Je, unajuwa kuwa Ukristo uliingia kwanza Zanzibar kabla ya kusambaa kwenye maeneo yote ya ndani ya Afrika Mashariki na Kati? Hiyo ilikuwa mwaka 1448. Unakumbuka kuwa jengo la Baitul-Ajab la pale Forodhani linaitwa hivyo kwa kuwa ilikuwa ajabu ya kweli wakati huo kwenye eneo lote la Afrika ya Mashariki na Kati? Lilijengwa mwaka 1833. Hapakuwahi kuwepo na jengo kubwa la namna ile, likiwa na umeme na lifti zaidi ya jengo hili. Unafahamu kuwa Zanzibar pia ilikuwa ya kwanza kuwa na treni yake yenyewe? Hiyo ilikuwa mwaka 1879. Umesoma mahala kuwa ni Zanzibar ambako magazeti yalianza kuandikwa na kusambazwa kwa mara ya kwanza ndani ya eneo zima la Afrika Mashariki na Kati? Gazeti la Samachar mwaka 1903. Kwenye siasa pia, tulikuwa wa mwanzo katika Afrika ya Mashariki kufanya uchaguzi kamili mwaka 1957, ambapo chama cha Afro-Shiraz kilishinda viti vitano kati ya sita vilivyowaniwa.

Orodha hii inaweza kuendelea na kuendelea hadi vitabu vikajaa. Lakini pia ukiiangalia Zanzibar ilipo sasa, unaweza kuona namna gani tulikuwa wa mwanzo kuweka rikodi kwenye mengi na kisha pia tunavyokuwa wa mwanzo kwenye kuzivunja rikodi hizo. Sisi ni watu wa kuweka historia. Ndio maana hivi sasa dunia nzima inatutambua kwa tukio la tarehe 28 Oktoba 2015, ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC, Jecha Salum Jecha, aliamua kuufuta uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba akiwa mafichoni na kinyume cha sheria.  Hadi anatoa tangazo hilo, hakukuwa na madai ya kisheria yaliyoulalamikia uchaguzi ule.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohammed

Kiukweli ni kuwa Jecha ameiingiza Zanzibar sio tu kwenye matatizo makubwa sana katika zama hizi, lakini pia kwenye historia mpya na ya ajabu duniani, ambapo hapajawahi kutokea mchezaji mechi anauchezesha mchezo mpaka unamalizika, kisha yeye – na sio wachezaji wala watazamaji – ndiye anayesema kuwa hakuridhika na uchezeshaji wake na hivyo anataka mechi hiyo irejewe.

Sambamba na historia hiyo, tayari Jecha ametangaza kile anachokiita “Uchaguzi Mkuu wa Marudio”, ambao utafanyika tareh 20 Machi mwaka huu, lakini vyama vingi miongoni mwa vyama 14 vilivyoshiriki ule uchaguzi wa 25 Oktoba aliosema ameufuta vimegomea uchaguzi wa Machi 20, na kuviacha vichache kushiriki, ikiwemo CCM.

ZEC waliviandikia barua vyama vilivyoshiriki uchaguzi wa 25 Oktoba kuwataka wathibitishe ushiriki wao katika uchaguzi wa marudio. Baadhi ya vyama hivyo vikajibu kwa maandishi kwamba haviko tayari kushiriki uchaguzi huo kwa sababu za mbali mbali wanazoziamini. Cha ajabu ni kuwa kwa mara nyengine tena, Jecha akajitokeza kutangaza “kutokuwaondoa” wagombea waliotangaza na kutuma barua zao kwa ZEC kwamba hawako tayari kushiriki katika uchaguzi huo wa marudio. Kada huyu wa muda mrefu wa CCM amesema picha za wagombea waliojitoa na nembo za vyama vyao zitatumika kama kawaida katika karatasi za uchaguzi huo wa marudio wa Machi 20.

Tayari mawakili na wanasheria maarufu wameshaikosoa kauli hiyo ya Jecha, wakisema kwamba kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi hakuna mahala panatambuliwa “uchaguzi wa marudio wa namna hio”. Wakili katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, Awadh Ali Said, anasema: “Utaratibu mzima wa kisheria kwa uchaguzi wa marudio wa namna hii haupo, kwa sababu sheria haikuakisi kuwepo kwa ufutwaji wa uchaguzi na marejeo ya uchaguzi yanayotokana na ufutwaji huo.” Lakini anachokifanya Jecha ni muendelezo wa yale yale maajabu yake ya kuzishangaza pembe zote nne za dunia.

Ikiwa kweli uchaguzi huu wa Machi 20 utafanyika kama ulivyopangwa na kupigiwa debe na ZEC na CCM, basi sijui historia ya demokrasia itaiandikaje Zanzibar na Tanzania, kwa kuwa haijawahi hata tume moja ya uchaguzi duniani kumlazimisha mtu lazima awe mgombea. Ndio kwanza mambo haya yanaonekana Zanzibar.

Mbali ya kuwa tayari katika kila jimbo la uchaguzi miongoni mwa majimbo 54 visiwani Zanzibar, kuna mshindi mwenye cheti cha ushindi halali kutoka ZEC hiyo hiyo, licha ya kuwa katika kila wadi kati ya wadi 111 kuna diwani ambaye ana cheti cha ushindi kutoka ZEC hiyo hiyo ya Jecha, pamoja na ZEC na Jecha kuyaelewa hayo, bado wanaitisha uchaguzi katika majimbo na wodi hizo.

Bado navuta picha nyengine ya ziada. Mmoja wa wagombea wanaolazimishwa na Jecha kwamba ni washiriki wa uchaguzi wa Machi 20 ni Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF kwa nafasi ya urais. Kwa sasa inasemekana hayupo nchini, na huenda akarejea baada ya uchaguzi huo kumalizika. Sasa vipi ule utamaduni wa wagombea wakuu kuuzungumzia uchaguzi mara tu baada ya kupiga kura? Lakini muache Maalim Seif.

Njoo kwa Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye atagombea kwa tiketi ya CCM. Sizungumzii la wagombea hao kujipigia kura zao wenyewe, maana hata Dk. Shein hakupiga kura Zanzibar kwenye uchaguzi wa 2010 uliomuweka madarakani, lakini nazungumzia vile atakavyojitokeza yeye mbele ya vyombo vya habari baada ya kupiga kura yake pale Bungi Miembe Mingi na kujilabu kuwa “upigaji kura unakwenda vyema, nina imani kubwa nitashinda kwenye uchaguzi huu.!”

One thought on “Jecha anapoendeleza sifa ya Zanzibar kuwa taifa la kuweka na kuvunja rikodi za kihistoria”

  1. Zanzibar Daima net ni mtandao unaojaribu kuelimisha jamii ya wazanzibari upo uwezekano wenye kushika mpini wa hicho kibutu cha kisu wakajaribu kuukata mtandao huu lkn hiyo ni sawa kufunga Banda farasi kashatoka

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.