Zanzibar ipo hatarini kupoteza mabilioni ya fedha  kufuatia hatua ya baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kutaka kusaini mkataba na Kampuni ya Kichina ya ZTE juu ya utekelezaji wa mradi wa E-health unaolenga kutoa huduma ya afya kwa njia ya kimtandao, mtandao wa Zanzibar Daima umefahamishwa.

Mradi wa e-Health ambao utakuwa wa pili kutekelezwa na kampuni hiyo ya ZTE visiwani Zanzibar baada ya ule wa mkonga ambao ulimalizika mwaka 2011 bila ya mafanikio, utawapelekea walipa kodi wa Zanzibar kupoteza fedha nyingi zaidi, kwani tayari kampuni iliyopewa tenda ya kukagua mradi huo imeshaonesha dosari nyingi ambazo zinaonesha mradi huo kutotekelezeka.

Mradi wa mkonga ama Fiber Backbone – ulizua masuala mengi kufuatia kampuni ya ZTE kufanya mradi huo chini ya kiwango huku rushwa kati ya viongozi wa SMZ na kampuni hiyo ikitajwa kuhusika.

Hapo awali, kwa mujibu wa mapendekezo yaliyofanywa na kampuni ya ZTE, mradi wa mkonga ulitarajiwa kuipatia SMZ mapato ya dola za Kimarekani zipatazo milioni 3,000,000 kwa mwaka baada ya kukamilika, lakini  lengo hilo halikufikiwa kutokana na mradi wenyewe “kufanywa chini ya kiwango”, kwa mujibu wa mpashaji habari wetu.

Makosa mengi, yakiwemo ubovu wa vifaa, ulazaji wa nyaya chini ya kiwango na ujenzi wa miundombinu ya mkonga huo karibu ya barabara bila ya kuwashirikisha Idara ya Ujenzi na Utunzaji Barabara, vilikuwa ni miongoni mwa kasoro nyingi zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi huo.

Dk. Shein azindulishwa mradi ‘bomu’

Mradi huo ambao ulizinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, ulikaa mwaka mzima bila ya kufanyiwa kazi yoyote hali ambayo imepelekea kupoteza warantii yake na hatimae mwaka 2012 mradi huo ulikabidhiwa kwa kampuni ya Zantel ambayo iliuendesha bila ya msaada wowote kutoka kampuni ya ZTE.

Dk. Ali Mohamed Shein
Dk. Ali Mohamed Shein

ZTE imeipelekea Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kuukata mkonga huo kila inapotanua barabara zake, ambapo bomoa bomoa inayofanyika  Fuoni imeshaathiri sehemu kubwa ya mkonga isiyoweza kurekebishika kwa pesa ndogo kutokana na kiwango kidogo cha ulazaji wa waya.

Hayo yametokana na usimamizi mbovu wakati wa ujenzi wa mkonga uliofanywa na Wizara ya Fedha ambao ulipelekea  kampuni ya ZTE kufanya itakavyo kwa  kuwanunua baadhi ya wakubwa hao ili na kuendelea  kuitia hasara Zanzibar.

Hali hiyo ilisababisha kampuni ya Zantel na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kurekebisha matatizo yanayojitokeza kila siku kutokana na ubovu wa vifaa.

Chanzo cha kuaminika kutoka Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano ambaye alisisitiza kutotajwa jina lake aliliambia Zanzibar Daima kuwa viongozi waliosimamia mradi wa mkonga hawakuzingatia maslahi mapana ya taifa na badala yake waliangalia maslahi yao tu.

Alisema kuwa kampuni ya ZTE haikukidhi vigezo kiasi cha kupewa tenda ya kukamilisha mradi huo kwani tokea hatua za awali walionekana kuwa ni wababaishaji.

“Unajua huu mradi wa mkonga haukukidhi vigezo kwani ulifanywa chini ya kiwango, lakini mimi nadhani hili halikufanyika kibahati mbaya, lilifanywa kwa makusudi na baadhi ya viongozi wetu ambao walijua watanufaika wao binafsi kupitia mradi huu” alidokeza.

Mmoja wa wafanyakazi wa wizara zinazohusika na usimamizi wa  miradi mbali mbali, ambaye pia alitoa masharti ya kutotaja jina lake, aliliambia Zanzibar Daima kuwa licha ya kampuni ya ZTE kusifika kwa rushwa na kutekeleza miradi mibovu kama huo wa mkonga, tayari viongozi wa SMZ wakiongozwa na kamati ya makatibu wakuu wanatarajia kukopa fedha nyengine kutoka benki ya Exim ya china na kuipa kampuni hiyo ili kutekeleza mradi mwengine wa E-health.

“Kwa kweli ni masikitiko makubwa, huo mkonga haujaanza kukusanya mapato yoyote na kuweza kulipa hizo fedha zilizokopwa Exim Bank ya china, lakini Serikali inakopa fedha nyengine kwa ajili ya mradi mwengine wa E-health ambao unategemea mkonga asilimia mia moja sasa huu si ubadhirifu ni kitu gani?”, alihoji.

Pia aliendelea kusema kuwa mradi huo wa e-Health haukupaswa kupewa tena kampuni ya ZTE kwani kampuni hiyo inasifika sana kwa rushwa kwani hapo awali ilishafeli kwenye mradi wa mkonga.

“Sio tatizo kukopa mara ya pili kwa ajili ya miradi lakini linalosikitisha ni kuwa mradi wa pili unategemea mradi wa kwanza ambao ZTE imeshauharibu na pia amepewa Baraka za kuenddelea na mradi mwengine,” aliongeza.

Afisa mwengine wa serikali, ambaye pia alikataa kutajwa jina, alisema kiilivyo “mradi wa e-Health unahitaji Mkonga kwa asilimia 100 na pia unahitaji  wataalamu kutoka Wizara ya Afya sambamba na wataalamu wa Tehama (teknolojia ya habari na mawasiliano) ambao watatoa mapendekezo yao, lakini kutokana na tabia ya kulindana na kustahamiliana ndani ya taasisi za serikali hata kama kuna uwoza unaofanyika, kamati ya makatibu wakuu ilikuwa ikiburuzwa na kupuuza hata baadhi ya vikao ilikuwa ikimuachilia Katibu Mkuu wa Fedha ambaye ndiye mpitishaji wa miradi afanye atakavyo.”

Waziri wa Fedha aliukataa mradi wa ‘e-Health’

Juhudi za Zanzibar Daima kumpata Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha zilishindikana, lakini mpashaji habari huyo alisema baada ya kuona uozo huo, Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee alitafuta kampuni nyengine ya uhakiki iitwayo Securitree ijaribu kupitia mradi huo wa E-health ili kujiridhisha na ndipo ilipouona uozo mkubwa wa kampuni ya ZTE kwenye mradi huo ambapo kampuni iliyoupitia mradi huo ilikuja na ripoti inayoonesha kasoro nyingi za kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kutotoa ufafanuzi wa kutosha katika utekelezaji wake.

IMG-20160114-WA0002

Licha ya kasoro hizo kubainika, na katika kile kinachonekana kuwa ni kutojali maslahi mapana ya nchi na wananchi wa Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha alikutana na Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, na kutafuta njia ya kuupeleka Tanzania Bara katika hatua za mwisho ambapo mwezi wa Agost 2015, walizungumza na Waziri wa Fedha wa Tanzania, Saada Mkuya, na kumtaka ahakikishe kuwa mradi huo unapita.

Mradi huo ulitarajiwa kutiwa saini Disemba 2015 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, pindi angekwenda  nchini  Afrika Kusini kwenye mkutano na kuweza kuonana na Rais wa China lakini Rais Magufuli hakuhudhuria na badala yake aliwakilishwa na Makamo wake Samia Suluhu Hassan.

Lakini hatua za kuipitisha miradi yote ya Tanzania katika miradi ya China kupitia Benki ya Exim imeshakamilika kupitia ubalozi wa Tanzania uliopo China tokea  Januari 2016 na kinachosubiriwa ni kampuni ya ZTE kupatiwa fedha na kuendelea na mradi huo ambao utaendeleza madeni kwa SMZ.

Licha ya Baraza la Wawakilishi kupigia  kelele mara kwa mara katika vikao vyake kuhusu  ubovu wa mkonga wa taifa na utapeli wa  kampuni ya ZTE katika miradi mbali mbali, lakini wakubwa waliendelea kulifumbia macho suala hilo.

Makampuni ya Ulaya yalijitokeza kuomba tenda ya kutekeleza mradi wa e-Health kwa bei nafuu ya dola za Kimarekani milioni 10 lakini hawakupewa tenda hiyo na badala yake viongozi hao wanataka kuwalipa kampuni ya china ya ZTE dola za kimarekani milioni 33 kutekeleza mradi huo.

Zanzibar Daima iliarifiwa na mmoja ya wafanyakazi kutoka Wizara ya Afya kuwa hadi sasa mradi huo haujaanza kutekelezwa rasmi lakini utaanza kutekelezwa wakati wowote licha ya kasoro hizo.

Mfanyakazi huyo alitoa rai ya kuangaliwa upya kampuni ya ZTE ili kubaini hizo kasoro zinazotajwa kabla ya kuingiza Zanzibar katika mlima wa madeni ambao utakuwa utakuwa ni vigumu kuupanda.

“Mimi nimesikia kuhusu utapeli wa hiyo kampuni lakini nadhani ni vyema viongozi wakaitathmini upya hiyo kampuni yenyewe ili ijiridhishe zaidi.” Alisema.

Mradi huo ni wa gharama kubwa sana na unatarajia kupoteza mamilioni ya fedha kwenda kwa Kampuni ambayo haijakidhi vigezo vya kutekeleza mradi huo na kwa watu wachache wanaopenda maslahi yao binafsi  wakati hospitali zetu zinakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kupimia, dawa, madaktari  bingwa, vyumba na vitanda vya wagonjwa huku hali za hospitali za wilaya zikiwa na hali mbaya zaidi.

Tayari kampuni hiyo imeripotiwa kufanya vibaya kwenye baadhi ya nchi ikiwemo Nigeria kwa kutekeleza miradi mibovu ambayo imepelekea hasara kubwa kwa nchi hiyo.

“ZTE ni kampuni inayojali fedha bila ya kuzingatia ufanisi wa miradi inayoiweka. Mradi wa kwanza uliofanywa na kampuni hiyo unasuasua na  unahitaji matengenezo makubwa. Hivyo ni wajibu wa Rais wetu akausitisha kwanza mradi huo na ajiridhishe kabla ya nchi kuingia hasara ya kupoteza mamilioni ya fedha ambayo kimsingi yanakwenda kwa watu wachache,” alionya mpashaji habari wetu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.