Mwishoni mwa wiki ilopita Rais wa Jamhuri ya Muungano alihutubia Wazee wa Dar es Salaam kuadhimisha siku 100 za sijui uongozi au utawala wake na kutoa matamshi juu ya hali inavyoendela kutokota huku Zanzibar.

Pengine kwa kimya kilichopo kauli ile inanekana kama imepokelewa na imepita lakini sisi tunaoijua Zanzibar na siasa zake ajue atakuja kukumbushwa miaka mingi ijayo kama kauli zilotolewa na wenziwe zenye hasara na maumivu kwa Zanzibar.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Rais wa nchi anabeba sifa nne. Kama Kiongozi Mkuu wa nchi na Kiongozi wa Serikali. Lakini pia kwa tafsiri nyengine yoyote ile yeye pia ndio alama ya nchi (national symbol) na ndio maana kauli yake ndani na nje ya nchi inaheshimika na ina nguvu ya kisheria.

Na Ally Saleh
Na Ally Saleh

Alipaswa, huu ndio ungekuwa uamuzi wake wa mwisho wa suala hili, kuwa kama alama ya kitaifa kwamba hairuhusu mpasuko, mgawanyo, magomvi, ila kwa uamuzi wake wa kuwa wacha nalitote kwa kuiokoa CCM, inaepeleka Zanzibar kubaya sana.

Itakuwa baibai Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Itakuwa baibai umoja ambao Wazanzibari walijirudishia 2009 baada ya siasa za kutengana za miongo mitatu. Kwa kuwa mchuma janga hula na wanawe, Rais Magufuli ajue kuwa mara baada ya Uchaguzi Marejeo kufanyika, hiyo ndio Zanzibar atakayokuwa nayo kwa kubali uroho wa madaraka wa CCM wa Unguja.

Kama si uroho nini? Wamewanyanga wapinzani 1995,2000,2005, 2010 na sasa 2015. Kama si nguvu nini? Kama si kukana demokrasia ni nini? Kama si kuamini wenye mamlaka ya kuongoza ni wao tu, basi ni nini?

Kitu gani kiwafanye Wazanzibari waiamini tena demokrasia?

Ikiwa utakuwapo mwaka 2020 hivi kweli Dk. Magufuli unataraji kutakuwa na uchaguzi huru na haki na demokrasia kuchukua mkondo wake? Hivi ndivyo itavyoiongoza Jamhuri ya Muungano?

Katika hotuba yake ya kufungua Bunge la 11, Rais Magufuli alisema anajua hali iliyoko Zanzibar na atafanya njia za kutafuta suluhu kwa kujua kuwa huo ni wajibu wake na ambao hawezi kuukwepa kwa hali yoyote.

Imepita miezi kadhaa sasa ndipo anaposema kuwa hana la kufanya na hali iliyomfanya atoe matamshi kuwa ataichukulia hatua imebaki kuwa vile vile kama si akhasi. Maana alipotoa kauli ile Bungeni hapakuwa na tamko la Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar kurudia uchaguzi.

Kwa hivyo ndio kusema sio tu Rais Magufuli ameuacha mgogoro wa Zanzibar kama ulivyokuwa lakini pia amebariki kufanyika uchaguzi wa marudio kama ulivyopangwa hapo Machi 20, baada ule wa Oktoba 25 kufutwa bila uhalali na ndio mzizi wa mgogoro wa Zanzibar. Anakwepa dhamana yake kama Rais kwa kujikinga na katiba na sheria.

Na kisha Dr. Magufuli kutoa kauli kuwa asieridhika na yanayoendelea Zanzibar aende mahakamani ni kauli ambayo si ya kutarajia kutoka Rais ambaye watu wote wanamtizama yeye kwa maamuzi. Kwangu ni kama njia rahisi ya kukimbia mgogoro ( easy abdication of duty) na hilo pia kwenye kumbukumbu refu ( long memory) ya Wazanzibari watalitunza.

Naamini anajua kuwa katika masuala haya huwezi kwenda Mahakamani, na jinsi ambavyo Mahakama zetu zilivyo na mlalio basi hata kabla Wapinzani hawajaenda Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Makungu ametoa kauli kuwa wamechelewa kufanya hivyo kisheria na kwamba walikuwa waende ndani ya siku 14 baada ya Uchaguzi.

Kuanzia sasa katika jambo hili mimi si katika wale watakaokuwa wakisema pengine Rais alishauriwa vibaya na watu wako na kuanzia sasa mimi naamini dhamana ya chochote kitakachotokea iko kwake, na kwake peke yake.

Inayonyesha tokea awali hakuwa na nia ya kulitatua tatizo hilo na ndio maana Maalim Seif akamuandikia barua 7 na hakujibu hata mara moja.

Na alikutana nae mara moja huku hali ikizidi kuwa mbaya. Hata hali ilipobadilika na Tume ya ZEC kutangaza Uchaguzi, Rais Magufuli hakuona haja ya kukutana tena na Maalim Seif. Hata mazungumzo yalipovunjika hakuona haja ya kushawishi kurudi tena mezani.
Amejipa muda wake wote kutumbua anachokiita majipu bila ya kujua kuwa Zanzibar ndio mama wa majipu yote ya Tanzania.

Kwa fikra zangu ni kuwa Rais Magufuli amepoteza nguvu ya kimaadili (moral authority) kwa kukubali kuliachia suala hili liende katika njia ambayo bila ya shaka italeta suitafahamu kubwa na kwa siasa za Zanzibar itakuwa ni ya kudumu.

Ila najiuliza hivi Rais Magufuli anajua athari ya Uchaguzi wa Marejeo Zanzibar kwa demokrasia na haiba ya Tanzania mbele ya macho ya kimataifa? Lakini kama hilo si muhimu anajua kovu ambayo itaachwa ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba kutokana na marejeo hayo ya Uchaguzi?

Au kwa kuwa hili litanufaisha CCM ndipo Rais Magufuli anapuuzia au hajali? Namkumbusha tu Rais wangu kuwa yeye ni Rais wa wote na sio CCM tu na kwamba miaka mingi atapokuwa yeye hayupo tena, dhambi ya marejeo haya zitakuwa zake na zitamfuata hata kaburini kwake, CCM hairudii uchaguzi ili ishindwe. Kuwataka CUF kukubali kurudia uchaguzi au kuwatarajia warudie ni kama kumpeleka n’gombe machinjioni ambako hana ujanja isipokuwa kuchinjwa. Tunajua CCM wamekaa vizuri kwa hilo.

Lakini CUF wamejitoa katika Uchaguzi huo wa marejeo na Rais Magufuli anaona ni sawa tu. Kwamba chama kikubwa chenye zaidi ya au karibu ya nusu ya wapiga kura, chenye ufuasi ulioenea kuwa kinasusia uchaguzi na Serikali yake inaidhinisha kuwa uchaguzi uendelee tu kwa sababu ni wao wenyewe wamejitoa.

Kwamba Rais Magufuli anaridhia kuwa nusu ya wapiga kura wasipige kura, si kwa kuwa wamechagua kutopiga kura, lakini ni kwa sababu ya kupinga (protest) basi bado ana wazo la kuubariki (to bless) matokeo ya Uchaguzi huo?

Kwamba Rais haoni kuwa huku ni kuanzisha mgogoro mpya kwa sababu ni wazi CCM itapata kwa vyovyote vile kura ambazo inazitaka, na kujipangia majimbo ambayo inayataka na bado uchaguzi huu uwe na uhalali? Kwamba ZEC inashikilia kutumia picha za wagombea wa CUF ili kuhalalisha kuwa walipigiwa kura, Mheshimiwa Rais analiona ni sawa tu?

Kwamba CUF hawatashiriki katika mchakato mzima na maamuzi kutolewa dhidi yao nalo pia Rais Magufuli analiona ni sawa tu? Washauri wake hawamwambii kuwa mwezi uliopita tu huko Haiti uchaguzi unaofanana na mazingira ya Zanzibar ulifutwa na marejeo nayo yakafutwa. Au kwa kuwa wananchi wa Haiti waliingia barabarani na CUF wanalinda amani?

Katika Uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 CUF ilipata majimbo yote 18 ya Pemba na kupata majimbo 9 ya Unguja. Kuwa uchaguzi wa matokeo utapangwa kwamba CCM ishinde majimbo ya kutosha kuwawezesha kuunda Serikali na kupata thuluthi mbili katika Baraza la Wawakilishi, na bado Rais Magufuli analiona hli ni sawa?

Au hata CCM iyawache majimbo ya Pemba maana itaonekana kichekesho kushinda hata moja, basi kwa yale 36 yaliobakia Unguja CCM haitaweza kupata nguvu na wingi mpaka pia iyapoke baadhi ya majimbo 9 ambayo CUF ilishinda Oktoba 25, basi bado Rais Magufuli anaona tu kutakuwa na uhalali wa Uchaguzi?

Tukija kwenye Urais, ambapo kama asilimia kubwa ya walioipigia CUF pale Oktoba 25, 2015 wakiitikia wito basi ni kuzungumzia wapiga kura karibu ya 200,000 na jee Rais Magufuli bado atakuwa anaona kuwa uchaguzi huo wa marejeo umeenda sawa? Kura ngapi atapewa Maalim Seif katika uchaguzi huu wa marejeo ni jambo ambalo limo katika kupikwa hivi sasa.

Hewallah Dr. Magufuli tumekusikia, lakini hili halijakaa vyema kabisa. Kwa fikra zangu ni kuwa itakuwa gharama kubwa kuendesha Serikali yako katika miaka mitano ijayo ikiwa uchaguzi wa marejeo utaendelea.

Itakupasa utumie muda mwingi kutafuta suluhu ya ndani, muda mwingi kujikosha katika medani ya kimataifa, muda mwingi kuomba kurudishwa katika jumuia ambazo Tanzania itafukuzwa, muda mwingi kuzungumza na wahisani lakini pia muda mwingi kubabiababia uchumi ambao katu Zanzibar ikachafuka au ikikosa demokrasia hautakuwa mzuri kwa Tanzania Bara.

Zanzibar pamoja na udogo wake ina umuhimu mkubwa kwa Tanzania Bara au Tanganyika sio tu kwa kuwa ni nchi na mshirika kamili katika Muungano, pamoja na kuwa hukupata kura nyingi za Rais kutoka kwao, lakini una wajibu wa kikatiba wa kuulinda upande huu usipotee katika machafuko na magumu ya kisiasa.

Rais Magufuli ni bora utafune jongoo leo ule nanasi kesho.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Mtanzania la tarehe 18 Februari 2016

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.