Sote tunaelewa kwamba visiwa vyetu vya Zanzibar vimeingia katika mgogoro wa uchaguzi na kikatiba, mgogoro ambao chanzo chake ni baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jecha Salum Jecha kusitisha kumalizia kutangaza Matokeo ya Uchaguzi uliofanyika tarehe 25/10/2015 na ilipofika tarehe 28/10/2015 alitangaza kufuta uchaguzi huo na matokeo yake yote.

Baada ya hapo pande zote mbili za CCM na CUF kila mmoja akabaki na kushabikia msimamo wa chama chake, ambapo kwa upande wa CCM wamesimamia kwamba uchaguzi umefutwa hivyo kuna haja ya kurudia uchaguzi mwengine ambapo siku ya tarehe ya uchaguzi wa marudio imeshatangazwa na Jecha Salum Jecha kwamba utafanyika tarehe 20/03/2016, kwa upande wa CUF wao tangu kufutwa kwa uchaguzi msimamo wao haujabadilika wala kuyumba, msimamo wa CUF ni kwamba uchaguzi wa Mwaka Jana tarehe 25/10/2015 haujafutika kisheria licha ya Jecha kutangaza kufuta, hivyo wao pamoja na baadhi ya vyama vyengine vilivyoshiriki uchaguzi huo wa Mwaka Jana kikiwemo APPT Maendeleo hawaoni kwamba kuna sababu ya msingi na ya kisheria kurejea uchaguzi.

Mbali ya vyama hivyo, vipo pia vyama chengine vya siasa kwa kupitia huu mgogoro wa kufutwa kwa uchaguzi na kutangazwa kwa uchaguzi wa marudio, navyo pia vimezaa mgogoro kutokana na misimamo tofauti baina ya viongozi na viongozi au viongozi na wagombea wa vyama vyao

Kwa mfano Chama cha ADC, mgombea wa urais  wa chama hicho Hamad Rashid yeye alitangaza kwamba ADC iko tayari kushiriki uchaguzi wa marudio lakini Ndugu Said Miraji akiwa ni kiongozi wa juu wa Chama hicho akapingana na mgombea wake na kusema kwamba huo sio msimamo wa ADC, mgogoro huo uliendelea na hadi kpuelekea bodi ya udhamini ya chama hicho kuingilia kati na kusimamia maamuzi ya chama hicho kwa muda.

Kwa upande wa CCK nako hali si shwari mgogoro umeibuka baada ya mgombea wake wa urais Ali Khatib kutamka hadharani kwamba CCK wameridhika na marejeo ya uchaguzi na kwamba watashiriki, kitendo kilichompelekea kusimamishwa uanachama siku ya Pili tu baada ya taarifa yake hiyo.

Kuna baadhi ya viongozi na wanasiasa ambao na  wadau wa siasa wanaubeza mgogoro huu kuona kwamba hauna athari yeyote kwa taifa na kuamua kulipigia chapuo tangazo la Jecha la kurudiwa uchaguzi.

Ama kwa upande wangu napenda niseme kwa hatua mgogoro ulivyokaa, nalazimika kusema mgogoro umekuwa mkubwa zaidi, kwa sababu ulianzia kwa sura ya vyama viwili lakini kila kukicha vyama vinaengezeka, na vikikosa kuelewana vinaingia katika mgogoro. Mbali ya mgogoro wa kivyama lakini pia nahofishwa na hali ya hewa kiusalama ilivyo, kwa usalama uliopo kwa sasa ni wa kulazimisha, tumeshudiia askari wakizagaa mitaani ili kuzuia viashiria vya uvunjifu wa amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo wa marudio.

Niseme kuwa amani hailazimishwi, ulimwengu ni Mdogo kwa sasa kutokana na ujio wa sayansi na teknolojia, tunashuhuria jinsi Pierre Nkurunzinza kueneza jeshi kila kona, ili aweze kutawala kwa amani lakini kila kukicha waasi wanabuni mbinu mpya za kufanya asitawale kwa amani, hapa kwetu tunasikia kila siku serikali kutoa tamko kwamba ulinzi utaimarishwa, lakini tukubaliane kwa pamoja kwamba adui na yeye anapanga na kuimarisha mikakati kila wewe unapoboresha yako.

Sina mana ya kwamba CUF, APPT Maendeleo, CCK na vyama vyengine vyenye nia ya kuususia uchaguzi huo kwamba watafanya uvunjifu wa amani kwa kuwa wana lengo la kususia uchaguzi, la hasha! Maana yangu ni kusema kwamba ndani ya makundi ya watu wema basi yamo makundi ya watu waovu, ambao wanatafuta uchochoro wa kujifichia ili wafanye yao waliyoyakusudia, tumeshuhudia hivi sasa kuna kundi kubwa tu ovu, ambalo limepewa jina ‘Mazombi’ au ‘Masoksi’, ambapo imeripotiwa Mara kadhaa kufanya uharamia kwa kuvunja makaazi ya watu, kupiga watu, kupora Mali za watu, serikali na jeshi LA polisi inasemekana wamekwisha kufanya upelelezi bila kubaini kundi hilo na wala kujua lengo na maelekezo yao yanatoka kwa nani.

Pia lipo kundi jengine limengezeka ambapo wao huamka alfajiri wakiwa na gari yao “Carry” iliyokuwa Haina nambari za usajili, huwakamata wale watu wanaonza shughuli zao alfajiri wakawatesa na kuwanyanganya Mali zao

Sishauri kufanyika uchaguzi wa vyama vingi vya siasa huku washiriki wakiwa wachache na kumuacha mdau ama chama kikuu kikiwa nje ya uchaguzi huo, hapo itakuwa demokrasia imeendelea kukandamizwa na kukanyagwa, ni vyema tukazitumia taasisi na jumuiya tulizonazo kutatua mgogoro kwa misingi ya katiba na sheria, ili tufanye mamo yetu ya kimaendeleo kwa amani.

Baraza la vyama vya siasa ni chombo kilochoundwa ili kuviweka vyama vya siasa vyote pamoja , lengo ni kujadili na kutoa maamuzi mbali mbali yamayohusu nchi na siasa zake, chimbuko la Baraza LA vyama vya siasa ni baada ya mgogoro wa uchaguzi wa Mwaka 2000 kule Zanzibar, ambapo mgogoro huo ulipelekea watu kuuwawa kule kisiwani Pemba, Baraza hili limeshatatua na kutoa maamuzi Mengi katika nchi ya Tanzania, mfano wa karibu ni ule mgogoro wa uchaguzi ambapo Tume ya Uchaguzi na Jeshi LA polisi walitangaza kwamba katika uchaguzi wa 25/10/2015, mtu akimaliza kupiga kura hatoruhusiwa kuwa karibu na kituo anatakiwa kurudi nyumbani.

Ambapo vyama vya upinzani vilipinga agizo hilo kwa kuwa halikuendana na matakwa ya kisheria za uchaguzi, ndipo baraza likakutana katika Hoteli ya bwawani Zanzibar kwa siku mbili mfululizo, wajumbe wote wa vyama wakahudhuria ikiwa ni upande mmoja wa mgogoro na kwa upande wa Pili wa mgogoro wakahudhuria Mwenyekiti wa NEC jaji Mstaafu Damian Lubuva, Mkurugenzi ZEC Salum Kassim Ali, kamishana wa Polisi Jamii na wajumbe wengine kutoka Jeshi LA polisi wakiwemo jaji  Francis Mutungi – Msajili wa vyama vya siasa na Ndugu Systil Nyahuza – Msaidizi Msajili wa vyama vya siasa ambapo kwa juhudi  Baraza la vyama vya siasa mgogoro ule ukatatuka kwa wepesi na kuziacha pande zote za mgogoro zikiwa zimeridhika maamuzi yaliyotolewa.

Hivyo rai yangu ni kusema kwamba tusilipuuze Baraza la vya siasa katika kutafuta suluhu ya mgogoro na mkwamo wa kisiasa Zanzibar, badala yake tusitishe uchaguzi wa marejeo ili tutoe nafasi kwa Baraza ili kutafuta suluhu ya mgogoro huu.

Tanbihi: Makala ya Ali Mohammed

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.