Laiti kama haya ya kufutwa kwa awamu ya pili ya msaada wa kimaendeleo wa shirika la misaada la Marekani (MCC) kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yangelitokea kwa Afrika Kusini wakati wa kufinywa kwa demokrasia na ubaguzi, basi tungelipiga makofi. Kama ilivyo kwa Tanzania, hata makaburu walichokuwa nacho wakati ule ni katiba, lakini jee ilitosheleza kusema kwamba wasiingiliwe katika masuala ya ndani yanayolindwa na katiba yao tulioiona ya kibaguzi na dhaifu? Hivi sheria ya mitandao ingeliwekwa na makaburu tungeliitetea kwa uzalendo?

Walichokuwa wakikifanya makaburu dhidi ya Waafrika Kusini kilikuwa ni kuingilia haki ya wananchi wao katika kuchaguwa kiongozi wao, na ndicho hicho hicho kilichofanywa na Jecha Salim Jecha katika macho ya waangalizi wa ndani na wa nje, ambao hadi hii leo hakuna hata mmoja aliyekubaliana na hoja kwamba uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 haukuwa huru. Sasa iweje tuwe wakali wa siasa za kikaburu za wakati ule na kuomba kuzuiwa kwa misaada inayoimarisha tawala za kikaburu zinazozuia upana wa demokrasia, lakini tuwe wakali kwa waliotunyima misaada kwa kosa hilo hilo la watawala kufuta uchaguzi na kutunga matokeo ya marudio kinyume na matakwa ya wananchi?

Na Foum Kimara
Na Foum Kimara

Waafrika tumekuwa wakali pale mwenye rangi tafauti na ya kwetu anapotunyanyasa, lakini tumekua tukifumba macho pale unyanysaji unapofanywa na Muafrika mwengine kwa mnyonge. Tumerithi ubaya wa kikoloni na kuendeleza vilio vya kupinga ukoloni pale tunapokosolewa kwa makosa tunayoyafanya yanayoendana au kuzidi matendo ya nyuma ya wakoloni dhidi yetu. Kumbuka mauaji ya Januari 2001 yangelifanywa na Mreno ingelikuwaje? Utekwaji wa Ulimboka? Kesi za kupandikiza? Kuwekwa ndani kwa wanasiasa? Hatuoni basi?

Hivi ingewezekana kupiga kelele za namna hii kuwapinga waliozuia msaada ingekuwa kwa mfano Angola iliofanya uchaguzi ulio huru mbele ya macho ya jumuia za ndani na nje, halafu utawala wa Kireno ukaufuta kwa visingizo vya ajabu, halafu ukafanya uchaguzi na matokeo ya kupikwa yaliompa Mreno ushindi wa asilimia 91 na kura 299,999? Hivi Waafrika tutatambua lini maana halisi ya haki isioegemea utashi?

Utashangaa leo hii kwamba hata nchi za Kiafrika zilizoweza kubadilisha watawala kwa misingi ya chaguzi huru kama Nigeria, zikawa kimnya pale nyengine zinapozuia demokrasia kufanya kazi? Muhammadu Buhari aliingia madarakani akiwa ni mpinzani na mtetea haki, lakini hutamsikia hata siku moja kupiga kelele nchi nyengine za Kiafrika zinapofanya mabaya dhidi ya wapinzani. Hutamuona Mecky Sally wa Senegal akijitenga na magurupu ya wababe kama Pierre Nkurunziza wa Burundi au Yoweri Museveni wa Uganda kwa wanayoyafanya dhidi ya wapinzani, kama vile wamesahau yale waliokuwa wakifanyiwa wakiwa nao katika kambi ya upinzani?

Kama ni suala la diplomasia, iweje basi kwa nchi za Magharibi ziweze kukosoa uvunjaji wa haki za binaadamu, lakini za Kiafrika zikashindwa? Iweje basi Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe aweze kuwatukana Wazungu hadharani, lakini ashindwe kwa madikteta wa kwetu? Nimesahau yeye mwenyewe dikteta, atawakemeaje madikteta wenziwe?

Tuwe wakweli. Sisi Waafrika tuna matatizo makubwa katika kusimamisha tawala za haki. Inashangaza mijitu inayotwambia kwamba demokrasia yetu ni changa mno kulazimishwa kuisimamisha, lakini wanasahau kwamba wakoloni waliyasema hayo hayo kama kisingizio cha kuchekewesha uhuru. Hivyo jee walikuwa sawa?

Uchanga wa demokrasia utautafsiri vipi wakati uchaguzi ulishafanyika, lakini aliyeshindwa akaufuta ili aje na mapishi mapya yatayoendelea kumuweka madarakani bila ya kupingwa? Huu ni uchanga au udikteta? Tafsiri ya uchanga ni kufuta pia chaguzi ulizoshindwa na kujitangaza mwenyewe?

Waafrika tuwe wakweli na kuitazama haki kama ilivyo badala ya uzalendo butu unaodumaza haki na kuzidisha mipasuko, visasi na mauaji ya wenyewe kwa wenyewe. Tukumbuke majanga makubwa ya dunia yametokea baada ya watawala kuitumia ngazi ya uzalendo kudidimiza haki za wengine na kuupa utukufu uzalendo wao kiasi kwamba Wajerumani walijihisi ni “master race” kuliko wengine. Adolf Hitler alifanikiwa kwa sababu aliungwa mkono na Wajerumani walio wengi walioamini kasumba ya uzalendo usio na misingi ya utu wala haki. Tuipinge dhulma kwa uhuru badala ya kuiwekea sababu za kuilinda kwa misingi ya aila, rangi na uzalendo, dhulma ni dhulma na kigezo chake kikuu na unyonge wa mdhulumiwa.

One thought on “Uzalendo unaoibuka kwa kufutiwa misaada ni unafiki”

  1. La kusikitisha zaidi kuwaona wasomi wa kimbelembele akina Pole Pole wakijaribu kupotoza kiini cha suala la MCC. Hawathubutu kuyakemea yaliyotokea na kupelekea kukosa huo msaada. Badili yake, wanatafuta ufahari kwa mgongo wa Wazanzibari walionyanganywa ushindi wao kweupe huku dunia nzima ikiwa shahidi. Tena wameshutshwa sana. Kwani ile fitina aliyoitapakaza Kinana katika gazeti la kule Marekani ianonyesha imepuzwa. Ingelikuwa wakutafakari wasingefanya uchaguzi wa marejeo. Eti 91%. Upuuzi Mtupu!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.