Kama unafuatilia jinsi maamuzi na matendo ya siku kwa siku ya Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ‘yanavyoiumba’ Tanzania aitakayo kwa ‘kuiumbua’ ile aliyoachiwa na mtangulizi wake, Jakaya Khalfani Mrisho Kikwete, unatoka na jawabu moja tu – kwamba Rais Magufuli anaamini kuwa bosi wake huyo wa zamani serikalini alikuwa amekosea kwenye kila jambo kwa muda wa miaka kumi ya utawala wake, isipokuwa kwenye suala la moja tu la Zanzibar

Uamuzi wa karibuni kabisa wa Rais Magufuli ni wa Alkhamis (Februari 18), ambapo aliamuru kufutwa kwa vibali vyote vya kuingiza sukari nchini, akisema unaathiri viwanda vya ndani na uzalishaji ambao ungelikuwa na manufaa zaidi kwa taifa. Kwamba sukari imekuwa ikiingizwa kutoka mataifa ya nje na hivyo kuligharimu taifa fedha za kigeni, ilhali nchi ina uwezo wa kutosha wa kuzalisha na kuisambaza pengine hata nje ya mipaka yake, kilikuwa kilio cha muda mrefu cha kambi ya upinzani, hasa kupitia kwa aliyekuwa Mwenyekiti ya Udhibiti wa Hisabu za Serikali Bungeni, Zitto Kabwe.

Haina haja ya kuyataja yale yanayoitwa majipu yaliyotumbuliwa na yanayoendelea kutumbuliwa kwenye maeneo mengine – bandarini, nishati, reli, elimu, afya na kadhalika na kadhalika, ila ni sinema ya kuvutia kuona ambavyo tangu waziri mkuu hadi mawaziri wengine na manaibu wao, wote, walivyojifunga vibwebwe vya ziara za kushitukizia (lakini zinazoandamana na mkururo wa wapigapicha na maripota), orodha isiyosomeka ya fukuzafukuza na maamuzi yasiyo idadi ya zimamoto. Nasikia hilo limeshuka hata kwa wakuu wa mikoa na wilaya. Kila mmoja anatafuta kijipu cha kutumbua, nusu vya uongo, nusu vya ukweli.

Akijitetea juu ya staili hii ya utawala, mwenyewe Rais Magufuli aliwaonya wakosoaji wake kuwa wasimuone yeye dikteta ama mwendawazimu, bali yuko timamu isipokuwa ameikuta nchi (hapana shaka akimaanisha serikali) ikiwa imeoza, naye anataka lazima iende mbele “na itakwenda tu.”

Kwamba Tanzania imeoza (au kwa usahihi zaidi, watendaji kwenye serikali ya Tanzania wameoza) kwa ufisadi wa kila aina, ni jambo linalofahamika na hata kuzoeleka, kiasi cha kwamba ndiyo mtindo wa kawaida. Jinsi ufisadi ulivyozama kwenye damu, basi afisa wa shirika la umma au idara ya serikali huonekana mzembe sana machoni pa wenziwe, ikiwa kwa muda mfupi anaokaa kwenye ofisi hiyo ya umma hakuweza kujijengea himaya ya kiuchumi na ukwasi wa kifedha. Mwizi, kwa hivyo, ndiye shujaa na muadilifu ndiye bwege, na bado ikawa inaaminishwa kuwa “nchi inakwenda mbele” na awamu nne za utawala zilizopita.

Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho ndicho kilichoitawala nchi kwa zaidi ya nusu karne (kikianzia na TANU ya Tanganyika na ASP ya Zanzibar), kimejenga jamii inayoishi na kuogelea kwenye ufisadi. Jamii inayoabudu mafanikio kwa njia ya mkato na inayochukia misingi ya uadilifu, uwajibikaji na haki. Matokeo yake, Tanzania iliyojaaliwa kila neema ya ardhini na baharini, ni miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani. Magufuli anasema umasikini huu hauna maelezo yoyote zaidi ya ukorofi wa walio kwenye nafasi za kuutengeneza uchumi wa nchi, na hivyo ameamua kupambana nao “na lazima nchi itakwenda tu” huku akitutaka tumuombee Mungu aufanikishe “wito huu wa kiroho” kabla hajarudi mbinguni kwa Muumba!

Miradi na mirija mingi ambayo utawala wake inadhani kwamba inavujisha fedha za walipakodi masikini walio wengi na kuziingiza kwenye makasha ya matajiri wachache, sasa inakaguliwa upya na mengine ama kuakhirishwa, kufungwa au kuhamishiwa kwengineko. Miongoni mwao ni Bandari ya Bagamoyo, nyumbani kwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete. Wateule kwenye nafasi za utendaji na uwakilishi, ambao wengine walijipatia nafasi hizo miezi michache tu kabla ya Kikwete kuondoka madarakani, wamejikuta ama wakipoteza kabisa nafasi zao kwenye utawala wa Magufuli au wakipelekwa maeneo tafauti na waliyokuwa nayo. Inawezekana katika fukuzafukuza na hamishahamisha hiyo munafunuliwa tandu kwa kufunikwa n’nge, lakini mkuu ameshajiapiza kuwa “lazima nchi iende na itakwenda tu.”

Kwa hivyo, japokuwa Magufuli amechukuwa takribani nusu na robo ya wanajeshi aliowakuta kwenye kikosi cha mapambano cha mtangulizi wake, hata yeye mwenyewe akiwa mmojawapo, lazima kukiri kwamba staili yake ya kutawala imewaambukiza alioingia nao mstari wa mbele wa mapambano. Ndio maana, mawaziri wale wale ambao chini ya Kikwete walikuwa wenyewe ni “mizigo” kwa lugha ya wakati huo na kwa mujibu wa tathmini ya Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, hivi leo wamegeuka kuwa “watumbuaji majipu” wakubwa, akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaaliwa. Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, ambaye daima alikuwa mwanadiplomasia tu wa Ikulu akifunikwa hata na Salva Rweyemamu, ghafla moja amegeuka kuwa sauti kali ya kutisha ambaye akitokeza tu mbele ya waandishi wa habari (na hujitokeza mara kwa mara), basi ujuwe kuna “jipu” limeshatumbuliwa.

Kwa ujumla, hadi sasa picha unayoipata ni kuwa katika mengi, Magufuli anajaribu kuchora mstari mwekundu baina ya pale utawala wa mtangulizi wake ulipoishia na pale wake yeye unapoanzia, au angalau anapotaka aonekane kuwa ameanzia. Mstari, hata hivyo, hauhusiani kabisa na suala la Zanzibar, ambako mtumbua majipu huyu anayeota kuchaguliwa amiri jeshi mkuu wa malaika baada ya kurudi kwa Muumba, ameshindwa kujipambanuwa utafauti wake na watangulizi wake, Kikwete na Benjamin Mkapa.

Kwa la Zanzibar, Magufuli ni mwana-CCM kama walivyo wana-CCM wengine wote, hasa wanapokuwa viongozi wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama ilivyo kwa Marekani, ambako kubadilisha rais kunaweza kusihusiane kabisa na kubadilika kwa sera ya nje ya taifa hilo, ndivyo ilivyo kwa Tanzania na sera yake ya Muungano kuelekea Zanzibar. Kutoka Mwalimu Julius Nyerere hadi John Pombe Magufuli, Zanzibar ni sehemu inayopaswa kuchukuliwa kama koloni na mshindani ambaye lau panakuwa na nafasi, basi angelizamishwa kwenye Bahari ya Hindi asionekane tena. Lakini kwa kuwa hakuna uwezekano huo, basi kinachopaswa kufanyika ni kuidhibiti kwa nguvu zote za kijeshi na kisiasa kusudi isifurukute, isitukutike.

Kama alivyofanya Mkapa kwa kumimina majeshi na vifaru mwaka 2000 na baadaye 2005 kuwazuwia Wazanzibari kufanya maamuzi juu ya khatima ya nchi yao, ndivyo alivyofanya Kikwete mwaka 2015 na anavyofanya Magufuli hivi leo. Hoja kuu ni kulinda Mapinduzi na kuimarisha Muungano dhidi ya wanaoleta ‘fyokofyoko’, neno ambalo kwa Kiswahili cha Kizanzibari ni matusi ya kitandani (Waswahili husema fyokonyoko). Kwa watawala wa Tanganyika, maana halisi ya kulinda Mapinduzi na kuimarisha Muungano ni kuzuia haki ya Zanzibar kujitawala na kujiamulia mambo yake yenyewe.

Kwao wao, Zanzibar inapaswa kuwa chini ya miguu yao milele, maana kinyume chake ni kuhatarisha siasa za mtawala, ambacho ni kitu kinachowaunganisha wote waliokikalia kiti cha enzi cha Magogoni kwenye kapu moja. Hivyo, Rais Magufuli anaweza kumuona Kikwete alikosea kwenye mradi wa Bandari ya Bagamoyo, anaweza kumuona hakuwa makini kwenye vibali vya sukari, akamuumbua kwenye usimamizi wa bandari, na mengine kadhaa wa kadha yaliyopo na yajayo, lakini kamwe hataweza kumuona alivurunda kwenye “Zanzibar Project”.  Na kwenye hilo, atamsitiri uso wake daima milele.

One thought on “‘Kikwete alikosea yote isipokuwa la Zanzibar’”

  1. Ahsante Ghassani. Umefika kukieleza kunachoonekana kivitendo na kauli za kebehi za viongozi wa Tanganyika katika kuiviza demokrasia.

    Ama katika uteuzi wa maneno wakati viongozi hawa wakiwa majukwani wanaonekana kutumia maneno ya ki-fasiki (kihuni). Mkapa aliwambia “wapinzani na wakome”, katika viwanja vya Lumumba. Kikwete ” wapinzani kazi yao ni kushindiza wakishindwa hudai wameibiwa” katika viwanja vya Kibanda maiti nk. Nae huyu ametumia neno akhas nisingependa kumsikia Rais akitumia neno “fyokofyoko” katika hutuba inayowahusu Watanzania.

    Uchaguzi wa October 25, 2015, una ushahidi wa ushindi wa CUF tokea kituturi kwa kituturi, shehia kwa shehia, jimbo kwa jimbo na matokeo yote yaliotolewa na wasimamizi wa majimbo 54. Wanajitia uzuti na wala hawanao. CCM imekataliwa na Wazanzibari.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.