Licha ya ukweli kwamba kundi la Boko Haram linafanya mauaji na mashambulizi dhidi ya raia wasio hatia, ikiwemo kuwateka wasichana kwenye maeneo wanayoyavamia nchini Nigeria, Cameroon na Chad, kuna hadithi za kuajibisha za baadhi ya mateka wa Boko Haram kuwapenda watekaji wao kama ilivyo hadithi ya msichana Zara.

Takribani mwaka mmoja tangu aokolewe kutoka mikononi mwa Boko Haram na jeshi la Nigeria, Zara John, msichana mwenye umri wa miaka 16, bado anampenda mmoja wa wanamgambo waliokuwa wamemteka.

Alipata furaha kubwa kujigundua kwamba ana ujazito wa mwanamme huyo, kufuatia kipimo cha mkojo na damu alichofanyiwa na daktari kwenye kambi ya wakimbizi alikokuwa amepelekwa baada ya kuokolewa.

“Nataka kumzaa mtoto huyu ili niwe na kumbukumbu za baba yake, kwa kuwa sitaweza kuonana naye tena,” anasema Zara, mmoja wa mamia ya wasichana waliotekwa na Boko Haram ndani ya kipindi cha miaka saba ya uasi wa kundi hilo linalojiita la Kiislamu, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Lakini uamuzi wowote kuhusu mtoto huyo haukuwa chini yake tena. Baba yake Zara alikufa maji kwenye mafuriko ya mwaka 2010, kwa hivyo wajomba zake wakaingilia kati. Wengine walikuwa na msimamo mkali kwamba wasingelitaka kuona damu ya Boko Haram kwenye ukoo wao. Wengine wakaona kuwa mtoto huyo hakupaswa kubeba lawama za uhalifu wa baba yake. Hatimaye, wengi wakapiga kura ya kumruhusu Zara abakie na mwanawe, kitoto cha kiume kilichopewa jina la Usman, ambacho kwa sasa kimetimu miezi saba.

“Kila mtu kwenye familia amempokea mtoto huyu”, Zara aliuambia Wakfu wa Thomson Reuters kwenye mahojiano nao kwa njia ya simu, huku akiomba mahala alipo pasitajwe. “Hivi ninavyokwambia, mjomba wangu ametoka kumnunulia kopo la Cerelac na maziwa.”

Zara alikuwa na umri wa miaka 14 wakati wapiganaji wa Boko Haram walipokivamia kijiji chake cha Izge, kaskazini mashariki mwa Nigeria, mwezi Februari 2014. Walichoma nyumba, wakawachinja wanaume na kuwapakia wanawake, wasichana na watoto kwenye malori.

Kaka zake wawili walikuwa nje ya mji wakati wanamgambo hao walipofanya uvamizi huo, moja ya mashambulizi yao ya papo kwa papo na pia uripuaji wa kujitoa muhanga kwenye maeneo ya ibada na masokoni.

Mama yake Zara alianguka kutoka moja ya malori yaliyokuwa yamewabeba, na ingawa alijaribu kulikimbilia gari lililokuwa limewachukuwa binti yake wa pekee na mvulana wake wa miaka minne, lakini akashindwa kutembea umbali wa kilomita 22 kuelekea eneo la Bita, ambalo lilikuwa chini ya udhibiti wa Boko Haram kwa wakati huo.

“Mara tu tulipofika, walitwambia kuwa sasa sisi ni watumwa wao,” anasema Zara, ambaye anakumbuka kwamba kuanzia hapo alianza kuishi maisha yake yote kwa kujifunza swala, kasida, na mafundisho ya dini yake mpya, Uislamu, hadi miezi miwili baadaye alipotakiwa kuolewa na Ali, kamanda wa Boko Haram, na akahamia kwenye nyumba yake na mumewe huyo.

“Baada ya kuwa mke wa kamanda, nikawa na uhuru. Nililala muda wote niliotaka, niliamka muda wowote niliotaka,” anasema msichana huyo ambaye maisha yamemgeuza mama.

“Alininunulia chakula na nguo na alinipa kila ambacho mwanamke anakihitaji kutoka kwa mwanamme”, anasema akiongeza kuwa Ali alimpa pia simu ya mkononi ikiwa na namba yake ya simu na kumchora tattoo ya jina lake tumboni mwake kama alama kuwa ni mke wa kamanda wa Boko Haram.

Ali alimuhakikishia kuwa mapigano hayo yangelimalizika hivi punde na kwamba wangelirejea kwenye mji wao wa Baga, ambako alikusudia mkewe huyo mpya aungane naye kwenye biashara yake ya samaki. Alimuambia kwamba alikuwa amewacha biashara yake hiyo na kujiunga na Boko Haram, baada ya baba yake na kaka zake wawili ambao wote walikuwa wavuvi kuuawa na wanajeshi wa Nigeria.

Katika ripoti yake ya mwezi Juni 2015, ambayo ilitokana na miaka kadhaa ya utafiti na uchambuzi wa ushahidi, shirika la haki za binaadamu la Amnesty International, lilisema jeshi la Nigeria lilikuwa linahusika na uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu na mauaji ya makusudi dhidi ya raia kwenye maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria, na likatoa wito wa kufanyika uchunguzi wa uhalifu wa kivita.

Ali hakuwepo nyumbani wakati jeshi la Nigeria lilipouvamia mji wa Bita mwezi Machi 2015 na kumuokoa Zara na wanawake wenziwe kadhaa kisha wakawapeleka kwenye kambi ya wakimbizi ya Yola. Uvamizi huo ulikuja baada ya shinikizo kubwa la kimataifa dhidi ya Nigeria kuongezeka, kufuatia kitendo cha Boko Haram kuwareka wasichana 200 wa skuli kijijini Chibok, mwezi Aprili 2014. Hata hivyo, hadi sasa wasichana hao hawajapatikana.

Lakini Ali na Zara waliendelea kuwasiliana kwa simu hadi pale wanajeshi walipogundua kuwa baadi ya wasichana kambini hapo bado walikuwa wakiwasiliana na watekaji wao, ndipo walipozichukuwa simu zao na kuwahamishia kambi nyengine hadi walipoungana na familia zao.

Sasa Zara anaishi na familia yake kubwa na mtoto wake kwenye mji ulio mbali na Izge. Kwenye familia yake, ndugu zake wa kiumbe ndio wenye udhibiti wa maisha yake, ambapo maombi ya kufanya mahojiano naye lazima yapitishwe nao, huku nyendo zake zote zikifuatiliwa na familia.

Lakini alipoulizwa kuhusu maoni yake, alisema angelipendelea zaidi kuishi na mume wake wa Boko Haram. “Ningeliweza, ningeliisaka namba yake ya simu aliyonipa,” anasema huku akijutia kutokuihifadhi namba hiyo.

Chanzo: DW

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.