Rais John Pombe Magufuli sasa amejidhihirisha rasmi kuwa mrithi wa mtangulizi wake, Jakaya Mrisho Kikwete. Anawaambia mabalozi wa kigeni eti “Watanzania walio wengi wanataka CUF ithibishe kuwa ilishinda uchaguzi wa Oktoba 25” kwa kurudia uchaguzi wa Machi 20.

Nasikia Rais Pombe ni mtaalamu wa hisabati. Hivyo natumai kama atajikumbusha kidogo tu kanuni ya hesabu za “Equations” itamweka sawa kuvunja hoja yake aliyoitoa ambayo haina na mashiko hata kidogo.

Magufuli alikuwa mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM kama ambavyo Shein alikuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho.

Naamini Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amempatia takwimu sahihi za NEC zinazoonesha kuwa yeye Magufuli alishindwa na mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, katika uchaguzi wa Rais wa Tanzania kwa upande wa Zanzibar.

Magufuli hajawahi kabla ya kuwa rais kuwatendea baya lolote Wazanzibari. Muda wote wa uwaziri wake alihudumu katika wizara za Tanganyika za kushughulikia barabara, uvuvi na madaraja. Kwa kuwa si mwanasiasa, hata katika vuguvugu la Katiba hakuwahi kutamka chochote cha kuwaudhi Wazanzibari – au mimi sina kumbukumbu hiyo.

Kinyume chake, Ali Mohamed Shein amewafanyia Wazanzibari dhambi mbili kubwa zisizosameheka kwao katika miaka 5 ya utawala wake. Ya kwanza ni dhulma aliyowafanyia mashekhe wao na ambayo inaendelea hadi sasa, na ya pili ni ya kuipiga mnada rasmi nchi yao kwa Tanganyika kupitia katiba ya Chenge iliyopitishwa Dodoma.

Wazanzibari walimpa Mungu ahadi kuwa watam’delete’ Shein kwa dhambi zake hizo.

Sasa hoja ya “Equations” kwa Magufuli inakuja hapa: ikiwa yeye alokuwa hajawafanyia baya lolote Wazanzibari walimkataa kwa sababu TU ya kuwa mgombea urais wa CCM, je wanaweza kweli kumpigia kura Shein na kumpa tena urais kwa ubaya aliowatendea?

Naamini hili tu linatosha kumnyamazisha Magufuli na mwengine yeyote anayedai eti CUF isiogope kushiriki tena uchaguzi kama ilishinda kweli Oktoba 25. Kwa sababu suala sio kushinda kwa CUF kunakohotaji kuthibitishwa. Ni kushindwa kwa CCM. Na CCM haiamini kwenye ushindi wa kura. Inataka tu kuitumia kura kuthibitisha ushindi wake wa bunduki.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Abdulfattah Mussa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.