“Nilipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niliapa kuulinda Muungano wa nchi yetu. Hata bila kiapo, mimi ni muumini wa dhati wa Muungano wetu wa kipekee uliounganisha nchi mbili zilizokuwa huru za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, tena kwa hiari na kwa wino wa kalamu, na si mtutu kama miungano mingine duniani. Naamini kwa dhati ya moyowangu kuwa Muungano wetu ndio umoja wetu, amani yetu na salama yetu. Ninayo kila sababu ya kuulinda na kuuenzi Muungano wetu adhimu na adimu. Ni azma yangukuwaona wananchi wa Zanzibar na Bara wakifurahia matunda ya Muungano wetu badala ya kuwa kikwazo kwaustawi wao na ustawi wa nchi yetu. Aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa siasa hususani vyama vya CUF na CCM tutahakikisha kuwa majaribu ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa salama na amani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie busara na hekima.”

Ni maneno hayo yaliyoifanya hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, ikamilike siku ile ya tarehe 20 Novemba 2015 bungeni. Hotuba yake hiyo mbele ya wageni mbali mbali wa kitaifa na kimataifa ilikuwa kurasa zaidi ya 15, lakini akitumia kurasa mbili pekee kuzungumzia upande wa Zanzibar, ambapo tangu tarehe 28 Oktoba 2015 Jecha Salum Jecha kutangaza kufuta uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 hadi sasa bado Zanzibar Imo katika mgogoro wa kisiasa.

Licha ya kutangazwa tarehe ya marudio ya uchaguzi,  sijui ni kigezo gani alichokitumia rais hadi kufikia maamuzi ya kuizungumzia Zanzibar kwa uchache, yawezekana nibkutokana na udogo wake kieneo na idadi mdogo ya watu ndicho kilichomfanya Rais Magufuli  kufupisha hotuba kwa upande wa Zanzibar au yawezekana ni kuendeleza dharau akifuata mkondo wa waliomtangulia, lakini napenda niseme hakutakiwa kusahau kwamba ni upande muhimu katika kulifanya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likamilike.

Pamoja na kutumia kurasa mbili pekee kuizungumzia Zanzibar, lakini nataka niseme ndio sehemu pekee taifa na mataifa waliyokuwa wakiisubiri kuona Magufuli atatoa ahadi gani kwa upande huo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo kurasa hizo mbili pekee zikatosha kuzifunika kurasa zaidi ya 15 zilizoizungumza Tanganyika.

Hata hivyo, ndani ya bunge tukufu la Tanzania, Rais Magufuli aliweza kuuhakikishia ulimwengu kwamba atashirikiana na CUF na CCM ili kumaliza majaribu ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar. Alikenda mbali zaidi kwa kusema atalifanya hilo kwa salama na amani, na kufika hadi kumkabili Mungu amsaidie, ndipo nyuso za waliokuepo bungeni zilizidi tabasamu na kofi zikarindima kwa wingi zaidi kuonyesha kwamba sehemu hiyo ya hotuba iliwavutia na kuifurahia zaidi.

Kabla ya uzinduzi wa bunge hilo la 11 kupitia hotuba ya rais, tayari serikali ya Rais Magufuli ilishapokea barua kutoka bodi ya “Mellenium Challenge Coperation” – MCC, barua hiyo ya Novemba 19 Mwaka jana, ambayo imesainiwa na Naibu Makamu wa Rais wa Idara ya Operesheni ya Miradi kwa Afrika, Jonathan O. Bloom kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, mfuko huo ulitaka maelezo kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar pamoja na ufafanuzi wa sheria ya uhalifu wa mtandaoni.

“MCC inashukuru kwa uongozi na dhamira yako wakati wa mchakato mzima wa maendeleo ya mradi huu. Msaada wa dola milioni 472 (ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 1 za Kitanzania), una nafasi kubwa ya kusaidia kuleta mageuzi katika sekta ya nishati na kuwaunganisha maelfu ya watu katika gridi.

“Lakini mgogoro wa Zanzibar na ukamataji watu wa hivi karibuni kupitia sheria mpya ya uhalifu mtandaoni umetutia wasiwasi.

“Kama ujuavyo, mataifa washirika wa MCC wanapaswa kuendeleza na kuonyesha dhamira ya utawala bora, ambayo ni pamoja na kufuata misingi ya demokrasia na kulinda uhuru wa kutoa mawazo.

“Hata hivyo, matukio ya karibuni yanaifanya MCC na wadau wetu kujawa na maswali kuhusu dhamira hiyo,” ilisomeka  barua hiyo ya MCC.

Mbali ya barua hio ya MCC katika mkutano wake wa mwanzo na mabalozi wa pamoja wawakilishi wa mashirika ya kimataifa waliopo nchini,  waziri wa Magufuli anaehusiana na Wizara ya  Ushirikiano wa kimataifa Balozi Augostino Mahiga alisikika
Pamoja na kueleza kwamba kilichosababisha mgogoro wa uchaguzi utokee Zanzibar kwamba ni utamaduni uliopo Zanzibar lakini pia aliahidi kutatua mgogoro huo.

Sasa leo hii sioni kama ni kosa pale ambapo mashirika ya kimataifa, mabalozi wa nchi za nje, washauri wa mambo ya siasa, Watanganyika na Wazanzibari wapenda haki na amani wakiulizia kuhusu ahadi zako za kuutatua mgogoro wa kisiasa na kikatiba wa Zanzibar ulizotoa kupitia mdomo wako na midomo ya mawaziri na wasemaji wako.

Ikiwa kuulizwa juu ya  ahadi zako hizo ni “fyokofyoko” kama ulivyodiriki kutamka tarehe 13 Februari 2016 mbele ya Wazee wa Dar es Salam, basi Rais Magufuli hakupaswa kunyooshea watu vidole na kuwatishia amani na kuahidi kuwabomoa kwa mizinga Wapemba na Waunguja, kwa kuwa ni Rais Magufuli mwenyewe ndiye ulietajitayarishia “fyoko fyoko” hizo.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ali Mohammed Ali.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.