba mwaka jana na ambao ulivunjwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.

Wazanzibari wengi sana hawana wazo la kuuvunja Muungano. Vivyohivyo walivyo Watanganyika wengi. Wengi wao hawajawahi kuishi katika nchi nyingine isipokuwa hii ya sasa yenye jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hawaijui ile Zanzibar kabla ya 1964. Vivyohivyo kwa Watanganyika. Ni wachache walio hai wanaijuwa Tanganyika. Suali linazushwa kila wakati ikiwa Muungano huu ni mzuri na wenye manufaa mbona nchi nyingine za jirani hazijavutiwa nao? Tukumbuke kwamba Muungano huo ulisadifu kufanyika katika wakati ambao viongozi waliouasisi walihitajiana. Na ingekuwa si wakati huo na matukeo yaliozunguka wakati huo, kama vile kutokea Mapinduzi ya Zanzibar na uhasama wa madola makuu uliokuweko wakati huo wa Vita Baridi, sidhani kwamba ingewezekana kuwa na Muungano wa Tanzania wa aina hii. Suala la Muungano wa damu, japokuwa ni muhimu, lakini ni la pembeni.

Licha ya yote hayo, inafaa pia tuachane na ile ambayo imekuwa dhana potofu hadi miaka ya karibuni kwamba kuhoji mambo fulani yanayofanyika ndani ya Muungano- ambayo hayatimizi lile lengo mama la awali la usawa baina ya pande mbili- ni uhaini, kukosa uzalendo au sawa na kuupinga Muungano wenyewe. Suala la kuhoji mambo ya yanayofanyika kuhusu Muungano, kuudadisi na kuudurusu baada ya kila muda ni jambo linaloupa afya Muungano pamoja na hewa mpya ya kupumua nayo kila wakati. Muungano ni zoezi endelevu na kila inapohitajika kuufanyia marekebisho au mabadiliko ni sahihi kabisa kufanya hivyo. Siasa za mkwamo hazisaidii. Watu wasigope kuja na ubunifu mpya kuhusu Muungano wao. Wakati mwingine woga ni mbaya zaidi kuliko yale magonjwa ya hatari sana kwa mwanadamu. Katika mchezo wa mpira inabidi wakati mwingine ubadilishe mbinu (tactics ) za mchezo ili ushinde. Vilevile kwa Watanzania juu ya Muungano wao.

Muungano mzuri na ulio wa amani ni ule unaowapa watu wote wa pande zote za Muungano haki ya kuchangia na kujiamilia mustakbali wao tangu kutoka ngazi za chini kabisa hadi juu kabisa. Chachu nyingine inayojenga Muungano imara ni kuheshimiwa haki za binadamu kwa raia wote ndani ya Muungano, raia wawe huru kuchagua mfumo wa kisiasa wanaoutaka na viongozi gani wanataka wawaongoze kwa ajili ya maendeleo yao ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Kwa vyovyote, kwamba Muungano wao umefikia miaka 52, licha ya matatizo yote, ni jambo la fahari kwa Watanzania. Wana kila haki ya kujivunia. Wamezipiku nchi nyingi zilizojaribu kufanya hivyo na zikashindwa njiani. Watanganyika na Wazanzibari kwa pamoja wamethibitisha kwamba mara nyingine “kupepesuka si kuanguka”. Happy Birthday Muungano.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.