Mimi nashangazwa sana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, na Chama chake cha Mapinduzi (CCM), kwani wamekuwa kama hawajuwi hasa kipi wanachokitaka na kama wanakijuwa, basi hawakisemi wazi tukakijuwa.

Hebu tuwaulize. Nini hasa sababu ya kufuta uchaguzi halali wa tarehe 25 Oktoba? Si ni katika kuhakikisha kuwa CCM haiondoki madarakani kwa karatasi?

Sasa nini lengo la kuitisha uchaguzi mwingine wa Machi 20? Si ni kuhakikisha kuwa CCM inashinda?

Sasa kama ipo njia ya kulipata hilo bila ya gharama yoyote wala usumbufu wowote, ya nini kujitia mashaka?

Chama cha Wananchi (CUF) pamoja na vyama vingine tisa kati ya 14 vilivyoshiriki uchaguzi wa Oktoba 25 vimeshasema hadharani havishiriki uchaguzi.

Jecha na CCM yake wanajua fika kuwa kama CUF haishiriki hakuna mahala popote ambapo watashindwa na chama kingine. Na Dk. Ali Mohammed Shein kasema wazi kuwa kushiriki uchaguzi ni hiyari ya chama. Sasa kwa nini wanalazimisha watu?

Wanaturudisha enzi za Salmin Amour wakati anamrithi Marehemu Idrissa Abdulwakil, ambapo ilikuwa kesi kama mtu haendi kupiga kura. Wazanzibari wenye fahamu timamu walikuwa wanajua kuwa mara baada ya kuondolewa Aboud Jumbe madarakani, waliikataa CCM moja kwa moja na walijua kuwa ni chama cha Tanganyika, wao waalikwa tu. Tuyaache hayo.

Nadhani Jecha na CCM hawana haja ya kupoteza pesa bure. Shilingi bilioni saba zipigwe mafungu wagawane wenyewe. Machi 20 jioni kwa upepo, Jecha akae Bwawani amtangaze Dk. Shein kuwa rais na wawakilishi wake 54 wa CCM.

Yaishe tupate kujenga nchi. Au wazo baya hilo?

TANBIHI: Waraka huu umeandikwa la Abdulfattah Mussa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.