Mjadala juu ya hatua ya Shirika la Misaada la Marekani la Changamoto ya Milenia (MCC) kuiondoa Tanzania katika orodha ya nchi zitakazonufaika na awamu ya pili ya misaada inayotolewa na shirika hilo ambayo ingekwenda moja kwa moja kusaidia huduma za maendeleo na zaidi maeneo ya vijijini katika masuala ya miundombinu ya barabara na umeme umechukuwa nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari rasmi.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi, kwa taaluma zao, wamefanya uchambuzi wa faida na hasara ya uamuzi wa MCC na wapi tulipojikwaa.

Wachache kwa mihemko tu ya ushabiki wa kisiasa – tena ukitizama maandiko yao ni wazi hawana taarifa zilizoshiba kuhusu ni nini MCC – wameendelea kupotosha suala hilo na kufikia hatua hata ya kuwaita wafadhili hao kuwa ni mabeberu.

Nimesoma kwa utulivu wa akili na mwili andiko la kaka’angu Bollen Ngetti, amegusia kuhusu uamuzi huo na namna suala hilo linavyojadiliwa, Ngetti huyu, andiko lake amelipa kichwa cha habari “KUFANYA MCC KUWA AJENDA NI UGAIDI”!

Na Ally Mohammed
Na Ally Mohammed

Kwanza nikiri Ngetti ni mmoja ya watu ninaowaheshimu katika taaluma hii, ni kioo changu katika uandishi, najua itakuwa umesahau kaka, ila nikwambie tu kwa mara ya kwanza nilikupigia simu mwaka 2008, wakati huo nikiwa kidato cha tatu (form three) pale Haile Selassie Secondary School, tulizungumza mambo mengi kaka na zaidi kuhusu ule mnyukano wa SAUTI HURU na KULIKONI, mpaka mukafikia kudhalilishana kwa kufananishana na wanyama tena kwenye ‘front page’, tuliongea sana na ukaniambia vitu vingi vya maana sana, najua itakuwa umesahau ila mimi nakumbuka mpaka leo zaid ya miaka 8 sasa.

Sio nia ya andiko hili kukujibu kaka yangu Ngetti, lakini pale ninapoona kuna harufu ya kupotoka, ni wajibu wetu kuwekana katika njia iliyonyooka.

Katika andiko lako ‘my brother’, umeandika vitu vingi na zaidi sifa za ‘kumwaga’ kwa Rais John Pombe Magufuli, umemsifu kama vile Magufuli ana hadhi ya Malaika (Astaghafirullah).

Suala la MCC linahitaji utulivu wa mwili na akili kulijadili kwa hoja zilizoshiba sio mihemko na ‘mizuka’ ya kikada na kutetea rangi za chama hata katika mambo yanayoligusa Taifa moja kwa moja.

Ukitoa sheria ya makosa ya mitandao jambo jengine lililoinyima Tanzania misaada ya MCC ni suala la Uchaguzi wa Zanzibar, kabla ya kuwaita MCC mabeberu, wanatuingilia (sijui kuingiliwa kupi) hatutaki misaada yao, ni muhimu tukapima uzito wa hoja zao.

My brother Ngetti, katika andiko lako umeitaja Zanzibar kuwa ni nchi huru, nikukumbushe tu MCC wameinyima Tanzania misaada kama nchi na hata Katiba ya Jamhuri hakuna sehemu inaitambua Zanzibar kama ni nchi huru, kama ipo njoo na andiko la katiba hapa.

Kushabikia uzalendo na kutokukubali kuyumbishwa na wafadhili huku watawala hao hao wakiminya sauti za wananchi kwa mtutu wa bunduki hicho ni kiwango cha kimataifa cha ukasuku na USHETANI.

Hatuwezi ‘kuwajejea’ (kuwadhihaki) MCC na kuacha kuyajadili ya Zanzibar hata kama tumekunywa maji ya bendera.

Andiko lako kaka limesisitiza kuwa MCC ni NGO tu na haina uhusiano na Serikali ya Marekani! Serious brother au ni mihemko tu? Ni kweli unaweza kulitafautisha Bunge la Marekani na Serikali ya nchi hiyo?

Umeeleza kasi nzuri ya Serikali ya JPM katika kukusanya kodi na kueleza kuwa tunaweza kujiendesha bila ya misaada.

Asilimia kubwa ya uliyoyachukuwa kuweka uhalali wa hilo ni kuwa eti Magufuli amesema anataka Tanzania ijiendeshe mpaka iweze kukopesha nchi nyengine.

Hapo ndiyo nimechoka, hivi Magufuli ametoka sayari gani mpaka kwa muda mfupi aibadilishe Tanzania kiasi hicho?

My brother Bollen Ngetti, Magufuli ni mwanasiasa kama walivyo wanasiasa wengine, na ninachokiona kwa Magufuli ni kama vile haamini kama kampeni za uchaguzi mkuu zimekwisha, wanasiasa na hasa wenye maamuzi wana kawaida ya kukurupuka na kutaka sifa za ghafla, rejea katika TAMKO lake (Magufuli) la elimu bure halafu utajua nilichokikusudia.

Wanasiasa wengi wa dunia ya tatu hawana dhamana, hawaweki kumbukumbu na wala hawapendi kuzishirikisha akili zao katika maamuzi na matamko yao.

Ngoja nikupe mfano, mara baada ya taarifa kuzagaa juu ya maamuzi ya MCC kwa Tanzania, alipohojiwa Balozi Seif Ali Idd, Kiongozi wa Shughuli zote za Serikali katika Baraza la Wawakilishi (chombo kinachopitisha bajeti ya Serikali), kwa kujua au kwa kutokujua alisema, “hii si mara ya kwanza kutunyima misaada yao (MCC), hata mwaka 1995 wakati wa Dkt. Salmin, walifanya hivyo, lakini tuliweza kujiendesha na kwa hili wala hatushughuliki”.

Balozi Augustino Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Kikanda, yeye alisema, “kuzuia misaada ya MCC itawaumiza wananchi wa vijijini ambapo miradi mingi ya MCC inakwenda kutoa huduma huko”.

Angalia hizo kauli kisha zioanishe kama zitaoana, hao ndiyo aina ya viongozi tulionao kaka, hatutakiwi kuwatetea tu tunapaswa kuwakemea kwa sauti maana wanakwenda kupotoka.

Jambo jengine ambalo linaonesha wazi ni uwezo mdogo wa kufikiria mambo na uhalisia wake, eti watu wanahoji kwamba mbona kuna mifano ya nchi nyengine ambazo zina sheria mbaya ya makosa ya mitandao na vile vile hawaheshimu demokrasia iweje iwe Tanzania tu?

Nasema huu ni uwezo mdogo wa kufikiria, binaadamu mwenye akili timamu katu hawezi kushindana kwa kutafuta mifano miovu na kujivika yeye, hata maandiko matakatifu (Qur’an na Biblia) yanatuhimiza tushindane katika mema.

Huwezi kutoa mfano wa ukandamizwaji wa demokrasia nchini Zimbabwe ukasema ya Zanzibar yana afadhali, kwa mifano ya aina hiyo, itakuwa rahisi na sisi kuhalalisha matendo ya keshetani ya kulawitiana na kusagana (wajinga wanaita ndoa ya jinsia moja) kwa sababu tu eti Malawi wameruhusu.
Nimalize kwa kusema hoja ya Uzalendo isiletwe kwa sababu ya maamuzi ya MCC tu bali viongizi wetu wawe wazalendo kwa kuruhusu sauti za wananchi zifanye maamuzi ya uongozi badala ya kutegemea huruma ya dola na Tume za Uchaguzi.

Tuendelee kujadili maamuzi ya MCC pande zote, hasi na chanya bila kuhemkwa na rangi za bendera na tusiwaogope watawala kuwaambia waache kusigina maamuzi ya wananchi kwa namna yeyote ile maana uongozi upo kwa utaratibu wa katiba yetu.

Tanzania haina uwezo wa kujitegemea leo, kesho na miaka 50 ijayo bado tutahitaji huruma za hao tunaowaita mabeberu, kuidhihaki misaada ya MCC kuwa haitushughulishi ni mwendelezo wa kiburi cha watawala na kikundi chao wanaofaidika na ‘keki’ ya Taifa hili.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.