Chama cha Wananchi (CUF) kinasema kinashangazwa na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kuwalazimisha waliokuwa wagombea wa uchaguzi mkuu halali wa tarehe 25 Oktoba 2015 kupitia chama hicho kushiriki kwenye uchaguzi haramu wa tarehe 20 Machi 2016 kwa kisingizio kuwa hakuna mgombea aliyejitoa kwenye uchaguzi huo. Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya, anasema sharti analolitaja Jecha kuwa halikutimizwa na wagombea hao kuweza kweli kujiondoa kwenye uchaguzi wa tarehe 20 Machi ni hoja dhaifu na ya kupuuzwa.

TAARIFA KWA UMMA: CUF HAINA SABABU ZA KULA KIAPO CHA KUJITOA

CUF – Chama cha Wananchi kinashangazwa na hoja dhaifu na zinaonyesha kuwa na utashi wa kisiasa zaidi kuliko Sheria ya Uchaguzi wa Zanzibar au Katiba ya Zanzibar.

Katika mambo ambayo hatupaswi kupoteza muda wa kutoa maelezo ni kauli yake ya jana. Ni kweli wagombea wa CUF na vyama vingine walipaswa kwenda mahakamani kula kiapo cha kujitoa kwenye ugombea wa nafasi mbalimbali, lakini hilo lingekuwa na nguvu kama wagombea hao wangekuwa wamejaza fomu za kugombea kwenye uchaguzi wa Machi 20, 2016.

Wagombea wa CUF na vyama vingine hawakuwa na sababu ya kwenda kujaza fomu na kula kiapo mahakamani kwa kuwa hawakujaza fomu za kugombea uchaguzi huo wa Machi 20, 2016. Wagombea wa CUF na wagombea wa vyama vingine walijaza fomu za kugombea uchaguzi wa Oktoba 25, 2015.

Kulazimisha CUF kuendelea kuwa na wagombea kwenye uchaguzi huo, ni sawa na kumlazimisha mwanamme kutoa talaka kwa mwanamke ambaye hakumuoa. CUF haishitushwi na utaratibu wa mtu anayejitekenya kisha akacheka mwenyewe.

Pamoja na hoja zake zote, je Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, anaweza kutuonyesha fomu iliyojazwa na Maalim Seif Sharif Hamad kwa ajili ya kugombea uchaguzi wa Machi 20, 2016 ili hoja yake ya kumtaka Maalim Seif akajitoe mahakamani kwa kula kiapo iwe na mashiko?

Hawezi kwa kuwa Maalim Seif alijaza fomu za uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 na si ya uchaguzi wa tarehe 20 Machi 2016. Kwa hivyo, si yeye wala si wawakilishi wala si madiwani wenye sababu ya kwenda kula kiapo cha kujitoa mahakamani.

HAKI SAWA KWA WOTE

Abdul Kambaya
Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma CUF TAIFA
Simu: +255 719 566 567

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.