Tunapoizungumzia Tanzania na diplomasia, tutakubaliana kwamba  ilikuwa  kwa miaka mingi  ya ya utawala wa Mwalimu Julius Nyerere na nafasi yake katika siasa za kimataifa na  hasa panapohusika na msimamo wa nchi zinazoendelea za Ulimwengu wa Tatu mkabala wa  mataifa  ya magharibi. Pindi  yaliojiri  Zanzibar kabla ya mapinduzi na baada ya Mapinduzi yasingetokea, basi huenda ama  nafasi hiyo ingekuwa ya  Tanganyika na Zanzibar au ya Zanzibar peke yake.

Ninasema ya  Tanganyika na Zanzibar,  kwa sababu tukiweka utashi wa kisiasa pembeni, Zanzibar ilikuwa na kiwango kikubwa cha  elimu na wasomi ukilinganisha na idadi yake kuliko Tanganyika.  Zanzibar ilikuwa na wasomi wengi wanawake na ni  miongoni mwa nchi za kwanza  barani Afrika kutuma wanafunzi wa kike katika vyuo vikuu nchi za nje , vikiwemo vya Uingereza. Pili mwamko wa siasa ulikuwa mkubwa visiwani kuliko Bara kabla ya Mapinduzi ya 1964 na muda mfupi baada ya Mapinduzi hayo.

Miongoni mwa vijana wa Kizanzibari wa wakati huo ni Salim Ahmed salim aliyeteuliwa kuwa balozi baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akiwa na umri wa miaka 22 tu.  Vijana weng wakati huo, akiwemo Marehemu Balozi Mohamed Ali Foum, Ahmed Hassan Diria, Abdul-Rahman Mohamed Babu, Khamis Abdullah Ameir, Ahmed Badawy Qullatein, Abdullah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na wengine, walikuwa na mwamko mkubwa wa kisiasa.

Nilizungumzia  neno kuweka kando “utashi wa kisiasa“ kwa makusudi, ili kuonyesha hicho nilichokiita kukomaa kisiasa na mapema kwa Wazanzibari kuliko Watanganyika.  Kwa mtazamo wa hao niliowataja  baadhi walikuwa ni Wana Afro Shirazi na wengine Wana Umma Party  au maarufu “makomredi” waliojiengua kutoka  Chama cha Hizbu –Zanzibar Nationalist Party, ZNP,  kwa sababu  ya tofauti  kimtazamo. Ni muhimu pamoja na hayo kukumbusha kwamba  ZNP, ambayo waasisi wake (na naomba radhi kwa kutumia urangi au ukabila) hawakuwa  Waarabu kama inavyopotoshwa na viongozi walioko madarakani hii leo, walikuwa ni Waswahili kabla ya kuongozwa baadaye na Ali Muhsin ambaye ni chotara aliyechanganya Uarabu, Umakonde na Umanyema.

Sawa na ilivyokuwa ASP, ZNP pia kilikuwa na watu wa  asili mbali mbali, kama ilivyojengeka jamii ya Wazanzibari. ZNP ilikuwa na muelekeo wa siasa za kizalendo na kimaendeleo na unaposoma historia ya siasa za Zanzibar bila kuipotosha, utaona jinsi Ali Muhsin alivyokuwa karibu na wanasiasa wazalendo waliopigania uhuru kwengineko Afrika kama Joshua Nkomo wa  Rhodesia Kusini, ambayo leo ni Zimbabwe, au hata Kwame Nkurumah wa  Ghana, sawa na  alivyokuwa  Abdulrahman Babu ingawa upeo wake kimataifa ulikuwa mkubwa zaidi tangu hata  kabla hajajiengua  na kuunda Umma Party.

Ali Muhsin, kwa mujibu wa watu waliokuwa karibu naye, hakupendelea kuwepo na ufalme na alivutiwa sana na  siasa za kiongozi wa Misri, Gamal Abdel Nasser. Kwa hakika, alitaka Zanzibar iwe hatimaye Jamhuri.  Kwa  wanaoimba kila uchao  wimbo wa  Waarabu na Usultani, swali ni  Zanzibar ingekuwaje Jamhuri bila ya kuondoa Usultani ? Kwa hakika mgawiko  kati ya  waliokuwa na fikra na mtazamo wa siasa za kimaendeleo ndani ya ZNP na wahafidhina ulitokana na wale mabwanyenye kutaka kutwaa  chama hicho na kuwa na usemi katika uongozi na mustakbali wake. Hiyo ni sehemu moja ya sarafu ya kile kilichofungua njia ya mambo kwenda kombo  hadi kutokea Mapinduzi.

Lakini yaliyopita si ndwele, tugange yajayo kwa kuyaangalia mapinduzi  na hapa ilipo Zanzibar leo. Huenda  pasingekuwepo na Muungano wa haraka au hata Muungano wa serikali tatu, Zanzibar  isingekuwa hapa ilipo leo na hasa  isingefanywa njama ya kuwapeleka wanasiasa  wote mahiri Bara na  utawala kuangukia mikononi mwa ushawishi wa  waliojita “Kamati ya Watu 14” na waliodai kuwa ndiyo hasa chimbuko la mapinduzi, wakiwemo  Seif Bakari, Saidi Washoto na Hafidh Suleiman “Sancho.“

Nyerere alihakikisha kina Abdul-Rahman Babu, Hasnu Makame, Idris Abdul Wakil na wanasiasa waliosoma wanahamishiwa Tanganyika kujiunga na Serikali ya Muungano, huku sera yake ya “Serikali Mbili” iliyoambiwa inaipa Zanzibar mamlaka yake ya ndani, ikiwapa nguvu kina Seif Bakari na kumtia hofu  Mzee Abeid Amani Karume aliyeanza kutawala kwa mkono wa chuma.  Yaliyotokea yakiwemo, mauaji, watu kupotea , ndoa za nguvu na kadhalika yanafahamika.

Yaliopita si ndwele, labda kutokana na kile kinachotajwa kwamba “mapinduzi ni mchakato na hufikia hadi kula wanamapinduzi wenyewe“, ndipo wanamapinduzi waliojaribu kupinga kilichokuwa kikifanywa na Seif Bakari na genge lake kwa kumdhibiti Karume, waliuwawa. Hao ni pamoja na Abdullah Kassim Hanga, Abdelaziz Twala, Idrisa Saddallah na Othman Shariff.

Hasara kwa diplomasia

Tangu matokeo ya uchaguzi wa Oktoba yalipofutwa na  Mwenyekiti wa  Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha, kwa kisingizio  cha hitilafu kubwa, wakati lilikuwa ni shinikizo la Chama cha Mapinduzi CCM baada ya kuonekana kimeshindwa, wito umezidi kutoka pembe mbalimbali kutaka uamuzi wa Wazanzibari uheshimiwe . Jumuiya ya kimataifa,  yakiwemo mataifa  wafadhili, imetamka wazi kwamba haikubaliani na  marudio ya uchaguzi, kama ilivyotangazwa na Jecha kuwa ni Machi 20. CCM imeshangiria, kana kwamba  sio mpangaji wa  njama yote hiyo ikimburuza Jecha kwa jina eti la Tume iliyogawika.

Baada ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Tanzania  Augustine Mahiga kuzungumza kwa kujiamini kuwa  Rais John Magufuli hawezi kuingilia  mgogoro wa Zanzibar kwa kuwa  visiwa hivyo vina mamlaka yake, tume yake na kadhalika, alikwenda umbali wa kuwataka mabalozi wa kigeni watakaokutana na viongozi wa kisiasa wa upinzani au asasi zisizokuwa n za serikali lazima wapate kibali cha wizara ya nje.

Kwa mshangao wa wengi, Mahiga alibadili mtazamo tena bila ya kupepesa macho wakati alipokuwa akizungumza na  mabalozi wa kigeni Ikulu mjini Dar es Salaam kwa niaba ya Magufuli, na kuwaomba mabalozi kumrai Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, washiriki  marudio ya uchaguzi, licha ya kwamba CUF na vyama vyengine  9 vimesema havitoshiriki.

Mimi nilitarajia  Mahiga  aliyewahi kuwa balozi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa na baadae mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, angedhihirisha kwamba kuweko katika nafasi hizo hakukuwa ni bahati mbaya. Lakini kwa hili la Zanzibar ameitia dosari diplomasia  ya Tanzania chini ya serikali ya awamu ya tano. Mahiga anataka dunia ihalalishe haramu mbele ya haki.

Jengine ambalo limetuacha tukipigwa na bumbuwazi ni pale alipozungumzia kwa nini Tanzania inapinga kupelekwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Matifa nchini Burundi. Sababu aliyoitoa ni kuwa kupelekwa kikosi hicho bila ya ridhaa ya serikali ya  nchi hiyo kutasababisha hali kuwa mbaya zaidi na wimbi la wakimbizi. Mahiga amesahau kwamba sababu cha  wazo hilo ni kuzuwia  mauaji  ya kila uchao, kunusuru nchi hiyo isirudi iliokokuwa kabla ya  mkataba wa Amani wa Arusha na pia kuepusha mgogoro huo kuchukuwa sura ya kikabila na kutokea sawa na yaliotokea Rwanda na mauaji ya kimbari  1994.

Mgogoro wa sasa Burundi  ni wa kisiasa, unaotokana na kiu cha madaraka baada ya Rais Pierre Nkurunziza  kuamua kuendelea kwa muhula wa tatu ambapo wapinzani wanasema ni kinyume na katiba ya nchi hiyo. Ni suala la kukiuka katiba sawa na ukiukaji  unaoendelea Zanzibar na kutetewa na CCM Bara.

Kama hayo hayatoshi, Mahiga alitoa mfano wa hatua ya Marekani kutuma jeshi nchini Somalia mwaka 1993 , akisema  matokeo yake kuna  askari wa Marekani waliuawa na maiti kufungwa  nyuma ya gari na kubururwa mitaani mjini Mogadishu. Akasema kwamba Marekani ilichukua hatua  hiyo bila ya ridhaa ya serikali ya Somalia.  Mahiga amesahau tena kuwa wakati huo wote Somalia ilikuwa  haina serikali na  mauaji yaliyokuwa yakiendelea ni katika vurugu za kuwania madaraka. Waliowauwa askari wa Marekani walikuwa wapiganaji wa Mohammed Farah Aideed, mmoja wa wababe wa kivita  wakati huo.

Zaidi linalonifanya nitikise kichwa wakati huu nikiandika makala haya, ni kwamba Mahiga mwenyewe anasahau uwepo wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa nchini Somalia (AMISOM) umesaidia kwa kiasi fulani katika kuwapa nafasi ya kuendelea na maisha yao wakaazi wa mji mkuu Mogadishu, ingawa usalama wao si wa uhakika.

Kuna kuteleza  katika diplomasia. Hata  enzi ya Nyerere, Tanzania iliteleza ilipounga mkono kujitenga kwa jimbo la mashariki mwa Nigeria lililotangazwa kuwa  Jamhuri ya Biafra na muasi Kanali  Odumegwu Ojukwu mwaka 1967, ambapo pamoja na Ivory Coast zikawa nchi mbili pekee barani humu kuitambua Jamhuri hiyo. Nyerere alichukuwa uamuzi huo wa makosa , licha ya kuwa ilikuwa ni serikali ya Shirikisho la Nigeria iliyotuma wanajeshi wake kusaidia ulinzi Tanganyika baada ya uasi wa Januari 1964 ulioutikisa  utawala wake.

Lakini hitilafu za mapema ikiwa ndiyo kwanza Februari 12  zimetimia  siku 100 tokea Rais Magufuli alipoapishwa, tayari zimeanza kuibuwa maswali. Mzozo wa Zanzibar ni mtihani mpya katika siasa ya  Tanzania kuelekea nchi za nje na hasa katika suala zima la demokrasia na utawala bora. Kauli  zimetolewa hata na wanasiasa wakongwe ndani ya CCM yenyewe,  wakiwemo Dk.  Salim Ahmed Salim, Benard Membe, Joseph Butiku na hivi majuzi tu Ibrahim Kaduma aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje, wote wakitaka: “Haki itendeke Zanzibar.“

Licha ya ujumbe kama wa Mzee Kaduma kuitaka CCM wajifunze kukubali kushindwa, bahati mbaya wenye kukamata mpini wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete, wanaelekea  hawataki kabisa kusikia, si la mwadhini wala mteka maji msikitini. Diplomasia ya Tanzania kwa kila hali iko mashakani.

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii ni msomaji na mchangiaji wa mara kwa mara kwenye Zanzibar Daima

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.