Binaadamu wanapoungana au kufanya umoja wa aina yo yote huwa wanayo shabaha ya kuunda muungano au/na umoja huo. Vitendo vyao vyote huwa vina shabaha hiyo moja; yaani kusudi la kuunda muungano huo vitakavyopelekea kupatikanwa kwa maslahi ya pamoja baina yao katika misingi ya usawa na uwazi. Vitendo vyao vizuri ni vile vinavyosaidia kuitimiza shabaha yao hiyo – na vibaya ni vile ambavyo vinapinga kutimizwa kwa shabaha hiyo.

Vitendo vyetu vilivyokuwa vikisaidia kutimiza shabaha yetu ya kuungana vilikuwa vizuri, na vile ambavyo vilikuwa vikipingana na utimizaji wa shabaha hiyo vilikuwa vibaya. Vitendo vyetu vilivyotusaidia kuimarisha mamlaka na uwezo wa nchi zetu vilikuwa vizuri, lakini vile vilivyokuwa vinapunguza au vinaashiria kupunguza uwezo, madaraka na mamlaka ya kitaifa na kimataifa miongoni mwa nchi zetu bila ya shaka vinapingana na shabaha yetu na vilikuwa vibaya; maana hatukuungana ili kupoteza utaifa wetu wala mamlaka yetu wala madaraka, bali tuliungana ili kuimarisha zaidi.

Muungano imara na ulio na maslahi sawa kwa wananchi wa pande husika unaoheshimu na kuimarisha madaraka na mamlaka (sovereignity) ya kila upande ni mambo muhimu sana katika kuimarisha mahusiano ya nchi zetu. Maana bila ya Muungano kusaidia kuimarisha nguvu, uwezo na mamlaka ya kila upande kitaifa na kimataifa – nchi zetu zitaendelea kuwa ‘viwanja vya watu wengine kuchezea’.

Msingi wa kila upande na watu wake kujiamulia mambo yao wenyewe, na uhuru wa kila taifa ndani na nje – ni sehemu ya shabaha za kidemokrasia; msingi ambao unatiliwa mkazo katika maandiko yote ya haki za binaadamu (right to self determination).

Khaleed Said Gwiji
Na Khaleed Said Gwiji

Siku zote Muungano wa nchi mbili au zaidi ni suala la kisheria ambalo huwa ni nyenzo ya mashirikiano ambayo yana shabaha ya kuwapatia washirika maslahi ya pamoja kwa misingi ya uhuru, uwazi na usawa. Kwa maneno mengine, Muungano ni mashirikiano ya kimaslahi juu ya misingi ya usawa baina ya pande husika. Pindi Muungano huo utapowapatia wabia maslahi ya pamoja kwa misingi hiyo ya usawa; ushirika huo huendelezwa; kinyume chake, Muungano huo utakapoonekanwa hautoi fursa sawa baina ya washirika na umegubikwa na viini macho na usiri na mmoja kumdhulumu mwengine, inabidi uwachwe ili kutoa muda kwa washirika kutathmini vyanzo vilivosababisha Muungano huo kushindwa kutimiza shabaha hiyo. Muungano mwema sio tu unaheshimu na kutambua mamlaka ya kila upande; bali ni lazima uwe na malengo ya kukuza ustawi mwema na maendeleo ya kielimu na kiuchumi ya jamii za nchi husika na mustakbal wao kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.

Tuna matatizo makubwa katika Muungano wetu na ni vizuri tukubali kwamba tuna matatizo makubwa ya Muungano. Halafu tuyazungumze katika ukubwa wake unaostahiki. Utamaduni wa kuficha matatizo makubwa, na kuyafanya kuwa si matatizo – ndilo tatizo kubwa tulilonalo.

Sisi ni watu na hivyo tuna mawazo tofauti, na kwa ajili hiyo lazima tutakhitilafiana. Na tunapokhitilafiana ni lazima tuseme kuwa tunakhitilafiana na kwanini tunakhitilafiana. Na sisi hatuwezi kuwa tunakhitilafiana na watu halafu tuseme hatukhitilafiani. Katika suala hili la Muungano, tunakhitilafiana kabisa na wale wanaosema tuendelee kuwa na aina ya Muungano wa Kikatiba badala ya kuleta mfumo mpya wa Mashirikiano ya Kimkataba kama; kama ambavyo tunahitilafiana kabisa na wale wanaotaka tujadili Katiba kabla ya kwanza kuujadili Muungano uliozaa Katiba hiyo.

Kihistoria, Muungano wa Tanzania uliundwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika tarehe 26 April 1964 ambapo karibuni utatimiza miaka 50; yaani nusu karne. Muungano huu uliundwa na nchi mbili zilizo na tofauti nyingi zaidi kuliko mfanano. Nchi ambazo zimekuwa na historia tofauti, ukubwa tofauti, idadi ya watu wake ni tofauti, uwiano wa dini wa wananchi wa nchi mbili hizi nao ni tofauti, utamaduni tofauti, aina ya uchumi wao ni tofauti, maumbile yao ni tofauti – ambapo nchi moja ni bara na nyengine ni visiwa.

Tofauti nyengine ni kuwa wakati wa kuundwa kwa Muungano, Tanganyika ilikua imeshapata uhuru wake kwa njia za amani kwa takriban miaka miwili na nusu na ilikua na utawala madhubuti, taasisi imara za uendeshaji na ilikuwa na Katiba kamili ya Jamhuri ya 1962 baada ya kurekebisha Katiba ya mwanzo ya Uhuru ya 1961, na ilikuwa na amani na utulivu wa kutosha pamoja na uzoefu wa kiutawala. Kwa upande mwengine, Zanzibar iliingizwa katika Muungano ikiwa ni siku takriban 100 tu tokea ilipofanya Mapinduzi ya umwagaji damu hapo tarehe 12 Januari 1964 ambayo yaliipindua Serikali iliyokabidhiwa uhuru ambayo ilidumu kwa siku 30 tu. Hivyo Zanzibar bado ilikua katika fukuto la mapinduzi, haikua katika utulivu na wakati huo haikua hata na Katiba baada ya kuifuta kwa Mapinduzi Katiba ya uhuru ya 1963.

Kwa jinsi Rais J.K. Nyerere alivyoulazimisha Muungano huu, wapo wanaodai kuwa muungano huu ulikua na lengo la kuimeza Zanzibar na kuifuta katika ramani ya dunia – dai ambalo linaaminiwa na wengi. Rais J.K. Nyerere aliona hiyo itakua njia sahihi ya kuweza kuidhibiti Zanzibar kutokana na hofu yake iliyojikita katika ukweli uliomo katika dhana inayosema “You pipe in Zanzibar, they dance in the lakes” ; yaani, likipigwa zumari Zanzibar, wanacheza watu wa maziwa – historia ni shahidi mzuri wa dhana hii. Kuingia kwa dini, ukoloni, matukio makubwa kama biashara ya utumwa na vuguvugu la uhuru yanaaminiwa kuanzia Zanzibar na kuelekea Bara. Hata yalipotokea Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 katika mwezi huo huo, moto wa Mapinduzi ulisambaa Tanganyika, Uganda na Kenya ambako kote kulitokea majaribio ya mapinduzi. Hata kwa historia ya karibuni inaaminika mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa yanayoendelea basi asili yake ni Zanzibar (ukianza vuguvugu la siasa za vyama vingi, mapambano ya kutanua Demokrasia, ubinafsishaji wa uchumi, utalii n.k). Ukweli huu ndio uliomfanya Rais J.K Nyerere atamke wazi kuwa haridhishwi kuviona visiwa vya Zanzibar vikiwa karibu naye na kama angekuwa na uwezo angelivikokota na angevitokomeza mbali katikati ya Bahari ya Hindi kama alivyosema: ‘If I could tow that island out into the middle of the Indian Ocean, I would do it … No I am not joking … I fear it will be a big headache for us” (Both quoted in Zanzibar and the Union Question, pg 34)
Na kwa vile hilo halikuwezekana, njia iliobaki ilikuwa ni kuvidhibiti visiwa vya Zanzibar au kuvimeza kabisa. Na ndio maana wapo wanaoamini kuwa agenda ya umezaji huo imefanikiwa lakini Zanzibar iliyomezwa imekataa kutulia ndani ya tumbo la chatu kama inavyoelezwa: “Dr Julius Nyerere, President of Tanganyika, managed half the work of a phython: he swallowed Zanzibar all right. But he did not crush its fighting force first. The live animal (Zanzibar) is a long time digesting, and its kicks are being felt hurtfully, and possibly even fattaly, deep inside Tanganyikas body politic” – (The Economist (London) Of June 13,1964).

Muungano huu umekuwa na utata mkubwa wa kisheria. Mfumo wetu ni ‘common law’ ambapo viongozi wakuu wa nchi wanaweza kuingia mikataba ya kimataifa kati ya nchi zao na nchi nyengine. Lakini sheria hizo hizo za ‘common law’ zinasema: Baada ya viongozi wakuu kuingia mkataba baina ya nchi zao, LAZIMA Mkataba huo urudishwe kwenye Mabunge ya nchi husika ili uridhiwe na kutungiwa sheria (local law) kuu – ‘domesticate’. Na kufanya hivyo sio tu ni kuitekeleza kivitendo ile falsafa, bali hata huo Mkataba wenyewe wa Muungano ukikisoma kifungu chake cha 8 kinasema: “sharti la awali” (condition precedent) ni kwamba, Mkataba wa Mungano urudishwe kwenye Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar ili upitishwe na kutungiwa sheria. Bunge la Tanganyika liliutungia Mkataba ule sheria nambari 22 ya 1964 chini ya Mwanasheria Mkuu wake (Attorney General) ambae alikuwa ni Muingereza Mr. Roland Brown pamoja na kiongozi mwandishi wa Bunge la Tanganyika Mr. P.R.Ninness Fifoot kuiridhia Mkataba ule wa Muungano na wakatoa kwenye gazeti la Serikali ya Tanganyika. Kwa upande wa Zanzibar mpaka leo (inakaribia nusu karne) hii hakuna sheria iliyotungwa kwa ajili ya Mkataba ule wa Muungano wala kuridhiwa na Baraza la Mapinduzi na/au Baraza la Wawakilishi.

Utata wa Muungano huu pia unaonekana katika kuyamega mambo ya Zanzibar kila kukicha. Kuimarisha muungano huu kwa mtazamo wa Serikali ya Tanganyika ni kuyamega mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar na kuyafanya ya Muungano (yalianza 11 sasa yako 42) pengine siku ya kumaliza jambo la mwisho la Zanzibar lisilo la Muungano na kulifanya la Muungano hapo mradi wa “uimarishaji” wa Muungano utakua umefikia kilele chake.

Swali la msingi ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza ni uhalali wa kikatiba wa ongezeko hili la mambo ya Muungano. La kwanza ni kuwa Zanzibar, tokea ilipoungana na Tanganyika inadaiwa ilipoteza uwezo wa kuingia mikataba ya kimataifa (SOVEREIGNITY), na ndio maana ilibanwa kujitoa kwenye OIC kwa vile haina mamlaka hayo ( Pia inashindwa hata kujiunga na FIFA) na ikaambiwa kufanya hivyo ni kuvunja katiba. Sasa kama Zanzibar ilipoteza uwezo huo kama inavyodaiwa, kwa vile katika mfumo wa kimataifa ni kuwa haitambuliki, inapata wapi uwezo, nguvu na uhalali wa ku “surrender” mambo yake yasiyo ya muungano na kuyaingiza katika kapu la muungano? Huku ni kuwa na sura mbili (double standard): Zanzibar inaambiwa kufanya Makubaliano na nchi nyenginezo haina uwezo, lakini Tanganyika kuyamega mambo ya Zanzibar tena pasi na makubaliano na kuyatia katika muungano inao uwezo!! “kizungumkuti”. Ukweli ni kwamba haiwezekani kuwa na sura mbili- ama inawezekana kuingia mikataba ya kimataifa au haiwezekani, na kama haiwezekani (msimamo unaoonekana kuwa na nguvu) basi ndio madai kuwa mambo ya ziada (baada ya yale 11 ya asili) hayana uhalali na hivyo yameingizwa “kinyemela” na hivyo yote ni batili katika mtazamo wa kisheria.

La pili, ni kuwa hata kama Zanzibar ina uwezo wa kuingia mikataba ya kimataifa katika haya yaliyoongezwa, ameingia mkataba na Taifa lipi kwa vile mshirika wake wa asili katika muungano huu (Tanganyika) alishajificha, ingawaje yupo na huyo aliezaliwa ni sehemu ya nafsi yake – Jee mtu anaweza kujiuzia mali yake yeye mwenyewe?

La mwisho la kuangalia katika kiinimacho hiki ni kuwa unaposoma vifungu vya 94 na 68 vya katiba ya Jamhuri ya muungano ya Tanzania ni kuwa bunge la JMTZ limepewa uwezo wa kuchukua kwa upande mmoja tu ( unillaterally ) mambo yote ya Zanzibar yasiyo ya muungano na kuyafanya ya muungano na hivyo kuweza kupelekea kutoweka kwa Zanzibar moja kwa moja katika uso wa dunia.

Jengine, viongozi na hata wasomi wa Tanganyika wamekuwa wakidai kuwa Zanzibar haiwezi kupata fursa na haki sawa baina yake na Tanganyika kwa madai kwamba Zanzibar ina eneo dogo ukilinganisha na lile la Tanganyika; na kwamba Zanzibar ina idadi ndogo ya watu ukilinganisha na ile ya Tanganyika. Wasichokijua ni kuwa si ukubwa wa eneo wala wingi wa idadi ya watu unaozingatiwa kuifanya nchi itambulike na kukubalika kuwa ni nchi. Ukisoma sheria za kimataifa utaona kuwa kuna nchi zaidi ya arobaini ambazo idadi za watu wake hazizidi laki tano – kumbuka kuwa Zanzibar ina watu zaidi ya milioni. Aidha, nchi kama Nauru iliyoko ‘South Pacific Ocean’ idadi ya watu wake haizidi elfu kumi tu, na inatambulika kimataifa kuwa ni nchi. Si hilo tu, Nauru ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Si hilo tu, Nauru ina haki na fursa sawa ndani ya Umoja wa Mataifa kama India yenye watu bilioni moja. Itakuwa Zanzibar yenye watu milioni na zaidi inyimwe haki na Tangnyika yenye watu milioni arobaini?

Baada ya yote hayo, Tanzania imeamua kuandika upya katiba yake. Mchakato huu wa Katiba na suala la muungano umeanza kwa kupitishwa sheria no 8/2011. Tayari mwanzo mbaya (false-start) imeonekana katika mchakato unaoundwa na sheria hiyo. Kasoro kubwa ya sheria hii ni kuwa HAITOI FURSA YA WAZI kwa wananchi (wamiliki na wadhamini wa Katiba) kuujadili muungano – na ukweli ni kuwa muungano ni ‘nguzo’ kuu ya katiba yenyewe. Hasa kwa upande wa Zanzibar, ambako wananchi wa Zanzibar uhusiano wao juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kupitia muungano. Yote yaliyo nje ya mambo ya muungano, upande wa Zanzibar hawana haki nayo kama ambavyo watanzania bara hawana haki na mambo ya Zanzibar (yasiyokuwa ya muungano). Ukisoma vifungu vya 8, 9 na 17 vya sheria hiyo ambavyo vimeainisha hadidu rejea (terms of reference) au mipaka (na kuna umuhimu gani wa kuwekea wananchi mipaka kuhusiana na mjadala wa Katiba yao?) ya kazi za tume ya katiba hamna hadidu rejea yo yote inayaotaja kuangalia suala la muungano. Na baya zaidi vifungu vya 9(1) (C) na 17(1) na 17(2)(d) vimeielekeza tume kutayarisha na kuwasilisha ripoti kwa “kuzingatia hadidu za rejea” – hivyo ni kuwa HATA kama wananchi watazungumza sana juu ya suala la muungano lakini kwa mujibu wa sheria hii tume haitoandika cho chote kuhusu mambo haya ya muungano. Tukizingatia ukweli wa kuwa wananchi wa nchi mbili hizi hawajawahi kupata fursa ya kutoa maoni yao juu ya suala la muungano ilitegemewa muungano uwe ndio hoja kuu ya mjadala wa katiba na kuacha kabisa kuendeleza utamaduni wa muda mrefu wa kulitenga suala la muungano na wananchi wenyewe – kulifanya halifikiki, halijadiliki wala haligusiki. Ni busara tusome alama za nyakati.

Jambo jengine ni kuwa tatizo lililojitokeza mwaka 1977 kuhusu kukosekanwa kwa ‘uwiano’ wa wajumbe katika kuunda Bunge la Katiba la wakati ule, linajikoteza tena mwaka 2012 katika kosa hilo hilo la kukosekanwa ‘uwiano’ wa kuunda Bunge la Katiba la sasa. Yaani hatukujifunza hata baada ya miaka karibu 35 au ndio muendelezo wa ile dhana ya kuwa lengo la Muungano ni nchi moja (Tanganyika) kuitawala nchi nyengine (Zanzibar)? Bunge la Katiba la 1977 lilikuwa na wajumbe 207: ambapo wajumbe 45 tu walitoka Zanzibar na wajumbe 162 walitoka Tanganyika. Na Bunge la Katiba la sasa kwa mujibu wa Sheria nambari 8 ya 2011 ya mchakato wa marekebisho ya Katiba linaeleza kuwa; kutakuwa na wajumbe takriban 600 wa Bunge la Katiba: ambapo wajumbe kutoka Zanzibar watakuwa kama 200, na wajumbe kutoka Tanganyika watakuwa kama 400. SUALA la kujiuliza: Mbona tunapoingia katika ushirikiano wa kimataifa na nchi nyengine, ‘principle ya equality of membership’ inafuatwa na kuheshimiwa? Kwa mfano Bunge la Afrika Mashariki lenye nchi wanachama: Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi: kila nchi wanachama imepeleka wajumbe tisa (9) tu katika Bunge la Katiba la Jumuia hii. Haikusemwa kwamba Tanzania kwa sababu tuko wengi kwa idadi ya watu milioni 43 hivyo inabidi tupeleke wajumbe wengi zaidi kulinganisha na Rwanda yenye watu milioni nane? Nchi zote hizo zilipeleka wajumbe tisa bila ya kujali wingi wa idadi ya watu wake au ukubwa wa eneo kwa sababu si ‘demograpy’ wala ‘geography’ zinazotumika katika kuzingatia vipimo vya mamlaka (sovereignity) ya nchi.

Sasa kwanini Bunge la Katiba la Tanzania liwe na wajumbe wachache kutoka Zanzibar; lakini liwe na wajumbe wengi kutoka Tanganyika? Mbona Tanzania hiyo hiyo inaifuata ‘principle’ ya usawa wa uwiano ikiwa nje ya nchi (kimataifa) lakini kwa makusudi inaipuuza ikiwa ndani ya nchi?

 

Tatizo kubwa jengine ambalo linajirudia kama ilivyotokea mwaka 1977: lile Bunge la Katiba la 1977 na hili la sasa kwa mujibu wa sheria nambari 8: YOTE mawili ni mabunge ya ‘kuteuliwa’ si Mabunge ya ‘kuchaguliwa’. Kwanini Mabunge haya yasichaguliwe na wananchi wenyewe na badala yake Rais ayateue? Je, yataweza ku – reflect wishes za wananchi?

Washiriki wakuu wa mchakato huo wa marekebisho ya Katiba ni WANANCHI ambapo mamlaka ya kuendesha nchi yanatokana na wananchi wenyewe. ‘Universal declaration of human rights’ inasema hivyo. Hiyo Katiba ya Muungano ya 1977 nayo inasema vivyo hivyo. Na Katiba ya Zanzibar ya 1984, Toleo la 2010 nayo inalitambua hilo pia. Ibara ya tisa inaeleza kuwa uwezo, nguvu na mamlaka yote ya kuendesha nchi yatatoka kwa wananchi wenyewe na si kwengineko. Kama hivyo ndivyo, iweje Tume ya Katiba iweke hadidu rejea (terms of references) ambayo maana yake ni MIPAKA? Unawawekeaje mipaka wananchi ambao sio tu ndio ‘wamiliki’ wa Katiba; bali ndio walio na MAMLAKA na HAKI kuhusiana na mustakbal wa taifa lao kama ibara ya 21 (2) ya Katiba ya Zanzibar inavyoeleza? Sheria nambari 8 ya 2011 ya marekebisho ya Katiba haiwezi KUWA JUU YA Katiba ya Zanzibar.

Wanaoutetea Muungano kwa madai kuwa ni mzuri na hauna matatizo na kwamba tuendelee nao kama tulivyo – wanaonekana sio tu ni wahafidhina wasiojua mambo (political naives); bali hawajui hata kusoma alama za nyakati na mahitaji na kwamba wanaonekana ni ‘politicians with NO politics’. ‘Essence’ ya marekebisho ya Katiba ya Muungano maana yake nn? Maana ya marekebisho ni kuwa kuna mapungufu na kasoro. Kitu kikiwa kizuri hakihitaji marekebisho. Ila, Muungano una kasoro na kero nyingi ambazo wao wenyewe wamekiri kushindwa kuzipatia ufumbuzi. Kwa wengine, Muungano umekuwa ndio kero yenyewe kutokana na kuonekanwa una dhamira ya nchi mmoja kuitawala nchi nyengine. Kwa mfano, ibara ya 55 (1) ya Katiba ya Muungano inasomeka: ” Mawaziri wote ambao ni wajumbe wa Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa ibara ya 54, watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu”. Sasa tujiulize, nani Rais na nani Waziri Mkuu? Rais ni Kikwete, Waziri Mkuu ni Pinda – iko wapi Zanzibar hapo? Eti hiyo ndiyo ‘cabinet’ inayoamua sera za mambo ya Muungano huu. Kwanini ibara isiseme kuwa Rais atateua Mawaziri baada ya kushauriana na Makamo wa Rais ambayo ndiyo formula katika Katiba isemayo kwamba – Rais akitoka upande mmoja wa Muungano, Makamu wa Rais anatoka upande mwengine? Halafu wahafidhina hawa watuambie tusiuzungumze Muungano huu uliojaa viini macho!? (To them politics is just a business; not a mission) !

Vil vile, Sheria nambari 8 ya 2011 ya marekebisho ya Katiba imeweka suala la ‘makosa’ na ‘adhabu’. Sheria ime – ‘creates’ makosa ya jinai kupitia kifungu cha 21 cha sheria ile. Makosa yenyewe ni pamoja na kuzuia Tume isifanye kazi ambapo kufanya hivyo ni kosa la jinai na utashtakiwa. Kuchochea mtu yo yote kuzuia Tume isifanye kazi zake au sekretarieti au mjumbe wa Tume asifanye kazi zake pia ni kosa la jinai na utashtakiwa chini ya kifungu hicho cha 21. Kubwa zaidi, yo yote anaetaka kufanya mikutano au makongamano nk yenye lengo la kuelimisha umma (public awareness programme) – kwa mujibu wa sheria hiyo analazimika afuate taratibu za sheria hiyo zinavyotaka. Hapo maana yake nini? Maana yake ni kuwa; sheria nambari 8 ya 2011 ya marekebisho ya Katiba inakana na kunyima ‘haki’ ya wananchi ya Kikatiba ya kutoa maoni yao kwa ‘uhuru kwa kuwalazimisha wafuate taratibu za sheria hiyo.

Bada ya kuyaona hayo, ukweli ni kuwa sio tu kuwa suala la muungano liwe ni msingi katika mjadala wa katiba; lakini suala la muungano lilistahiki kuamuliwa mwanzo na ndiyo baadae lije suala la katiba. Vipi tusiuzungumze Muungano ambao ndio uliozaa Katiba? Tuliungana kwanza kabla ya kuwa na Katiba. Muungano ndio uliozaa katiba tulizonazo, katiba zote mbili (ya Zanzibar 1984 na ya Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania 1977) ni matokeo ya muundo wa muungano huu. Muundo ambao uliunda mamlaka tatu (three Jurisdictions): ya Tanganyika, ya Zanzibar, na ya Muungano na baada ya hapo mamlaka mbili za Tanganyika na ya Muungano zikachanganywa (fused) na kuwa chini ya serikali moja na mamlaka ya Zanzibar kuwa chini ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hivyo pakawa na Serikali mbili na katiba mbili. Na huu ndio msingi unaowafanya wengi ( Aboud Jumbe, 1994 & Dourado, 1999 nk) wakasisitiza kuwa mkataba wa muungano ulikusudia mamlaka 3 na serikali 3 na ule utaratibu wa mamlaka 3 chini ya serikali 2 na hivyo katiba mbili ulikuwa ni wa muda wa mwaka mmoja tu mpaka utapoundwa mfumo wa katiba mpya ndani ya mwaka mmoja kuanzia siku uliposainiwa mkataba wa muungano. Mkataba wa Muungano unataja kipindi hicho kuwa ni “interim period” – Angalia kifungu (iii) cha Mkataba wa Muungano: “During the interim period, the Constitution of United Republic shall be the constitution of Tanganyika so modified as to provide for ”. Mkataba ulielekeza kuundwa kwa tume ya katiba (kifungu vii) ambayo ingeundwa kwa makubaliano kamili ya Marais ‘wawili’ wa nchi zilizoungana. La kushangaza ni kuwa hilo lilikwepwa kabisa, tena kwa amri ya upande mmoja tu (Tanganyika chini ya Nyerere) alipoamua kivyake – vyake tu (uniletarally) kupitisha sheria (Act no 18 of 1965) na kuliakhirisha hilo kwa muda usiojulikana mpaka hapo lilipoibuka tena miaka 14 baadae kwa kuunda katiba ya 1977 wakati huo ikiwa ni sawa na kuvuta shuka wakati kumeshakucha kwani mkataba wenyewe ulishajeruhiwa vya kutosha. Sheria hii ndio iliyovuruga kabisa Mkataba wa Muungano na ikafungua milango kwa upande mmoja wa Muungano kuamua watakalo. Kuanzia hapo ndipo balaa ilipoanza kwa vile Katiba hakiundwa tena kama walivyokubaliana na kama Mkataba wa Muungano ulivyoelekeza hadi mwaka 1977; mwaka ambao mambo yote nyeti ya Zanzibar yalikwishaingizwa kwenye Muungano kinyemela. Mwaka huo wa 1977 hata maaamuzi ya Serikali ya Zanzibar yalikwisha dhoofishwa kwa jina la Muungano kwa kutiwa ndani ya Chama. Na ni hapo Zanzibar iliponyimwa mamlaka kama ni nchi, na badala yake mamlaka yote yakaingizwa ndani ya Chama. Aidha, mwaka huo huo ikatungwa Katiba ya 1977 baada ya kuunganishwa vyama vya ASP na TANU. Baya zaidi, Tume ili ile iliyotumika kutunga Katiba ya Chama ndio pia iliyotumika kutunga Katiba ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania ya tarehe 26 April, 1977

Sasa tujiulize endapo Wazanzibari ambao wataamua, katika maoni yao, kuwa hawataki muungano na kwamba muungano kwao ndio kero yenyewe – ni vipi bunge la katiba litakuwa na wajumbe kutoka Zanzibar? Inakuaje leo wanaodai kuukataa Muungano waonekana maadui na hata ifikie hadi kukamatwa na kupigwa mabomu? Huku si ni kwenda kinyume na Katiba ambazo zinaeleza kuwa mamlaka, uwezo na nguvu zote za Serikali zitatoka kwa wananchi? Na hata Nyerere mwenyewe wakati akiwa Uingereza, tarehe 20 April, 1968 alisema na maneno yake kunukuliwa ndani ya makala ya London Observer akisema:

” If the mass of the people of Zanzibar should, without external manipulation, and for some reason of their own, decide that the union was prejudicial to their existence, I Nyerere could not BOMB Zanzibaris into submission. The union would have ceased to exist when the consent of its constituent members was with drawn”; yaani, Endapo umma wa Wazanzibari wataamua bila ya ushawishi kutoka nje kwa hoja zao wenyewe, wakaamua kukoma kwa Muungano, mimi Nyerere sitoweza kuwapiga mabomu. Muungano utasita pale tu utakapokosa ridhaa ya wananchi.

Sasa kama hivyo ndivyo, iweje leo viongozi wa Serikali wawapige MABOMU wananchi halali kwa kuitumia haki yao hiyo Kikatiba na ya ‘right to self – determination’ kuukataa Muungano uliowagharimu kila kilicho chao? Wanaodai kuwa wao ni watetezi wa ‘Muungano’ wanadai kuwa tuudumishe ‘Muungano’ ili kuwaenzi marehemu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume wakiwa ni waasisi wa ‘Muungano’ huo. Suala: Vipi tuwaenzi ‘marehemu’ tena wawili kwa kuwadhulumu ‘waliohai’ kwa mamilioni? Je, ni nani alie na maana na thamani zaidi kati ya marehemu na aliehai? Tuwaenzi kwa kuudumisha hata kama unatugharimu kila kilicho chetu? Muhimu si kuwaenzi marehemu; muhimu ni MASLAHI ya waliohai. (The damage is HERE; the damage is NOW). Na kwa hakika Wazanzibari walio wengi kama ni kumuenzi Karume basi wanamuenzi sio tu kwa maneno matupu; bali wanamuenzi kwa vitendo kwa kuisimamia hoja yake kuwa ‘Muungano’ ni sawa na kushona koti, ukiona linakubana, UNALIVUA, hoja ambayo aliizungumza wakati bado Nyerere yuhai! Lakini na Watanganyika nao watamuenzi Nyerere kwa kuwaachia Wazanzibari wajiamulie walitakalo bila ya kuwapiga mabomu kama alivyoeleza Nyerere alipokuwa Uingereza 1968.

Hata suala la kuamini kuwa Katiba ya Jamhuri iko juu ya Katiba ya Zanzibar ni suala linalozungumzwa sana. Haya ni masuala ya kisheria. Suala ni zinasimama vipi Katiba zote mbili: ile ya Zanzibar ya 1984, Toleo la 2010, na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Kumekuwa na msimamo wa muda mrefu kwa upande wa wasomi wa Tanganyika kujaribu kuleta sura kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano iko juu ya Katiba ya Zanzibar. Sasa hapo ndipo penye matatizo, kwa sababu Katiba zote mbili ni Katiba sawa. Hakuna iliyoko juu ya mwenzake. Na kisheria, kipimo cha mwisho na cha juu kabisa cha Katiba zote mbili ni ule Mkataba wa Muungano. Zanzibar na Tanganyika ni nchi mbili ambazo zilikuwa dola kamili zenye uhuru wake na uwezo kamili ambazo ziliamua kuungana April 26, 1964 zikiwa ni Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Wanasahau kuwa nchi hizi ziliungana kupitia Mkataba wa Muungano na si kupitia Katiba. Mkataba ule, kwa mujibu wa sheria, ni mkataba wa kimataifa, (it’s an international treaty) na ndiyo unaoongoza mahusiano kati ya Zanzibar na Tanganyika na ndio uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kusema hivyo maana yake nini? Maana yake, Katiba, ambayo ni sheria kama zilivyo sheria nyengine, zote zinapaswa zitafsiri yale mapatano au makubaliano yaliyofikiwa kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zilipoungana kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Serikali ya Tanganyika imekuwa ikifanya makusudi kuiendeleza dhamira yao ya kutaka kuimeza Zanzibar, kwa sababu kwa bahati mbaya Zanzibar iliingia katika Muungano huu kwa nia njema ya kujaribu kuleta umoja wa Afrika na kushirikiana – wenzetu walikuwa na dhamira na fikra za kikoloni za kuamini kuwa wanaitawala Zanzibar.
Kwa hiyo wanapenda isahaulike kwamba kulikuwa na Mkataba wa Muungano ambao ndio ungepaswa kuongoza mahusiano haya. Na ndiyo maana Mkataba wa Muungano hauonekani katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Wanajaribu kuonesha kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano eti ndio sheria kuu. Lakini kwa Mwanasheria yo yote ukimuuliza, atakwambia kuwa sheria kuu, sheria mama (grundnorm) katika Muungano wetu ilipaswa kuwa ni Hati za Muungano/Mkataba wa Muungano ambao ni mkataba wa kimataifa na sio Katiba ya Muungano.
Na kama kweli Serikali ya Tanganyika ina nia njema na Zanzibar na kuamini juu ya misingi ya Muungano wenye maslahi ya pamoja na fursa sawa (win – win situation) na kwamba Zanzibar inafaidika na mfumo wa Muungano uliopo kama wanavyodai ! SUALA:
Je, Serikali ya Tanganyika iko tayari katika kufuata mfumo na utaratibu huo huo iliyouasisi kwa kuona Zanzibar ambayo ni mbia na mshirika wake – inafutika, na badala yake iingie ndani ya Serikali ya Muungano kama vile ilivyo sasa Tanganyika imefutika na imo ndani ya Serikali ya Muungano? Yaani tuwe na Serikali ya Tanganyika na ile ya Muungano badala ya kuwa na Serikali ya Zanzibar na ile ya Muungano. Na kwamba Makao Makuu ya Serikali ya Muungano yawe Zanzibar? Na kwamba Tanganyika ipate 4.5% katika mgao wa mambo ya Muungano kama inavyopata sasa Zanzibar? Na kwamba Tanganyika kwa kipindi cha miaka 48 ijayo isiwe na: Polisi yake, usalama wake, usafiri wa anga, bandari, leseni za viwanda, ushirikiano wa kimataifa, utafiti, takwimu, ushuru wa bidhaa, kodi ya mapato, biashara za nje, simu, posta, elimu ya juu, mafuta na gesi asilia, uraia, uhamiaji, Mahakama ya rufaa, mambo ya nje, mikopo ya nje, sensa ya watu na baraza lake la mitihani – na kwamba yote haya yawe chini ya mamlaka ya Zanzibar? Je, itakubalika tubadilishane kwa utaratibu huu waliouweka?
Wakati umefika wa kuzirudisha Jamhuri zilizounda na kuzaa Muungano huu. Tunaposema tunataka kurudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na ile ya Tanganyika, tunasimama juu ya hoja kwamba: ilikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na sio wa TANU, na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na sio wa ASP ambao waliingia katika “Mkataba wa Muungano” 1964.
Sisi ni waumini kuwa hatari za kuvunjika “Muungano” haiko katika kuwaruhusu Wazanzibari kuirudisha Jamhuri yao ya Watu wa Zanzibar Kikatiba itakayokuwa na mamlaka ndani na nje; bali hatari ipo katika kuendelea kun’ang’ania kuinyima nafasi hiyo.

Katika uandikaji wa katiba mpya ya Tanzania, busara, uhalisia na ukweli wa mambo unataka kwanza liamuliwe suala la muungano, na baadae lifuate la katiba. Ikiamuliwa wananchi wanataka muungano wa serikali moja, tutakuwa na katiba moja. Ikiamuliwa wananchi wanataka muungano au serikali mbili (katika muundo wa sasa) tutabaki na katiba mbili, ikiamuliwa wananchi wanataka muungano wa serikali tatu , tutakuwa na katiba 3, wakiamua hawataki kabisa muungano , tutarudi tulivyokuwa kabla ya muungano na kila nchi na katiba yake na mambo yake. Wakiamua wanataka mashirikiano ya aina ya makubaliano ya kimkataba (Treaty) watakuwa na katiba zao na Mkataba Wa Ushirikiano – hivyo akili ya kawaida ingetuelekeza kwanza tupate uamuzi juu ya muungano na muundo wake badala ya kulazimisha suala la mchakato wa Katiba.

Tunapozungumzia Muungano wa Serikali moja ni aina ya Muungano ambayo mataifa ya asili yanayoungana yanapotea kabisa na kuwa na mfumo mmoja wa kiserikali na nchi. Si aina ya Muungano unaopendelewa hasa kwa nchi zilizo na tofauti kubwa kama Zanzibar na Tanganyika.

Muundo wa serikali mbili ndio uliopo hivi sasa ambao umekuwa ndio chanzo cha migogoro karibu yote ya muungano huu. Watanzania wote ni mashahidi wa jinsi muundo huu ulivyoshindwa kuweka utulivu na maridhiano katika mahusiano ya muungano. Zaidi ya yote umeshapitwa na wakati na hauwezi kuhimili mageuzi ya kikanda na kimataifa yanayotokea. Mbali na kero kadhaa za humu humu ndani, lakini tuchukulie mfano mdogo wa kuwepo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na ushiriki wa Tanzania. Zanzibar haimo kama mwanachama katika Jumuiya hii bali iliyomo ni Tanzania. Kati ya mambo 18 yanayoshughulikiwa na Jumuiya hii, ni mambo 4 tu ambayo ni ya muungano na ambayo Tanzania ina mamlaka ya kisheria kuiwakilisha Zanzibar. Kwa yaliyobakia 14 Tanzania kuiwakilisha Zanzibar ni kwenda kinyume na Katiba. Hata suala la Zanzibar kujiunga na OIC lilikwamishwa kutokana na mfumo wa muundo huu na Tanzania ikadai ingejiunga kwa vile ndio yenye mamlaka. Takriban inakaribia miaka 20 tokea kutolewa kwa ahadi hio lakini umma haujaelezwa maombi yalikwama wapi. Hata hivyo hili la OIC ni utashi wa kisiasa au kidini tu ndio uliokwamisha; lakini muundo wa Muungano huu unasutwa hata na maumbile ya mataifa haya yaliyoungana. Kwa mfano upo umoja wa visiwa vya Bahari ya Hindi ambao Zanzibar kama kisiwa wanastahiki kujiunga, lakini haina mamlaka, na hio Tanzania yenye mamlaka haiwezi kujiunga kwa vile sio kisiwa – hii imepelekea Zanzibar kukosa haki zake mbali mbali za kimaendeleo.

Athari nyengine za Muungano huu wa Serikali mbili ni pamoja na kumfanya Rais wa Zanzbar kuwa ni mjumbe katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Katiba ya Muungano inasomeka: “Kutakuwa na Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake watakuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na Mawaziri wote”. “Rais atahudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri na ndiye atakayeongoza mikutano hiyo. Na endapo Rais hayupo basi mikutano itaongozwa na Makamu wa Rais na kama wote wawili Rais na Makamu wa Rais hawapo Waziri Mkuu ndiye ataongoza Mikutano hiyo”. Baada ya kuwa Mawaziri wote wamo ndani ya Baraza la Mawaziri, akiwemo Rais wa Zanzibar, wote watakuwa ni Baraza la Mawaziri na watakuwa chini ya Waziri Mkuu. Huku ni kumdhalilisha na kukidhalilisha kiti cha Rais wa Zanzibar.

Muungano mwengine ni ule wa Serikali tatu. Hii ni aina ya Muungano wa Shirikisho. Nchi zilizoungana hubaki na serikali zao na serikali ya Shirikisho hubaki na yale mambo ya Muungano tu. Aina hii ya Muungano inadai kuwepo na Serikali ya Tanganyika, ya Zanzibar na ya Muungano. Hapa zitakuwepo nchi mbili, mamlaka tatu na serikali tatu. Kwa kuangalia uendeshaji wa mambo ya ndani ya nchi, huu unaweza kuwa muundo unaoweza kuondoa kidogo mtafaruku uliopo ; lakini ukiangalia uwakilishi wa nchi hizi na serikali zao katika mambo ya nje, muundo huu nao umeshapitwa na wakati. Tujiulize kwa mfano, kwa kuangalia mfano ule ule wa karibu wa Jumuiya Ya Afrika Mashariki, ni ipi kati ya serikali tatu hizo itajiunga na EAC? Kama ni serikali hizi 2 za Zanzibar na Tanganyika suali linakuja jee ni nani atawakilisha kuhusiana na masuala yaliyo chini ya serikali ya Muungano/Shirikisho ambayo serikali mbili hizi hawatakuwa na mamlaka nayo. Na vivyo hivyo endapo itayojiunga ni Serikali ya Muungano nayo itawakilishaje kuhusiana na yale mambo yaliyo chini ya Serikali ya Zanzibar na Tanganyika ambayo haina mamlaka nayo. Huu ni muundo ambao umeshapitwa na wakati.
Njia pekee kwa sasa ambayo itakata mzizi wa fitina ni kuwa na Mashirikiano/Muungano wa Mkataba. Huu ni muungano ambao kila nchi inajitegemea na inabaki na serikali yake, na uendeshaji wa mambo yake , utaifa wake nk na huingia katika mashirikiano kwa njia ya Mkataba (Treaty) juu ya mambo na kwa utaratibu wanaokubaliana hizo pande mbili au zaidi zinazoungana. Mifano ya miungano ya aina hii ni kama EAC (Kenya , Uganda , Tanzania Rwanda na Burundi) na Europena Union ulio na nchi wanachama 27. Uzuri wa muundo huu ni kuwa unatoa fursa kwa nchi zilizoungana kuweza kuuagalia kila inapobidi ule mkataba wao bila vikwazo vya Kikatiba na hivyo kusukuma mbele maslahi yao bila kumezana, kubebana au kuoneana. Hili ndio tulitakalo na Wazanzibari kwa pamoja na umoja wetu tukaliseme wakati Tume itakapopita kuchukua maoni.

Serikali zetu hazina haja ya kuogopa mawazo mapya kutoka kwa wananchi wake ya kutaka kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar itakayokuwa na mamlaka kitaifa na kimataifa na kufuatiwa na ‘mikataba ya mashirikiano mema’ na Tanganyika na nchi nyenginezo. Na kwa kweli tunahitaji kugundua njia mpya za mashirikiano badala ya ‘Miungano ya Kikatiba’ iliyopitwa na wakati (invalid). Ni kazi ya Serikali zetu kuzitafuta njia hizi mpya za ‘mashirikiano ya mikataba’ badala ya ‘Miungano ya Kikatiba’. Serikali zetu zisione aibu wala ugumu kuzipokea njia hizo zinapotolewa na wengine.

Kwa upande wa Zanzibar, Serikali yetu ya Umoja wa Kitaifa inaweza tu kuthibitisha umuhimu wake katika dunia ya leo kwa kutenda yale wanayoyahitajia wananchi wakiwa ndio ‘wadhamini na wamiliki’ wa Katiba. Katiba ya Zanzibar, Toleo la 2010, ibara ya 9 inaeleza kuwa nguvu, uwezo na mamlaka yote ya kuendesha nchi yatatoka kwa wananchi wenyewe. Aidha, Katiba inaeleza: “Kila Mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye maisha yake au yanayolihusu Taifa”. Ibara ya 21 (2) ya Katiba ya Zanzibar, Toleo la 2010. Hii ina maana gni? Ina maana kuwa shabaha ya Serikali ni WATU: heshima yao na haki yao ya kujiendeleza wenyewe katika hali ya uhuru bila ya kuingiliwa na watu kutoka nje. Katika kufikia shabaha hiyo, Tunahitajia Baraza la Wawakilishi lenye wajumbe safi na walio na unyenyekevu kwa Wazanzibari; lakini pia tunahitaji Baraza lenye Wawakilishi wenye mawazo yao wenyewe, na wanaoweza kujadili jinsi Wazanzibari tunavyoweza kutimiza shabaha yetu ya kuyarudisha mamlaka yetu ya Zanzibar vizuri zaidi. Baraza litakalojaa wajumbe wanaoweza tu kusema ‘ndiyo’ ‘ndiyo’ kufuatia mawazo ya watu wengine halitasaidia shabaha yetu hata kidogo.

Kitakachotuwezesha kuijenga Zanzibar mpya yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa ni KWANZA kudumisha umoja wetu, amani, utulivu na mshikamano baina ya Wazanzibari na Watanganyika WOTE. Tunajua kuwa mambo haya yanawaudhi WACHACHE wasioitakia mema nchi na kutimia kwa shabaha yetu; lakini tunayo hakika na yakini kuwa mambo hayo ni kwa manufaa ya Wazanzibari na Watanganyika walio WENGI.

Kwa upande wa Zanzibar, Uzanzibari utuunganishe ili kuweza kuirudishia Zanzibar mamlaka yake ndani na nje na kufuatiwa na ‘mikataba ya mashirikiano mema’ na kila nchi jirani itakayoandaliwa kitaalamu na itakayopata ridhaa ya wananchi wa pande husika na yenye kutoa fursa sawa katika maslahi ya pamoja katika misingi ya amani na utulivu.
Kurudi kwa Zanzibar yenye mamlaka yake kamili ya ndani na ya nje ni hoja yenye uhalali mkubwa kisheria na hakuna mwenye uwezo wa kupingana nayo kwa sababu Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ndiye mshirika/mbia mkuu wa huo unaoitwa Muungano.
Baada ya kuona hilo, msingi mzima wa siasa katika maongozi ya tawala za kidemokrasia, unahusu RIDHAA (mandate) ambayo wanaoongozwa huitoa kwa waongozi na hivyo kuwapa uhalali wa kusimamia mambo yao. Lakini ridhaa hiyo haitolewi hivi hivi tu, inaambatana na AMANA (trust) kwamba waongozi watatekeleza DHAMANA (obligations) na WAJIBU (duties) kwa makubaliano na maelewano ya kufuata barabara na kuheshimu kanuni na maadili yanayoiongoza jamii husika kwa maslahi ya wananchi.

Kuyafanikisha hayo, panahitajika mafahamiano mapya ya mahusiano kati ya waongozi na wanaoongozwa na kati ya Wazanzibari na Watanganyika. Na haya yanaweza kupatikana kwa kuwa na dira ya maslahi ya pamoja yatakayotuunganisha sote (Common vision for all).

Mungu ibariki Zanzibar.
Wazanzibari wote lazima tuamue hatma na mustakbal wa nchi yetu kwa kuirudishia mamlaka yake kitaifa na kimataifa. Sote kwa umoja wetu ni lazima tuifanye kazi hiyo na sote tuzikubali kanuni tunazojiwekea za kuidumisha amani ya nchi yetu na kuendeleza mchakato huu wa kudai haki yetu katika spirit ile ile ya Maridhiano.

Mamlaka tunayoyataka ni mamlaka ya Wazanzibari wote; yaletwe na Wazanzibari wote; yaendelezwe na Wazanzibari wote; na kwa hakika yatawafaa na kuwanufaisha Wzanzibari WOTE. Wazanzibari wote lazima tuamue hatma na mustakbal wa nchi yetu kwa kuirudishia mamlaka yake kitaifa na kimataifa. Sote kwa umoja wetu ni lazima tuifanye kazi hiyo na sote tuzikubali kanuni tunazojiwekea za kuidumisha amani ya nchi yetu na kuendeleza mchakato huu wa kudai haki yetu katika spirit ile ile ya Maridhiano.

Mamlaka tunayoyataka ni mamlaka ya Wazanzibari wote; yaletwe na Wazanzibari wote; yaendelezwe na Wazanzibari wote; na kwa hakika yatawafaa na kuwanufaisha Wzanzibari WOTE.

·        Wazanzibari wote lazima tuamue hatma na mustakbal wa nchi yetu kwa kuirudishia mamlaka yake kitaifa na kimataifa. Sote kwa umoja wetu ni lazima tuifanye kazi hiyo na sote tuzikubali kanuni tunazojiwekea za kuidumisha amani ya nchi yetu na kuendeleza mchakato huu wa kudai haki yetu katika spirit ile ile ya Maridhiano.

Mamlaka tunayoyataka ni mamlaka ya Wazanzibari wote; yaletwe na Wazanzibari wote; yaendelezwe na Wazanzibari wote; na kwa hakika yatawafaa na kuwanufaisha Wzanzibari WOTE.Wazanzibari wote lazima tuamue hatma na mustakbal wa nchi yetu kwa kuirudishia mamlaka yake kitaifa na kimataifa. Sote kwa umoja wetu ni lazima tuifanye kazi hiyo na sote tuzikubali kanuni tunazojiwekea za kuidumisha amani ya nchi yetu na kuendeleza mchakato huu wa kudai haki yetu katika spirit ile ile ya Maridhiano.

Mamlaka tunayoyataka ni mamlaka ya Wazanzibari wote; yaletwe na Wazanzibari wote; yaendelezwe na Wazanzibari wote; na kwa hakika yatawafaa na kuwanufaisha Wzanzibari WOTE.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.