President Maalim Seif

Siku ya Jumamosi, tarehe 2 Aprili, 2016, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama Cha Wananchi – CUF, lilifanya kikao chake cha kawaida cha siku mbili katika hoteli ya Mazsons, iliyopo Shangani, mjini Unguja, chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho, Twaha Taslima.

Pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, limetoa taarifa (MAAZIMIO) ya mwelekeo wa Chama Cha Wananchi – CUF kuhusu hali ya kisiasa nchini na hususan visiwani Zanzibar mara baada ya kukamilika kile kilichoitwa “Uchaguzi Mkuu wa Marudio” uliofanyika Machi 20, mwaka huu ambao ulisusiwa na vyama zaidi ya tisa (9) kikiwemo chana cha CUF kati ya vyama kumi na nne (14) vilivyoshiriki katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015 na matokeo yake kufutwa Oktoba 28, 2015, na mtu anayeitwa Jecha Salim Jecha (Mwenyekiti wa ZEC).

Leo, Jumatatu, Aprili 4, 2016, Baraza Kuu la Uongozi la CUF, Taifa, wamefanya mkutano na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya Chama hicho, iliyopo maeneo ya Vuga, mjini Unguja.

Na Ally Mohammed
Na Ally Mohammed

Lengo la mkutano huo na waandishi wa habari ni kutoa taarifa (MAAZIMIO) ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi ambacho kilikutana kwa muda wa siku mbili.

Taarifa hiyo ilikuwa na MAAZIMIO kumi na tatu (13), pamoja na mambo mengine yaliyotolewa katika MAAZIMIO hayo, hoja kubwa zilikuwa ni tatu.

  1. Kuendelea kuwataka wananchi waendelee kuitunza amani.
  2. Kusisitiza kutoutambua utawala wa SMZ uliopo madarakani kwa sasa.

  3. Kuendelea kuitafuta haki ya wanachi kwa njia ya demokrasia.

Kwa msingi wa kusimamia hoja yangu niliyoikusudia hapa, naomba nilinukuu AZIMIO la kumi na mbili (12).

“…..inaendelea kuwataka Wazanzibari, kuwa watulivu na kulinda amani iliyopo na linawahakikishia kwamba, CUF inaendelea na juhudi zake za kutafuta haki yao na kusimamia maamuzi yao waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015, kwa njia za amani na za kidemokrasia”.

“Njia hizo za amani zimefanikiwa na kuungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa, ambayo imeanza kuchukua hatua dhidi ya ubakwaji wa demokrasia uliofanyika”. Mwisho wa nukuu.

Ni maneno yenye mantiki na busara ya hali ya juu kwa anayetambua nafasi ya kiongozi anayetakiwa kuwa na busara.

Busara inahitajika wakati ambao kauli yeyote kwa wakati huo atakayoitoa kiongozi inaweza kubadili hali ya mambo aidha kuwa hasi au chanya na kwa hili la CUF ni wazi limekuja na taswira chanya.

Nimesukumwa na kuandika makala hii baada ya kuona baadhi ya watu wakikosoa vikali tena kwa dharau kubwa eti hakuna jipya, ni yale yale, wamefeli, imebaki stori na kauli nyengine za aina hiyo zenye kejeli, dharau na ni wazi zinatoka kwa aidha, watu waliokata tamaa au wasiojua siasa na kupigania haki kwa misingi ya demokrasia za kistaarabu na za kisomi.

Nasema ni watu waliokata tamaa au wasiojua siasa za kistaarabu kwa sababu, nimefundishwa ukitaka kupinga kitu chochote ni lazima uwe na hoja madhubuti ambayo itakuwa na uzito na utaweza kuitetea.

Lakini huwezi kupinga na kudharau kitu bila kushauri njia mbadala ambazo wewe unaziona ni nzuri na zingefaa kutumika kwa wakati huo kwa kile unachokiona.

Kuna watu walidhani pengine CUF wangekuja na MATAMKO mazito, yenye kuhamasisha vurugu, chuki, fitna na uhasama kwa jamii, huu ni uwendawazimu na upetevu wa kiwango cha kidhalimu usiopaswa kuwazwa na binaadamu mwenye akili timamu hata dakika moja.

Kwamba CUF watoe MAAZIMIO ya kuhamasisha watu wake waingie barabarani na kufanya vurugu, kweli? Katika kipindi hichi ambacho Vikosi vya Ulinzi na Usalama vipo ‘moto’ na vimejiandaa vya kutosha kukabiliana na hata sisimizi atayeleta ‘fyokofyoko’!

Nitakuwa mtu wa mwisho kuunga mkono CUF kuhamasisha vurugu katika kipindi kibaya zaidi cha tahadhari tunachokipita kwa wakati huu.

Ningewashangaa CUF (Uongozi), na kuwatoa thamani viongozi wote wa chama hicho kama wangekuja na MATAMKO ya kuchochea vurugu kwa wanachama na wafuasi wake.

Sifa kubwa ya kiongozi ni kutawaliwa na busara katika kipindi ambacho kauli au uamuzi wake wowote utaleta matokeo hasi, katika hili CUF wamefaulu kwa asilimia zote.

Ni wazi, kuna wafuasi wa Chama hicho (CUF) wanaonekana kukata tamaa na kuona matamko ya Chama chao hayana athari yeyote kwa sasa na pengine mawazo yao wanaona hayana hata haja ya kutolewa, wao wanataka kusikia kauli ya kuhamasishwa kuingia barabarani na kufanya vurugu.

Hiki ni kiwango kibaya zaidi cha kufikiria kwa binaadamu mwenye uelewa, mwenye kuzitambua siasa za Tanzania na hasa Zanzibar, mwenye kutumia ‘jicho la tatu’ kuangalia mambo kwa uhalisia wake na matokeo yake ya baadae.

Ni kipindi ambacho busara inahitajika zaidi kuliko kibri, ni kipindi ambacho wenye elimu na busara wanalazimika kufikiria zaidi ya upeo wao ili kufanya maamuzi ya busara.

Unapokuja na kauli za dharau, kejeli, kashfa, kukata tamaa kwa kisingizo eti, MAAZIMIO ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF hayana jipya wala hayawezi kubadilisha kitu, hivi tulitaka CUF waje na kauli gani nyengine?

Kwamba CUF iseme “tumechoka na sasa tunawataka wananchi wote waingie barabarani kudai haki yao kwa nguvu” tulitaka CUF waseme hivyo? Tunazishirikisha akili zetu katika kufikiri au ni mihemko tu?

Uongozi sio kiburi na hasira, kwa wenye familia tuangalie hata mfano tu wa familia zetu zinapokuwa kinzani, tunatumia njia gani kutafuta suluhisho? Na Matokeo ya njia hizo ni nini?

Watu waache kuongozwa na ‘sauti za shetani’ kila wakati, kuwa kwa kuwa wameminywa sauti yao, basi njia nyengine iliyobaki ni kuitafuta haki yao kwa njia za vurugu.

Ni nani aliyetarajia kuwa tungepita katika kipindi hichi kwa utulivu mkubwa, je, tumesahau kuwa tulijianda kwa kunua vyakula na mahitaji yote muhimu tukiamini kutatokea vurugu kubwa wakati wa uchaguzi?

Ni nani anajitoa fahamu na kutokuiona nguvu kubwa ya Chama Cha Wananchi – CUF katika kuhamasisha amani na utulivu na wafuasi wao wakatii hilo?

Tuwe na desturi ya kuchanganua mambo kwa kuangali leo, kesho na mtondogoo, hasara na faida na matarajio yetu ni yapi badala ya kuwa na akili ya kuipinga busara bila kuwa na suluhisho lenye matokeo chanya.

Kulalamika kusikokuwa na mpango mkakati wa baadae, hakuna msaada zaidi ya kupoteza muda na kupunguza uwezo wa kufikiri.

MWISHO.

Ally Mohammed pia anapatikana kwa barua-pepe ya allymohammed01@gmail.com

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.