Zimebaki siku 35 za uchaguzi wa marejeo wa Zanzibar kufuatia ule wa awali uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015 kutangazwa kufutwa matokeo yake na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kinyume na matakwa ya kisheria na kikatiba.Tarehe 28 Oktoba 2015 ilikuwa ndio siku ya mwisho kisheria kwa tume ya uchaguzi kukamilisha zoezi zima la uchaguzi huo, lakini kwa bahati mbaya sana Jecha hakujulikana alikozamia asubuhi nzima hadi mchana wake alionekana katika televisheni ya ZBC na kutangaza kuufuta uchaguzi wote na matokeo yake, kutoka hapo kimya kikatawala hadi kufikia tarehe 22/01/2016, ndipo kwa mara ya pili Jecha akazamuka na kutangaza marudio ya uchaguzi aliyoufuta.

Sambamba na Jecha kutangaza tarehe hiyo ya marudio mnamo tarehe 25 Januari 2016 nae Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC, Salum Kassim Ali, akatoa barua kwa kila chama cha siasa ambacho kilishiriki uchaguzi kwa ngazi yeyote katika uchaguzi wa mwaka jana Oktoba 25 kithibitishe ushiriki wake.

Hivyo kuna vyama kadhaa vikajibu barua ile ya tarehe 25 Januari 2016 ambayo ilisainiwa na Kassim, Chama cha Wananchi (CUF) ndicho kilichokuwa cha pili  kufanya hivyo kupitia Katibu Mkuu wake Maalim Seif Sharif Hamad, barua hio ya Maalim Seif iliwasilishwa ZEC mnamo tarehe 8 Februari 2016, chama cha APPT-Maendeleo ndicho kilichokuwa cha mwanzo kuithibitishia Tume  kwamba hakitoshiriki uchaguzi huo wa Marudio unaotarajiwa kufanyika 20 Machi mwaka huu, ingawa APPT – Maendeleo haikusimamisha mgombea urais lakini ilisimamisha wagombea wa Uwakilishi na udiwani katika baadhi ya majimbo ya Unguja na Pemba.

Lakini cha kushangaza kufikia tarehe 14/02/2016 magazeti yameripoti kwamba “ZEC yagoma kuondoa picha ya Maalim” ambapo taarifa zinasema ZEC imegoma  kuondoa  picha  za  wagombea urais, udiwani na uwakilishi  kutoka  vyama  vilivyotangaza  kutoshiriki uchaguzi wa marudio,ikiwemo jina na picha Maalim Seif Sharif Hamad.

Taarifa hiyo ikaendelea zaidi kwa kumnukuu kiongozi mmoja wa Tume ya Uchaguzi ambaye hakutaka jina lake litumike kwamba, “kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  36  cha  sheria  ya  uchaguzi  namba  11  ya  mwaka  1984, mgombea hawezi kujiondoa kwa utashi wake baada ya Tume kukamilisha kazi ya uteuzi ambayo ilishafanyika kabla ya Oktoba 25 mwaka jana”.

Kitendo cha Tume kuweka mkwala wa kutoondoa picha za wagombea waliotangaza na kuwasilisha barua kwa Tume kwamba hawatoshiriki uchaguzi wa marudio na waondoshwe katika orodha ya wagombea, kwa kweli ni kizungumkuti, kinachohojiwa hapa ni kwamba kwa nini tume waviambie vyama na wagombea wathibitishe ushiriki wao katika barua yao ya tarehe 25 Februari 2016?

Mbali ya hilo la kuthibitishwa kwa wagombea kuna wagombea ambao wamesimamishwa uanachama wao, kuna waliofukuzwa uanachama moja kwa moja katika vyama vyao, ambao kisheria wote hawa hawastahiki kuwa wagombea kwa kuwa hawana vyama wanavyoviwakilisha, ukizingatia katiba ya Zanzibar 1984 na Tanzania ya 1977 zote hazijaidhinisha mgombea huru.

Ikiwa ZEC itasimamia msimamo wake huo wa kuchapisha karatasi za kura zenye picha ya Maalim Seif na wagombea ambao waliitaka tume kuondoa majina yao katika uchaguzi huo wa Machi 20 mwaka huu sambamba na wale wote ambao wamesimamishwa uanachama pamoja na waliofukuzwa chama, kuna khatari ya uchaguzi huo kubatilika, pamoja na kwamba Jumuiya za kimataifa, baadhi ya vyama vya siasa, nchi wahisani na waangalizi wa uchaguzi wa 25 Oktoba mwaka jana wote kwa pamoja wanaamini uchaguzi wa marudio si halali na haukubaliki.

Ni vyema ZEC mkawa waungwana mkatenda haki kwa kukamilisha uchaguzi uliokwisha kufanyika mwaka jana 25 Oktoba ambapo matokeo yake yapo, nashauri hivyo kwa sababu ikiwa ZEC mutalazimisha kurudia uchaguzi,  basi na huo pia kuna hatari ya kuwa batili, kwa kuwa hakutakuwa na saini ya mgombea aliyeshindwa wala mawakala wanaokubalika na  wagombea katika uchaguzi huo, hivyo matokeo yake hayatakubalika na wagombea na endapo wakipinga uchaguzi huo na matokeo yake yote na kuamuliwa kwamba kweli uchaguzi ulibatilika, je ZEC mtarejea uchaguzi mara ngapi?

TANBIHI: Makala ya Ali Mohammed.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.