Familia ya msichana wa miaka 23, ambaye ndiyo kwanza alikuwa anamaliza masomo yake ya Chuo Kikuu nchini Afrika Kusini akiwa tayari mwanaharakati wa chama cha ukombozi cha ANC, Nokuthula Simelane, kamwe haijaweza kuuona mwili wa binti yao tangu akamatwe, kubakwa na kuuawa mwaka 1983. Huo ni mwaka ambao mimi nilikuwa ndio kwanza naingia darasa la kwanza nikiwa na miaka 6 kijiji kwetu.

Maafisa wa polisi wa utawala wa kibaguzi waliohusika na mkasa huo walikuja kukiri baadaye mbele ya Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Askofu Desmond Tutu kwamba ni kweli waliteka na kumtesa Nokuthula, ambaye alikuwa akifanya kazi ya kuwapelekea silaha wapiganaji wa tawi la kijeshi la ANC, Umkotho we Sizwe, lakini walimuachia baada ya kuwapa taarifa walizozitaka na pia kukubali kuwa jasusi wao dhidi ya ANC. Haijulikani ilikuwaje, lakini maafisa hao walikuja kusamehewa baada ya kukiri kwao huko bila ya idhini ya familia ya Nokuthula, ambayo inaamini kabisa kuwa binti yao aliuawa kikatili.

Ijumaa ya leo (Februari 26), maafisa hao wanne wamepandishwa kizimbani na kupatiwa dhamana, lakini masharti ya kuwa wasije wakajaribu kuingilia uchunguzi dhidi yao. Mwendesha mashitaka wa serikali, Luvuyo Mfaku, anasema wana imani kubwa kuwa “ushahidi madhubuti waliokwishaukusanya unaweza kabisa kuyaendeleza mbele mashitaka ya mauaji dhidi yao. Baada ya kucheleweshwa kote huko, baada ya danadana zote, hatimaye Nokuthula, ambaye sanamu yake imewekwa kwenye mji wa Bethal, jimbo la Mpumalanga kwa kuuheshimu mchango wake kwenye mapambano ya ukombozi, ameibuka mbele ya mahakama ya sheria, akitaka haki itendeke kwake.

Mkasa huu una mafunzo makubwa kwa jamii zote ambazo zinapitia kwenye harakati za kudai haki dhidi ya dhuluma, mapambano ya ukweli dhidi ya batili, halali dhidi ya haramu, kama ilivyo Zanzibar yetu. Unasema kwamba licha ya kuchukuwa muda mrefu, lakini mwishoni mwa pango kutakuwa na nuru – kama wasemavyo wanafalsafa.

 

 

One thought on “Mifupa inapoinuka kaburini”

  1. Kwa kweli hicho kisa ndio kwanza nakisikia leo,lakini ni kisa chenye kusikitisha sana na kinatuonesha kuwa haki inaweza kuchelewa lakini haiwezi kupotea. Na kwetu Zanzibar tusione kuwa tumeachwa mkono katika hiki tunachokipigania. Ushindi wa haki mbele ya batil lazma utapatikana, ni suala la muda tu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.