Mnamo tarehe 28 Oktoba 2015, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, alitakiwa kuripoti katika ofisi zilizotengwa maalum kwa kutangazia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba zilizopo Salama Hall katika Hoteli ya Kitalii ya Bwawani kabla ya saa 4:00 za asubuhi ili kumaliazia kutoa matokeo ya urais kutoka majimbo ya uchaguzi ya Unguja na Pemba, kwa kuwa usiku wa tarehe 27 Oktoba 2015 alitowa tangazo la kuakhirisha shughuli hiyo hadi siku ya pili yake.

Alitoa tangazo hilo mbele ya mawakala wa vyama vya siasa, vyombo vya habari vya nje na ndani, waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania na Zanzibar na wadau mbali mbali wa siasa na uchaguzi. Pamoja na kutohudhuria kwake katika eneo hilo, kufikia muda wa mchana Jecha akajitokeza katika Televisheni ya Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) akitangaza kutokea eneo lisilojulikana kwamba ameufuta uchaguzi mzima. Tangu siku hiyo, ZEC na Mwenyekiti wake wakabakia kimya hadi kufikia tarehe 22 Januari 2016 kwa staili ile ile aliyotumika kufuta uchaguzi, Jecha akatangaza tena marudio ya uchaguzi, akisema kwamba ungelifanyika Jumapili ya tarehe 20 Machi 2016.

Kabla na baada ya kufutwa kwa uchaguzi huo kulikuwa na vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi wa Oktoba 25, ambavyo vilikuwa vikizungumzia kutokukubaliana na Tume iliyopo chini ya mwenyekiti wake Jecha, kwa kuwa walikosa imani na jinsi chombo hicho chenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi nchini kilivyouendesha uchaguzi huo. Imani hiyo iliendana sambamba na baadhi ya vyama kupinga namna matokeo yalivyokuwa yakitolewa kwa mwenendo wa kusuasua. Wengine walipinga kwa kusema kulikuwa na dosari nyingi na hujuma katika baadhi ya majimbo dhidi ya vyama vyao zilizofanywa na ZEC na maafisa wake. Baadhi ya vyama vilifika mbali zaidi kwa kusema kwamba muundo mzima wa Tume iliyopo wote haufai na kutaka ivunjwe ili iundwe tume nyengine ambayo itasimamia jukuma lake kwa uadilifu.

Siku moja kabla ya kufutwa kwa uchaguzi huo, yaani tarehe 27 Oktoba,  wakati tume ya ZEC ikiendelea kutoa matokeo, alisikika Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ali Vuai, akisema kwamba chama chake hakina imani na ZEC katika uendeshaji nzima wa uchaguzi. Vuai alikuwa akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa na alisema baadhi ya maeneo mawakala wa Chama chao walinyimwa vitambulisho jambo ambalo limekifanya chama hicho kutokuridhika na utaratibu huo. Alifika mbali zaidi na kusema siku moja kabla ya uchaguzi walifika Tume ya Uchaguzi kuhakiki vitambulisho vya mawakala wao wote na vilikuwepo, lakini cha kushangaza ni kuwa siku ya kura vitambulisho vya mawakala hao havikuonekana wala hakujulikana nani alivichukua na “kutokana na hali hii tunakosa imani na ZEC,” alisema Vuai.

Ni jambao la kushangaza, kwa hivyo, kwamba sasa CCM hiyo hiyo ndiyo ambayo inakubaliana kwa asilimia 100 na kurejewa kwa uchaguzi chini ya Tume hiyo hiyo ambayo hadi tarehe 27 Oktoba walikuwa hawana imani nayo hata kidogo.

Vyama vyengine ambavyo vimetoa saa tamko la kushiriki uchaguzi wa marudio ni pamoja na ADA – Tadea na AFP. Mnamo tarehe 02 Novemba 2015, kulifanyika mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar Es Salaam, ambao ulikuwa maalum kwa ajili ya kumuaga Rais  Jakaya Mrisho Kikwete aliyekuwa akimaliza muhula wake wa kuiongoza Tanzania. Waandishi wa habari walipata nafasi ya kuwahoji wanasiasa mbalimbali katika ukumbi huo, wakitaka kusikia kutoka kwa wagombea wa urais wa Zanzibar wa uchaguzi wa Oktoba 25, na ndipo Said Soud wa AFP alisema, “Mimi kwa upande wangu nimeona kuwa uchaguzi ulikuwa una mapungufu mengi ikiwa kuna watu ambao wamekutwa wakiwa wana kura feki, kupigana kwa wajumbe wa ZEC pia kuonekana kwa watu ambao si mawakala wala si wasimamizi wa uchaguzi ndani ya vituo”.

Siku hiyo hiyo, mgombea urais wa ADA TADEA, Juma Ali Khhatiba, naye akasema ingawa aliridhia kufutwa kwa uchaguzi, lakini:  alisema kwamba, “Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeboronga na haikuwajibika ipasavyo ndio sababu ya kuliingiza taifa kwenye mgororo huu”. Kwa maneno hayo ya Vuai Ali Vuai, kutamka hadharani kwamba CCM hakina imani na Tume ya Uchaguzi iliyosimamia uchaguzi ule, lawama za AFP kupitia Said Soud Said kwamba tume ilikiyosimamia Uchaguzi huo ilikuwa na mapungufu juu ya usimamizi wake na kupitia kauli ya moja kwa moja aliyoitoa Mgombea wa ADA Tadea,Khatib, kwamba Tume ya Jecha iliyosimamia uchaguzi huo wa Oktoba 26 “iliboronga”, ni dhahiri kwamba wote wanaungana na kwa kutokuwa na imani na Tume yaJecha.

Kwa mana hiyo basi sioni kama ni sahihi kwa vyama hivyo kukubali kushiriki uchaguzi wa marudio ambao utasimamiwa na tume ile ile, ambayo inasimamiwa na mwenyekiti yule yule aliyesimamia uchaguzi ambao wao kwa nyakati tofauti walisema tume hiyo haifai, labda kinyume chake iwe ni ‘unafiki’.

One thought on “Ukiacha unafiki, hakuna kinachovifanya vyama hivi kurejea uchaguzi”

  1. Ndio jadi yao ASP tokea kale kuwa wanafiki, mwaka 1960 matokeo yalitoka sare baina ya vyama kwa kupata majimbo 11 v/s 11 ,ASP walilazimisha kurejewa kwa uchaguzi na Juni 1961 uchaguzi uliporejewa waliuwa wanachama wa ZNP/ZPPP 69. Mwaka 1995 CCM walilazimisha kurejewa kwa uchaguzi wilaya ya mjini baada ya kuona kwamba wanashindwa waliufuta uchaguzi. Mwaka 1985 Marehemu Idrisa hakushinda uchaguzi wa chama kimoja lakini aliwekwa kukisitiri chama. Pia uchaguzi wa Salmini Amour wa kujaza pengo la Idrisa alipojiuzulu , watu waliojiandikisha hawakufika asilimia hata 50 ya wapiga kura lakini pia alipachikwa tu kwa sababu ni chama kimoja . Kura za maruhani Pemba hakuna mbunge wa CCM aliyeshinda walipata kura mathalani 200 kati ya kura 4000. walikataliwa ila walipachikwa .CCM kazi yao unafiki ,dhulma ,husda, choyo, uzushi ,fitna , wizi, uongo na kila aina ya jeuri ,ufedhuli na kibri na majivuno juu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.