Serikali ya awamu ya kwanza ya Zanzibar chini ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kwa hakika iliakisi kuitwa serikali. Sikuwepo zama hizo, lakini kwa hadithi za waliokuwepo na manung’uniko wanayolalamikia serikali zilizokuja baadaye zinaonesha ya Karume ilijitahidi kuwa serikali ya Zanzibar kwa ajili ya Zanzibar.

Pamoja na baadhi kuizungumza vibaya serikali hiyo kwa jinsi ilivyopatikana hadi kuundwa kwake, lakini inaonekana ilikuwa ni serikali ya wananchi, iliyoundwa kwa ajili yao. Hadithi nilizowahi kuhadithiwa na bibi na babu zangu, pamoja na hotuba za Hayati Mzee Karume zinanipa picha kuwa alikuwa akiwashirikisha wananchi kwenye baadhi ya mambo muhimu yanayohusiana na maslahi ya taifa.

Japokuwa hakukuwa na chombo cha kuwashirikisha kama ilivyo leo tulipo na wawakilishi na madiwani, lakini alikuwa akiwaitisha watu kwenye mikutano, ambamo akiwaeleza mipango yake juu ya maendeleo ya nchi. Ni kweli Mzee Karume hakuwa na elimu ya chuo kikuu, lakini kwa akili ya kawaida aliyokuwa nayo ukijumlisha na kuishi na watu wa makabila mbalimbali wakati alipokuwa baharia melini na kuzunguka pembe za dunia, aliweza kugundua kwamba kila kitu kina faida na hasara.

Wengi tumesikia hadithi ya mwaka 1972, ambapo inasemekana Mzee Karume aliwaitisha watu mkutano ili kuwaeleza juu ya ujenzi wa nyumba za kisasa kwa wakati huo (Michenzani, Kilimani, Mkoani, Gamba na kwengineko), akisema kwamba “hatuna uwezo wa kutekeleza mipango yote miwili yaani kuagiza chakula na kujenga majumba hayo, kwa kuwa Makaazi yalikuwa na umuhimu wake wananchi wakakubaliana kujengwa majumba hayo huku wakivumilia njaa kwa kuwa chakula kitakuwa kikiuzwa madukani kwa siku maalum na kwa kiwango maalum na pia alisisitiza watu wajisaidie kwa kilimo.

Serikali tuliyonayo sasa imeigawa Zanzibar na hata dunia kwa ujumla kwenye makundi mawili kuhusiana na uhalali na uharamu wake. Mimi nimo kwenye kundi linaloamini kwenye uharamu wa utawala wa sasa baada ya tarehe 4 Novemba 2015, lakini kwa madhumuni ya makala hii, nataka nikubaliane na kundi linalosema kwamba serikali iliyopo ni halali na viongozi wake wote kuanzia Dkt. Ali Mohammed Shein hadi makamo wake wawili na mawaziri wote hata wale waliotangaza kujitowa, wote wapo madarakani kihalali.

Kama ni hivyo basi, kwa nini sasa Dkt. Shein asivae viatu vya Mzee Karume akawashirikisha wananchi juu ya maamuzi haya magumu serikali yetu inayokwenda kuyachukua ziikiwa zimebaki siku 20 pekee kufikia tarehe ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20? Namnasihi Dkt. Shein kufanya hivyo, kwa kuwa uchaguzi huo wa marudio umekataliwa na washirika wengi kwa kusisitiza kuwa uchaguzi ulishafandika tarehe 25 Oktoba 2015.

Sitaki nizungumzie umuhimu wa vyama vya siasa vilivyosusia, lakini napenda nizungumzie wadau wengine wa shughuli za kimaendeleo ambao wao pia wameususia uchaguzi huu wa marudio. Tuwe wakweli katika hili si Zanzibar tu, bali hata Tanzania kwa ujumla bajeti yetu haiwezi kutimia bila kuongezea fedha za wafadhili. Miradi yetu mingi inategemea wafadhili, mfano mdogo tumeona MCC wamegoma kutoa fedha na tayari kuna miradi kadhaa imeshaathirika.

Kuna watu watapinga hili kwa kupigia mfano kwamba Rais John Pombe Magufuli amaefanya makusanyo ya fedha zaidi ya trilioni moja kwa kupitia bandari, hivyo nchi inaweza kwenda bila wafadhili. Anayefikiria hivyo, basi huyo najidanganya. Kama ulikuwa ukifuatilia namna ya makusanyo hayo, basi utagundua kwamba fedha hiyo iliyokusanywa ni fedha ya wa mrithi wake, Jakaya Kikwete, na hivyo ni kusema kwamba ni makusanyo ya miezi kadhaa ambayo hayakuwa yamelipwa. Makusanyo mapya bado hayajajulikana.

Naamini iwapo uchaguzi utafanyika na hawa washirika wetu wakiendelea na msimamo wao, vikwazo kwa nchi yetu vitaibuka, mahusiano yaliyojengeka kwa muda mrefu yatavunjika kwa muda mchache, heshima na sifa njema kwa viongozi wetu wastaafu zitaondoka na hivyo kupelekea wawekezaji kuzidi kupungua.

Mimi, kama kijana wa Kizanzibari, ninamuomba Dkt. Shein awaitishe wawakilishi wa wananchi wazumgumze si kutafuta muafaka wa uchaguzi, bali awaeleze wananchi hasara na faida ya uchaguzi huu wa marudio, ili na wao wawe wamebariki katika kile kitakachotokezea kama alivyokuwa akifanya Marehemu Mzee Karume. Akifanya hivyo, lawama hazitokuwa zako peke yake pindi mambo yatakapochafuka, lakini yakitengenea jina lake ndilo litakaloandikwa kwa wino wa dhahabu.

TANBIHI: Makala ya Ali Mohammed

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.