Kwenye taaluma ya lugha, tunaamini majina mengi (nomino) yanayotumika kuitwa vitu ni matokeo ya unasibu, yaani kubahatisha, kwa kuwa hakuna uwiano wa moja kwa moja baina ya nomino ‘kiti’, kwa mfano, na hicho kiti chenyewe. Kwa nini ng’ombe tumuite ng’ombe na sio punda? Huwa tunajiuliza. Lakini kwenye taaluma ya sheria – ambayo nikiri kuwa si uwanja wangu – inaonekana kunachukuliwa tahadhari ya hali ya juu sana kwa kila jambo linalohusiana na kadhia fulani. Wanasheria huzingatia sio tu lugha inayotumika, bali pia namna inavyotumika, mpangilio wake wa maneno, herufi, na hata alama kama vile kituo kikuu, kituo kidogo na mengineyo.

Na hapa ndipo inapoingia mada yangu ya leo. Mtu mmoja ninayemuhisabu kuwa kiongozi wangu kimaisha amenitumia ujumbe wa maandishi kwa simu usiku huu (Februari 22) wenye maneno haya: “Naomba msaada wako unifahamishe jambo kidogo. Uchaguzi ukifutwa maana yake ni nini hasa? Jecha alitangaza kuufuta uchaguzi na matokeo yake. Je, ukifuta unakuwa unarejea au unafanya mwengine?”

Mimi si mwanasheria, nilimuambia, lakini labda kwa uzoefu wa taaluma za uandishi, lugha na mawasiliano tuliangalie jambo hili kwa kutumia fani ya mantiki – moja ya matawi manne ya taaluma ya falsafa. Hebu chukuwa penseli, raba na karatasi nyeupe. Andika jina lako kwa kutumia hiyo penseli kwenye hiyo karatasi. Kisha lifute hilo jina kwa raba hadi liwe halionekani kabisa. Sasa chukuwa tena penseli, raba na karatasi nyeupe. Andika jina lako kwa kutumia hiyo penseli kwenye karatasi yako nyeupe. Je, unajiona kuwa unafanya marejeo au unaandika tena?

Bila ya shaka, majibu haya yenye swali nayo pia yanataka ufafanuzi mwengine wa kifalsafa kwa kutumia matawi mengine mawili ya falsafa – metafizikia (taaluma ya uwepo au study of existence) na epistimolojia (taaluma ya uelewa, au study of knowledge). Kilichomo akilini wakati mchakato wa pili unafanyika kina umuhimu mkubwa sana kwenye kuelezea maana ya kitu chenyewe na hivyo kukipa jina linalofaa.

Inaelekea sana kuwa kwenye akili ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha, baada ya kulifuta jina lake kwa kutumia raba katika karatasi nyeupe tuliyompa, aliliandika mara ya pili kwa kutumia karatasi ile ile, penseli ile ile na anapitishia mule mule alimokuwa ameandika jina lake mara ya mwanzo. Akilini mwake anarejeshea kama vile tulipokuwa wadogo tulipokuwa tukichukuwa karatasi nyeupe tukaipaka mafuta ya nazi kichwani mwetu, kisha tukaiweka juu ya picha kitabuni mwetu, tukaanza kupitishia penseli kwenye mchoro wa bata. Kukopiria, ndivyo tulivyokuwa tukiita.

Lakini je, huo ndio uhalisia kwa kila mtu? Hapana. Akilini mwetu wengine, tunauona mchakato huu umeanza tena kwa kuchukuwa penseli, raba na karatasi nyeupe. Hivyo tumeanza upya. Inawezekana kuwa kuna muunganiko wa kimawazo kuwa masaa machache nyuma niliandika jina langu kwenye karatasi nyeupe, hivyo ule uzoefu wa kuandika jina langu bado ninao, na basi kwa kiwango cha uzoefu mimi sianzi mwanzo.

Bali kwenye kiwango cha utekelezaji, ninachofanya ni kuanza mwanzo kabisa. Msemo mmoja wa Kijapani kwenye kadhia kama hii unasema: “Hakuna anayeweza kuuchupa mto mmoja mara mbili”, kwa maana ya kuwa mchupaji na mto wenyewe hubadilika kila mara – maji ya mto yanayopita sasa anapochupa sio atakayopita baadaye na hisia alizonazo sasa anapochupa, sizo atakazokuwa nazo baadaye.

Kwa hivyo basi, kuna mambo mawili ambayo Jecha alipaswa kuyafanya: kwanza, kufafanua anachomaanisha katika hiki alichokiitisha kutendeka tarehe 20 Machi. Hata tukiamua kuachana na utata wa kisheria ambao upo, hadi sasa kada huyu wa muda mrefu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) anajizungusha pingu mwenyewe kwa mwenyewe.

Kwa mfano, licha ya kuwa kwenye tangazo lake la tarehe 28 Oktoba 2015 alisema kuwa aliufuta uchaguzi na matokeo yake yote lakini baadaye kwenye Gazeti Rasmi la Serikali akasema alikuwa amefuta matokeo ya uchaguzi huo. Lipi ni lipi? Ikiwa la kwenye Gazeti Rasmi ndilo rasmi, basi kwa vile matokeo ya uchaguzi yanamaanisha kitu cha mwisho kabisa kabla ya kutangazwa kwake rasmi na mshindi kujuilikana, maana yake ni kuwa kila kitu kilichokuwa nyuma ya hapo kinabakia kama kilivyo na hakukifuta. Ikiwa hivyo ndivyo, vipi kuhusu siku, tarehe, saa, wino, kalamu, wapigakura, na yote mengineyo? Kwa nini basi atangaze tarehe mpya ya kufanyika kwa uchaguzi, wakati alichokifuta si uchaguzi bali matokeo yake tu?

La pili, Jecha anapaswa kuusaka msamiati makhsusi wa kukielezea hiki alichotangaza kuwa kitafanyika siku ya tarehe 20 Machi, maana mpaka sasa msamiati aliokuja nao hauakisi kitu chenyewe. Uchaguzi ni mchakato na sio tukio moja. Mkufu wake una vikuku vingi kwa ngazi nyingi pia – ndani ya Tume yake na ndani ya vyama, hadi kwa wananchi na wapigakura. Uteuzi na upitishwaji wa wagombea. Uchukuwaji fomu na urejeshaji wake. Kampeni. Ilani na sera.

Ikiwa yote hayo yanabakia kama yalivyokuwa na hayatahusika na tukio la tarehe 20 Machi, maana yake yanabakia matukio mawili matatu ya mwisho – kupiga kura na kutangaza matokeo (ndani ya masaa 72 baada ya kura). Hiyo maana yake ni kuwa kumbe kinachofanyika tarehe hiyo si uchaguzi, bali upigaji kura tu. Jina muafaka, ninalopendekeza, liwe “Upigaji kura mkuu wa marejeo.”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.