Chama cha ACT Wazalendo kimewasimamisha uwanachama viongozi wake wawili wa ngazi za juu visiwani Zanzibar, akiwemo aliyekuwa mgombea wake wa urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 25, kwa kile kinachosema ni kupingana na msimamo wa chama kwa maslahi yao binafsi, baada ya viongozi hao kuiandikia barua Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutaka kushiriki uchaguzi wa marudio wa Machi 20. Soma tamko rasmi lililosainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Zanzibar, Juma Said Sanani hapo chini.

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUSIMAMISHWA UANACHAMA NDUGU KHAMIS IDD LILA NA NDUGU ALI MAKAME ISSA

Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT – Wazalendo) katika kikao chake cha Kamati Maalum ya Zanzibar cha tarehe 19 Februari, 2016 kimepokea taarifa rasmi kuwa aliyekuwa mgombea wa urais wa zanzibar ndugu Khamis Idd Lila kwa kushirikiana na ndugu Ali makame Issa huku wakitambua msimamo wa Chama kwa makusudi wameamua kupingana na msimamo huo kwa maslahi yao binafsi na kukidhalilisha na kuingiza mgogoro usiokuwa na sababu kwa kuandika barua ya kushiriki uchaguzi wa marudio ambao Chama kilishapeleka barua rasmi tarehe 09 Februari,2016 ya kutoshiriki uchaguzi hiuo.

Kwa kitendo chao hicho na kwa mujibu wa Katiba, Kanuni na maadili ya chama Kamati maalum ya Zanzibar imewasimamisha rasmi uanachama kwa mujibu wa katiba ya ACT Ibara ya 11 (2) kuanzia leo tarehe 19 Februri,2016 kwa ukiukwaji mkubwa wa katiba Ibara ya 7(3)(5)(9),ibara ya 10 (2)(c)(d),Ibara ya 22(1)(2)(4).

Kwa mujibu wa Katiba ya ACT Wazalendo masuala yote ya kinadhamu kwa viongozi na wanachama yanashughulikiwa na Kamati za uadilifu za ngazi husika na kwa kuwa kwa sasa Kamati hizo hazijaundwa Kamati ya Uongozi ya Taifa ndio inayoshughulikia na mambo yote ya kinidhamu.

Hivyo jambo hili linawasilishwa mbele ya Kamati ya Uongozi ya Taifa kwa hatua zaidi na kwa taarifa zaidi naambatanisha na tamko la Chama katika kikao cha tarehe 13 Februari,2016 kilichofanyika Dar es Salaam.

Imetolewa leo tarehe 20 Februari, 2016

Juma Said Sanani
Naibu Katibu Mkuu
Zanzibar

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.