Sifa njema ya taasisi hupatikana kwa mambo mengi ambayo huchukuwa muda mrefu hadi kufahamika kwake kuwa ni miongoni mwa taasisi zenye sifa hiyo. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni taasisi yenye hadhi sana, inayoheshimika nje na ndani ya nchi, lakini kitendo kilichotokea cha Rais John Magufuli kuyatembelea makao yake makuu kwa kushtukiza, kimewafanya watu wengi kupitia vyombo vya habari kutafsiri kwamba tayari jipu limeshatumbuliwa BoT na tayari taswira na heshima ya taasisi hiyo na wafanyakazi wake imeanza kupotea. Lakini ni kweli Magufuli katumbua jipu la BoT?

Kuzuia malipo na kuagiza fedha zirudishwe Wizara ya Fedha bado haijawa jipu limetumbuliwa, ni utaratibu wakawaida kwa mkubwa anapokuwa na wasiwasi kuagiza uhakiki ufanywe upya au hata mda mwengine hufanya yeye mwenyewe iwapo anataaluma nacho, sijui lipi hapa kilichowapa watu hamasa hadi kutangaza kwamba jipu la BOT limetumbuliwa, labda niseme ni kutokana na aina ya uzungumzaji wa kimsisitizo wa Rais Magufuli.

Hivyo ikiwa ulipaji wa Fedha hizo zilizorejeshwa Wizara ya Fedha kwa kufanyiwa uhakiki malipo yake ni jipu, basi ni hadi pale ukaguzi na uhakiki ulioagizwa na rais utakapotolewa na majibu yake na sio baada ya Rais Magufuli kuagiza zirejeshwe kua ndio ishakuwa jipu.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohamed

Nimesikia pia baadhi ya magazeti na waaandishi katika mitandao ya kijamii kwamba BoT nusu ya wafanyakazi ni hewa, hivyo nalo ni jipu na wengine hadi kufikia kutoa idadi ya wafanyakazi wanaofanya kazi halali na hao wanaowasema ni hewa.

Mini niwaombe wanaotoa taarifa kwa rais lazima watumie ueledi na uchunguzi kwanza kabla ya kumfikishia rais taarifa za ubadhirifu unaodhaniwa kutendeka katika taasisi fulani, kwa sababu kinyume na hivyo tunaweza kumdharaulisha rais na pia kuharibu sifa za taasisi zetu zisiaminike ndani na nje ya nchi.

Kwa mfano Rais Magufuli alionekana akifanya uchambuzi wa orodha ya wafanyakazi wa BoT, huku akiwa ameshikilia nyaraka zinazoonyesha idadi ya wafanyakazi wa ‘BOT’ ambazo amepatiwa na watu anaowaamini kumpatia taarifa za majipu.

Rais Magufuli alitakiwa pia kuomba orodha ya malipo ya BoT ili alinganishe idadi ya wafanyakazi aliopatiwa na mtu wake ambao imefikia idadi ya watu 1,391 kisha aone ikiwa kweli BoT inalipa idadi hiyo ya wafanyakazi?

Kwa sababu katika taasisi hasa za serikali kuna taratibu nyingi zinafanyika juu ya wafanyakazi, kwa utafiti wangu mdogo niliufanya nimegundua ile orodha ni orodha ya wafanyakazi wote waliofanyakazi kwa miaka kumi nyuma (10), hivyo yawezekana hata Jina la Mh. Mwigulu Nchemba limo mule, na orodha hile imewekwa kama orodha ya kupatia habari za waajiriwa (Directory) wa ‘BOT’ waliopo na walioondoka na kimewekwa kwa sababu maalum, ikiwemo kuisaidia serikali yenyewe kupata taarifa sahihi za wafafanyakazi wake.

Hivyo endapo Mheshiwa Rais angeomba “Payroll” mbele ya hadhara ile basi angeweza kujua kwamba lile ni ‘jipu’ au ‘uvimbe’, kupata nafasi ya kutumbua jipu katika taasisi kama ‘BoT’ kunahitaji lazima raisi ampate mtu ambaye ni mtendaji wa taasisi hiyo, nasema hivyo kwa kuwa naamini majipu yamo lakini ni ya kitaalamu sana kwa kuwa kumbukumbu zinaonyesha TAKUKURU hawana muda mrefu kumaliza upelelezi hapo BoT.

Kitu kingine alichogundua Rais Magufuli ni kwamba kuna baadhi ya wafanyakazi wameazimwa katika taasisi nyengine (secondment), huo ni utaratibu wa kawaida serikali unapokuwa unamuhitaji mtaalamu fulani katika taasisi fulani ya serikali, basi unamuomba mtaalamu yule ukikubaliwa ndio anapata uhamisho wa muda baadae anarudi, sasa ilionekana kuna baadhi ya waheshimiwa wa BoT wanafanyakazi Wizara ya Fedha lakini malipo ya mfanyakazi huyo bado yanatoka BoT moja kwa moja kwenda akaunti yake na sio yatoke BoT yaende kwa Wizara ya Fedha kama wafanyakazi waengine wa wizara hio halafu yaende kwake.

Sasa hilo si jipu ni mambo kawaida kwa kuwa mfanyakazi yule hajahamishwa bali ameazimwa (Secondment), kilichotakiwa kufanya ni kuangalia ni Jee Wizara ya Fedha inamlipa pia mfanyakazi yule au laa?

Hivyo nimuombe Rais Magufuli, kwa hili la BoT aendelee na upelelezi zaidi huku akitaka msaada zaidi kwa watu wa juu wanaohusika na taasisi hiyo ya juu ya nchi, naamini majipu yamo na atayagundua. Lakini endapo kwa kutumia sababu zilizozungumzwa pale juzi, Rais Magufuli atapangua safu ya BoT, basi itakuwa hakuitendea haki taasisi hiyo, na atakuwa yeye ndiye sababu ya kuipaka matope ndani na nje ya nchi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.