Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa marudio umepangwa kufanyika Machi 20 mwaka huu kuwania nafasi ya urais wa visiwa hivyo, wajumbe wa Baraza la Wakilishi (BLW) na udiwani. Uchaguzi huu umekuja baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kuufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Wakati Jecha akitangaza uchaguzi wa marudio Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kipo madarakani kimekubali na kusema kuwa kitashiriki uchaguzi huo huku baadhi ya vyama kikiwamo chama kikuu cha upinzani Zanzibar, Chama cha Wananchi (CUF) vikigoma kushiriki.

CUF kilieleza kuwa hakitashiriki uchaguzi huo wa marudio kwa vile kufanya hivyo kutakuwa ni kubariki haramu iliyofanywa na Jecha ya kuufuta Uchaguzi Mkuu uliopita ambao inadai ulikuwa huru na haki. Jecha alifuta uchaguzi huo licha ya waangalizi wa ndani na kimataifa kueleza kwamba ulikuwa huru na haki na uliendeshwa kwa amani katika visiwa vyote vya Unguja na Pemba.

Mwenyekiti huyo alifuta matokeo ya uchaguzi wakati madiwani na wajumbe Baraza la Wakilishi walishatangazwa na kukabidhiwa vyeti vya ushindi na wasimamizi wa uchaguzi wa kata na majimbo kama sheria inavyotaka ushindi huo ulipaswa kuhojiwa mahakamani.

Maelezo ya Jecha

Akitangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio, Jecha alisema wagombea watakuwa ni walewale waliokuwapo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka jana na hakuna ruhusa ya kuingiza mgombea mpya. Pia, alisema katika uchaguzi huo hakutakuwa na kampeni.

Mwenyekiti huyo wa ZEC anaweza kupanga lolote katika uchaguzi huo kwa vile masuala yote yapo chini ya mamlaka yake, lakini siyo haki kuwalazimisha wagombea ambao hawataki kushiriki uchaguzi huo kugombea uongozi kwa lazima.

Kugombea uongozi kwa nafasi yoyote ile ni hiari ya mtu kwa hiyo haipaswi hata kidogo kumlazimisha mgombea wakati mwenyewe hataki kufanya hivyo.

Baadhi ya vyama vimeeleza kuwa havitaki kushiriki uchaguzi huo wa marudio kwa hiyo siyo halali kwa wanachama wake kugombea nafasi yoyote katika uchaguzi huo, ambao haufanyiki kwa ridhaa ya vyama vyote vya siasa.

Uchaguzi ni jambo la kihistoria katika nchi kwa hiyo mgombea anastahili kugombea pale na ridhaa ya kutaka kuwania uongozi na matokeo yoyote yatakayotokea ataridhika nayo kwa vile aliingia kwenye uchaguzi kwa hiari yake.

Ukiingiza jina la mgombea kwa nguvu na huku wafuasi wake wamesusia kupiga kura ni kumtafutia aibu ya kushindwa isiyo na sababu hata kama eneo analogombea ana wafuasi wengi kuliko mpinzani wake.

Kwa hiyo Jecha anapaswa kutafakari upya suala hili na asiwalazimishe wagombea kuingia katika uchaguzi ambao hawana ridhaa nao na ni kwa ajili ya masilahi ya watu wachache wanaoshinikiza ufanyike.

Ushauri kwa Jecha

Jecha na wenzake wasimamie uchaguzi huo kwa kuyaondoa majina yote ya wagombea ambao vyama vyao vya siasa havitaki kushiriki uchaguzi huo wa marudio ili mambo yaende bila ya kuwaudhi wengine hata kama yatabakia majina ya chama kimoja.

Iwapo itatokea hivyo chama kitakachoshiriki uchaguzi huo kitabaki kimoja itakuwa kazi rahisi zaidi kwa Jecha kuwatangaza wagombea wake kuwa ni washindi na kuokoa mabilioni ya shilingi ambayo yangetumika katika uchaguzi huo.

Njia hiyo itasaidia kuokoa fedha hizo ambazo zinaweza kuelekezwa kwenye matumizi mengine ya maendeleo ya wananchi chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Tume ya Uchaguzi Zanzibar inabidi ijipange vizuri ili ihakikishe wagombea ambao hawataki kushiriki uchaguzi huo wa marudio majina yao yanafutwa katika karatasi ya kupigia kura.

Ni lazima ZEC iheshimu haki ya kila mgombea kwani kushiriki uchaguzi ni ridhaa ya mgombea na siyo haki ya tume hiyo ambayo kazi yake ni kusimamia uchaguzi huo na siyo kuchagua wagombea.

Wagombea walioomba kushiriki Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana hawana ulazima wowote wa kushiriki uchaguzi wa marudio kama hawataki na kama vyama vyao vya siasa havitaki kushiriki.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar isilichukulie jambo hilo kirahisi kama Jecha alivyofuta uchaguzi, kwani masuala ya kushiriki uchaguzi ni haki ya msingi ya binadamu na hakuna yeyote anayeruhusiwa kumlazimisha kama hataki kushiriki.

Iwapo ZEC itayafuta majina ya wasiotaka kugombea kwenye uchaguzi huo wa marudio itawarahisishia wapigakura kazi yao ya upigaji kura iwapo itatokea CCM itakuwa na mpinzani katika uchaguzi huo wa marudio.

Ingekuwa raha kama tume hiyo ingeviruhusu vyama vya siasa vinavyotaka kugombea kufanya mchakato mpya wa wagombea wao katika nafasi mbalimbali, ili kuwaondoa wale ambao imewaona hawakuwasidia katika uchaguzi uliopita.

Fursa hiyo pia, ingesaidia kwa baadhi ya wagombea ambao vyama vyao vitashiriki katika uchaguzi huo, lakini wao hawataki tena kugombea kujitoa na kuwaachia nafasi hiyo watu wengine.

Kinachoshangaza zaidi ni kwa Jecha kutangaza kuwa hakuna kampeni katika uchaguzi huo jambo ambalo linaondosha ladha yote ya Uchaguzi Mkuu. Hii ndiyo hatari ya kutenda kosa inakulazimisha kufanya makosa mengine zaidi.

Ni vyema ZEC kwa kushirikiana na chama kilicho madarakani kujiandaa vyema katika kuusimamia uchaguzi huu wa marudio kwani hakuna dalili inayoonyesha kuwa uchaguzi wa upande mmoja Zanzibar katika vyama vingi vya Siasa unaweza kufanyika kwa amani.

Huu ni uchaguzi wa kushangaza kwani kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na Sheria ya uchaguzi hakuna kitu kama hicho kinachoitwa uchaguzi wa marudio.

Mbali na vyama vya upinzani hata Jumuiya ya Kimataifa imekataa kufanyika kwa uchaguzi huo wa marudio na kupendekeza itafutwe njia mwafaka ikiwamo ya mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa Zanzibar.

TANBIHI: Makala ya Masoud Saanani kwenye gazeti la Mwananchi la tarehe 10 Februari 2016

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.