Licha ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kujitokeza tena akisisitiza kuwa hakuna chama wala mgombea hata mmoja aliyefuata masharti yanayotakiwa kuweza kujitoa kwenye uchaguzi wa marudio unaotazamiwa kufanyika tarehe 20 Machi visiwani humo na hivyo ni wagombea halali kwenye uchaguzi huo, chama cha ACT-Wazalendo nacho kimejitokeza tena kushikilia msimamo wake wa kutoshiriki kikisema kuwa hakitakuwa “muhuri wa kuwasafisha wabakaji wa demokrasia.”

TAARIFA KWA UMMA:

Tumekuwa tukipokea simu za waandishi mbali mbali baada ya kauli ya jana ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC),Jecha Salum Jecha kuwa hakuna chama kilichojitoa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika machi 20 mwaka huu.

Msimamo wa ACT-Wazalendo ni kuwa hatutashiriki Uchaguzi huo kama ilivyoazimiwa katika kikao cha kamati kuu cha Februari 14 mwaka huu.

Hatushiriki kwa kuwa tunaamini kuwa hakuna sababu ya kufanyika uchaguzi mwingine nje ya ule uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.

Taarifa hii ya kutoshiriki uchaguzi wa machi 20 mwaka huu imewasilishwa katika ofisi ya ZEC Zanzibar february 9 mwaka huu baada ya wao kututaka tuthibitishe kwa maandishi kama tutashiriki au la.

Hivyo kauli ya Jecha kuwa hakuna chama kilichofuata utaratibu ni muendelezo mwingine wa kutaka kuhalalisha haramu kuwa halali kama walivyofanya katika kufuta uchaguzi wa Oktoba 25.

Kwa kuthibitisha dhamira yetu hii ya kutoshiriki hivi karibuni kamati Maalum ya uongozi Zanzibar ilimsimamisha uanachama ndugu Khamis Idi Lila, aliyedhaminiwa na chama kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar katika uchaguzi uliofutwa kwa “Zengwe” hivyo hatuna mwanachama anayewania nafasi hiyo.

Jecha amezungumzia Sheria ya Uchaguzi na wajibu wa mgombea aliyedhaminiwa na chama kuthibitisha ushiriki wake,huku akiacha kwa makusudi kuainisha udhamini huo ni katika uchaguzi gani.

ACT-Wazalendo haijamdhamini mwanachama wake yeyote kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Machi 20 na hili lilipewa msisitizo katika kikao cha kamati kuu iliyofanyika Februari 14 na taarifa kutolewa kwa umma siku iliyofuata.

Tunaomba wananchi wapuuze ulazimishaji huu wa ZEC kwa kutaka kuionesha dunia kuwa vyama vimeshiriki uchaguzi huo haramu.

ACT wazalendo katika kikao chake cha kamati kuu iliazimia kuwa haitakuwa muhuri wa kuwasafisha wabakaji wa demokrasia kwa kushiriki uchaguzi wa Machi 20.

Abdallah Khamis
Afisa Habari

ACT Wazalendo
22/2/2016

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.