MOHAMED Ahmed Sultan pengine linaweza kuwa jina geni kwa wengi na itakuwa vigumu kufahamika kwa haraka bila kutumia jina lililozoelekea na wengi hapa visiwani Zanzibar. Namzunguzia ‘Eddy Riyami, naam, hapa utaeleweka kwa haraka zaidi ni nani unayemzungumzia.

Eddy Riyami halikuwa jina kubwa katika siasa za Zanzibar licha ya kuwa alikuwa ni mmoja ya watu mashuhuri katika kufanikisha mikakati ya ushindi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ukuaji wa jina lake zaidi ukianzia baada kuasisiwa kamati iliyopewa jina la “Kamati ya Maridhiano Zanzibar”.

Hii ni kamati iliyotokana na mazungumzo ya Novemba 02, 2009, Ikulu ya Zanzibar, yakiwahusisha Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi – CUF, Maalim Seif Shariff Hamad na Rais mstaafu wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume.

Ingawa kamati hiyo ya maridhiano haikuonekana kuungwa mkono na upande wa Chama Cha Mapinduzi kutokana na kauli zilizowahi kutolewa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, ambao walionesha waziwazi kutokukubaliana na kamati hiyo lakini ilihusisha wajumbe kutoka CCM na CUF na miongoni nwa wajumbe hao ni Mohammed Ahmed Sultan, ‘Eddy Riyami’.

Na Ally Mohammed
Na Ally Mohammed

Moja ya kazi kubwa walizofanya Kamati ya Maridhiano ni kuwaunganisha Wazanzibari bila kujali itikadi zao, waliifanya kazi hiyo kwa kuanzisha mijadala ya wazi kwa kutumia vyombo vya habari kama vile midahalo, makongamano na mikutano ya hadhara hapa ndiyo kwa kiasi kikubwa jina Eddy Riyami lilipata kukua na kuwa miongoni mwa watu maarufu katika siasa za Zanzibar kwa kizazi cha sasa.
Nakumbuka ilikuwa ni katika kongamano la Kamati ya Maridhiano lililofanyika katika Ukumbi wa Salama katika Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar, hapo ndipo Eddy Riyami alipotangaza rasmi kujiweka pembeni na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kamati ya Maridhiano iliendelea kufanya shughuli zake ingawa haikuwa ikitambuliwa na upande wa CCM na hii ilitokana na msimamo wa kamati hiyo wa kujitangaza kutaka Muungano wa ‘mkataba’ ambao ni kinyume na maoni ya CCM.

Itakumbukwa pamoja na sababu nyingine lakini sababu ya kuunga mkono Muungano wa Mkataba na Zanzibar yenye Mamlaka Kamili ndiyo sababu zilizopelekea kuvuliwa uanachama wa CCM kwa wajumbe wawili wa Kamati hiyo ambao ni miongoni mwa waasisi wa Chama Cha Mapinduzi, Mzee Hassan Nassor Moyo na aliyewahi kuwa mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki (CCM) na Waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mansour Yussuf Himid.

Baada ya hapo majina ya watu waliokuwemo katika kamati ya maridhiano yakawa ni kivutio katika makongamano na mijadala iliyoandaliwa na kamati hiyo, na hapo Eddy Riyami akabatizwa jina jingine la Mzee wa ‘ku-delete’ kutokana na kupenda sana kutumia maneno “delete kabisa” katika hadhara.

Hatimaye Eddy Riyami au Mzee wa ‘ku-delete’ akaingizwa rasmi katika Timu ya Kampeni ya Chama Cha Wananchi – CUF, katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana (Oktoba 25) ambao matokeo yake yalifutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa kile kilichoelezwa kuwepo kwa kasoro nyingi katika uchaguzi huo, Timu hii ya kampeni ya CUF ilifahamika zaidi kama “Timu ya Ushindi” kwa kiasi kikubwa iliendelea kulijenga jina la Eddy Riyami.

Hata hivyo kasi ya umaarufu wa jina la Eddy Riyami ilikua zaidi na zaidi kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii pale siku ya Jumanne, tarehe 16 Februari mwaka huu, kuwa Riyami amepokea barua rasmi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar, akitakiwa kufika bila kukosa Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliyopo Ziwani, Mjini Unguja, siku ya Jumatano tarehe 17 februari, 2016, saa mbili asubuhi bila kukosa.

Barua hiyo ilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na hata katika ukurasa wake wa ‘facebook’ Eddy Riyami aliiweka barua hiyo huku akiiandikia maneno yaliyosomeka “NAENDA KUPEWA CHEO NA WAZIRI Hamad Masauni … MKISIKIA NI KAMISHNA MPYA MTEULE MSOJE SHITUKA! RUNGU ANALO MASAUNI”.

Ingawa barua hiyo haikutaja lengo la kuitwa kwake lakini ilieleza kuwa kuna mambo muhimu yanamuhusu Eddy ambayo Jeshi la Polisi walitaka kuzungumza naye. Eddy Riyami aliitikia wito huo na kufika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar na kuonana na SSP Simon S. Pasua wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID).

Hata hivyo, hakuhojiwa na badala yake alipewa simu na kutakiwa azungumze na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Salum Msangi ambaye alimwambia arudi tena Jumatatu, tarehe 22 Februari, 2016.

Alirudi tena kama alivyotakiwa na alipofika hapo alihojiwa na Polisi na baadae mwanasheria aliyefuatana naye akatakiwa kutafuta wadhamini wawili watakaomdhamini hadi atakapoitwa tena. Wakati mwanasheria wake aliporudi na wadhamini, akaelezwa kwamba Polisi imebadili uamuzi wake na imeamua kumuweka ndani hadi tarehe 23 Februari, 2016.

Mwanasheria na familia yake wakatakiwa kwenda tena Makao Makuu ya Polisi hiyo tarehe 23, saa 3 asubuhi. Walipofika wakaambiwa kwamba DCI kaacha maagizo kuwa suala la Eddy Riyami liachwe kwanza na wao warudi tena saa 6 mchana na hakukuwa na maelezo ya kueleweka kutoka kwa Jeshi la Polisi juu ya kushikiliwa kwake, kwanini anashikiliwa?

Kwanini amekataliwa dhamana? Kwanini polisi hawataki kumpeleka mahakamani? Haya ni maswali yaliyozusha taharuki katika jamii na kuamsha hisia kuwa huenda ni mchezo wa siasa unaofanywa dhidi yake baada ya kuibuka tetesi kuwa kuna njama za makusudi zinazopangwa na Jeshi la Polisi kuwashughulikia wote waliokuwa katika Kamati ya Kampeni ya CUF (Timu ya Ushindi).

Wengi wamehoji wakiwemo wanasheria iweje polisi wamshikilie mtuhumiwa na kumnyima dhamna (haki yake ya msingi kulingana na kosa lake) na kisha wanashindwa kumpeleka mahakamani ndani ya saa 24 kama matakwa ya sheria yalivyo?

Wasiwasi wa tukio la kuwekwa ndani kwa Eddy Riyami na kuhusishwa na sababu za kisiasa kulichagizwa na viashiria vifuatavyo; kwanza tetesi za kuwepo mpango maalumu wa kuwakamata wote waliokuwemo kwenye timu ya Ushindi ya CUF hivyo, kukamatwa kwake akiwa ni miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo kwa asilimia kubwa imeakisi tetesi hizo kwa vile Jeshi la Polisi wameshindwa kumfikisha mahakamni ndani ya siku mbili ukizingatia walimuweka ndani katikati ya wiki.

Pili hata kosa lake limeshindwa kuwekwa wazi na polisi wenyewe hawakuwa na majibu ya kueleweka katika hili na pengine ndiyo sababu iliyowafanya washindwe kumfikisha mahakamani, maana wanampeleka kwa tuhuma gani? Kwa ushahidi upi? Tatu kuna sauti (audio) inayotembea katika mitandao ya kijamii inayosadikiwa ni ya Eddy Riyami wakati sauti za aina hiyo ziko za aina nyingi na wakati mwengine hutengenezwa kwa makusudi kuigiza sauti za watu mashuhuri kuonekana labda ni wao wanaofanya hivyo na hufanywa hivyo kwa lengo maalum.

Nne kuna tetesi pia kwa wakati tulionao yeyote ambae atajitolea na kuonesha kuweka mbele maslahi ya Zanzibar kwanza bila kuyumbishwa basi lolote litakalotokea kwake na zaidi likiwa na mtazamo hasi basi litasambaa kwa haraka sana na kuwafika walio wengi na zaidi watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Jingine na pengine la mwisho, taharuki imekuja kutokana na aina ya mazingira aliyokamatwa yakitawaliwa na usiri mkubwa ukizingatia alikataliwa dhamana, aliviziwa mwanasheria wake alipotoka ndipo akatiwa ndani, familia yake kutomuona na kutofuatwa kwa sheria kwa jumla maana hata mke wake alipofika kituo cha polisi cha Madema alipokuwa akishikiliwa kwa ajili ya kwenda kumuona, hakuruhusiwa kumuona.

Mpaka naandika makala haya, Eddy Riyami yupo nje kwa dhamana ya polisi. Dhamana hiyo ilitolewa siku ya Alhamisi, tarehe 25, Februari, 2016, huku tuhuma zinazomkabili ikiwa bado ni kitendawili na kutia ‘mbolea’ kuwa ni kutumika kisiasa kwa jeshi la polisi dhidi ya wapinzani

Wananchi wanasema kuwa umefika wakati kwa Jeshi la Polisi kufanya kazi zake kitaalamu kama sheria na kanuni zao zinavyoagiza badala ya kuwatumikia wanasiasa na kufanya kazi kwa mihemko ya kisiasa na kuwabambikizia watu kesi ambazo hata wao hawana ushahidi nazo.

Kinyume chake ni kujengeka kwa imani kuwa jeshi hilo lipo kwa maslahi ya kukilinda chama tawala na kuwashughulikia wapinzani wa serikali.

Tanbihi: Makala hii ilichapishwa kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 2 Machi 2016 ikiwa na kichwa cha habari: “Ni nani huyu Eddy Riyami?”

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.