Jumatatu ya tarehe 21 Machi 2016, Dk. Ali Mohamed Shein ataamka mapema kisha atasimama mbele ya kioo chake kujiangalia. Ile taswira kwenye kioo itamuambia: “Wewe ni Ali tu!” Mwangwi wa sauti hiyo utatoka nje na kumchoma moyoni, naye kwa hasira atajibu: “Hapana. Mimi sio Ali tu. Mimi ni Rais Dk. Ali Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, niliyechaguliwa na asilimia 70 ya kura halali.” Akikiangalia tena kioo, ile taswira itamuambia tena: “Wewe ni Ali tu!” Ataamua kukiadhibu kioo chake mwenyewe – pengine kwa kukivunjilia mbali, pengine kwa kuamuru kihamishiwe stoo milele.

Hivyo ndivyo hali itakavyokuwa kwake kwa siku zote zitakazounda miaka mitano inayoanza sasa. Kila siku, atapaswa kukabiliana na kivuli chake mwenyewe, ambacho kitakuwa kinamsuta kwa kumueleza yeye ni nani hasa, naye kila siku atataka kuthibitisha vile anavyojidhani ndivyo alivyo.

Tafauti na Rais Ali Mohamed Shein wa 2010 hadi 2015, huyu wa 2016 na kuendelea atakuwa na miaka migumu mno maishani mwake. Sababu ni kuwa nafsi yake inajuwa kuwa alipo sipo na aliyepo hapo si yeye. Hata katika kilele cha kujitoa fahamu anachojikuta kuwa nacho, bado kuna kitu ndani yake kinamrejesha kwenye ukweli wa mambo na ukweli huo unamuonesha taswira ya kwenye kioo – Ali tu.

Jamii yako inapokumbwa na matatizo yanayotokana na dhuluma ya mwenye nguvu dhidi ya mnyonge, ile dhana waliyonayo wajiitao wasomi ya “kutokuwa na upande” huwa ni alama ya ujinga wao, kwa sababu huwa wanamsaidia dhalimu kwenye vita vyake dhidi ya mnyonge. Kushirikiana moja kwa moja na dhalimu dhidi ya mnyonge huwa ni ukatili.

Namzungumzia myonge wa Zanzibar ambaye tayari alishakuwa taabani kwa kuwa serikali yake iliamua kutumia makundi ya uhalifu wa kisiasa yanayolindwa na vyombo vya dola, yampige, yamtese na yamuharibie mali zake. Vyombo hivyo vya dola, ambavyo kimsingi vilikuwa na wajibu wa kumlinda, tayari vilishamueleza kuwa yeye hasa ndiye muhalifu na hivyo asitazamie ulinzi wowote. Ndio ujumbe uliomo kwenye kauli ya Mkurugenzi wa Upelelezi, Salum Msangi, anaposema “wanaodai kupigwa na mazombi ni wahalifu ambao wamekutana na wahalifu wenzao.”

Kinachotokea Zanzibar hivi sasa kinatuhitaji kuchagua upande upi tunasimama, nami nimechaguwa upande alio mnyonge ambaye, licha ya kutokuwa na uwezo wowote wa kujitetea, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kummiminia wanajeshi wa vyombo vya ulinzi na usalama kila kona ya mji wake. Hadithi za kupigwa kwa watu wazima – wanaume na wanawake, kuchomewa moto nyumba zao, ofisi za vyama na vituo vya afya, maeneo ya kukusanyika, na kukamatwa kwa hadi watoto wa miaka 14 zimekuwa za kawaida sasa.

Yote yanahusishwa na hicho kinachoitwa uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, ambao lengo lake pekee ni kumpatia Dk. Shein jina la urais wa Zanzibar na uwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Mimi nimechaguwa upande na wala sitakaa nikasema ninajipumbaza kusaka mizania ya mambo kwenye hili, kwa sababu si jambo lenye mizania. Amri ya Amiri Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli, kuwashughulikia waleta fyokofyoko visiwani Zanzibar haiwezi kutiwa kwenye mizania na kauli za viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) waliolalamikia kuwa wamekuwa wakiteswa, kuadhibiwa na kudhalilishwa na sasa wamechoka. Kuchoka kwao hakuwezi kuwekwa sawa na kuzidi kuumizwa kwa wananchi visiwani Zanzibar.

Mimi nimechaguwa upande wa kumuambia Dk. Shein kwamba ikiwa gharama za yeye kuitwa rais ni hizi tunazozishuhudia sasa, basi kioo chake kitaendelea kumkumbusha kuwa yeye ni Ali tu. Ataendelea kupigiwa ving’ora. Ataendelea kufungwa nyuzi za viatu. Ataendelea kupigiwa saluti. Ataendelea kwenda na kurudi Ikulu. Lakini yote hayo hayatakuwa na maana ya kumfanya kweli kiongozi anayezitawala nafsi za wale anaodhani kuwa wako chini ya utawala wake. Kwao wao, yeye atabakia kuwa ni Ali tu kama anavyoonekana na kioo chake.

Nimechaguwa upande wa mnyonge aliyepanga foleni siku ya tarehe 25 Oktoba 2015 kutoka Bungi Miembe Mingi hadi Msuka Mtongani na akapaza sauti yake ya nani awe nani kwenye nafasi za uongozi wa nchi yake kwa miaka mitano hii. Nilimuona. Nilimsikia. Na hadi sasa nikifunga macho usiku gizani, naweza kuuhisi uwepo wake ndani yangu. Alikuwa sahihi wakati ule na yuko sahihi leo hii.

Niko upande wa mnyonge huyu pale anaposema kuwa kwake uchaguzi ulishafanyika na kumalizika Jumapili ile ya Oktoba 25 na hautambui mwengine kabla ya mwaka 2020. Ikiwa leo hii anaadhibiwa kwa msimamo wake huo, basi mimi niko pamoja naye. Inawezekana, kuwa kwa sote wawili – mimi na yeye – tu wanyonge, basi kuwa kwangu pamoja naye kusipunguze chochote kwenye maumivu anayoelemezewa na utawala ambao hautaki kusikia neno “HAPANA” kutoka kwake. Lakini angalau nakumpe moyo kuwa hayuko peke yake, na kamwe hatokuwa.

One thought on “Dk. Shein, kioo kitakuambia wewe ni Ali tu”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.