Baada ya kumsoma Prof. Issa Shivji katika makala iliyochapishwa hivi karibuni katika Gazeti la Raia Mwema, nimezidi kuthibitisha ile dhana kuwa Tanzania ina nakisi kubwa ya mchango wa Wanazuoni katika kuleta MABADILIKO NA USTAWI mwema katika jamii yetu.

Wengi wao (ukiacha baadhi yao ambao wamejipambanua kuwa wanaitambua dhima yao) huwa wanastaajabisha kwa jinsi wanavyokuwa ni sehemu ya kuunga mkono uovu kwa mtindo wa aina yake. Na moja ya njia zao ni kuelekeza lawama kwa MABEBERU kwa kila jambo linaloashiria kushindwa kwetu.

Wanazuoni wetu hawa wamekuwa wakiendeleza tabia ya makusudi ya kujaribu kutuondoa kwenye tatizo la msingi na ambalo ndio kiini cha kushindwa kwetu na kutupiga mzubaisho kuwa kiini cha matatizo yetu ni UBEBERU.

Ukweli ni kuwa matatizo yetu mengi sana ni matokeo ya tabia, nyenendo na udhaifu wetu wenyewe katika kujipangia na kujiendeshea mambo yetu. Badala yake Wasomi wetu hao wamekuwa wabunifu stadi wa kutuelekeza pahala pa kurushia lawama zeru (UBEBERU ); na kwa kufanya hivyo, sio tu kwa madhumuni ya kunusuru TAWALA zetu ambazo ndio khasa zinazostahiki lawama, bali kutufanya tuzionee huruma na tuamshe hamasa za uzalendo. Ni kama mtu anayeamua kufanya mambo kinyume na maamrisho ya Dini yake, halafu akamsingizia IBILIS. Kwa hivyo, IBILIS/BEBERU ndio inayotumika kama sababu au kinga ya kushindwa kwetu?

Kwa mfano, hebu tuchukuliye hili suala  la MCC. Kama tutaliangalia kwa makini suala hili, tunaweza kujiuliza kuna ubeberu gani hapa? Aliyevuruga mambo ni BEBERU au Mzee JECHA na wenzake? Profesa wetu kakwepa kwa makusudi kabisa kugundua kiini cha kadhia hii. Hio ndio aina/mtindo wa mzubaisho wanaoutumia Wasomi wetu hao daima.

Ndugu zetu “tuliowapa” madaraka wanafanya ufisadi uliokithiri, wanakandamiza demokrasia, wanavunja haki za binadamu, wanaingia mikataba mibovu, kulindana, upendeleo, wizi wa wazi wazi, upindishaji mambo, ukosefu wa nidhamu, almuradi mambo mchafukoge. Matokeo yake, nchi haina maendeleo, huduma za kijamii ziko duni – halafu, ati unaambiwa kuwa tatizo ni UBEBERU.

Kazi kubwa ya Wanazuoni wetu hawa ni kuenzi na kuwalinda WATAWALA; na pale wanapoamua kukosoa, basi hukosoa baada ya miaka 30 ya MTAWALA kuondoka; huwaoni wala huwasikii kusimama kidete kupaza sauti zao wakati ule ambapo mambo yako motomoto yanaharibika.

Kwa kweli, tuna safari ndefu.

TANBIHI:Makala hii imeandikwa na mwanasheria Awadh Ali Said.

One thought on “Wasomi wetu na ukakasi wa mabadiliko”

  1. Ni kweli kabisa ni wanazuoni wachache wanaoweza kuwapinga, kusema kweli au hata kuwaelekeza viongozi. Mfano ni dhahiri kuwa Serikali ya Sheni na kaumu yake ni serikali haramu kabisa isiyoridhiwa na wananchi ,lakini wanasheria wenye sauti wameufyata na pia wale wasomi wa vyuo vikuu wamekuwa wote makhanithi kwa wanasiasa waovu kama Shein na hata Magufuli. Siku moja nilihudhuria kozi fupi coastal ecology pamoja na wanafunzi kutoka Marekani pale Chuo kikuu Dar-es salaam na Profesa mmoja alikuja kutoa mada inayohusiana na mambo ya historia, utamaduni na siasa ya Tz,. Bwana huyu alipwagaa na baada ya lecture yake , kwa kutumia maskhara na kweli mumo nikamwambia profesa lau kama research /thesis yako ungechagua wasimamizi kutoka wanywa kahawa wa Mkungu bobo kule Chake chake Pemba basi thesis yako ingekuwa ni reference tosha kwa wasomaji. Nikiwa na maana kwamba aliyokuwa anayasema hayakuwa na mantik wala ukweli wowote kuhusiana na histori na siasa hasa za Zanzibar.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.