Ninapoyaona yanayoendelea kutendwa na jeshi letu la polisi dhidi ya raia, natafakari sana, nikikumbuka mengi na kisha najiuliza faida ya yote haya ni nini? Madaraka tu? Matumizi ya nguvu, ubabe, amri, kipigo, risasi za moto kwa raia maskini asiye hata na rungu. Kwa nini?

Tarehe 1 Machi 2016, gazeti la Mtanzania liliweka picha ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph akiwa amezingirwa na askari watano – wote wakimpa kipigo kwa kuwa eti ameshiriki maandamano yasiyo na kibali. Hivi kulikuwa na ulazima gani wa kumpiga mwanafunzi huyo? Hivi wangemkamata na kumpeleka kituoni bila kumpiga asingefika? Askari watano wenye wenye bunduki munamzingira mwanafunzi mmoja asiye hata na fimbo?

Matukio haya yananikumbusha mwaka 1999, pale kijana Michael Skupya aliyekuwa waziri mkuu wa serikali ya wanafunzi Shule ya Sekondari ya Ufundi Iyunga (Mbeya) alipodaiwa kuuawa kikatili na jeshi la polisi.

Malisa Godlisten
Na Malisa Godlisten

Kwa mujibu wa gazeti la Uwazi lililoripoti habari hiyo kwa kina, kulikuwa kumetokea mgomo shuleni hapo. Askari wakaitwa kutuliza mgomo huo. Wanafumzi wakakimbia baada ya kuona askari. Michael akakimbilia nyumbani kwa mkuu wa shule. Alipofika akapumzika sebuleni. Yule mwalimu akaenda kuwaambia askari kuwa “kiongozi wa mgomo yupo kwangu.”

Askari wakafika na kumpiga sana. Akajeruhiwa sehemu za kichwani na maeneo mengine ya mwili. Akaingizwa kwenye karandinga. Kutokana na maumivu makali ya kipigo akashindwa kusimama. Akaomba akae, akakataliwa. Akavumilia kusimama lakini nguvu zikamuishia, akaanguka.

Askari wakadhani anajifanya tu. Wakampiga mateke ili aamke lakini hakuamka. Wakamkanyaga juu. Kufika kituoni akashindwa kutoka. Badala ya kuwekwa rumande, ikabidi akimbizwe hospitalini. Kufika huko akafanyiwa vipimo na kuonekana ameumia sana sehemu za kichwa. Wakati huo alikuwa ameshapoteza fahamu.

Akalazwa wodi ya wagonjwa mahututi. Hawezi kula, hawezi kuongea, hawezi kupumua vizuri, hajui lolote linaloendelea.. Amepoteza fahamu. Anapumua kwa mashine ya oksijini. Madaktari wakajitahidi kuokoa uhai wake lakini ikaonekana damu ilivujia sehemu ya ubongo kutokana na kipigo, na baada ya siku akafariki dunia.

Baadaye polisi wakatoa taarifa kuwa Michael alikufa kwa kupigwa mawe na wanafunzi wenziwe. Baba yake akaikataa taarifa hiyo na akakataa kupokea mwili wa marehemu. Akaomba uchunguzi ufanywe upya.. Na ndipo ilipobainika kuwa kifo cha mwanawe kilitokana na kipigo cha polisi.

Ni tukio la unyama ambalo siwezi kulisahau kamwe katika maisha yangu. Najiuliza kwa nini polisi mufanye hivi? Nyinyi ni binaadamu  kama sisi, kwa nini musiwe na huruma japo kidogo? Kwa nini munatumia nguvu hata mahali pasipohitajika? Sisi ni ndugu zenu, ni kaka zenu, ni dada zenu, ni wadogo zenu, ni wazazi wenu pia. Kwa nini hamutaki kujali utu wetu?

Siongei haya kwa sababu nawachukia polisi. Hapana. Baba yangu alikua polisi, tena wa cheo kikubwa. Nimezaliwa kwenye kota za polisi, nimekulia huko. Nayajua maisha ya polisi. Lakini naumia kuona polisi wanaumiza ndugu zao ili tu kuwaridhisha watawala.

Hao wanaowatumeni wanawapa nini kinachozidi utu wenu na wa ndugu zenu? Wewe Polisi unayenipiga leo na kunitia ulemavu wa kudumu, umewahi kufikiria kama ningelikuwa mwanao, ungenifanyia hivyo? Askari muliomuua Michael Skupya kikatili, vipi watoto wenu wangeuawa kwa namna hiyohiyo?

Naongea kwa uchungu mkubwa kwa sababu nataka mjiweke kwenye nafasi zetu, mutafakari munayofanya. Najua hamuwezi kukataa amri mnazopewa na watawala, lakini zipimeni amri hizo. Hivi ukiambiwa ukampige mama yako mzazi, utatii kwa sababu tu umeagizwa na watawala?

Mwanamke mmoja aitwae Bhoke Chacha wa Tarime mkoani Mara aliwahi kulalamika kuwa alipigwa na polisi hadi mimba yake kuharibika. Nikajiuliza hivi kweli kulikua na ulazima gani wa kutumia nguvu kwa mwanamke tena mwenye mimba? Kama ana kosa si mumkamate tu na kumpeleka kituoni?

Kwa nini mnajitafutia laana kwa nguvu? Wakati mwingine mnaishi maisha magumu baada ya kustaafu kwa sababu ya laana ya Watanzania wenzenu. Wakati mwingine munakumbwa na mikosi isiyoisha kwa sababu ya laana za Watanzania. Wakati mwingine watoto wenu hawaendelei na hata wakisoma wanaishia kufeli tu kwa sababu ya laana za Watanzania.

Kama umemuua mtoto waMtanzania mwenzio, unategemea mwanao asome na afanikiwe? Jiulize marehemu Michael Skupya angekuwa hai leo angekua wapi? Pengine angekuwa mbunge, waziri au daktari akiwahudumia Watanzania wenziwe na kusaidia familia yake. Pengine alikuwa mtoto anayetegemewa na baba yake, lakini polisi mukamuua kikatili, mukakatisha ndoto zake, mukamshusha kuzimu, na hatimaye Michael akalala mauti.

Kidonda mlichoweka katika familia hii hakitakaa kipone hadi Yesu arudipo kulichukua Kanisa. Mzazi wa Michael (kama yupo hai) unadhani anawaonaje? Anawafikiriaje? Anaumia kiasi gani juu ya mwanawe?

Munadhani maneno yake yatawaacha salama askari waliomuua mwanawe? Munadhani familia za hao askari zinaishi kwa amani? Munadhani watoto wao watafanikiwa? Kamwe huwezi kuua mtoto wa mwenzio, halafu utegemee wa kwako afanikiwe. Laana ya kumwaga damu huwa haiishi. Mungu alimwambia Kaini: “Naisikia damu ya ndugu yako Habili ikinililia kutoka ardhini!”

Nitoe rai kwa askari wetu. Jaribuni kuwa na utu. Kama nilivyotangulia kusema sisi raia wa kawaida ni ndugu zenu, ni kaka zenu ni dada zenu ni wazazi wenu, na ni watoto wenu pia. Simaanishi kuwa musitumie kabisa nguvu, lakini tumieni nguvu pale inapobidi inayostahili tu. Na Sio lazima kila mahali mtumie nguvu. Wakati mwingine, mnahitaji kutumia busara tu na mkafanikisha kazi yenu.

Msitumike kwa faida ya watawala. Msinyanyase raia ili kuwafurahisha watawala. Msimkosee Mungu wenu ili kuwaridhisha watalawa. Hizi mamlaka za dunia zinapita, lakini ipo siku mutahitajika kutoa hesabu mbele za Mungu za mliyofanya duniani. Mtajibu nini?

One thought on “Damu ya Habil yalia kutoka ardhini”

  1. Mada ya nguvu na vipigo vya polisi kwa raia ni mada ndefu inayoendelea kila uchao hivi karibuni Wete Pemba sehemu ya Shengejuu palitokea mtu ambaye nyumba yake ya makuti ilishika moto wa paani sehemu ya kisusi ilikua inawaka akapiga mayowe jirani walipofika wakakimbilia kutaka kuokoa vilokuemo ndani kwa mshangao mkubwa wakakuta vitu vyote vishatolewa tafsiri ya wengi ilikua mwenye nyumba alijuaje kua moto utaivamia nyumba yake hata katoa vitu vyote kabla kupiga Mayowe kilichofuata mtu mwingine alituhumiwa kuhusika Usiku ule ule na kuhukumiwa kwa kushushiwa kipiga cha mbwa koko na kutupwa kilomita 8 m bali ya sehemu ya tukio

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.