ALFAJIRI ya Ijumaa iliyopita, Rais John Pombe Magufuli aliamka na tabasamu ya aina yake. Palipopambazuka alikuwa amekwishatimiza siku zake 100 za mwanzo tangu ashike hatamu za uongozi wa taifa.
Alipojiangalia kwenye kioo alizidi kutabasamu.

Hatujui tabasamu yake ilikuwa ya rangi gani au ya umbo gani lakini ikichezacheza hata kwenye kope za macho yake.
Siku 100 ni nyingi na si nyingi katika uhai wa taifa au katika kipindi cha uongozi wa taifa. Imekuwa mtindo miaka hii kwingi duniani kuziangalia siku 100 za mwanzo za kiongozi mpya kuwa kama zinazoweza kuashiria muelekeo wa uongozi wake.

Hizi za Magufuli zinakanganya. Zilianza kwa mguu wa kheri. Wengi walimwagia sifa alipoonyesha dalili njema kwa ujasiri aliouonyesha. Alishangiliwa kwa hatua zake za kuacha isirafu na ubadhirifu wa fedha za umma, kupiga vita uzembe serikalini na kwa kupasua yale ayaitayo “majipu”.

Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Lakini haikuchukuwa muda huo mguu mwema ukateleza. Hoja yangu ni kwamba si bahati mbaya iliyoufanya mguu huo uteleze. Uliteleza kwa sababu ulikuwa hauna budi ila uteleze kwa vile umekuwa ukizifuata nyayo za uongozi uliotangulia ambazo nazo zilikwishateleza.

Ili asimame imara, Magufuli alihitaji kuukanya na kuachana nao kabisa urathi alioachiwa. Kufanya hivyo anaona muhali na, hata akitaka, hawezi.

Hakika ya mambo ni kwamba amekuwa mateka wa wababe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wenye kuamini kwamba serikali zote mbili, ya Muungano na ile ya Zanzibar, lazima ziendeshwe na chama chao. Hawa ndio wataomkorofisha na hatimaye kulikorofisha taifa zima.

Magufuli analijuwa hilo lakini hana budi ila aicheze ngoma inayopigwa na waliomteua awe mgombea wa urais wa chama chao. Si kwamba analipa fadhila tu lakini pia anatimiza masharti ya kuachiwa uongozi wa taifa.

Sharti moja na kuu kushinda yote ni kuhakikisha ya kuwa Chama cha Wananchi (CUF) katu hakishiki madaraka Zanzibar. Kisingizio kinachotumiwa ni kwamba eti CUF kikishika madaraka kitauvunja Muungano na, kwa hivyo, kuna haja ya kufa au kupona ya kuliepusha hilo.

Kasumba hiyo imewajaa wababe wa CCM ilhali msimamo wa CUF daima umekuwa ni wa kudai muundo wa Muungano ubadilishwe ili uwe wa haki na usawa kwa nchi zote mbili zinazounda huo Muungano.

Hiyo ndiyo sababu kwa nini nasaha za ndani ya nchi na ng’ambo za kutaka matokeo uchaguzi wa Zanzibar wa Oktoba 2015 yamalizwe kutangazwa hazikufua dafu. Nasaha hizo zimekaa kama zinaangukia kwenye masikio mafu ya watawala wetu. Wababe wameazimia kwamba katu hawatoruhusu upinzani utawale.

Si kwamba hawajui ya kuwa walishindwakatika uchaguzi wa urais wa Zanzibar. Hilo wanalijuwa vizuri. Pia wanazijuwa sababu zilizowafanya washindwe Pemba na Unguja. Kwa hili hawana hoja.

Hoja waliyo nayo ni hoja ya nguvu, ya utumizi wa mabavu na wanaelewa kwamba kwa hilo wapinzani hawana bao. Kwa hivyo, wako tayari kufanya watakalo, hata iwe kuhatarisha amani ilimradi wayapate wayatakayo.

Leo wanafanya hivyo Zanzibar, walikokwishazoea kufanya wakatalo,na iko siku watajaribu Tanzania nzima. Watafanya juu chini madaraka yasiwaponyoke. Yote haya ni kwa sababu bado hawajaukubali mfumo wa demokrasia.

Tunapotayafakari yanayojiri Zanzibar ndipo tunapozidi kutambua kwamba mwaka 1992, CCM kiliufanyia ulimwengu kiini macho uamini kwamba kiliukubali kidhati mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa. Kigezo kikubwa cha mfumo huo ni kwamba chama kinachoshindwa katika uchaguzi kinakipisha kilichoshinda kiunde serikali.

Sasa tunaelewa kwamba hata kilipouanzisha tena mfumo huo, CCM kiliazimia kutawala daima dawamu, wananchi wakitaka wasitake. Kiko tayari kuviruhusu vyama vya upinzani viwe na wabunge na wawakilishi, lakini serikali daima zitakuwa mikononi mwake.

Ni dhahiri pia kwamba hao wababe wa CCM hawaijali katiba wala hawaziheshimu sheria za nchi endapo lengo lao la kutawala litakuwa hatarini. Potelea mbali nchi ikivurugika ilimradi CCM iwe madarakani.

Matamshi yao wenyewe wakuu wa CCM yanathibitisha haya. Kwa mfano, mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete, aliyekula yamini kuilinda katiba ya nchi alipoushika urais amethubutu kusema kwamba alimkubalia kichwa upande Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kuufuta uchaguzi.

Yeye angehiyari Jecha amtangazie ushindi mgombea wa CCM wa urais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein.

Ni kusema kwamba angeridhika Jecha angemtangaza Shein rais kwa mabavu. Sasa ni katiba na sheria gani alizoapa kuzilinda kiongozi huyu? Na jeuri hii kaipataje kama si msimamo wa chama chake? Na nyayo zake si ndio hizo anazozifuata Magufuli?

Tunasikia kwamba mabalozi wengi wa kigeni walio Tanzania wanalalamika kwamba hawajakubaliwa maombi yao ya kuonana na Rais. Magufuli alizidi kuwapa kisogo alipoamua kutohudhuria hafla aliyowaandalia yeye mwenyewe kueleza sera ya serikali yake kuhusu mahusiano ya Tanzania na mataifa mengine.
Kuhudhuria kwake kwenye hafla hiyo kungeliwapa fursa mabalozi wenye shauku ya kumuona Rais wasiyemjuwa. Badala yake, Magufuli aliwakilishwa na waziri wake wa Mambo ya Nje, Dakta Augustine Mahiga, amwakilishe na awasomee hotuba yake.

Miongoni mwa yaliyosemwa katika hotuba hiyo ni kwamba Watanzania wengi wangependa kukiona chama cha CUF kinashiriki katika uchaguzi mwingine ili kuthibitisha madai ya ushindi wao na kwamba hakuna “jinsi nyingine” ya kutatua suala hilo ila kukubali kufanya uchaguzi wa marudio.

Mheshimiwa Rais amekosea. Kwanza, si kweli kwamba Watanzania wengi wangependa kukiona CUF kinashiriki katika uchaguzi mwingine na kuufuta wa Oktoba.

Pili, ipo njia ya kutatua suala hili. Nayo ni kuendelea kuyatangaza matokeo ya uchaguzi ambao waangalizi wote wa ndani na kutoka nje ya nchi wamesema ulifanywa kwa haki. Njia pekee ndiyo hiyo ya kuheshimu haki ya wananchi na kura walizokwishazipiga sio kukifanya chama cha CUF kama mtoto mdogo na kukilaghai kishiriki katika uchaguzi usio halali.

Msimamo huo wa Magufuli ulikwishaelezwa na Mahiga hata kabla ya hotuba aliyoisoma kwa niaba yake. Matamshi ya Mahiga yalikuwa ya kusikitisha hasa kwa kuwa anatambua vizuri ya kuwa hakuna cha haki wala sheria inayozingatiwa katika wito wa kurudiwa uchaguzi.

Ya kusikitisha pia ni maagizo ya ajabuajabu yaliyotolewa na wizara yake kama, kwa mfano, amri ya kuwataka mabalozi wa kigeni wasionane na wapinzani bila ya idhini ya serikali na kuwataka wapinzani nao wasionane na wawakilishi wa mataifa ya nje bila ya ruhusa ya serikali.

Sasa naelewa kwa nini Wasomali walikuwa haweshi kumshambulia Mahiga alipokuwa akiishughulikia nchi yao kwa niaba ya Ban Ki-Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Walichoka naye wakaanza kumchora kwenye katuni au vibonzo na kumkebehi katika mitandao ya kijamii na magazeti ya Somalia. Mfano ni kile kibanzo cha Novemba 2011, kilichomuonyesha akiwa kwenye mkutano na viongozi wa Somalia na msaidizi wake wa kike akimvuta tai na kumwambia: “Niachie mimi niendeshe mkutano huu.”

Nakumbuka pia video ya hafla moja aliyohudhuria Minnesota, Marekani, iliyowekwa kwenye mtandao wa YouTube katika jaribio la kumkashifu.

Jumamosi iliyopita, Magufuli, kwa upande wake, alizidi kuwasikitisha wengi kwa hotuba aliyoitoa alipokutana na wazee wa CCM wa Dar es Salaam. Kwenye hotuba hiyo alisema kinagaubaga kwamba hatochukuwa hatua yo yote ya kuzuia uchaguzi wa marudio Zanzibar.

Hilo, kusema kweli, halikunishangaza kwani ilikuwa wazi tangu alfajiri kwamba huo ndio msimamo wake. Kilichonishangaza ni kumsikia akidai kwamba Tume ya ZEC ni huru.

Ameyasema hayo mchana kweupe wakati ulimwengu ukitambua kwamba balaa lote hili lililozuka Zanzibar limeanzishwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Salim Jecha Salim, baada ya kulazimishwa na wababe wa Zanzibar aufute uchaguzi walipotanabahi kwamba CCM imeshindwa katika uchaguzi wa urais.

Tungemuasa Magufuli aache ndaro na lugha ya kitisho cha “kutumia nguvu za dola kuwashughulikia” wananchi kwa “fyokofyoko” ambayo haikutokea. Angelizitumia sasa hizo nguvu za dola kuwanasa magaidi wanaojulikana mitaani kwa jina la “mazombi”. Hawa wamekuwa wakiyashambulia maeneo yenye wafuasi wengi wa CUF na wanakoishi Wapemba.

Inashangaza kumuona Amiri Jeshi wa majeshi yote ya Tanzania akikaa kimya bila ya kuwawajibisha waziri na wakuu wengine wenye kusimamia usalama wa wananchi kuhusu mashambulizi hayo.

Kichekesho ni kumsikia mkuu wa polisi wa Zanzibar akiwa na uso wa kusema kwamba hana taarifa za mashambulio yanayoripotiwa kufanywa na hao waitwao mazombi. Kama huu si upofu basi ni unafik uliopitiliza.

Kinyume na anavyohubiri Magufuli kufanyika kwa uchaguzi wa marudio hakutosaidia kuondoa mvutano wa kisiasa uliopo. Kitachotokea endapo uchaguzi huo utafanyika, na ukifanyika utafanyika kwa mabavu, ni kuutanua mpasuko huo.

Huhitaji kusomeshwa rasmi somo la mantiki kuliona hili. Liko wazi kabisa. Na yale Maridhiano yaliyofikiwa baina ya Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF, yaliyoleta hali ya utulivu na amani, yatakwenda arijojo.

Hilo ndilo walitakalo wababe wa CCM. Watalipata lakini uhasama, chuki na machafuko yataifanya nchi isikalike.

Hali hiyo ya kutisha ndiyo inayohofiwa na wenye busara ya kuona mbali hata ndani ya CCM kwenyewe. Akina Joseph Butiku, Salim Ahmed Salim, Ibrahim Kaduma na Jaji Joseph Warioba sio peke yao ndani ya CCM waliovunjika moyo kwa vitimbi vya chama chao.

Hata wanachama wao wa kawaida wanaona haya kwa vituko vya Zanzibar. Kaduma amesema kwa niaba ya wengi wao wanaotaka chama chao kikubali kwamba kilishindwa Zanzibar.

Viongozi wa CCM walioko Bara wasidanganyike wakafikiri kwamba wanachama wao wa Zanzibar wanaviunga mkono mia kwa mia vitimbi vya wababe wao.

Wengi wameamua kukaa kimya kwani kila mmojawao anaandamwa ajulikane nini msimamo wake. Kadhalika wasisahau kuwa CCM-Zanzibar ni mti mkubwa wenye kuzaa matunda ya fedha zinazotumiwa kuwahonga wakereketwa wake.

Sijui kama wanaoshika hatamu ya uongozi wa taifa hili wanatambua dhamana kubwa waliyonayo. Wala sijui kwa nini hawakioni ulimwengu unachokiona na hawasikii wanayoambiwa na ulimwengu.
Inafaa tu wakumbuke kwamba tawala zinazojikita juu ya misingi ya kibri na dhulma zinapoanguka huanguka kwa kishindo kikubwa.

Na walio juu ya tawala hizo huwa na mwisho mbaya.

Chanzo: Raia Mwema, 18 Februari 2016

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.