Kwamba amiri jeshi mkuu wa awamu ya nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, anakanusha kuhusika na ‘uhuni’ wa tarehe 28 Oktoba 2015 visiwani Zanzibar, ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha, alitangaza ‘kuufuta’ uchaguzi uliotajwa na waangalizi wote wa ndani na wa kimataifa kuwa “huru na wa haki zaidi kuwahi kufanyika”, ni jambo lililotegemewa. Kwamba Kikwete anatazamia kuwa Wazanzibari – waliopiga kura zao tano siku ya Jumapili ya tarehe 25 Oktoba 2015 na kisha kura hiyo ikaambiwa imekwenda pata-potea siku tatu baadye kama yalivyokwenda maamuzi yaliyokuwamo ndani yake – wamuamini, ni jambo la kuchekesha. Hivyo, mawili hayo yasingelikuwa na nafasi ya kujadiliwa tena.

Lakini yanaambatana na la tatu – ukweli kwamba kuna sababu ambazo zinamlazimisha sasa Kikwete kujitokeza kukanusha shutuma hizo dhidi yake. Hili ni jambo linalowavutia wadadisi kuchimba undani wa mambo. Kiongozi huyu ambaye aliitumia miaka yake 10 madarakani kujijengea sifa za kimataifa, anaonekana kuhofia kupoteza heshima yake hiyo. Kukanusha kwake, kwa hivyo, ni katika vita vyake vya ndani ya nafsi kutaka kushikilia kile ambacho anakiona kinaweza kumpotea hivi punde. Safari za kimataifa zenye ukwasi na heshima kama kiongozi mstaafu aliyefanikiwa. Nani anataka kuzeekea hivyo, baada ya kuishi kwenye kilele cha utukufu kwa miaka 10 mutawaliya?

Si zamani sana tangu Kikwete ajikute akilazimika kukanusha ushiriki wake na wa familia yake katika kashfa za ufisadi na upendeleo wakati akiwa madarakani, kufuatia utawala wa mrithi wake kuibua yale yanayoitwa ‘majipu’ kwenye maeneo mengi ya sekta za umma, na majina ya akina Kikwete kutajwa na vyombo vya habari. Alikuwa anauona upepo unamuelekea sivyo.

Uwezekano ni kuwa na hili la Zanzibar nalo limeshaanza kumlizia bundi mbya kwenye umri wake wa kustaafu. Hivi karibuni, Umoja wa Mataifa ulimpa nafasi ya kuwa mjumbe wa jopo la afya ya uzazi, kisha Umoja wa Afrika nao ukamkabidhi ujumbe maalum katika mzozo wa Libya. Hapana shaka, hizo ni heshima za kimataifa.

Lakini huko huko kwenye mataifa anakokwenda, ushahidi unawasilishwa ukimuweka yeye kwenye nafasi ya juu kabisa kwenye kile kilichotokea Zanzibar, akiwa amiri jeshi mkuu, mwenyekiti wa chama tawala na juu ya yote kiongozi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jumuiya zote za kimataifa zinazohusika na uangalizi wa uchaguzi, sambamba na wafadhili wakubwa wa kimaendeleo wa Tanzania, wameweka msimamo wao wazi kwenye hili – kilichotokea Zanzibar hakikubaliki.

Kama ambavyo kuna wachache waliouamini utetezi wake kwenye “majipu”, Kikwete pia anaaminiwa na wachache kwenye suala la Zanzibar. Wengine hatukuwahi kumuamini tangu siku ya kwanza alipoingia madarakani, sikwambii sasa akiwa ameshayaacha. Hapana shaka, ukosefu huu wa imani unahusiana zaidi na kile tunachoamini kuwa ni siasa ya Muungano kuelekea Zanzibar – siasa ya mkaliaji dhidi ya mkaliwaji.

Nilishayaeleza haya si mara moja wala mbili. Miaka 10 iliyopita, Kikwete alifanya kama ambavyo hivi karibuni alifanya mfuatizi wake, Rais John Pombe Magufuli – kusimama bungeni na kuelezea masikitiko yake kwa kile alichokiita wakati huo ‘mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar’ na kuahidi kuwa atatumia uwezo wake wote kama kiongozi mkuu wa nchi kuhakikisha kuwa anautatua. Nakumbuka ilikuwa tarehe 30 Disemba 2005 kwenye hotuba yake ya mwanzo kabisa bungeni akiwa rais.

Lakini licha ya kupongezwa na waliompongeza kwa ‘uthubutu’ wake huo wa kuyasema hayo kwenye muhimili huo mkuu wa nchi, mimi nilikuwa miongoni mwa wale walioona kuwa katikati ya maneno yake, Kikwete hakuwa hamaanishi anachokizungumza, bali alikuwa akicheza ‘politiki’. Mifano aliyoitumia kuuzungumzia huo mpasuko, yenyewe ilikuwa inaonesha kupasuka kwa dhamira yake vipande vipande. Alitumia migomo ya wakaazi wa kisiwa cha Pemba ambao wanaunga mkono upinzani dhidi ya wenzao wanaounga mkono Chama chake cha Mapinduzi (CCM). Aliutaja kuwa ni mpasuko baina ya Pemba na sehemu nyengine za Jamhuri ya Muungano licha ya Pemba kuwa sehemu ya Jamhuri hiyo na Wapemba kuwa wanaofaidi zaidi kwenye Muungano huo. Alipotoka yeye mwenyewe, akawapotosha na wamsikilizao na wamuaminio.

Kauli kama hizo akazirejea mara mbili ndani ya mwaka mmoja uliofuatia. Kwanza kisiwani Pemba kwenyewe na kisha kisiwani Unguja alikokwenda kuwashukuru wapigakura waliomchaguwa kwenye uchaguzi wa 2005. Akazirejea tena mwaka mmoja kabla ya kuondoka madarakani, pale alipohutubia tena mjini Dodoma,  safari hii likiwa ni katika ufunguzi wa Bunge Maalum la Katiba. Alionya kuwa mfumo wa Muungano wa Serikali Tatu ungeliuvunja Muungano na hivyo kuhatarisha maisha ya Wapemba “walima vitunguu”, kwa msamiati alioutumia yeye.

Nyuma ya hapo, tarehe 25 Januari 2009 akiwa kisiwani Unguja kwenye uwanja wa Kibandamaiti, Kikwete alitumia muda wake jukwaani kuwatisha wale aliowaita “wanaochezea Mapinduzi”. Kama majuzi Rais Magufuli alipotumia kauli ya karaha kuwazungumzia wanaokosoa kufutwa uchaguzi wa Oktoba 25 na kuitishwa wa Machi 20 (waleta fyokofyoko) kwa kuwatisha kuwa atawatumia vyombo vya dola kuwashughulikia, ndivyo siku hiyo naye Kikwete alivyotumia vitisho kwa hao wachezea Mapinduzi: “Kama mtu hajipendi, achezee Mapinduzi aone,” alisema.

Maana ya kuchezea Mapinduzi, kama ilivyo ya kufanya fyokofyoko, inamaanisha kupingana na sera ya Muungano kuelekea Zanzibar. Inamaanisha kujaribu kukiondosha chama cha Kikwete na Magufuli madarakani, hata kwa njia halali iliyotarajmiwa iwe “kura moja mtu mmoja” kila baada ya miaka mitano.

Baada ya mtiririko wa kila kauli ambayo Kikwete amewahi kuisema dhidi ya wanaopingana na siasa za chama chake visiwani Zanzibar, ni rahisi kuunganisha vitojo vitojo na kufahamu kile kilichotokea tarehe 27 Oktoba 2015, pale kituo cha kujumuisha matokeo ya uchaguzi cha ZEC kilipovamiwa na luteka la kijeshi, yeye akiwa Amiri Jeshi Mkuu. Kilichokuja kudhihirika siku moja baadaye hakikuwa cha ajabu tena.

Hivyo, kujipapatua kwa Kikwete kwenye hili hakumsaidii chochote kwa kuwa hawezi kuaminika. Yeye na mfuatizi wake wanapotumia kichaka cha uhuru wa tume za uchaguzi, ni wachache wasiojuwa kile wanachojifichia.

Uhuru wa tume hizo una matomotomo kibao, sio tu kwenye uteuzi wake bali pia kwenye shakhsia zinazoziongoza taasisi hizo. Kwa mfano, Jecha ni mwanachama wa CCM ambaye hadi mwaka 2010 alikuwa mgombea tiketi ya uwakilishi kupitia chama chake jimbo la Amani.Haikuwa ajabu, kwa mfano, kumuona Jaji Augustine Ramadhani – aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa ZEC wakati mmoja – akiingia kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Muungano mwaka 2015. Watu kama hawa wanapokuwa ndio viongozi wa tume za uchaguzi, anasema mwanasheria Awadh Ali Said, hawana haja ya “kuingiliwa uhuru wao” na yeyote, maana tayari wenyewe wanajuwa nini cha kukifanya kwa maslahi ya chama chao.

Kwa hivyo, Kikwete ana kila aina ya uhusika kwenye suala la Zanzibar – kama amiri jeshi mkuu, kama kiongozi mkuu wa nchi na kama mwenyekiti wa chama tawala, ambacho ndicho kilicho nyuma ya uamuzi uliotamkwa kwa kinywa cha Jecha siku ya tarehe 28 Oktoba 2015.

Zanzibar inajuwa hivyo na dunia inajuwa hivyo. Ni Kikwete.

2 thoughts on “Ndiyo Kikwete, ni wewe”

  1. asante sana muandishi na mmiliki wa blog hii,kwani unazidi kunifumbua macho.kikwete tafuta watanganyika wenzako wasiotaka kuujua ukweli na wenye nia kama yako ya kuona damu ya wazanzibari inamwagika huku nyinyi munakula na kushiba na wake zenu.kikwete wewe ndie muhusika mkuu wa zec.hivi nani anaemili jeshi.ni wewew uluiwatuma jeshi kumteka jecha na naibu wake na kumlazimisha afute uchaguzi.mimi nilikjua zamzni huna nia safi na wazanzibari na hata waislamu wenzako wa tanganyika,ila fahamu unajichimbi handaki.usifikirie kwamba iko siku utakuja kuwaomba radhi wazanzibari tukakusamehe,

  2. Sijui nguvu za blog kama hii inauwezo gani kwa wananchi wa visiwa hivi nikiwa na maana kuelimisha kuhabarisha lakini natamani kama ungekuepo uwezo yanayoelezwa yakawafikia jamii yote ya Wazanzibari bila kulenga Imani zao za Kisiasa basi kesho tungeamka sote wenye kufahamu nini Haki ya kuwa Mzalendo hata hivo nategemea na school kumuona Mola awasaidie nyote kufikisha ujumbe na awape ridhaa wapokeaji wote

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.