Chama cha Wananchi (CUF) kimekanusha vikali kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kwamba chama hicho hakijawahi kujitoa kwenye uchaguzi wa marudio alioupanga kufanyika tarehe 20 Machi na kwamba wagombea wake wote bado ni halali kwa mujibu wa sheria. CUF inasema Jecha analazimisha kuigeuza haramu kuwa halali, lakini hakuna namna yoyote ambayo hilo litafanikiwa.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tarehe: 23 Februari, 2016

Juzi, tarehe 21 Februari, 2016, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alitoa taarifa kuhusu kile alichokiita “Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Marudio unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 Machi 2016”.

Jecha aliwashangaza wananchi wengi pale alipotangaza kwamba eti hakuna chama cha siasa wala mgombea aliyefuata taratibu za kujitoa katika hicho anachokiita “uchaguzi mkuu wa marudio” huku akinukuu Kanuni ya 28 ya Kanuni ya Uchaguzi, 2015 ambayo inataka mgombea au chama kinachojitoa kuambatanisha tamko la kisheria lililotolewa na kutiwa saini na mgombea mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu kwa Mgombea wa Urais na Hakimu kwa mgombea wa Uwakilishi au Udiwani.

Jecha alikwenda mbali zaidi kwa kusema uongo kwamba eti “hakuna chama hata kimoja kati ya vyama ambavyo vimejinadi kuwa havitashiriki katika uchaguzi kilichoiandikia Tume kuwa kimefuta udhamini wa wagombea wake kushiriki katika uchaguzi.” Huu ni uongo na uzandiki. Hata hivyo, hili si jipya tena kwa Jecha. Tokea alipotangaza kwamba eti ameufuta uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 amekuwa akitoa taarifa za uongo ili kuhalalisha kitendo chake hicho haramu. Lakini hiyo ndiyo kawaida ya HARAMU. Ili kulazimisha kuifanya HARAMU ionekane HALALI, huwa unalazimika kufanya HARAMU nyingi ukidhani unahalalisha HARAMU ya kwanza. Hiyo ndiyo hali ya Jecha Salim Jecha tokea tarehe 28 Oktoba, 2015.

Chama Cha Wananchi (CUF) kilimuandikia barua rasmi Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar tarehe 05/02/2016 ambayo ilitiwa saini na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Mhe. Nassor Ahmed Mazrui kuiarifu Tume kwamba hakina mgombea wa Urais kwenye huo unaoitwa uchaguzi wa marudio. Makatibu wa Wilaya wa CUF nao wote waliwaandikia Wasimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya zao kuwaarifu kwamba CUF haina wagombea wa Uwakilishi na Udiwani katika huo unaoitwa uchaguzi wa marudio.

Zaidi ya hatua hiyo, waliokuwa wagombea wa CUF kwa nafasi zote za Urais wa Zanzibar, Uwakilishi na Udiwani kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 waliiandikia Tume kuiarifu kwamba hawautambui huo unaoitwa uchaguzi wa marudio na kwamba wao wanajua uchaguzi mkuu ulishafanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 na ndiyo wanaoutambua.

Lakini kama hiyo haitoshi, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) wa CUF, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui alimwandikia tena Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar barua rasmi tarehe 8 Februari, 2016 kujibu barua ya Tume kwa vyama vya siasa ya tarehe 25 Januari, 2016 kumueleza kwamba CUF haitambui hicho kinachoitwa uchaguzi wa marudio na kwamba kwa CUF uchaguzi ulishafanyika tarehe 25 Oktoba, 2015. Hitimisho la barua hiyo ya CUF ya tarehe 8 Februari, 2016 kwenda kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC lilikuwa kama ifuatavyo:

“Kutokana na sababu na maelezo haya, naomba nisisitize tena kwamba CUF haitambaui kufutwa isivyo halali kwa uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kwa msingi huo huo, haitambui uchaguzi batili mnaouita wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016. Kwa hoja hizo, CUF haithibitishi mgombea yeyote kwa nafasi yoyote kuanzia ya Urais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani kwa ajili ya uchaguzi huo batili wa tarehe 20 Machi, 2016 na kwa barua hii, tunasisitiza tena kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuhakikisha haitumii jina, alama wala picha ya mgombea yeyote kupitia CUF katika karatasi za kura.”

Kwa maelezo haya, tunawaarifu wananchi wote wa Zanzibar, Tanzania na jumuiya ya kimataifa kutambua kwamba Jecha Salim Jecha ametoa taarifa ya uongo ili kuendeleza HARAMU yake aliyoianzisha kwa tamko lake HARAMU la tarehe 28 Oktoba, 2015.

Chama Cha Wananchi (CUF) kinatambua kwamba Jecha Salim Jecha anaendelea kutumikia maagizo ya chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho baada ya kushindwa vibaya sana katika uchaguzi mkuu halali wa tarehe 25 Oktoba, 2015 kwa nafasi za Urais, Uwakilishi na Madiwani kiliona hakina manusura zaidi ya kumtumia yeye kufanya alivyofanya. Hata hivyo, tunamtaka Jecha atambue kwamba HARAMU itaendelea kuwa HARAMU tu, na katu haiwezi kuwa HALALI kupitia taarifa za kizushi na kizandiki anazozitoa.

Kwa hakika inashangaza kwamba baada ya wananchi wa Zanzibar kukiadhibu na kukiangusha vibaya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kura zao halali hapo tarehe 25 Oktoba, 2015, na chama hicho kukimbilia kwa Jecha wakidhani atawanusuru, bado wanalazimisha vyama vyengine kushiriki katika HARAMU yao ya hicho wanachokiita uchaguzi wa marudio ambao hadi leo wameshindwa kusema unafanyika kwa vifungu gani vya Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi wa Zanzibar.

Sisi katika CUF tulidhani ilivyokuwa CCM wameamua kula HARAMU basi wataendelea tu kula HARAMU na hawana haja ya kutafuta washirika wa kula nao HARAMU yao. Tulidhani wao na Jecha wanayemtumia wanatosha kuendelea na HARAMU yao. Tunasisitiza kwamba CUF haitashiriki katika HARAMU hiyo waliyoipanga kuifanya tarehe 20 Machi, 2016. Waendelee tu kujitangazia ushindi wa asilimia 99.9 ya Urais, viti vyote 54 vya Uwakilishi na viti vyote 111 vya Udiwani.

Chama Cha Wananchi (CUF) kikiwa chama makini cha siasa kinachoheshimu Katiba na Sheria kinawahakikishia wananchi wa Zanzibar kwamba kitaendelea kusimamia maamuzi yao waliyoyafanya kupitia kura zao halali walizopiga katika uchaguzi mkuu halali wa tarehe 25 Oktoba, 2015.

Tunamtaka Jecha Salim Jecha na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wawache vitendo vyao vya kukanyaga Katiba na Sheria ya Uchaguzi na wamtangaze mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 ili aungane na washindi waliokwisha tangazwa wa nafasi za Uwakilishi na Udiwani kuunda Serikali mpya ya Umoja wa Kitaifa kuwahudumia Wazanzibari kwa miaka mitano ijayo.

HAKI SAWA KWA WOTE

HAMAD MASOUD HAMAD
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI NA MAWASILIANO NA UMMA – CUF

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.