Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, amewataka washirika wa maendeleo wakishawishi Chama Cha Wananchi (CUF) kishiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar ili kuwatendea haki wanachama wake.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalumu mjini Dodoma, Balozi Mahiga alisema wahisani wanapaswa kuchukua jukumu hilo ili CUF iache kususia uchaguzi uliopangwa kurudiwa Machi 20, mwaka huu na kuendelea kumsimamisha mgombea wao wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa vile wao (wahisani) ndio wanaoonekana kusikilizwa zaidi na chama hicho kuliko serikali.

Alisema CUF ambayo miongoni mwa viongozi wake, Katibu Mkuu Maalim Seif, imekuwa karibu zaidi na wahisani ndiyo maana  wameonyesha ghadhabu dhidi ya Serikali ya Tanzania kwa kukatisha misaada, ikiwamo inayotoka Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC).

Zanzibar iko katika mkwamo wa kisiasa baada ya Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015 kutokana na kile kilichoelezwa na mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, kwamba ulijawa na kasoro nyingi zilizoupotezea sifa ya kuwa ‘huru na wa haki’.

Maalim Seif na wanachama wenzake wametangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio na badala yake kusisitiza ZEC iendelee na majumuisho ya kura ili mshindi ajulikane.

Hata hivyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichomsimamisha Dk. Ali Mohamed Shein kutetea nafasi yake ya urais, kinaungana na ZEC kuwa uchaguzi ni lazima urudiwe.

Akieleza zaidi kuhusu suala hilo la Zanzibar, Balozi Mahiga alisema pamoja na mvutano uliopo sasa visiwani humo, anaamini bado kuna nafasi ya kutosha kwa pande zote kuzungumza ili kufikia maridhiano, ingawa mojawapo ya changamoto zilizopo ni pamoja na hali ya kutoaminiana.

“Naona kwa sababu sisi wenyewe ile inaitwa confidence (kuaminiana) haipo sana. Kati ya sasa na Machi tuendelee na kipindi cha kujenga kuaminiana kwani bado kuna nafasi ya mazungumzo,” alisema Mahiga.

Aliongeza kuwa katika kipindi hiki (sasa hadi Machi), kuwe na ushawishi kwa pande zote kuhusiana na uchaguzi huo.

“Kupeana ushawishi wa namna fulani… unataka kuwe na maandalizi ya namna gani, ushiriki wa namna gani, tuna karibu siku 50. Lakini pia marafiki zao (CUF) wawashawishi,” alisema Balozi Mahiga.

Alipoulizwa ni kwa nini anaona CUF iko karibu zaidi na wahisani hadi kusema ni marafiki zao, alisema; “Ni kwa sababu ya ile ghadhabu wanayoifanyia serikali ya  Tanzania.   Ni kama vile kwa nini huyu mmemfanyia hivi.”

Kadhalika, Balozi Mahiga alisema leo atakutana na mabalozi wa nchi zote waliopo nchini na kwamba miongoni mwa mambo yatakayopata nafasi ya kuzungumziwa ni pamoja na suala la Zanzibar.

Kwa hivyo hivi, mimi tarehe 8 (leo), nakutana na mabalozi wote, kwa niaba ya Rais. Nitazungumza hata na hili, ninavyosema rafiki zao ni kwamba wao si tu wanawasikiliza, wanawafuata… jamani eeh, hivi na hivi, na wale wanawasikiliza. Watu wa upinzani wanawafuata wale (wahisani), inawezekana wana imani zaidi na wale wanaowafuata, na wale wanawasikiliza,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Jamani ni hivi na hivi na hivi… sasa sisi wenyewe, imani kati ya sisi kwa sisi imepungua. Lakini wakikimbilia kule wanasikilizwa, ndiyo tunasema mnavyozungumza na hao marafiki, au kama siyo marafiki, basi  hao watu wanaokuja, mjaribu kuwashawishi.

“Hebu fikiria, chama ambacho kina wafuasi wengi wasishiriki katika uchaguzi… tutakuwa na miaka mitano ya aina gani? Tutarudi kule nyuma tulipotoka. Siyo sahihi, hatuwatendei haki watu wa Zanzibar, hatuwatendei haki Watanzania wengine ambao wote tunabeba mzigo sasa hivi kwa sababu ya maamuzi tu ya chama kimoja.”

Bila kufafanua, alisema watu wanaadhibiwa kwa kitu ambacho kina majibu, huku akisema kwenye siasa lazima watu wakubali kuwa na machaguo mbalimbali na siyo kung’ang’ania msimamo mmoja.

Alisema amekuwa akiulizwa sana suala la hali ya Zanzibar kila anapokwenda nje, lakini yeye amekuwa akiwaeleza uhalisia wa mambo ulivyokuwa mpaka uchaguzi ukafutwa.

Dk. Mahiga alisema jibu ambalo huwapa ni kwamba pamoja na kuwa Tanzania ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Zanzibar ina madaraka tosha ya mambo yake ya ndani, serikali yake, Katiba, Bunge (Baraza la Wawakilishi)  na Tume ya Uchaguzi.

Pia alisema huwaeleza kwamba uchaguzi wa Zanzibar ni tofauti na ule wa Tanzania na namna hata walivyomchagua Rais wa Muungano, John Magufuli.

“Serikali ya Zanzibar ina uamuzi wake, utaratibu wake, na  utamaduni wake wa kisiasa ambao ni tofauti. Kwa hiyo mtu akisema ni Tanzania lakini Zanzibar  haikuwa hivi, Tanzania si mkoa, Tanzania ni serikali… kwa hiyo hilo lazima lijulikane hivyo,” alisema.

Aliongeza kuwa katika  mantiki hiyo ya Zanzibar kuwa na aina yake ya serikali na mwelekeo wake, pia wana utamaduni wa kutatua matatizo yao wenyewe.

“Tuliona huko nyuma wakati ule kuna matatizo kati ya vyama na serikali, na vyama vya upinzani, hatimaye wakakaa na tukapata muafaka wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hii ilikuwa wao tu pamoja na kuwa watu walisaidia na kuwaambia jamani zungumzeni,” alisema.

Balozi Mahiga alisema Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) iliona kuna tatizo Pemba, ambapo idadi ya wapigakura ilikuwa kubwa kuliko walioandikishwa na pia kulikuwa na matatizo katika kuhesabu  kura, hivyo wakaona hata wakitangaza matokeo bado kutakuwa na tatizo.

“Kwa hiyo wakasitisha kuhesabu kura. Zingine zilikamilika pamoja na kuwa zilikuwa na utata, zingine wala hazikuhesabiwa na likatokea tamko kwamba uchaguzi umesitishwa.

“Baadhi ya watu, mashirika, European Union, Marekani, Commonwealth na wote waliona kwamba tume haikutenda haki… kwamba ingemaliza kuhesabu na matangazo yatoke. Lakini tume iliona kabisa kwamba ikifanya hivyo itakuwa imekiuka maadili  yake,“ alisema.

“Kwa hiyo kukawa na mvutano. Kwamba kwa upande wa vyama, walivyopewa maamuzi haya ya tume, wakakaa kuona wafanye nini. Na tukadhani katika hivi vyama kuzungumza kule, na sisi bara watatukaribisha, au Serikali ya Muungano watatukaribisha. Lakini wakasema hata, hili mtuachie sisi wenyewe tutalizungumza kuhusu huu uamuzi wa tume,” aliongeza Balozi Mahiga.

Alisema mazungumzo baina ya CUF na CCM yalianza na kufanya takriban vikao sita huku kukiwa hakuna kitu kinachosemwa juu ya kinachoojadiliwa.

“Tukasema jamani eeeh, mbona hatusikii tamko lolote? Na hapo ndipo Rais Dk. John Magufuli akachukua uamuzi wa kuzungumza na pande zote mbili. Akazungumza na Masalim Seif (mgombea urais wa CUF), na Dk. Shein kwamba jamani vipi?

“Na wao walisema wanazungumza wenyewe na wamejumuisha marais wa zamani wa Zanzibar, si marais wa zamani wa Tanzania. Na kila mtu akawa anauliza hivyo, jamani vipi? Sasa wakati wanazungumza hivyo, baadhi ya wadau wetu wa maendeleo na marafiki zetu wakawa wanasema, Jamhuri ya Muungano hawafanyi vya kutosha kusukuma na kutatua suala hili,” alisema.

“Wengine wakasema hata misaada tunasimamisha, kama vile Marekani (MCC) tunasimamisha kwa sababu sisi tunaona haya mazungumzo hayatoi majibu na afadhali tu yatangazwe (matokeo ya uchaguzi) kama yalivyokuwa, lakini katika hilo baadaye tume ikasema jamani, afadhali tuite uchaguzi mwingine.

“Sasa mimi ninaloeleza katika hili kwa marafiki zetu ni kwamba kama upinzani wanadai waliungwa mkono na kushinda, sasa hivi hawana cha kuogopa… wana uchaguzi mwingine. Wale waliowachagua na wanaodai kwamba waliwapa ushindi kwa nini wasiwachague kama walivyowachagua huko (awali),” alisema Balozi Mahiga.

Alisema jambo kubwa hivi sasa ni kuhakikisha uchaguzi huu utapangwa kwa namna ambayo ni ya wazi na utakuwa wa haki na unasimamiwa ipasavyo na watu mbalimbali, ikiwezekana hata wa nje wakaribishwe tena ili watazame.

Alisema anaona kufanya uchaguzi mwingine ni suluhisho kuliko kusema, ‘sisi tumeshinda tutangazwe’, jambo ambalo katikati ya utata uliopo linaweza kuleta fujo.

Alisema kwa sababu inaonekana wahisani na nchi zingine wanazungumza zaidi na CUF na wanawabebea mabango, wawaambie kama kweli wana uhakika kwamba walishinda uchaguzi, hawana cha kuogopa bali waende tena kwenye uchaguzi.

Balozi Mahiga alisema jambo la msingi ni kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanakuwa huru na haki.

SURA YA TANZANIA NJE

Alisema kwa nafasi aliyopewa na Rais Magufuli, atahakikisha sura ya Tanzania nje inakuwa nzuri wakati kiongozi huyo wa nchi (Magufuli) akiendelea kupambana na changamoto za ndani ya nchi.

“Nataka kumsaidia Rais ili yeye aunganishe siasa za ndani na maendeleo anayotaka kuyaleta na wizara yangu itakayokuwa inafanya huko nje ya nchi,” alisema.

Balozi Mahiga alisema kwa miaka 15, Tanzania imekuwa ikifanya diplomasia ya uchumi, jambo ambalo amepanga kulipeleka mbele zaidi.

Alisema katika kuendesha diplomasia hiyo, atahakikisha mkakati wa Rais Magufuli wa kufikia uchumi wa kati na ule wa viwanda, unafanikiwa.

“Kuna mambo yanatakiwa kufanyika ili kufika hapo… moja ni kuhakikisha balozi zetu zikishirikiana huku wanapewa majukumu mapya na uwezo mpya. Lazima tufanye uchambuzi kuona ni mambo gani mapya yanatakiwa yafanywe, siyo tu kusema kuleta wawekezaji na kutafuta biashara. Lazima tuende mbali na kusema ni biashara gani,  kama ni mazao, ni yepi? Viwanda vipi,” alisema.

Alisema kuna masuala mapya ambayo kama nchi,  yanapaswa kufanyika ikiwa ni pamoja na kuboresha  ushirikiano wa Afrika Mashariki, kikanda na kimataifa.

Alisema ushirikiano ni fursa ya kipekee kwani hakuna nchi inayoweza kuendelea yenyewe na pia kwenye jumuiya hizo kuna fursa nyingi.

Aliongeza kuwa hata wahisani, wengi wao siku hizi hutoa misaada na mambo mengi kupitia kwenye nchi zilizoungana, hivyo kwa kuwa wizara yake hata jina lake limebadilika na kuhusisha mambo ya Kikanda, Afrika Mashariki na Kimataifa, atahakikisha anafanikisha jambo hilo.

MIGOGORO

Akizungumzia mgogoro wa Ziwa Nyasa, alisema mazungumzo yanaendelea vizuri na kwamba sasa wasuluhishi wanaandaa ripoti ya pili.

Kuhusu mgogoro wa Burundi, alisema Tanzania inatambua kwamba kuna tatizo lakini isichoafiki ni Umoja wa Afrika kupeleka jeshi bila ridhaa ya Serikali ya Burundi.

Alisema hatua hiyo itasababisha taharuki na watu wataendelea kukimbia na hata kuongeza idadi ya wakimbizi nchini.

Alisema hata Marekani iliwahi kupeleka wanajeshi Somalia bila ridhaa ya Serikali ya nchi hiyo, matokeo yake askari wake walikuwa wakiuliwa hovyo na miili yao kuburuzwa mitaani.

Kutokana na hali hiyo, alisema Tanzania imefanikiwa kuushawishi Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa (UN) kuhusiana na Burundi na tayari wamebadilisha uamuzi wao wa kupeleka jeshi nchini humo (Burundi).

Alisema hivi sasa, uwezekano unaotakiwa kuangalia ni kuhakikisha mazungumzo yanafanyika na kumalizika na kuangalia uwezekano wa kutumia zaidi polisi kutunza amani na wanajeshi wa kukaa kwenye mpaka wa Burundi ama kunyang’anya silaha kutoka mikononi mwa vikundi visivyostahili kuwa nazo.

CHANZO: NIPASHE la tarehe 8 Februari 2016

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.