Katika siku za karibuni, Jeshi la Polisi Zanzibar mara kwa mara limekuwa likitoa tahadhari kwa wananchi kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha kuchafuka kwa amani visiwani.

Taarifa ya karibuni ya Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Salum Msangi, imeeleza kwamba polisi wanawasaka watu wanaodaiwa kuendesha kampeni ya vitisho kwa kuchora alama ya X katika nyumba wanazoziona ni za wapinzani wao na wengine wanaosambaza vipeperushi.

Tarifa hizi ni muhimu na kwa kiasi fulani Polisi inafaa kupongezwa kwa hatua hii ya kuwakumbusha wananchi wajibu wao katika kuhakikisha nchi inabakia kuwa na amani na utulivu.

Kwa upande mwingine, wakati polisi ikitoa tahadhari hizi, ni vyema ikaeleza hatua ilizochukua kuwawajibisha waliohatarisha amani kwa kupiga watu mitaani na majumbani, kutia moto majengo, kuvunja nyumba na maduka na kupora fedha na bidhaa.

Ni kwa kufanya hivyo, ndipo wananchi waliopoteza imani na polisi, wataona kwa vitendo kuwa jeshi lao linasimamia imara kaulimbiu ya usalama wa raia na mali zao.

Kwa sasa wapo wanoutilia shaka utendaji kazi wa Jeshi la Polisi, na wanadai linafanya kazi kisiasa badala ya kisheria.

Vijana hawa wanaoitwa janjaweed wa Zanzibar au mazombi ambao Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Yusuf Masauni anatueleza hana taarifa za kuwapo kwao, licha ya habari na picha zao kutolewa kwenye vyombo vya habari pia, wamepiga waandishi wa habari na kuchoma moto kituo kimoja cha redio binafsi.

Polisi nao, wanasema hawana taarifa juu ya kuwapo watu hawa ambao wamekuwa wakionekana hata katika soko kuu la Darajani, Mjini Unguja, nyakati za asubuhi wakipiga watu na kupora fedha, simu, saa na bidhaa.

salim said salim
Na Salim Said Salim

Mara mbili niliwaona wakifanya unyama huu Darajani na walikuwapo askari polisi, lakini linaloshangaza tunawasikia maofisa wa polisi wakitaka wananchi watoe taarifa. Nilidhani hao askari waliokuwapo hapo ndiyo wangekuwa wa kwanza kuwaarifu wakubwa wao wa kazi juu ya vitendo vya hawa janjaweed.

Msangi anatuambia polisi hawana taarifa na inawezekana wanaopigwa ni wahalifu na wanaowapiga ni wahalifu wenzao. Shabbash…hivyo nchi yetu inawaachia wahalifu wapigane na hata wakaribie kutoana roho na polisi inawatazama tu?

Kwa taarifa ya Msangi na maafande wengine wa Jeshi la Polisi, vitendo vya kihalifu vya mazombi, vinaendelea na wiki iliopita vijana hao wanaoitwa Janjaweed au mazombi walivunja msikiti wa mabati uliopo Magogoni kwa Mabata.

Kama polisi watawauliza watu wa eneo la Magogoni jinsi hawa mazombi walivyozusha hofu na kuweka roho juu, utashangaa na kujiuliza hivyo kweli hiyo amani na utulivu unaosemekana kuwapo Zanzibar ipo au vinginevyo?

Polisi wapewe taarifa

Ili polisi kupata habari zaidi, kama kweli hawana taarifa, ni vizuri jeshi hilo likafanya uchunguzi katika hospitali mbalimbali za mjini Unguja na wanapofanya hivyo wafuatane na waandishi wa habari ili wao na jamii kupata maelezo ya kina, juu ya watu wengi waliofika huko kupata matibabu baada ya kupigwa na mazombi.

Taarifa nyingine ni za kuvunjwa maduka maeneo ya Kisauni na Daraja Bovu, ambako mazombi wanasemekana kupora fedha na bidhaa.

Matangazo yenye matusi ya nguoni na ubaguzi na vitisho vinavyoashiria uchochezi, yapo wazi kwenye maeneo mbalimbali na hasa maskani ya CCM ya Kisonge, Mjini Unguja.

Wapo juu ya sheria?

Vijana hao ambao wanajiona kuwa juu ya sheria za nchi wanathubutu hata kuingia katika Uwanja wa Amani, wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi wakiwa na mabango ya uchochezi.

Hivyo, kweli Polisi wanataka kutuambia hawajawaona wale vijana waliobeba mabango yanayochochea ubaguzi katika Uwanja wa Amani au kuona habari hizi na picha katika vyombo vya habari?

Zoezi hili la vitisho sasa linasemekana kuenea Pemba na siyo ajabu tukaanza kuona watu wanasota mahabusu kwa miezi, kama ilivyotokea siku za nyuma, kwa madai ya kuhusika na uhalifu huo na baadaye kuachiwa huru kwa kukosekana ushahidi.

Kama tumeshindwa kuwa waadilifu katika kuheshimu haki na uhuru wa raia siku za nyuma, basi angalau tuache kuudharau hivi sasa. Uonevu, iwe kwa sababu za kisiasa au jambo jingine, siyo kitu kizuri na hatari yake ni kwamba ukifurahia yanapomfika mwenzako leo, utaiona dunia imekugeukia pale yatapokufika wewe.

Duni yetu hii ni hadaa kwani mambo hubadilika na aliye juu huporomoka na kushindwa siyo kutembea, bali hata kutambaa. Tumeona yaliowakuta viongozi mbalimbali, wakiwamo wale walioshika nyadhifa za juu za nchi yetu ambao siku hizi wamepewa adhabu ya kufanya huduma za usafi. Tujifunze.

Jamani, mwenye macho haambiwi tazama na mwenye masikio haambiwi sikiliza. Kutowakamata wahusika na kuwawajibisha kisheria ni dosari iiyo wazi ya Jeshi la Polisi na inayapa nguvu madai yanayotolewa na baadhi ya watu kwamba Polisi Zanzibar inafanya kazi kisiasa.

Sasa tunaambiwa vipo vipeperushi vyenye maelezo ya vitisho. Hili limezusha mjadala na zipo tetesi zisizokuwa na uthibitisho kuwa hii ni mbinu ya kupata kisingizio cha kukamata watu na kuwafungulia kesi bandia.

Vipeperushi

Kwa upande mwingine, kuonekana kwa vipeperushi hivi siyo jambo la kushangaza kwa sababu mara nyingi vimegawiwa vipeperushi, vikiwamo vinavyowakashifu viongozi wastaafu na hatujaona hata mtu kuwajibishwa kisheria.

Hali kama hii inawapa jeuri watu wanaopenda ‘chokochoko’ kuendeleza mwenendo wao huo wa kuwaweka watu katika hofu na wasiwasi kwa vile wanaelewa kuwa watanyamaza na hakuna atakayekamatwa na kuwajibishwa kisheria.

Sitaki kuamini kuwa ni kazi kubwa kuwasaka hawa mazombi, kwani hata ukichunguza baadhi ya picha za vijana hawa ziliosambazwa kwenye mitandao na nyingine kutolewa kwenye magazeti, uwezekano wa kuwatambua watu wawili au watatu ni mkubwa.

Hata ile picha ya waliochukua mabango yanayochochea ubaguzi, inaonyesha wazi sura za vijana waliobeba mabango yale.

Suala ni kwa nini hawajakamatwa na wakitokea vijana wengine kutembeza mabango ya kibaguzi au matusi ya nguoni wataachiwa? Maafande wa Jeshi la Polisi wanapaswa kufahamu kuwa wao kisheria ndiyo dhamana ya usalama wa raia na mali zao na hili hawawezi kulikwepa kwa kisingizio cha aina yoyote ile.

Nchi nyingi ambazo Serikali zake zilijitia ‘pingu’ na kufumbia macho uhalifu wa vijana kama hawa mazombi sasa zinajijutia, hasa baada ya kuona waliohusika kuwachochea vijana hao wanakamatwa na wengine kuburuzwa katika mahakama za kimataifa.

Ni hatari kuiweka nchi rehani mikononi mwa wahuni wachache wanaokuwa huru kupiga watu, kusambaza vipeperushi vya vitisho, kubomoa na kutia moto nyumba na maduka na kupora watu fedha na mali zao, baya zaidi ni pale wahuni hao wanapokwenda mbali zaidi na kukashifu dini na hata kubomoa misikiti kwa kisingizio cha kulinda au kupinga mapinduzi.

Hivyo, tujiulize Mapinduzi ya Zanzibar yana uhusiano gani na nyumba za ibada? Nimesema mara nyingi na ninarudia kuwa watu wanapotaka kufanya mchezo watafute mpira, kete, karata au gololi kuchezea na siyo dini au masuala ya ukabila.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.