Imepita kama miaka mitatu hivi lakini sitakaa nisahau. Siku hiyo nilikwenda kumfuata baba yangu kwenye mkutano wa CHADEMA eneo la Soweto, Arusha. Wakati huo, mimi sina hata kadi ya chama ila baba yangu alikuwa mwana-CHADEMA ‘damu.’

Nakumbuka ulikuwa ni msiba wa dada mmoja aliyeuwawa kwa kupigwa risasi. Dakika chache baada ya kufika Soweto, polisi walianza kuwatawanya watu uwanjani kwa mabomu na risasi. Nakumbuka walikuwa polisi kama 300 na kidogo.

Baba yangu ni mlemavu, jambo ambalo ndo lilinitia wasiwasi zaidi. Sikuweza kukimbia na kumuwacha. Katika vurumai ile, baba yangu alianguka, nami sikuweza kumnyanyua na badala yake nikamlalia juu yake. Wakati huo polisi walishatufikia. Walianza kutushambulia kwa virungu. Tuliwaomba msamaha nakuwasihi wasimpige baba yangu ni mlemavu. Lakini hawakuwa na huruma. Tulipigwa sana.

Walinivua hereni, pochi yangu ilikuwa na shilingi 75,000 wakazichukua na simu zangu mbili, moja kubwa na nyengine ndogo. Hakika tulipigwa.

Wema Malisa
Na Wema Malisa

Walikuwa wanatupiga kwa awamu – wakitoka hawa, wanakuja hawa. Kwa kuwa nilikuwa nimemlalia baba kwa juu, kila rungu iliyoshuka nilikuwa naipokea mimi. Wakaniambia: “Huyu ni hawara yako si baba yako!” Baba aliwaomba kwa machozi waniache. Akawaambia mimi ni mtoto wake na vitambulisho ataonyesha. Lakini wapi!

Nilianza kupoteza fahamu, sababu nilishavunjika mkono na mguu vyote vya kushoto. Na virungu vingi kichwani. Alitokea mmoja wao akanivua kwa kuchana nguo zangu na kusema “Tunakubaka!” Nilijikojolea kwa maumivu na woga wa kubakwa mbele ya baba yangu mzazi. Wakanizomea: “Cheki limejichafua!”

Mmoja akaja kwa hasira akatunyooshea bunduki, akasema: “Tuwaondoe hawa. Tuondoe ushahidi.” Wakatokea wawili wenye huruma wakamnyang’anya ile silaha na wakaanza kugombana wenyewe kwa wenyewe. Nilijaribu kunyanyuka niombe watusamehe maana nilikuwa nimeacha mtoto mdogo ana miezi kadhaa nyumbani, lakini nikadondoka kifudifudi. Hapo ndo sikunyanyuka tena.

Alikuja dada mmoja, nadhani ni mpelelezi, akawaomba wanipeleke hospitali. Wakachukua machela, nikabebwa kama mzoga kisha nikatupiwa kwenye gari na baba yangu, bila kujali kuwa yeye ni mlemavu. Waliliondoa lile gari kwa kasi ambayo kama lingeanguka basi asingetoka mtu – hata wao wangeokotwa nyama.

Wakati huo bado walikuwa wakitupa risasi huko na huko. Walitufikisha Hospitali ya Mount Meru, nilipokelewa na kwanza kufanyiwa uchunguzi. Mwili ulikuwa kama nyama. Nilikuwa nimevunjika. Nililazwa kwa siku tano. Baada ya miezi kadhaa kwenda kufungua POP mkono ukawa umepinda nikavunjwa tena nakuwekewa chuma katika Hospitali ya Selian. Mguu haukuunga nikarudishiwa POP kwa mara ya pili. Niliteseka sana ukizingatia nilikuwa nanyonyesha.

Nilinusurika na kifo ila nashukuru Mungu baba yangu alikuwa na majeraha kidogo. Nisingekuwepo wangemuua. Hii ni historia ya maisha yangu. Siwapendi polisi na nitamuomba Mungu hata kwenye uzao wangu asitokee polisi.

Habari hizi ziliandikwa kwenye gazeti la Mwananchi. Yapo mambo mengi sana walitufanyia hawa askari siwezi kuyaandika, maana ni mengi hasa pamoja na maneno yao waliyokuwa wanaongea. Fikiria tulianza kupigwa saa 8:00 mchana mpaka saa 1:00 usiku ndio tunapelekwa hospitali.

Mimi naona ni mkono wa Mungu tu ulituweka hai. Ile ilikuwa ni siku ya kifo changu na baba yangu.

2 thoughts on ““Polisi waliniambia watanibaka mbele ya baba yangu mzazi””

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.