Rais John Magufuli amerejelea msimamo wa Chama chake cha Mapinduzi (CCM) kuwa lazima uchaguzi urejewe visiwani Zanzibar, kwani ndiyo “suluhu ya pekee” kwa mkwamo uliopo.

Ameyaeleza hayo katika hotuba yake kwa mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania iliyosomwa kwa niaba yake na waziri wa mambo ya nje, ushirikiano wa Afrika Mashariki, kikanda na kimataifa Balozi Augustine Mahiga leo ikulu jijini Dar es salaam.

Katika hotuba hiyo, Rais Magufuli amewaeleza mabalozi hao kuwa licha ya Tanzania kuwa nchi moja, Zanzibar ina mfumo wake wa siasa, ina serikali yake, Katiba yake na pia tume yake ya uchaguzi inayojitegemea.

Amesema tume hiyo ilifuta uchaguzi kutokana na mapungufu yaliyojitokeza kisiwani Pemba, na kwamba tayari tarehe mpya ya uchaguzi wa marudio imekwisha tangazwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Amesema mazungumzo ya kutatua mgogoro huo yalifanyika bila mafanikio ambapo chama kikuu cha upinzani (CUF) kimeendelea kupinga uchaguzi wa marudio huku vyama vingine kikiwemo chama tawala vikionesha uhitaji wa uchaguzi huo wa marudio.

Amesema kwa hali ilivyo, busara inahitajika ili kunusuru suala hilo, na kwamba kususia uchaguzi siyo suluhu bali kutumia nafasi iliyopo sasa kujadili namna ya kuufanya uchaguzi wa marudio kuwa huru na wa haki.

Amewaeleza mabalozi hao kuwa serikali pamoja na watanzania walio wengi wangependa kuona CUF inathibitisha madai yake ya kushinda uchaguzi huo kupitia sanduku la kura katika uchaguzi wa marudio.

“Tunakiasa chama cha CUF kama ambavyo watanzania wengi wangependa kuona, kuthibitisha madai ya ushindi wao katika sanduku la kura, hakuna jinsi nyingine ya kutatua suala hili zaidi ya kukubali kufanya uchaguzi wa marudio” imesema sehemu ya hotuba hiyo.

Rais Magufuli amewahakikishia mabalozi hao kuwa nchi ni salama na hali ya amani na utulivu ni ya kuridhisha katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi wa marudio.

Chanzo: JamiiForum

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.