Kijana wa CCM

Kama kuna jambo linatuunganisha Wazanzibari licha ya tafauti zetu za kisiasa, ni hiyo hiyo siasa yenyewe. Tunatakhitalifiana kwenye kuyatafsiri mambo fulani fulani kwenye siasa na zaidi kwenye historia ya siasa ya visiwa vyetu. Tunafautiana kwenye maana ya misemo ya kisiasa na matumizi yake, lakini sote tunaitumia misemo hiyo kwenye kuelezea upinzani wetu huo huo.

Mfano mmojawapo ni hii nyimbo maarufu ya kimapinduzi “Sisi Sote Tumegomboka.” Kuelekea vuguvugu la Katiba Mpya tangu mwaka 2012 ilikuwa alama kubwa ya wanaharakati wanaopigania kile wanachokiita “Mamlaka Kamili ya Zanzibar”. Takribani kwenye kila mkusanyiko wao, ilikuwa lazima iimbwe kama vile zindiko na kiapo chao, kushadidia na kuhakikisha dhamira yao.

Nakumbuka kwenye semina moja ya ndani juu ya Katiba Mpya iliyowakusanya viongozi wa SMZ na wawakilishi wa pande zote mbili za kisiasa, wimbo huu uliimbwa kwa ari na hamasa ya hali ya juu. Hiyo ilikuwa mwaka 2012. Lakini punde, baada ya kuona kuwa muelekeo ni kuwa ajenda ya Katiba Mpya kwa Zanzibar ulikuwa ni kuondoa mamlaka makubwa ya Serikali ya Muungano, wajumbe wa CCM wakaanza kidogo kidogo kujitenga na msimamo huo na hivyo na wimbo wenyewe. Badala yake, ukaanza kusikika majukwaani kwao wimbo wa “Mwana wa Nyoka ni Nyoka”, Naibu Katibu Mkuu Vuai Ali Vuai, akiwa kiongozi wa wimbo huo. Hiyo ni muda mchache kabla ya kwenda kwenye Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma na hata baada ya kurejea.

Nikashangaa na nikakaribia kutokwa na machozi, pale siku ya tarehe 23 Oktoba 2015, wakati wa kufunga kampeni zake katika viwanja vya Demokrasia, Kibandamaiti Ungua, mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, alipowaomba waliohudhuria kusimama na kuimba pamoja naye: “Sisi sote tumegomboka kwa ndugu zetu walopotea…”

Ghafla nikaona safu ya hadhira, wazee kwa vijana, wake kwa waume, wanainuka kwa hamasa na raghba. Upande mmoja, ilikuwa alama ya faraja inayoonesha kuwa uzalendo wa Zanzibar unatembea kwenye damu yao. Kichwani nikajenga picha, lau hadhira ya mkutano uliofanywa na CUF siku moja nyuma kwenye viwanja vya Maisara kwa madhumuni hayo hayo ya kufunga kampeni za urais, ingelikutana na hadhira hii ya Kibandamaiti, kisha kwa pamoja wakaimba “Sisi sote tumegomboka”, ingelikuwaje?

Kwamba ungelikuwa muungano wa sauti hilo hapana shaka. Zanzibar ingelizizima au kutikisika kwa sauti kubwa ya pamoja kama hiyo. Lakini je, muungano huo wa sauti ungelimaanisha muungano wa dhamira? Muungano wa maana? Je, mwana-CCM wa Zanzibar akiimba wimbo huo, huwa munapita picha gani akilini mwake? Je, mwana-CUF wa Zanzibar naye akiimba wimbo huo huo, munakuwa na taswira gani anayoivuta?

 

 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.