Dk. John Pombe Magufuli amekuja na misamiati kazi miwili. Na yote kwa bahati imepata umaarufu kiasi cha kutosha. Makala hii si ya kupima ukubwa wa umaarufu wake zaidi inakusudia kutizama juu ya utekelezaji wake.

Utekelezaji wa misamiati kazi hiyo ni katika kutafuta raghba ya kusukuma ilani ya chama hicho ambayo ilikuwa na bango la Hapa Kazi Tu ambalo lilitumika hadi kujulikana na kila mpiga kura kama sio kila Mtanzania.

Na linaendelea kutumika bango hilo hadi leo kwa sababu ndio lebo kuu ya CCM na ndilo ambalo kila mara linawarudisha katika njia ya reli pale ambapo wanakuwa wanaishiwa na pumzi au wanapotea katika utekelezaji wa manifesto ya chama hicho.

Lakini pamoja na bango la Hapa Kazi Tu basi Dk. Magufuli akaja na msemo mwengine ambao nao umekuwa maarufu na umekuwa ukitumika katika kukabili magumu katika jamii na kukabili uozo katika maeneo ya rushwa, ukwepaji kazi, ushindwaji wajibu, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma na mengine kama hayo ambayo yanadumaza maendeleo ya nchi.

Hii ni ile dhana ya kutumbua majipu. Kutumbua majipu imekuwa ndio staili ya utendaji wa Dk. Magufuli na timu yake ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Nchi hii inatumbuliwa majipu usiku na mchana lakini kila uchao mengine mapya yanajitokeza.

Na Ally Saleh
Na Ally Saleh

Hivi sasa kuna Watanzania hawajui chochote na hawaamini chochote zaidi ya kutumbua majipu na kwamba wanajua bila ya Dk. Magufuli majipu hayo yasingetumbuka maana yamekuwepo miaka na miaka na mengine yakitishia hata afya ya taifa la Tanzania, maana jipu lisilotumbuliwa hugeuka kuwa sumu katika damu kwa kuwa usaha haukubaliki kukaa mwilini.

Majipu yametumbuliwa sehemu nyingi lakini kusema kwli hasa ni Dar es salaam ambako ni makao makuu ya majipu yote ya Tanzania. Kusema kweli kwengine kote kuna vipele tu ila majipu kwa maana ya majipu yote yapo Dar es salaam, labda mizizi yake tu ndio itakuwa imetapakaa kwengineko.

Kwa fikra zangu ni kuwa jipu kubwa kuliko yote ambayo hadi sasa yametumbuliwa ni jipu la Umeya wa Dar es salaam. Dar es salaam ni jipu kubwa kwa sababu nyingi tu. Iwe kwa hadhi na haiba, uwezo na fedha, uwepo mkakati na mtapanyiko wake, biashara na uchumi. Almuradi Dar es salaam ni jipu.

Dar es salaam ndio Tanzania Bara kiuwezo. Ni kama kusema California ndio Marekani. Sina takwimu mkononi lakini taasafu kusema kuwa Dar es salaam ina zaidi ya nusu ya uchumi wa Tanzania na kwa hivyo saa zote ni jipu.

Dar es salaam imekuwa jipu kwa miaka mingi kwa maana ni wazi inanokeana kuwa kimwendo uchumi wake haulingani na wala huafanani na kiwango chako cha maendeleo na suala zima la utengezaji ajira na ustawi. Jiji ni jipu na kichaka cha majipu kabisa.

Kwa hivyo Dk Magufuli anajua kuwa mama wa majipu yote ni Dar es salaam ambayo siku zote yapo chini ya CCM. CCM imekuwa ikiyalinda majipu hayo miaka nenda miaka rudi na ubaya zaidi CCM na Dk. Magufuli mwenyewe naamini wanataka kuendelea na majipu hayo.

Lakini CCM na Dk. Magufuli ina khofu kubwa majipu hayo yasijulikane maana yamekaa pahala pabaya, tena pabaya sana. Dk. Magufuli na watu wake wako tayari kuyaficha majipu hayo kwa gharama yoyote ile maana yatapoonekana hadharani wataambuka kabisa.

Pia majipu hayo yatapoonekana hadharani yatafichua siri ya miaka mingi kuwa kumbe kuliko na majipu makubwa tena kwa Kiswahili yale banguzi na ambayo ajabu ya mambo hayakuweza kutumbuliwa kabisa kabisa.

Maana sioni kwa sababu gani nyengine kama si majipu yaliokaa pabaya kwa nini CCM na Dk. Magufuli hawataki kabisa Umeya wa Dar es salaam uende kwa upande wa Upinzani au UKAWA na kufanya kila aina ya uharamu na uharamia kufanikisha nia hiyo ovu.

Na kwa hakika namhusisha moja kwa moja Rais Dk Magufuli kwa sababu analijua hili kwa kila hali na undani kwa vile lazima atakuwa amemuuliza Waziri anaesimamia masuala ya tawala za mikoa na wizara ambayo iko chini yake moja kwa moja.

Pili haiwezekani, Dk. Magufuli asiulize kunani huko Dar es salaam jiji lenye makao yake ya nchi ambapo miezi mitano toka Uchaguzi Mkuu mpaka leo hakuna Meya na akijua umuhimu mkubwa wa kuwa na Meya kwa aina kadhaa ya mistakabali. Yupo wapi Meya hajawaji kuuliza akaambiwa?

Itakuwaje Rais Magufuli asitake shauri hilo lifikiwe tamati? Au jee huku ndiko kutumbua majipu anakokusema yeye kwamba jipu kuu la Dar es salaam lisitumbuliwe maana halitumbuliki kwa kuwa liko pabaya tena pasipoweza kutumbulika?

Itakuwaje Dk. Magufuli haoni hili ni jipu wakati inaharibu taswira na dhana nzima ya demokrasia na utawala bora katika nchi? Na jee Dk. Magufuli yupo tayari kusubiri muda gani jiji hilo la Dar es salaam liwe na Meya wake alichaguliwa na upande ambao unawapiga kura wengi kupitia madiwani wake ambao ni ule wa UKAWA?

Jipu la Dar es salaam litatumbukaje bila ya utaratibu halali wa kura za wajumbe walio halali katika kikao cha madiwani? Dk. Magufuli na CCM yangu wanataka kutuonyesha njia gani nyengine zamani zaidi ya kunyoga demokrasia na wakitaraji jamani UKAWA wakae kimya?

CCM wanaogopa UKAWA wasishike Serikali ya Dar es salaam jiji lenye Ikulu na Wizara zote na kila ofisi kuu ya shirika lolote lile muhimu hapa Tanzania mbali ya mabalozi wote nchini.

Sasa kama jipu liko pabaya na mtu hawezi kulitumbua si uwape watu wengile wakutumbue au walitumbue? Itakuwaje ukaa na jipu kisha ulalamike maradhi na vilio vya usiku au kwa maana ya hapa uwanyoge wananchi kwa huduma mbovu za kila aina?

Bila ya shaka watetezi wa Dk. Magufuli kwa maana ya Serikali yake pia watatetea kuwa Rais anaheshimu utaratibu wa kikatiba na kisheria. Lakini hapa pana Katiba gani na pana sheria gani? Kilichopo ni kuficha jipu na kuficha kwenyewe ndio jipu lenyewe ambalo limekaa pabaya na mwenye jipu hana njia mpaka atumbuliwe.

Kama ilivyosemwa kuwike jogoo kusiwike basi kutakucha na katika hili lifichwe na lilindwe lakini jipu la Dar es salaam litatumbuliwa tu pamoja na kukaa kwake pahala pabaya.

TANBIHI: Makala hii imechapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Mtanzania ikiwa na kichwa cha habari “Jipu linapokaa pabaya”

One thought on “Umeya Dar alama nyengine ya udhaifu wa Magufuli”

  1. Magufuli hawezi kuingilia Umeya kama alivo shindwa kuingilia la Zanzibar sababu hilo linawahusu waswahili (mwambao) wakati yeye ni Raisi wa Bara (Sukumaland) mabwana ccm haijawa tayari kuona mageuzi ya kweli niliwahi kusema wakae tayari kuona ya mageuzi ya kina Gabachev tunaomba asitokee Yestin mwingine kwani walevi maamuzi Yao Hitma pale anpokua Tila Tila

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.