Nassor Ahmed Mazrui

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, ambaye alikuwa ameitwa na jeshi la polisi asubuhi ya leo (Machi 3), ameachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa kwa kile polisi inachosema ni “kauli za uchochezi.”

Mazrui, ambaye alifika makao makuu ya jeshi hilo saa 2:00 asubuhi akiambatana na wakili wake, ndiye aliyekuwa mkuu wa timu ya kampeni ya mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, katika uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, ambao chama chake kinaamini kuwa kilishinda.

Mapema, ulinzi uliimarishwa kwenye mitaa na njia za kuelekea yalipo makao ya polisi, Ziwani. Ujumbe ulikuwa umesambazwa jana mitandaoni kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi kumsindikiza kiongozi wao huyo kwenda polisi, lakini hakuna taarifa za ikiwa waliambatana naye hadi kituoni.

Ingawa hadi sasa hakuna undani wa mashitaka rasmi yanayomkabili kiongozi huyo, lakini Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Hamad Masoud Hamad, aliiambia Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle kwa njia ya simu kuwa walisikia Mazrui angelikamatwa kwa kauli yake aliyoitoa hivi karibuni akiwa Dunga, katikati mwa kisiwa cha Unguja, ambapo alisema CUF imechoka na udhalilishaji na kwamba isingevumilia tena kupigiwa watu wake wala kuharibiwa mali zake na makundi yanayofadhiliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) maarufu kama “mazombi.”

Katika rikodi ya sauti iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuchapishwa hapa Zanzibar Daima, Mazrui anasema kwamba ingelijinda dhidi ya uchokozi, ingawa hatowi wito wa wanachama wa chama hicho kuanzisha mashambulizi yoyote.

Mazrui anakuwa kiongozi wa pili kwenye timu ya kampeni ya CUF kuitwa na kushikiliwa na polisi ndani ya kipindi cha wiki zisizofika mbili. Mwishoni mwa mwezi uliopita, jeshi la polisi lilimshikilia kwa siku tatu mkuu wa ufundi kwenye timu hiyo, Mohamed Ahmed Sultan (Edi Riyami), kwa madai ya kusikika akimtukana Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, katika sauti iliyorikodiwa.

Hata hivyo, walimuachia baadaye kwa dhamana, huku akitakiwa kuripoti tena kituo cha polisi.

Haya yanajiri wakati mitaa ya mji wa Unguja ikishuhudia askari wa vikosi kadhaa vya ulinzi na usalama katika wakati ambapo tarehe ya kile kinachoitwa “uchaguzi mkuu wa marudio” wa tarehe 20 Machi ukikaribia. CUF imekataa kushiriki uchaguzi huo inaouita “muendelezo wa batili” kinachotaka na uamuzi haramu wa kufuta uchaguzi wa 25 Oktoba uliokuwa umekipatia chama hicho ushindi.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.