RAIS Abeid Amani Karume wa Zanzibar, siku zote hakufurahia muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (baadaye ukaitwa Tanzania) ulivyokuwa, tangu ulipoanzishwa, Aprili 26, 1964 hadi kifo chake, Aprili 7, 1972 akidai kwamba ni “koti” lililombana na alitamani daima kulivua.

Kwa sababu hii alihakikisha kwamba, Muungano haumpunguzii madaraka yake Visiwani; aliiongoza Zanzibar kama “nchi huru” hata kwa mambo ambayo yalikuwa ya Muungano sawa na kwamba juhudi zake za kujiimarisha kimadaraka zilikuwa ni kutafuta “uhuru” wa Zanzibar nje ya Muungano.

Karume hakujali mgawanyo wa mamlaka na madaraka kati ya yale ya Muungano na yale ya Zanzibar. Ukiacha mambo ya Nje, Zanzibar iliendelea kudhibiti kivyake madaraka na mambo yote juu ya Uhamiaji, Biashara ya Nje na Mikopo, Utumishi wa Umma, Bandari, Posta na Simu, Jeshi na Usalama wa Taifa ambayo vinginevyo yalipashwa kusimamiwa na Serikali ya Muungano.

Na kwa chukizo kwa Nyerere, alitangaza kuwa asingeruhusu uchaguzi kufanyika Visiwani kwa miaka 50; akatangaza ukuu (supremacy) wa Chama cha Afro Shirazi (ASP) kuwa juu ya taasisi zote, ikiwamo Katiba ya Jamhuri ya Muungano na taasisi zake.

Kana kwamba alikuwa akiimarisha Taifa huru la Zanzibar nje ya Muungano, Amri yake (Decree) juu ya ukuu wa ASP ilianzisha Idara za Jeshi, Usalama wa Taifa (la Zanzibar), Polisi, Vijana, kina mama wa ASP ili kwamba mambo hayo yashughulikiwe kiserikali chini ya idara husika nje ya Muungano.

Kufikia mwaka 1971, Vyeo kama “Rais wa Zanzibar” (chenye kutambuliwa na Katiba ya Muungano), Mawaziri na Manaibu Mawaziri, vilibadilishwa kuitwa “Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi” (badala ya Rais), Mawaziri na Manaibu Mawaziri wakaitwa Wenyeviti na Manaibu Wenyeviti wa Idara; yote haya ilikuwa ni chenga kimamlaka kufanya Katiba ya Muungano isiwe na pa kushika kiutawala Visiwani.

Kufikia hapo, ASP kilikuwa ndiyo Serikali na Serikali ilikuwa ndio ASP wakati ikifahamika kwamba, Vyama vya Siasa (ASP na TANU) havikuwa jambo la Muungano. Ikumbukwe kwamba, wakati huo Zanzibar haikuwa na Katiba ambapo ilitawaliwa kwa Amri (Decrees) za Rais zisizohojika.

Na vivyo hivyo, Jamhuri ya Muungano ilitawaliwa na kuongozwa kwa Katiba ya Mpito (Interim Constitution) ambayo ilimpa madaraka Rais wa Jamhuri ya Muungano, kuifanyia marekebisho kadri alivyoona inafaa katika kipindi cha mpito cha mwaka mmoja kuelekea Katiba ya kudumu, isipokuwa kwa mambo kumi na moja ya Muungano (kutopunguza au kuongeza) yenye kulindwa na Mkataba wa Muungano (Articles of Union), uliotiwa sahihi na waasisi wake, Aprili 22, 1964.

Kitendo cha Karume kuendelea kudhibiti baadhi ya mambo ya Muungano Visiwani, kilitafsiriwa kuwa cha mabavu na “usaliti” kwa Muungano.

Suala la Fedha lazua tafrani

Kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, nchi nne za Afrika Mashariki – Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar, zilikuwa Wanachama wa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board – EACB), iliyosimamia na kuratibu sarafu ya pamoja chini ya usimamizi na maelekezo ya Waziri wa Makoloni wa Uingereza.

Nchi hizo wanachama wa EACB zilimiliki kwa pamoja katika Bodi hiyo hisa na mali, na zilistahili gawio la faida pamoja na mikopo ya muda mfupi kila moja kadri ya uwekezaji wake katika Bodi.

Kufuatia uhuru wa nchi hizo, usimamizi na uratibu wa sarafu uliofanywa na EACB ulihamishiwa kwa Serikali mpya za nchi hizo, huku juhudi zikifanywa kuunda Shirikisho la nchi za Afrika Mashariki (EAF) ambapo shughuli za EACB zingechukuliwa na Shirikisho hilo. Na ilipoonekana juhudi za kuunda EAF kushindwa, nchi za Kenya, Uganda na Tanganyika ziliamua kuanzisha Benki Kuu na Bodi zake za sarafu.

Baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana mwaka 1964 katika kipindi hiki cha mpito kwa nchi hizi kuanzisha Benki Kuu na sarafu yake, mgogoro mkubwa ulizuka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar juu ya mambo matatu: la kwanza, ni kama Zanzibar iendelee kuhudhuria au la, vikao vya EACB kama nchi; pili, kama Zanzibar bado ilistahili gawiwo la faida kutokana na uwekezaji wake baada ya EACB kuvunjwa.

Hoja iliibuliwa pia juu ya nafasi na hadhi ya Zanzibar (kama nchi ndani ya Muungano) kuhusiana na mambo ya fedha chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliyokusudiwa; na mwisho, hadhi ya “Benki Kuu ya Taifa la Zanzibar” (BoZ) iliyotarajiwa kuundwa, ndani ya Muungano.

Ukwasi na Chimbuko la BoZ

Tangu kufikiwa kwa Muungano, Aprili 26, 1964; na kufuatia kuvunjika kwa EACB, Zanzibar ilikuwa na shauku hai ya kuanzisha Benki Kuu (BoZ) yake. Wizara ya Fedha Zanzibar, chini ya Waziri makini Abdulaziz Twala, ilianza mchakato huo kwa kupeleka vijana nchini Ujerumani Mashariki kwa mafunzo ya Fedha na Usimamizi wa Fedha, Ukaguzi na shughuli za Benki.

Na katika kuhakikisha kwamba akiba yake ya fedha za kigeni haikodolewi macho wala kuguswa na Serikali ya Muungano au Benki za Kiingereza, Zanzibar ilihamisha haraka jumla ya pauni za Uingereza 700,000 kutoka Benki ya Uingereza ya Grindlays, kwenda “Norodony Moscow Bank”, Tawi la London, Uingereza; kitendo ambacho kililaaniwa vikali na Serikali ya Muungano.

Ukwasi wa Zanzibar, ikilinganishwa na Tanganyika, ulikuwa wa kiwango cha juu wakati wa Karume kutokana na bei nzuri ya karafuu katika soko la dunia, ambapo ilipanda kutoka dola za Kimarekani 550 hadi dola 1,500 kwa tani, kiasi kwamba kufikia mwaka 1971, Zanzibar ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni ya pauni za Uingereza (£) 14,000,000, ikilinganishwa na 6,500,000 za Tanzania Bara.

Akiba hiyo nono, mbali na kutokana na bei nzuri ya Karafuu, ilitokana pia na Serikali ya Zanzibar kuwapunja wakulima bei ya mazao yao kwa kuwalipa asilimia 10 tu ya bei, na sehemu kubwa ya mauzo kubakia Serikalini.

Kwa mfano, wakati karafuu iliuzwa kwa bei kati ya sawa na shilingi 14/= [Indonesia] na shilingi 21/= [India] kwa ratili, mkulima alilipwa na Serikali ya Zanzibar bei ya Shs. 1.50 tu kwa ratili; wakati huo, kwa Tanzania Bara na nchini Kenya, bei kwa mkulima ilikuwa kati ya shilingi 8/= na 10/= kwa ratili.

Wazanzibari walioumizwa zaidi ni Wapemba wa Visiwa vya Pemba ambao ndio walikuwa wazalishaji wakubwa wa karafuu Visiwani.

Ukakasi juu ya ushiriki au la, wa Zanzibar katika EACB, umiliki wa hisa, gawiwo la faida za EACB na kuhusu uanzishaji wa BoZ kufuatia Muungano na Tanganyika, ulimalizwa na Katibu wa EACB, H.R. Hirst, katika ufafanuzi wake kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha wa Serikali ya Muungano wa wakati huo, D. Namfua, akisema, “Katiba ya Mpito ya Jamhuri ya Muungano, haikuhamishia mambo ya Fedha na Sarafu ya nchi hizi kwa Serikali ya Muungano na hivyo uanachama wa Zanzibar wa EACB haukuathirika”, akimaanisha kuwa, mambo ya Fedha na Sarafu hayakuwa ya Muungano hivi kwamba kila nchi ilikuwa na uhuru wa kuwa na Benki Kuu na sarafu yake.

Tanzania Bara na Uingereza, kupitia Mjumbe wake katika EACB, J. B. Loyness, zilitaka ima faima, Zanzibar iondolewe kwenye EACB kuanzia kikao cha Septemba 8, 1964; lakini Hirst, mapema Januari 1965 baadaye, akawashushua kwa kumwandikia Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Fedha, Edwin Mtei, kumtaka nchi yake kuheshimu nafasi ya Zanzibar.

Stahiki ya mgawo wa Zanzibar EACB

Akichangia Bungeni kuhusu muswada wa Benki Kuu (BoT) mwaka 2006, aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Muungano kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Rashid, alidai kuwa, kufikia mwaka 1987, Zanzibar ilikuwa ikiidai Serikali ya Muungano riba ya pauni za Uingereza milioni 1,006 kwa mali na fedha za Zanzibar ilizochukua kutoka EACB kati ya mwaka 1964 – 1966.

Hamad aliikumbusha Serikali kuwa, mgawo wa Zanzibar kutoka EACB ulikuwa asilimia 11.0, na kwamba kati ya mwaka 1965 na 1993, Zanzibar ilikuwa haijalipwa faida kutokana na hisa zake, na pia kwamba, kati ya mwaka 1964 na 2004, ililipwa na Serikali ya Muungano kiasi kiduchu cha shilingi bilioni 3.76 kwa fomula iliyowekwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya asilimia 4.5, kinyume na asilimia 11.05 ambapo ingestahili kulipwa shilingi bilioni 82. Hoja hii imepingwa mara nyingi na Serikali ikidai kwamba, kilicholipwa ndiyo hesabu stahiki na kamili.

Mkakati wasukwa kuikabili Zanzibar

Ule ukweli kwamba mambo ya Fedha, Sarafu na uhalali wa Zanzibar kuanzisha BoZ hayakuwa mambo ya Muungano wakati huo, uliipa matumaini na haki isiyohojika kuweza kunufaika na kile ilichowekeza kwenye EACB kabla na baada ya Muungano, jambo ambalo halikupokelewa vyema na Serikali ya Muungano.

Bila Zanzibar kufahamu, Mwalimu Nyerere aliwaita kwa siri wanasheria wake, wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Roland Brown, na kuwaelekeza “wafanye kitu” juu ya Zanzibar isiendelee kutamba kwa fedha zake.

Roland Brown ndiye huyo huyo aliyeelekezwa na Mwalimu kabla ya hapo mwezi Aprili 1964, kuandaa kwa njia ya dharura, Hati ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar “bila mtu mwingine yeyote kujua”, baada ya juhudi za Mwalimu za kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki (EAF) kushindwa na kugeukia Muungano finyu kati ya Tanganyika na Zanzibar badala yake.

Taarifa za wakati huo zinaonesha kwamba, katika mazingira hasi na hatarishi kwake, Karume alishinikizwa kutia sahihi Hati hiyo ambayo baadhi ya mambo yaliyomo aliyakana baadaye kwamba alidanganywa au kuchengwa kutokana na yeye kutojua lugha ya Kiingereza ndani ya Hati hiyo, ikizingatiwa pia kwamba alinyimwa ushauri wa kisheria, baada ya kulazimishwa kumpa likizo ya lazima ya siku saba, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Wolfgang Dourado hadi mchakato wa Muungano ukamilike.

Haraka haraka ukaandaliwa Muswada wa Marekebisho ya Katiba (The Interim Constitution Ammendment Bill; baadaye kupitishwa kuwa Sheria Na. 21 ya 1965) kufanya sarafu, Fedha za Kigeni na udhibiti wake kuwa mambo ya Muungano ili kuwasilishwa Bungeni kupitishwa kuwa Sheria.

Karume asaini Muswada kuridhia asichokijua

Muswada wa Marekebisho ya Katiba kufanya mambo ya Fedha na Sarafu kuwa ya Muungano uliwasilishwa kwenye Bunge la kawaida, tarehe 10 Juni 1965, na kupitishwa kwa kasi isiyo kawaida. Wakati huo, Mwalimu Nyerere alikuwa safari nje ya nchi.

Kutokana na Mwalimu kutokuwepo nchini, mzigo wa kutia sahihi Muswada huo kuwa Sheria ulimwangukia Makamu wa Kwanza wa Rais, Sheikh Abeid Amani Karume kwa wadhifa wake kama Kaimu Rais wa Jamhuri ya Muungano kipindi hicho. Siku hiyo, Juni 10, 1965, mjini Dar es Salaam, Karume aliwekewa mezani Muswada huo; naye bila ya kuhisi chochote, alitia sahihi hima Muswada huo kuwa Sheria na kuanza kutumika siku hiyo hiyo ya kupitishwa na Bunge na kabla hata wino haujakauka.

Ni dhahiri Karume hakujua (kama ambavyo tu hakujua alipotia sahihi Hati ya Mkataba wa Muungano mwezi mmoja kabla ya hapo) alichokuwa akitia sahihi. Wala Wabunge kutoka Zanzibar kwenye Bunge la Muungano, siku hiyo, hawakujua madhara ya Muswada waliopitisha kwa Zanzibar. Chini ya Marekebisho hayo, michango yote ya Zanzibar, hisa na mapato ya riba kwenye EACB, yalifanywa kuwa mali stahiki ya Serikali ya Muungano.
Bado kuna ukinzani wa kisheria miongoni mwa wanasheria kuhusu uhalali na uwezo wa Bunge la wakati huo, wa kufanyia marekebisho Katiba ya Mpito ya mwaka 1964, kwa kuongeza jambo la Fedha kuwa la 12 juu ya Mambo kumi na moja asilia ya Muungano.

Katiba ya Mpito ilitoa uwezo huo kwa Rais wa Jamhuri pekee kwa mujibu na kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union) ambapo hata hivyo, si kiasi cha kubomoa wala kurekebisha msingi mkuu wa Muungano, yaani yale mambo kumi na moja ya Muungano.

Kwa kuwa uwezo huo wa kufanyia marekebisho Katiba hiyo ya Mpito ulikuwa wa Rais pekee kwa njia ya Amri ya Rais (Presidential Decrees), hatua iliyochukuliwa na Bunge la kawaida ilivuka mipaka yake na hivyo ilikuwa batili na haramu pamoja na marekebisho yake, tangu mwanzo

Ni pale aliporejea Zanzibar baada ya kutia sahihi Muswada huo, Karume alipofafanuliwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Wolfgang Dourado, kwamba kile alichotia sahihi ni Hati ya kujinyonga yeye na Zanzibar, kwa kukubali kuingizwa kwenye Muungano jambo kama hilo muhimu kwa uchumi wa Zanzibar; lakini wapi, alikuwa amechelewa.

Kama kawaida, hilo halikumnyima usingizi Karume; aliendelea na Mpango wake wa kuanzisha BoZ na mambo mengine ya fedha, kwa kuteua Tume kuanzisha mchakato huo kwa chukizo la Serikali ya Muungano iliyodai (Karume) alikuwa akivunja Katiba kwa jeuri na kiburi.

Aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Muungano wa wakati huo, Amir Habib Jamal, katika barua yake ya 18 Machi, 1966 kwa Waziri Twala, aliweka wazi msimamo wa Kikatiba dhidi ya “jeuri” ya Karume kwa kusema, “Gavana wa BoT atakuwa ndiye mwakilishi pekee wa Tanzania na Zanzibar kwenye vikao vya EACB; mgawo wote wa mali na au faida utakaofanywa na EACB kwa ajili ya Tanzania na Zanzibar, utalipwa na kuchukuliwa na Serikali ya Muungano”.

Na kuhusu BoZ, Jamal alisema, “Benki hiyo inaweza kuanzishwa kama Benki nyingine ya kawaida chini ya Sheria za Zanzibar kufanya shughuli zisizokuwa za Benki Kuu”.
Zanzibar yasalimu amri

Ubishi wa Zanzibar ulifikia kikomo mwaka 1966 baada ya kuanzishwa kwa BoT, pale Sheria ya Benki na Sheria ya Udhibiti wa fedha za Kigeni (the Banking Ordinance” na “The Exchange Control Ordinance” – Cap 139), zilipofanyiwa marekebisho kuweza kutumika pia Zanzibar.

Jamal, kwa kuhuzunishwa na msimamo mkali wa Zanzibar na Karume, wa kuendeleza mchakato wa kuanzisha BoZ kwa Amri ya Rais Karume, chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma (Zanzibar Public Enterprises Decree, 1966), katika barua yake Kumb: TYC.46/08 ya 23 Machi 1966, kwa Serikali ya Zanzibar alisema, hatua hiyo ni ya “kuvuka mipaka na isiyokuwa na nguvu ya Kisheria kwa kuzingatia Katiba ya Muda/Mpito ya Muungano”.

Kwa kusalimu amri na shinikizo, ilibidi Benki ya Zanzibar ianzishwe kama Kampuni binafsi, na kuitwa “Benki ya Watu wa Zanzibar (The People’s Bank of Zanzibar – PBZ) yenye Wanahisa wawili, mmoja wa wawili hao akiwa Karume mwenyewe.

Hata hivyo, Karume aliendelea kubeza Sheria ya BoT kwa kuendelea kutunza fedha za kigeni za Serikali yake nje ya nchi; huku PBZ ikiendelea kufanya kazi kama Benki ya Serikali ya Zanzibar hadi baada ya kifo chake, pale BoT ilipoweza kufungua Tawi Visiwani.

Muungano wetu umedumu na utaendelea kudumu; lakini umepitia na unaendelea kusukwasukwa na mawimbi. Na ili kuweza kutuliza bahari iliyochafuka, yatupasa kutizama nyuma (na kujisahihisha) ili tuweze kwenda mbele kwa uhakika zaidi.

Chanzo: Gazeti la Raia Mwema la tarehe 10 Februari 2016

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.